Arsenal 4-1 Fulham: Unai Emery aeleza sababu ya kumtoa Alexandre Lacazette uwanjani

Chanzo cha picha, PA
Meneja wa klabu ya Arsenal Unai Emery ametetea uamuzi wake wa kumtoa uwanjani mfungaji bao Alexandre Lacazette wakati wa mechi yao dhidi ya Fulham ambapo waliwalaza 4-1.
Kiungo huyo mshambuliaji kutoka Ufaransa aliwafungia The Gunners bao lao la pili kipindi cha pili kunako dakika ya 55, lakini aliondolewa uwanjani kipindi cha pili na nafasi yake akaingia raia wa Wales Aaron Ramsey.
Mambo wakati huo yalikuwa 2-1 wakati wake kuondoka uwanjani, baada ya Aboubakar Kamara kufunga dakika ya 69.
Uamuzi wa kumtoa Lacazette ulikosolewa vikali na wengi wa mashabiki uwanjani Emirates.
Lakini Ramsey alilipa imani ya Emery kwa kufunga bao dakika ya 79, na kisha Aubameyang akawafungia bao la kukamilisha ushindi wao dakika ya 83.
"Nawaelewa mashabiki," alisema Emery baada ya mechi hiyo ambayo iliwasaidia kupunguza mwanya kati yao na Chelsea walio nafasi ya nne kuwa alama mbili, ingawa Chelsea wanatarajiwa kucheza na Southampton Jumatano.
"Kiufundi, tulifikiri wakati huo kwamba tulihitaji kubadilisha ili kuiweka timu sawa zaidi. Zaidi ya yote, tulikuwa tunajua kwamba kiungo wa kati wa Fulham Jean Michael Seri alikuwa anaingia uwanjani na hivyo tulihitaji mchezaji wa kumfuata na kumkaba, ili asiwe na wakati rahisi kuupata mpira na kucheza.
"Ramsey anaweza kufanya hivyo na pia kutusaidia katika mashambulio, na alifunga. Sababu ndiyo hiyo. Nahitaji kufanya kazi yangu. Na sio labda, kwa sababu kila shabiki anaweza kuwa na maoni tofauti, ni mambo ya kiufundi."
Gunners walikuwa wamepokezwa kipigo chao kikubwa zaidi msimu huu Jumamosi walipolazwa 5-1 uwanjani Anfield na Liverpool lakini mabao hayo yao ya Jumanne kutoka kwa Granit Xhaka, Lacazette, Ramsey na Pierre-Emerick Aubameyang yaliwawezesha kushinda mechi yao ya pili katika mechi sita walizocheza karibuni.

Chanzo cha picha, Reuters
Arsenal walikuwa tena bila Mesut Ozil, kwani Mjerumani huyo bado anauguza jeraha la goti lililomzuia kucheza mechi hiyo dhidi ya Liverpool wikendi.

Chanzo cha picha, AFP
Ramsey, ambaye mkataba wake unafikia kikomo mwisho wa msimu, amekuwa akitafutwa na klabu kubwa za Ulaya zikiwemo Bayern Munich, Inter Milan, Juventus, Paris St-Germain na Real Madrid.
Nini kinafuata?
Klabu zote mbili sasa zinajiandaa kucheza raundi ya tatu Kombe la FA, Arsenal watakuwa ugenini katika klabu ya League One ya Blackpool Jumamosi, 5 Januari nao Fulham wacheze na klabu ya Oldham Athletic inayocheza League Two Jumapili.
Katika Ligi Kuu England, 12 Januari, Arsenal watakuwa ugenini West Ham, nao Fulham ugenini Burnley.












