Shirikisho la soka nchini Nigeria limeanza uchunguzi wa awali dhidi ya Salisu Yusuf

    • Author, Na Oluwashina Okeleji
    • Nafasi, BBC Michezo, Nigeria

Shirikisho la Soka nchini Nigeria (NFF) linachunguza madai ya rushwa dhidi ya kocha Salisu Yusuf.

Yusuf,56 alinaswa na kamera akichukua fedha kutoka kwa watu wanaoelezwa kuwa wakala wa mchezo wa mpira wa miguu ambao walikuwa wanataka wachezaji wawili wachaguliwe kwa ajili ya michuano ya mabara.

''Ni kweli kuwa NFF wameanza uchunguzi wa awali kuhusu jambo hilo kusaidi akamati ya maadili'', alieleza mkurugenzi wa mawasiliano Ademola Olajire alipozungumza na BBC.

''Hili ni jambo linalochukuliwa kwa umakini wake na uchunguzi makini unahitajika na mamlaka hii''.

''Kwa sasa hakutakuwa na neno zaidi kuhusu jambo hili''.Olajire aliongeza.

Majina ya wachezaji hayajawekwa wazi na Yusuf, ambaye alikuwa kocha msaidizi wa Gernot Rohr katika michuano ya Kombe la Dunia, amekana shutuma dhidi yake.

Yusuf amejitetea kuwa pesa alizopokea ni zawadi na kuwa wachezaji walichaguliwa kwa kuzingatia uwezo wao.

''Katika madai hayo hakuna sehemu inayoonyesha kuwa niliomba fedha kutoka kwa mawakala,isipokuwa wakala alinipatia pesa baada ya kueleza 'matumaini' kuwa wachezaji hao watashiriki michuano hiyo'',Alieleza Yusuf

''Nilipokea fedha hizo kutoka kwa mmoja wa mawakala,ambapo baadae nilibaini kuwa ni dola 750 na si 1000''.

Umoja wa makocha nchini Nigeria wamesema wako upande wa Yusuf ambaye aliiongoza Nigeria katika michuano ya mataifa ya Afrika (CHAN) nchini Morocco mwaka huu.

Kwa hivi sasa Yusuf anapata matibabu nchini England.Kocha mkuu huyo wa Super Eagles anatarajiwa kuongoza kikosi cha Nigeria kwenye michuano ya Olimpiki mwaka 2020.