Meneja wa zamani wa Man City Manuel Pellegrini aporwa na majambazi wenye bunduki

Muda wa kusoma: Dakika 1

Meneja wa West Ham Manuel Pellegrini ameporwa na majambazi waliokuwa na bunduki nchini Chile.

Mkufunzi huyo maarufu sana duniani ambaye aliwahi kuwa meneja wa mabingwa wa England Manchester City alikuwa njiani kuelekea kwenye mgahawa mmoja mjini mkuu wa Chile, Santiago, akiwa na mke na marafiki wawili pale walipovamiwa.

Msemaji wa West Ham United amesema: "Tuna furaha kusikia kwamba Manuel na mkewe wako salama, hawakudhuriwa."

Kupitia ujumbe wa Twitter aliouandika kwa Kihispania, Pellegrini amewashukuru polisi wa Chile kwa ujasiri wao na kwa kufika eneo la tukio upesi sana.

Pellegrini, ambaye ni mzaliwa wa Chile, aliteuliwa meneja wa West Ham mwezi Mei.

Mwenyekiti mwenza wa klabu hiyo David Sullivan amesema amewasiliana naye kuma ujumbe wa heri na kumpa pole.

Gazeti la Chile La Cuarta limesema kipochi cha mke wa pellegrini kimeibiwa.

Afisa mmoja wa serikali ameambia gazeti hilo kwamba genge hilo la majambazi liliwafyatulia polisi risasi kabla ya kutoroka kwa kuutmia gari aina ya Porsche ambalo walikuwa wameliiba.

Meneja huyo wa zamani wa Manchester City na Real Madrid aliacha kazi klabu ya Hebei China Fortune ya China mwezi jana.

Alishinda Liig ya Premia akiwa na City mwaka 2014.