Newcastle United 0-2 Manchester United: Ole Gunnar Solskjaer aiga Sir Matt Busby, Chelsea wakwamishwa darajani na Southampton

Romelu Lukaku

Chanzo cha picha, Rex Features

Mshambuliaji Mbelgiji Romelu Lukaku aliingia kama nguvu mpya na kufunga mara yake ya kwanza kuugusa mpira na kuwawezesha Manchester United kuwalaza Newcastle United 2-0.

Ushindi wao umemfanya meneja wao mpya Ole Gunnar Solskjaer kuwa meneja wa pili katika historia ya klabu hiyo kushinda mechi zake za kwanza nne.

Raia huyo wa Norway ameiga meneja maarufu Sir Matt Busby aliyefanya hivyo mwaka 1946.

Lukaku, aliyekuwa amekaa uwanjani sekunde 38 pekee, aliupata mpira kufuatia kosa la kipa Martin Dubravka kutoka Slovakia aliyeutema mpira baada ya frikiki iliyopigwa na Marcus Rashford dakika ya 64.

Rashford aliongeza bao la pili dakika ya 80 baada ya uchezaji wa kuridhisha ulioshirikisha Lukaku na Alexis Sanchez ambaye pia alikuwa ameanza mechi akiwa benchi.

Matokeo ya mechi za EPL Jumatano 2 Januari, 2019

  • Bournemouth 3-3 Watford
  • Chelsea 0-0 Southampton
  • Huddersfield 1-2 Burnley
  • West Ham 2-2 Brighton
  • Wolves0-2 Crystal Palace
  • Newcastle 0-2 Man Utd

Newcastle walishindwa kwenye mechi yao ya nane ligini msimu huu.

Nafasi bora zaidi kwa Newcastle ilimwangukia Mhispania Ayoze Perez aliyefanikiwa kuwakwepa walinzi wa Man Utd lakini Luke Shaw akafanikiwa kumzuia.

Romelu Lukaku

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha, Romelu Lukaku amechangia ufungaji wa mabao 11 katika mechi 12 za EPL alizocheza dhidi ya Newcastle - kufunga mabao saba, na kusaidia ufungaji wa manne

Wenyeji walikuwa na bahati kumaliza na wachezaji 11 uwanjani baada ya nguvu mpya Jonjo Shelvey kumkaba Paul Pogba kutoka nyuma, lakini hakuadhibiwa na mwamuzi.

Man Utd waendelea kuimarika chini ya Solskjaer

Baada ya ushindi wa kuridhisha dhidi ya Cardiff, Huddersfield na Bournemouth, mechi hiyo ya Jumatano ilikuwa mtihani mkubwa zaidi kwa Manchester United chini ya Solskjaer.

Mechi kama hiyo msimu uliopita, walikuwa wameshindwa 1-0, lakini walicheza vyema sana kwa kushambulia na kuonyesha mchezo wa kupendeza.

Ingawa hakufunga, baada ya kufunga mabao manne katika mechi zake mbili za awali, Pogba alitekeleza mchango muhimu mechi hiyo dhidi ya Newcastle.

Marcus Rashford

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha, Marcus Rashford alitawazwa mchezaji bora wa mechi - alitoa makombora saba, manne yakalenga goli na akafunga bao moja

Ole Gunnar Solskjaer alisemaje?

"Utafurahi sana ukipata ushindi wa mechi nne kutoka kwa mechi nne - hatujafungwa pia kutoka kwa mchezo wazi.

"Tulianza kwa mwendo pole kiasi kipindi cha kwanza lakini tuliidhibiti mechi vyema, tulikuwa makini sana na kwa jumla ulikuwa uchezaji mzuri.

"Kwa kipindi cha dakika tano, tuliwapa fursa mbili au tatu hivi lakini tukatulia tena.

"Marcus Rashford kidogo anafanana na Cristiano kwa makombora yake, hujipinda na kuyumba, lakini nililipenda bao lake la leo. Alijituliza, na kulitumbukiza wavuni. Hongera.

"Ana miaka 21 pekee, ni lazima ukumbuke hilo. Inakubidi kumchokoza Paul Pogba wakati mwingine na kumzindua, ametufaa sana."

Chelsea taabu

Eden Hazard

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chelsea walikuwa wamewashinda Southampton katika mechi saba za karibuni zaidi walizocheza mashindano yote

Mkufunzi mkuu wa Chelsea Maurizio Sarri amedokeza haja kubwa kwa klabu yake kumnunua mshambuliaji mpya baada yao kushindwa kuwapangua Southampton uwanjani Stamford Bridge. Mechi ilimalizika sare 0-0.

Wenyeji walidhibiti mpira 72% lakini hawakuweza kupenya ngome ya Watakatifu hao ambayo ililindwa ikalindika.

"Nafikiri tulicheza vyema kwa mita 80 uwanjani, lakini hizo mita 20 nyingine tulipata taabu," Sarri alisema baada ya mechi.

Chelsea kwa sasa mshambuliaji wao pekee anayeweza kucheza ni Alvaro Morata, Olivier Giroud anauguza jeraha la kifundo cha mguu.

"Ni lazima tujaribu kutatua tatizo hilo la mita 15, 20 za mwisho. Na klabu hii inafahamu maoni yangu. Nafikiri tunahitaji kitu chenye sifa tofauti.

"Silidhibiti soko. Ni lazima nijaribu kuwaboresha wachezaji wangu, timu yangu, safu yangu ya ushambuliaji, au hata zaidi hatua yangu ya mashambulizi mita 20 za mwisho.

"Klabu yangu inafahamu msimamo wangu, maoni yangu. Bodi ndilo sasa kuamua."

Sarri hata hivyo amefutilia mbali uwezekano wa kuwaita washambuliaji walio nje kwa mkopo - Michy Batshuayi na Tammy Abraham walio Valencia na Aston Villa mtawalia.

Nini kinafuata?

Manchester United pia watakuwa wenyeji wa klabu ya Championship katika Kombe la FA Jumamosi kabla ya kukutana na Tottenham uwanjani Wembley Ligi Kuu ya England 13 Januari.

Newcastle watakutana na klabu ya Championship Blackburn Rovers katika raundi ya tatu Kombe la FA Jumamosi kabla ya kusafiri Stamford Bridge kukutana na Chelsea Ligi ya Premia 12 Januari.

Chelsea watakutana na klabu ya Championship Nottingham Forest raundi ya tatu Kombe la FA Jumamosi 5 Januari, na kisha wakutane na Tottenham ugenini mechi ya kwanza nusufainali ya Kombe la Carabao Jumanne, 8 Januari na kisha warejee ligini Jumamosi 12 Januari dhidi ya Newcastle.

Southampton watacheza Kombe la FA ugenini Derby Jumamosi kisha wasafiri tena East Midlands kwa mechi dhidi ya Leicester ligini wiki moja baadaye