Paka mtabiri anoa baada ya Nigeria kushindwa na Argentina

Paka Achilles aliyetabiri vyema matakeo ya mechi zote tatu katika mashindano ya dunia alinoa alipotabiri kuwa Nigeria ingeishinda Argentina wakati kabla ya timu hizo kukutana jana Jumanne lakini Argentina waliwashinda Nigeria kwa mabao 2-1.

Achilles, anayeishi makavazi ya Hermitage ya mji St Petersburg, aliwekwa tayari kwa wapiga picha na kuletewa sahani mbili za chakula, moja kikiwa na bendera ya Nigeria na nyingine ya Argentina kuwekwa mebele yake.

Paka huyo wa rangi nyeupe ambaye ni kiziwi, hubashiri mshindi kwa kuchagua moja kati ya bakuli mbili ambazo zimewekwa bendera za mataifa yanayocheza.

Paka huyo ni miongoni mwa paka wanaofugwa kukabiliana na panya katika makumbusho ya Hermitage mjini St Petersburg, ingawa sasa ana majukumu hayo mapya.

Baada ya muda mfupi Achilles alichagua sahani ya Nigeria na kwa pupa akala chakula kilichokuwa sahani ya bendera ya Nigeria, ishara kuwa Nigeria ingeishinda Argentina.

Hata hivyo Achilles alitabiri sawa Iran kuishinda Morocco, Urusi kuishinda Misri na Brazil kuishinda Costa Rica.

Licha ya Achilles kutabiri ushindi wa Nigeria dhidi ya Argentina, Nigeria ilibanduliwa kutoka mashindano baada ya kushindwa kwa mabao mawili kwa mamoja na Argentina.

Paka huyo ni kati ya wanyama wanajaribu uwezo wao wa kutabiri matokeo ya kombe la Dunia wakiwemo wengine huko Kaliningrad, Yekaterinburg na Sochi.

Wana matumaini ya kumuiga Paul the octopus ambaye alipata umarufu duniani wakati alitabiri vyema matokeo ya mechi zote za Ujerumani kwenye mechi za Kombe Dunia za mwaka 2010 na kuchagua Uhispania kama mshindi.

.