Mwanamume akwama baada ya lami kuyeyuka barabarani Newcastle, Uingereza

Mwanamume mmoja nchini Uingereza amewashangaza wengi baada ya kukwama kwenye lami iliyokuwa imeyeyuka katika barabara moja akielekea dukani kununua staftahi.

Kijana huyo wa miaka 24 aliwapigia maafisa wa huduma za dharura kupitia nambari 999 baada ya mguu wake wa kushoto kukwama barabarani.

Mguu wake ulikuwa umetumbukia hadi karibu pajani katika barabara moja ya pembeni eneo la Heaton, Newcastle.

Maafisa wa huduma za dharura walilazimika kuchimbua barabara eneo alipokuwa amekwama wakitumia nyundo na patasi kuutoa mguu wake.

Wanasema alinusurika bila jeraha kutokana na hali kwamba alikuwa amevalia "buti la babu yake aina ya Dr Martens" ambazo hufika hadi magotini.

Msemaji wa zima moto amesema tukio hilo lilisababishwa na jua kali ambalo limekuwa likiwaka eneo hilo.

Amesema: "Wakati kuna jua, tahadhari mambo kama haya yanaweza kutokea - kuweni makini zaidi hasa mnapotembea."

Kisa hicho kimetokea siku chache baada ya lori la kusafirisha taka kudidimia kwenye barabara moja ya lami Newbury, Berkshire.

Maeneo mengi kaskazini na kusini mwa dunia yamekuwa yakishuhudia jua kali.

Lami yayeyuka Queensland, Australia

Nchini Australia, wenye magari katika eneo la Atherton Tablelands jimbo la Queensland walilazimika kuyaacha magari yao baada ya lami kuanza kuyeyuka barabarani.

Tairi za magari ziliharibiwa vibaya na lami na sasa madereva takriban 50 wanadai fidia.

Maafisa wanasema kisa hicho kilisababishwa na jua kali, pamoja na hali kwamba ukarabati ulikuwa umefanyika wiki iliyopita.

Watu 33 wauawa na joto kali Canada

Nchini Canada, watu 33 wamefariki dunia wiki hii baada ya kutokea kwa joto kali katika maeneo ya kusini mwa Quebec.

Joto kali lilianza Ijumaa ambapo kiwango cha joto kilifikia 35C (95F) pamoja na kiwango cha unyevu kwenye hewa kupanda.

wengi wa waliofariki ni wa kati ya miaka 50 na 80.

Wakazi wamehimizwa kunywa maji kwa wingi na kukaa kivulini.

Watu 18 kati ya hao waliofariki walikuwa jijini Montreal.

Kiwango cha joto mjini humo wakati kama wa sasa huwa ni 25C.

Barabara huyeyuka wakati gani (Uingereza)?

•Lami kwenye barabara nyingi huweza kuyeyuka kiwango cha joto kikifikia 50C

•Takriban 5% ya barabara 80C

•Barabara za lami hushika joto sana na hivyo kiwango chake cha joto kinaweza kufikia 50C jua kali likiwaka.