Ballon d'Or: Sergio Aguero na Gareth Bale miongoni mwa wanaoshindania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani

Chanzo cha picha, Reuters
Nyota wa Juventus Cristiano Ronaldo na mshambuliaji wa Manchester City Sergio Aguero, ni miongoni mwa wachezaji walioteuliwa kushindania tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu.
Kuna pia wachezaji wa Chelsea Eden Hazard na N'Golo Kante.
Mshambuliaji wa Wales Gareth Bale anayechezea Real Madrid pia ameorodheshwa kushindania.
Waandalizi wa tuzo hiyo watakuwa wakiwatangaza wachezaji watakaowania tuzo hiyo mwaka huu kwa mafungu siku yote hadi wafike wachezaji 30.

Chanzo cha picha, Reuters
Waliotangazwa kufikia sasa
- Sergio Aguero (Manchester City)
- Alisson (Liverpool)
- Gareth Bale (Real Madrid)
- Karim Benzema (Real Madrid)
- Edinson Cavani (PSG)
- Thibaut Courtois (Real Madrid)
- Cristiano Ronaldo (Juventus)
- Kevin de Bruyne (Manchester City)
- Roberto Firmino (Liverpool)
- Diego Godin (Atletico Madrid)
- Antoine Griezmann (Atletico Madrid)
- Eden Hazard (Chelsea)
- Isco (Real Madrid)
- Harry Kane (Tottenham)
- N'Golo Kante (Chelsea)
- Hugo Lloris (Tottenham)
- Mario Mandzukic (Juventus Turin)
- Sadio Mané (Liverpool)
- Marcelo (Real Madrid)
- Kylian Mbappé (PSG)
- Lionel Messi (FC Barcelona)
- Luka Modric (Real Madrid)
- Neymar (PSG)
- Jan Oblak (Atlético Madrid)
- Paul Pogba (Manchester United)
- Ivan Rakitic (Barcelona)
- Sergio Ramos (Real Madrid)
- Mohamed Salah (Liverpool)
- Luis Suarez (Barcelona)
- Raphaël Varane (Real)

Chanzo cha picha, Getty Images
Ballon d'Or ni tuzo mashuhuri ambayo imekuwa ikitolewa tangu mwaka 1956 na hutolewa kwa mchezaji bora zaidi wa mwaka wa kiume duniani.
Sherehe ya kumtangaza mshindi itafanyika mjini Paris mnamo 3 Desemba.
Mchezaji bora wa kike duniani pia atatunukiwa kwa mara ya kwanza.
Mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo, aliyehamia Juventus kutoka Real Madrid majira ya joto. alishinda tuzo ya Ballon d'Or mwaka jana.
Ballon d'Or ni tuzo ya aina gani?
Tuzo ya Ballon d'Or ambalo kwa Kifaransa maana yake ni Mpira wa Dhahabu imekuwa ikitolea na jarida la France Football ekila mwaka tangu 1956, na mshindi wa kwanza alikuwa mchezaji wa zamani wa kimataifa wa England Sir Stanley Matthews.
Orodha ya wanaoshindania huandaliwa na wafanyakazi wa jarida hilo la Ufaransa, na mshindi kuchaguliwa kwa kupigiwa kura na waandishi wa habari za michezo kutoka kote duniani. Kila taifa huwakilishwa na mwandishi mmoja.
Kwa miaka sita, kulikuwa na ushirikiano na Shirikisho la Soka Duniani Fifa na jina lake likawa Fifa Ballon d'Or.
Hata hivyo, Fifa walifikisha kikomo ushirikiano huo mwezi Septemba 2016, na sasa kunatolewa tuzo ya Ballon d'Or na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Fifa.

Chanzo cha picha, Fifa/getty image
Washindi wa tuzo za Fifa walitangazwa Septemba ambapo kiungo wa kati wa Croatia na Real Madrid Luka Modric alitawazwa mchezaji bora wa kiume duniani.
Mchezaji wa Brazil na Orlando Pride Marta alitawazwa mchezaji bora wa kike.
Ronaldo alikuwa ameshinda tuzo hiyo mwaka 2016 na 2017.













