Watu 135 wamefariki katika mkanyagano Guinea kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu

Makundi hayo yanasema makadirio hayo yanatokana na taarifa kutoka hospitali, makaburi, mashahidi katika uwanja huo, familia za wahanga, misikiti, makanisa na vyombo vya habari vya ndani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma, Mariam Mjahid & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa matangazo ya moja kwa moja, tukutane kesho.

  2. Sanamu la aliyekuwa mkuu wa Wagner lazinduliwa Afrika ya Kati

    k

    Chanzo cha picha, AFP

    Sanamu la ukumbusho la marehemu kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner wa Urusi, Yevgeny Prigozhin, limezinduliwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

    Sanamu la Prigozhin na msaidizi wake Dmitru Utkin, ambao wote walifariki katika ajali ya ndege mwaka jana, yamewekwa katika mji mkuu wa Bangui.

    Wapiganaji wa Kundi la Wagner wamekuwa CAR tangu 2018, walipoalikwa na Rais Faustin-Archange Touadéra kusaidia kukabiliana na vikundi vya waasi.

    Makampuni tanzu ya kikundi hicho yalipata kandarasi za kuendesha migodi ya dhahabu na almasi. Pia Wagner wanafanya kazi katika nchi nyingine kadhaa za Afrika.

    Prigozhin na Utkin walikufa pamoja na wengine, tarehe 23 Agosti 2023, baada ya ndege yao ya kibinafsi kudondoka kaskazini-magharibi mwa Moscow, na kuwaua wote waliokuwa ndani.

    Ilikuwa ni miezi miwili tu baada ya uasi wa kundi hilo huko Urusi. Kremlin ilikanusha uvumi kuwa ndio ilihusika na ajali hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Nani kuibuka mshindi kati ya Arsenal na Man United leo usiku?

    k

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kocha mpya wa Man United, Reuben Amorim na kocha wa Arsenal, Mike Arteta

    Arsenal itatathmini ubora wa Gabriel, Mikel Merino, Thomas Partey na Ricardo Calafiori lakini wote wanne "wanataka kucheza," kulingana na meneja Mikel Arteta.

    Takehiro Tomiyasu bado atakuwa nje.

    Nahodha wa Manchester United Bruno Fernandes atacheza baada ya kutolewa kama tahadhari wakati wa ushindi wa 4-0 dhidi ya Everton Jumapili.

    Lisandro Martinez na Kobbie Mainoo hawatocheza kutokana na na kuwa na mlimbikizano wa kadi tano msimu huu.

    Leny Yoro anaweza kucheza katika kikosi cha siku ya mechi ya Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupona majeraha ya mifupa.

    Je, nani ataibuka mshindi? Dakika 90+ zitajibu hilo swali.

  4. Namibia yamchagua rais wa kwanza mwanamke

    cx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Netumbo Nandi-Ndaitwah amekuwa makamu wa rais tangu Februari

    Netumbo Nandi-Ndaitwah, kutoka Chama tawala cha South West Africa People's Organisation (Swapo), amepigiwa kura kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Namibia baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita.

    Tume ya uchaguzi ilisema ameshinda zaidi ya 57% ya kura, huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata 26%.

    Kufuatia matatizo ya vifaa na kuongezwa kwa siku tatu kwa upigaji kura katika baadhi ya maeneo ya nchi, Itula alisema mchakato wa uchaguzi "una dosari kubwa."

    Chama chake cha Independent Patriots for Change (IPC) kimesema kinapinga matokeo hayo mahakamani.

    Vyama vingi vya upinzani vilisusia matokeo yaliyotagazwa Jumanne jioni katika mji mkuu, Windhoek, gazeti la Namibia linaripoti.

    Swapo imekuwa madarakani katika nchi hiyo kubwa lakini yenye wakazi wachache kusini mwa Afrika tangu uhuru mwaka 1990.

    Nandi-Ndaitwah, ambaye kwa sasa ni makamu wa rais, amehudumu katika nafasi kubwa za serikali kwa robo karne.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Watu nane mbaroni Tanzania kwa jaribio la utekaji

    DC

    Chanzo cha picha, MITANDAO

    Maelezo ya picha, Picha za CCTV zikionyesha Deogratius Tarimo akichukuliwa kwa nguvu na watu watatu kutoka hotelini.

