Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ballon d'Or: Lionel Messi ni watano kwa ubora duniani? Meneja wa Barcelona Ernesto Valverde hakubali
Meneja wa Barcelona amesema kwake hali kwamba Lionel Messi aliorodheshwa wa tano kwenye tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya Ballon d'Or ni jambo linalokaa kama kioja.
Ernesto Valverde amesema ni jambo lisiloeleweka kamwe.
Kiungo wa kati wa Real Madrid Luka Modric alishinda tuzo huyo, ambayo hutolewa kila mwaka na jarida la France Football na mshindi hupigiwa kura na waandishi 180.
Nyota wa Barcelona na Argentina Messi, 31, aliorodheshwa nje ya tatu bora kwa mara ya kwanza tangu 2006.
Amewahi kushinda tuzo hiyo mara tano.
"Tunampongeza Modric kwa kushinda Ballon d'Or lakini Messi kuorodheshwa wa tano ni kituko," amesema Valverde.
"Sitazungumzia mambo mengi yasiyoeleweka kuhusu tuzo hiyo."
Messi alishinda tuzo ya mfungaji bora wa mabao Ulaya kwa mara ya tano msimu uliopita, baada ya kufunga mabao 34 akichezea Barcelona ambapo walishinda La Liga na Copa del Rey.
Messi alikuwa na alama 280 baada ya kura za Ballon d'Or kupigwa.
Mshindi Modric alikuwa na kura 753.
Raia huyo wa Argentina alikuwa ameachwa kwa mbali na hasimu wake mkuu wa awali Cristiano Ronaldo (476) aliyekuwa anachezea Real lakini sasa anachezea Juventus ya Italia.
Waliowafuata Modric na Ronaldo ni mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann (414) na kinda wa Paris St-Germain Kylian Mbappe (347).