Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Klabu Bingwa Ulaya: Manchester United kuminyana na Juve ya Cristiano Ronaldo
Pazia la michuano ya klabu bingwa Ulaya msimu wa 2018/19 limefunguliwa kwa kupangwa makundi ambapo klabu ya Manchester United inapambana na nyota wake wa zamani Cristiano Ronaldo aliyehamia klabu ya Juventus.
Ronaldo alikipiga na United kwa miaka sita (2003-2009) kisha akachezea Real Madrid kwa miaka tisa na mwezi Julai mwaka huu akahamia klabu ya Juventus, maarufu kama Bibi Kizee wa Turin. Ronaldo ameifunga United mara mbili walipocheza na Real Madrid katika michuano kama hii mwezi Februari na Machi 2013.
United na Juve zimepangwa katika kundi H pamoja na Valencia na Young Boys ya Uswizi.
Bingwa mtetezi Real Madrid wapo katika kundi G pamoja na Roma ya Italia, CSKA Moscow ya Urusi na Plzen ya Ucheki.
Liverpool wapo kwenye kundi gumu la C na watapambana na Paris St. Germain, Napoli na Red Star ya Serbia.
Tottenham pia wapo kwenye kundi gumu lenye timu konge kama Barcelona, PSV na Inter Milan.
Mabingwa wa EPL Manchester City wapo kundi F pamoja na Shakhtar Donetsk, Lyon na Hoffenheim.
Makundi kamili:
Kundi A: Atletico Madrid, Borussia Dortmund, Monaco, Club Brugge.
Kundi B: Barcelona, Tottenham, PSV Eindhoven, Inter Milan.
Kundi C: Paris St-Germain, Napoli, Liverpool, Red Star Belgrade.
Kundi D: Lokomotiv Moscow, Porto, Schalke, Galatasaray.
Kundi E: Bayern Munich, Benfica, Ajax, AEK Athens.
Kundi F: Manchester City, Shakhtar Donetsk, Lyon, Hoffenheim.
Kundi G: Real Madrid, Roma, CSKA Moscow, Viktoria Plzen.
Kundi H: Juventus, Manchester United, Valencia, Young Boys.
Luka Modric mchezaji bora Ulaya
Timu ya Real Madrid ambayo ilinyakua ubingwa kwa kuwafunga 3-1 katika fainali ya msimu uliopita wameondoka na ushindi mwengine baada ya wachezaji wake kunyakua tuzo zote zilizoshindaniwa.
Luka Modric amenyakua tuzo ya kiungo bora wa mwaka pamoja na ya mchezaji bora wa bara Ulaya.
Keylor Navas amenyakua tuzo ya kipa bora, Sergio Ramos beki bora na Cristiano Ronaldo mshambuliaji bora.
Mchezaji wa zamani wa Manchester United na Real Madrid David Beckham alipewa tuzo ya heshima ya Rais wa Shirikisho la Soka la Bara la Ulaya UEFA.
"Kuanzia kunyakua ubingwa wa Ulaya na Real Madrid na kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Dudia na timu ya taifa langu ya Croatia mpaka kupata tuzo hii, nasikia fahari sana kwa kila nilichofanikisha mwaka huu. Huu ni mwaka bora kabisa katika maisha yangu ya mpira," alisema Modric.