    Jeshi la Polisi Kanda Maalum, Dar es Salaam, Tanzania, limesema linawashikilia watu 8 kwa tuhuma za tukio la kujaribu kuteka la Novemba 11, 2024, katika mkoa huo.

    Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi, Muliro J. Muliro - amesema watuhumiwa wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika Mikoa ya Dar es Salaam, Songea, Ruvuma na Morogoro, pia wamekamata gari aina ya Toyota Raum waliyoitumia wakati wa tukio ikiwa na namba T 237 EGE ambayo si halisi, na uchunguzi umebaini namba halisi ni T237 ECF.

    Amewataja waliokamatwa kuwa ni Bato Bahati Tweve 32, Yusuph Abdallah 32, Fredrick Juma 31, Nelson Elimusa Msela 24, Benk Daniel Mwakalebela 40, Thomas Ephraim Mwakagile (45), Anitha Alfred Temba 27 na Isack Mwaifani Bondia.

    Novemba 11 video ilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii, ikionyesha watu kadhaa wakijaribu kumuingiza kwenye gari kwa nguvu mfanyabiashara, Deogratius Tarimo, Mkazi wa Kibaha.

    Tangazo la polisi linakuja siku chache tangu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo kutangazwa kutekwa kabla ya kuachiliwa akiwa na majera katika jiji la Dar es Salaam.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Watu 135 wamefariki katika mkanyagano Guinea kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu

    FDC

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Guinea yanasema yanaamini zaidi ya mashabiki 135 wa kandanda walifariki katika mkanyagano katika uwanja wa mpira siku ya Jumapili, wengi wao wakiwa watoto.

    Idadi hiyo, ambayo haijathibitishwa, ni kubwa kuliko idadi rasmi ya vifo ambayo ni watu 56.

    Makundi hayo yanasema makadirio hayo yanatokana na taarifa kutoka hospitali, makaburi, mashahidi katika uwanja huo, familia za wahanga, misikiti, makanisa na vyombo vya habari vya ndani. Watu wengine 50 bado hawajulikani walipo, ilisema.

    Hata hivyo, serikali ya kijeshi, imeonya dhidi ya kueneza habari "ambazo hazijathibitishwa," ikisema uchunguzi wake unaendelea kuhusu mkasa huo katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo, Nzérékoré.

    Tukio hilo baya lilitokea baada ya uamuzi wa kutatanisha wa mwamuzi wakati wa mechi, ambao ulisababisha vurugu. Polisi walijibu kwa kurusha mabomu ya machozi, wakati watu wakijaribu kukimbia.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kulikuwa na matumizi ya kupindukia ya gesi ya kutoa machozi katika eneo dogo, na kuongeza kuwa magari yaliyokuwa yamewabeba maafisa waliokuwa wakitoka uwanjani pia yaliwagonga raia waliokuwa wakijaribu kutoroka.

    Waziri Mkuu Mamadou Oury Bah Jumanne alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa waathiriwa.

    Guinea ni miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika ambazo kwa sasa zimepigwa marufuku kufanya mechi za kimataifa za soka kwa kutokidhi viwango vya kimataifa.

    Nchi nyingine zilizozuiliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kufanya mechi za kimataifa ni pamoja na Ethiopia, Gambia, Chad na Sierra Leone.

  7. Boti ya Ufilipino yagongwa na Walinzi wa Pwani ya China

    trg

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Ufilipino ilitoa video inayoonyesha boti ya walinzi wa pwani ya China ikiirushia maji boti yake

    Ufilipino inasema walinzi wa Pwani ya China wamerusha maji ya kuwasha na kuigonga boti yake katika Bahari ya China Kusini.

    Tukio hilo lilitokea karibu na eneo linalozozaniwa la Scarborough Shoal na Beijing inasema ilitenda "kulingana na sheria."

    Balozi wa Marekani nchini Ufilipino alilaani China kwa "matumizi yasiyo halali ya mizinga ya maji na kitendo cha hatari.”

    Bahari ya China Kusini ndio kitovu cha mzozo wa kieneo kati ya China, Ufilipino na nchi zingine. Lakini mvutano kati ya Manila na Beijing umeongezeka sana katika mwaka uliopita.

    Siku ya Jumatano, Manila ilitoa video inayoonyesha meli ya walinzi wa pwani ya China ikiirushia maji boti ya idara ya uvuvi ya Ufilipino.

    BBC haijathibitisha picha hizo.

