Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ligi Kuu England: Uamuzi ambao ungebatilishwa na VAR mechi za EPL, Sane angepata bao la pili
Uamuzi mmoja katika mechi tano za Ligi Kuu ya England zilizochezwa wikendi ungebatilishwa iwapo teknolojia ya kutumia video kuwasaidia waamuzi uwanjani ingetumiwa uwanjani Jumamosi.
Hii ni baada ya teknolojia hiyo kufanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza katika zaidi ya mechi moja katika ligi hiyo.
Bao la Mjerumani Leroy Sane lilikataliwa na mwamuzi kwa kuwa alikuwa ameotea, lakini VAR inaonesha kwamba hakuwa ameotea.
Hii ina maana kwamba badala ya ushindi wa 3-0 ambao Manchester City waliupata dhidi ya Fulham wakiwa kwao nyumbani, matokeo yalifaa kuwa 4-0.
Sane ndiye aliyekuwa ametangulia kuwafungia City dakika ya 2, bao la kasi zaidi EPL msimu huu.
David Silva alifunga la pili dakika ya 21 kabla ya bao hilo la Sane kukataliwa muda mfupi kabla ya mapumziko. Raheem Sterling aliongeza la tatu dakika ya 47.
Majaribio hayo yalikuwa yanadhibitiwa kutoka kituo kimoja kikuu cha VAR.
Hakukuwa na mawasiliano ya aina yoyote na waamuzi uwanjani mechi zilipokuwa zikiendelea.
Taarifa zinasema wasimamizi wa Ligi ya Premia walifurahishwa na jinsi majaribio hayo yalivyoendelea.
Uamuzi mwingine wa utata ulikuwa na mkwaju wa penalti uliozawadiwa Bournemouth baada ya mchezaji wao kunawa mpira eneo la hatari. Walishinda 4-2.
VAR inaonesha mwamuzi hakukosea.
Mechi ambazo VAR ilifanyiwa majaribio
- AFC Bournemouth 4-2 Leicester City
- Chelsea 4-1 Cardiff City
- Huddersfield Town 0-1 Crystal Palace
- Manchester City 3-0 Fulham
- Newcastle United 1-2 Arsenal
Aprili, klabu za Ligi ya Premia zilipiga kura dhidi ya kutumiwa kwa teknolojia hiyo msimu wa 2018-19.
Baada ya kujaribiwa katika mechi moja moja msimu uliopita, wasimamizi wa Ligi ya Premia walitaka kuona iwapo teknolojia hiyo inaweza kufanikiwa ikitumiwa katika mechi kadha kwa wakati mmoja.
Sawa na msimu uliopita, VAR itatumiwa tu katika Kombe la EFL na Kombe la FA lakini katika viwanja vya klabu zinazocheza ligi kuu.
Ilitumiwa katika mechi 19 msimu uliopita, na msimu huu inatarajiwa kutumiwa katika mechi takriban 60.