Mambo 5 makuu kuhusu mashindano ya ubingwa wa riadha Afrika yanayoanza Asaba Nigeria

Zaidi ya mataifa 52 yanatarajiwa kushiriki katika mashindano ya riadha barani Afrika yatakayofanyika mjini Asaba, Jimbo la Delta, Nigeria wiki hii.

Shirikisho la riadha Afrika CAA linakutana leo Jumatatu kabla ya kuwapokea wageni hapo kesho Jumanne tarehe 31 Julai.

Wakati huo huo, wanariadha wakongwe na nyota wa miaka 10 iliyopita, watatuzwa kwenye karamu itakayofanyika ndani ya kipindi cha mashindano.

Sherehe rasmi ya ufunguzi itafanyika siku ya Jumatano, Lakini kabla ya hayo yote, je ni mambo gani muhimu ya kuyafahamu kuhusu mashindano haya?

Wenyeji watawika tena?

Ngoma ilipopigwa kwao 2016 - Afrika Kusini - walitamalaki mbio hizo lakini wengi wanauliza iwapo Nigeria - ambayo imekuwa maarufu katika soka ambapo ilikuwa Kombe la Dunia licha ya kutolewa hatua ya makundi - italeta tabasamu kwenye nyuso za mashabiki.

Mshindi wa mbio fupi mashindano ya Jumuia ya Madola 2014 Blessing Okagbare-Ighoteguonor ni mmoja wa wanaotegemewa na timu ya wanariadha 95 iliyotajwa.

Matumani ya Nigeria yamepigwa jeki kwa kushiriki mwanariadha wa zamani wa Uingereza Michael Edwards, ambaye alikuwa bingwa wa mashindano ya kuruka taifa hilo.

Edwards alizuiwa na shirikisho la riadha duniani IAAF dhidi ya kuiwakilisha Nigeria mashindano ya Jumuia ya Madola ya hivi majuzi, Gold Coast, Australia.

Edwards, amechagua kuiwakliisha Nigeria kama alivyofanya nyota wa Arsenal, Alex Iwobi.

Wanariadha wengine ni Ese Brume, Divine Oduduru, Tobi Amusan, Queen Obisesan, Seye Ogunlewe na Kelechi Nwanaga.

Kulingana na wasimamizi, kufikia sasa, wanariadha 473 wa kiume na 400 wa kike watakuwa wakikimbiza upepo pamoja na mashindano mengine. Wanariadha hao watakuwa wakiandamana na maafisa 205.

Mataifa yenye vikosi vingi ni Afrika Kusini, Nigeria, na Kenya. Kenya inawakilishwa na wanariadha 61.

Nini umuhimu wa mashindano haya?

Wanariadha bora yaani watakaomaliza katika nafasi tatu za kwanza na kuandikisha muda au matokeo mazuri, wataiwakilisha Afrika mwezi Septemba katika Jamhuri ya Czech kwa mbio kati ya wanariadha kutoka pembe tofauti za dunia.

Wanariadha hao watafika mjini Ostrava kuanzia mwezi Septemba mwaka huu na kujiunga na mamia ya wanariadha bora kutoka bara tofauti.

Jamhuri ya Czech itakuwa mwandalizi kwa mara ya kwanza huku kinyang'anyiro hicho kikibandkwa jina 'mkwaruzano wa mabingwa'.

Aidha, Taifa bora litakuwa mwakilishi wa Afrika Kombe la Dunia la riadha ambao taifa litakaloongoza jedwali mbio hizi za Nigeria mwaka huu , litapewa nafasi ya kuwa na mwanariadha mmoja wa kiume na mmoja wa kike kuiwakilisha kwenye kipute hicho.

Makala ya kombe la Dunia la riadha 2018 yalimalizika Uingereza huku Afrika Kusini ikiiwakilisha Afrika.

Afrika Kusini kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo?

Bingwa mtetezi Afrika Kusini ambaye analenga kuwa timu bora kwa kuwa kileleni kwenye orodha ya dhahabu kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuvuma makala yaliyopita walipokuwa wenyeji mjini Durban na Marrakech Moroco.

Katika makala yaliyopita 2016, timu ya wanariadha 96, ilizoa medali 33 - 16 za dhahabu, 9 za fedha na 8 za shaba.

Caster Semenya aling'aa mbele ya mashabiki wa nyumbani kwa kunyakua ubingwa mbio za mita 800m, mbio za kupokezana vijiti za mita 400 na mbio za mita 1500.

Nyota wa mita 400 Wayde van Niekerk ni mmoja wa wale wanaotegemewa na Afrika Kusini lakini haitabiriki iwapo ataibuka na ubingwa tena kwenye mbio za mita 200 alizomaliza wa kwanza 2016.

Wengine ni Wenda Nel ambaye aliwatimulia vumbi wapinzani wake mbio za mita 400 kuruka vizuizi.

Mkenya Julius Yego atakuwa na upinzani mkali dhidi ya Phil-Mar Janse van Rensburg aliyetwaa ubingwa kurusha mkuki katika makala ya 2016.

Mwandalizi kujiondoa kabla ya shindano:

Ingawa shirikisho la riadha Afrika liliipa Nigeria tiketi ya kuandaa mashindano hayo, ni mji huu wa Asaba usiozidi watu milioni moja, uliokubali kuwa mwandalizi baada ya mji mkuu wa Lagos kukataa kuchukua majukumu hayo.

Washiriki wakiwemo waandishi, wanariadha, waamuzi na wasimamizi wa vikosi wanasafiri hadi eneo la Asaba lililoko kilomita 300 nje ya Lagos.

Uwanja utakaotumika:

Jina la uwanja linatokana na mkufunzi wa zamani wa Nigeria, Marehemu Stephen Keshi na lilipewa jina hilo kama njia ya kumtunuku kwa kuiwezesha Super Eagles Kubeba kombe la Afcon mnamo mwaka wa 2012.

Uamuzi huo ulifanywa na Gavana wa zamani wa eneo hilo Emmanuel Uduaghan.

Lakini ujenzi wake haukukamilishwa licha ya kutarajiwa kumalizika ndani ya muda wa miezi sita.

Uga wa Stephen Keshi ni wa kwanza nchini Nigeria kuwa na sehemu tisa kwenye uwanja wa mbio na pia sehemu yake ya kuandaa soka umethibitishwa kuwa bora na FIFA.

Aidha, uwanja huo una uwezo wa kuandaa mbio mbili za mita 100 wakati mmoja.

Uwanja huo uko chini ya usimamizi wa jimbo la Delta linaloongozwa na Gavana WA 16, Dr. Ifeanyi Okowa.

Tayari naibu rais wa Mshirikisho ya riaha Afrika Gungaram Gerard Vivian na Lamine Faty ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa bodi hiyo inayosimamia riadha barani wamehakikisha uwanja huo uko katika hali nzuri.

Mashindano ya riadha ya Asaba 2018 yatatumika kuwasaka wawakilishi wa bara Afrika kwenye mashindano ya riadha ya dunia ya 2019 na Kombe la Dunia la Riadha 2019.