    Walinzi wa pwani ya Ufilipino walisema boti ya walinzi wa pwani ya China "iliigonga pembeni kwa makusudi" boti hiyo na kisha "kuanzisha shambulio la pili la maji ya kuwasha dhidi ya boti hiyo hiyo".

    Walinzi wa pwani wa China walisema katika taarifa yao kwamba boti ya Ufilipino iliikaribia boti yao na hatua zilizochukuliwa ni kwa mujibu wa sheria".

    Hili ni tukio la hivi punde zaidi katika msururu wa matukio hatari katika mwaka jana kati ya pande hizo mbili katika Bahari ya Kusini ya China.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Raila kuchuana na wapinzani wawili kwenye mdahalo wa kuwania uenyekiti wa Kamisheni ya AU

    d

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Raila Odinga ni kiongozi wa upinzani wa muda mrefu nchini Kenya

    Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga atashiriki katika mdahalo wa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika katika Makao Makuu ya AU huko Addis Ababa, Ethiopia Desemba 13, 2024.

    Wakati wa mdahalo huo, Raila atachuana vikali na wagombeaji wengine wawili; Mahmoud Ali Youssouf (Djibouti), Richard Randriamandrato (Madagascar).

    Ni mdahalo utakaofanyika kabla ya uchaguzi wa Februari 2025, ili kumpata mrithi wa mwenyekiti wa sasa wa kamisheni hiyo Moussa Faki Mahama kutoka Chad.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Anayetafutwa na FBI afikishwa mahakamani Uingereza

    fdc

    Chanzo cha picha, Elizabeth Cook / PA

    Maelezo ya picha, San Diego alifikishwa katika Mahakama ya Westminster mjini London

    Mmoja wa watu wanaosakwa sana na Marekani ambaye alikamatwa kaskazini mwa Wales wiki iliyopita amefikishwa mahakamani Uingereza.

    Daniel Andreas San Diego, 46, alizuiliwa huko Maenan, Conwy baada ya operesheni ya polisi wa kukabiliana na ugaidi na Polisi wa Wales Kaskazini.

    Alitafutwa na FBI kwa madai ya kulipua majengo mawili huko San Francisco mwaka 2003.

    Atafikishwa mahakamani tena tarehe 31 Disemba. Kabla ya kukamatwa wiki jana, San Diego, ambaye alizaliwa Berkeley, California, alikuwa mafichoni kwa miaka 21.

    Kulikuwa na zawadi ya dola za Kimarekani 250,000 (£198,000) kwa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwake moja kwa moja.

    Tarehe 28 Agosti 2003, mabomu mawili yalilipuka huko Emeryville. Kisha, tarehe 26 Septemba 2003, bomu moja lililofungwa misumari lililipuka huko Pleasanton.

  10. Mwandishi maarufu wa riwaya wa China afariki kwa kujiua

    df

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Chiung Yao, mwandishi maarufu wa riwaya za mapenzi

    Chiung Yao, mwandishi maarufu wa riwaya za mapenzi kwa lugha ya Kichina, amefariki kwa kujiua.

    Vyombo vya habari vimeripoti, mwili wa bibi huyo mwenye umri wa miaka 86 ulipatikana nyumbani kwake katika Jiji la New Taipei siku ya Jumatano.

    Kulingana na Shirika la Habari la Taiwan, limeripoti kuwa watoa huduma za dharura wanasema alijiua.

    Chiung Yao alianza kuandika akiwa na umri wa miaka 18 na kuchapisha zaidi ya riwaya 60, nyingi kati ya hizo zilibadilishwa kuwa filamu na mfululizo wa vipindi vya TV na kubaki kuwa maarufu kwa miongo kadhaa.

    Mojawapo ya kazi zake maarufu ni tamthilia ya Runinga ya My Fair Princess, ambayo iliigizwa na nyota wenye majina makubwa.

    Alizaliwa Chen Che huko Sichuan, China mwaka 1938. Chiung Yao ni jina lake la uandishi.

    Chapisho lake kwenye akaunti yake ya Facebook siku ya Jumatano linasomeka: "Kwaheri, wapendwa wangu. Najihisi mwenye bahati nimekutana na ninyi katika maisha haya."

    Haijabainika ikiwa ikiwa chapisho hilo lilichapishwa kabla au baada ya mwili wake kupatikana.

  11. Mamake Eminem, Debbie Nelson, afariki akiwa na umri wa miaka 69

    ref

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Debbie Nelson, mama wa mwanamuziki Eminem,

    Debbie Nelson, mama wa mwanamuziki Eminem, ambaye alikuwa na uhusiano wa vuta nikuvute na mwanawe, amefariki akiwa na umri wa miaka 69.

    Mwakilishi wa rapa huyo, Dennis Dennehy, amethibitisha kifo cha mama yake kwenye vyombo vya habari vya Marekani.

    Chanzo cha kifo bado hakijaelezwa lakini Nelson alijulikana kuwa na saratani ya mapafu. Eminem bado hajasema hadharani kuhusu kifo cha mama yake.

    Uhusiano mbaya na mama yake ulifichuka zaidi kwenye mojawapo ya kibao chake maarufu, Cleanin' Out My Closet.

    Katika wimbo huo wa mwaka 2002, Eminem anamshutumu mamake kwa matumizi mabaya ya dawa za kulevya na kumtelekeza.

    Nelson alimshtaki mwanawe kwa kumharibia jina mwaka 1999 kutokana na wimbo wake mwingine, My Name Is, lakini baadaye akasema ni wazo la wakili wake na kesi hiyo ikamalizwa nje ya mahakama.

    Mwaka 2008, Nelson aliandika kitabu cha kumbukumbu kiitwacho My Son Marshall, My Son Eminem, ambapo anasema "alivunjika moyo" juu ya madai ya mtoto wake kuhusu yeye.

    Lakini uhusiano wao ulionekana kuimarika. Katika wimbo wake wa 2013, Headlights, rapa huyo alionyesha kujutia baadhi ya nyimbo zake za awali.

    "Samahani, Mama, kwa Cleanin' Out My Closet," aliimba. "Wakati huo nilikuwa na hasira. Sikukusudia kuipeleka mbali hivyo."

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mshukiwa wa mauaji ya 1977 arudishwa Australia

    dc

    Chanzo cha picha, Victoria Police

    Maelezo ya picha, Polisi wamekuwa wakijaribu kutatua fumbo la mauaji ya Susan Bartlett na Suzanne Armstrong kwa karibu miaka 50

    Mwanaume anayesakwa kwa kesi ya mauaji nchini Australia, inayoitwa mauaji ya Easey Street, amepelekwa Melbourne, Australia akitokea Italy.

    Suzanne Armstrong, 27, na Susan Bartlett, 28, walidungwa kisu hadi kufa katika nyumba yao huko Melbourne mwaka 1977, katika kesi ambayo imekuwa ikisumbua taifa tangu wakati huo.

    Polisi walisema mshukiwa Perry Kouroumblis, mwenye umri wa miaka 65, ndiye aliyekuwa kitovu cha uchunguzi wao katika miaka ya hivi karibuni baada ya mafanikio ya upimaji wa DNA.

    Kouroumblis raia wa Ugiriki na Australia - ambaye hajafunguliwa mashtaka na anasema hana hatia - alizuiliwa nchini Italia mwezi Septemba.

    Iwapo atashtakiwa, anatarajiwa kufikishwa mahakamani baadaye wiki hii, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.

    Kouroumblis alikwenda polisi kwa mara ya kwanza wiki moja baada ya mauaji hayo, wakati akiwa na umri wa miaka 17, na kuwaeleza kuwa amepata kisu kilichokuwa na damu karibu na eneo la tukio katika mtaa wa Easey, Collingwood.

    Miili ya marafiki hao wa shule ya upili iligunduliwa siku tatu baada ya kuonekana wakiwa hai mara ya mwisho. Mtoto wa kiume wa Bi Armstrong mwenye umri wa mwaka mmoja alipatikana katika nyumba hiyo, akiwa hana jeraha kwenye kitanda chake.

    Polisi wanasema, wanawake wote wawili walidungwa kisu zaidi ya mara kumi na Armstrong alishambuliwa kingono.

    Mwaka 2017, Polisi walitoa zawadi ya dola za Kimarekani 647,600) kwa atakayetoa taarifa.

  13. Muuguzi muuaji wa watoto wachanga ahojiwa tena katika uchunguzi mpya

    ed

    Chanzo cha picha, Cheshire Constabulary

    Maelezo ya picha, Lucy Leby anatumikia kifungo cha maisha

    Lucy Letby amehojiwa na polisi gerezani kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu vifo vya watoto katika hospitali mbili, ripoti zinaeleza.

    Wapelelezi walizungumza na muuguzi huyo wa zamani wa watoto wachanga juu ya vifo na kuzimia kwa wagonjwa katika Hospitali ya Chester na Hospitali ya Wanawake ya Liverpool.

    Letby alipatikana na hatia ya mauaji ya watoto saba na jaribio la kuwaua wengine saba katika hospitali ya Chester kati ya 2015 na 2016.

    Inafahamika kuwa hajawahi kuhojiwa juu ya vifo katika hospitali ya Liverpool, ambapo alifanya kazi kwa zamu 30 kati ya 2012 na 2015.

    Letby mwenye umri wa miaka 34, anatumikia kifungo cha maisha kwa mauaji ya watoto saba na kujaribu kuwaua watoto wengine saba kati ya Juni 2015 na Juni 2016.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Diddy ashtakiwa kwa kumning’iniza mwanamke kwenye roshani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Sean "Diddy" Combs ameshtakiwa katika kesi mpya ya kumning’iniza mwanamke kutoka kwenye roshani ya ghorofa ya 17 wakati wa ugomvi.

    Kesi hiyo iliyowasilishwa Los Angeles na mwanamitindo Bryana "Bana" Bongolan inadai kisa hicho kilitokea 2016 akiwa nyumbani kwa aliyekuwa mpenzi wa Combs wakati huo Casandra "Cassie" Ventura.

    Ni kesi ya hivi punde katika zaidi ya nyingine 24 zinazomtuhumu Bw Combs kwa makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, dawa za kulevya, kutishia mashahidi na kusababisha madhara ya kimwili.

    Gwiji huyo wa muziki pia anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na biashara ya ngono.

    Hata hivyo, Combs amekanusha madai yote, ikiwa ni pamoja na ya hivi karibuni.

    Mwakilishi aliiambia BBC Jumanne kwamba "anakanusha vikali madai haya mazito" katika kesi hiyo mpya na "anasalia na imani kwamba yatathibitishwa kuwa hayana msingi".

    Katika kesi hiyo, Bi Bongolan anasema alikuwa kwenye nyumba ya Bi Ventura usiku huo wakati Bw Combs alipoanza kupiga kelele na kugonga mlango wa mbele.

    Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, Bw Combs anadaiwa kumkabili Bi Bongolan, ambaye alikuwa kwenye roshani wakati huo.

    Kesi hiyo inasema alimshika na kumdhalilisha.

    Kisha akamwinua na kuanza kumning'iniza kwenye roshoni ya nyumba hiyo, kesi hiyo inadai.

    Soma zaidi:

  15. Msako unaendelea kumtafuta mwanamke anayeaminika kunaswa kwenye shimo

    .

    Chanzo cha picha, Police handout

    Maafisa huko Pennsylvania wanamtafuta mwanamke ambaye yuko chini ya ardhi anayeaminika kutumbukia kwenye shimo lenye kina cha futi 30 (9m) ambalo huenda lilifunguka wakati akimtafuta paka wake aliyepotea.

    Elizabeth Pollard, 64, aliripotiwa kutoweka na wanafamilia baada ya kwenda kumtafuta paka huyo Jumatatu usiku.

    Maafisa waliofika kwanza kwenye eneo la tukio nusura waanguke kwenye shimo hilo hilo, ambalo wanasema limeunganishwa na mgodi wa makaa ya mawe uliotelekezwa.

    Maikrofoni na kamera zimeshushwa ndani ya shimo, lakini Bibi Pollard bado hajapatikana. Maafisa wanasema kamera zao ziliona kile kilichoonekana kuwa kiatu.

    Gari la Bi Pollard lilipatikana limeegeshwa nyuma ya mkahawa katika mji wa Marguerite, maili 40 (65km) mashariki mwa Pittsburgh, mapema Jumanne asubuhi.

    Mjukuu wake wa kike mwenye umri wa miaka mitano alikuwa ndani ya gari, maafisa walisema, na kuongeza kwamba msichana alikuwa baridi lakini hakuumia.

    Maafisa wa Polisi wa Jimbo la Pennsylvania Stephen Limani aliwaambia waandishi wa habari kwamba shimo hilo lina ukubwa wa kifuniko cha shimo la jiji.

  16. Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol akabiliwa na hoja ya kutokuwa na imani naye

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol anakabiliwa na hoja ya kutokuwa na imani naye baada ya wabunge wa upinzani kuwasilisha hoja ya kumuondoa kutokana na jaribio lake lililoshindikana la kulazimisha sheria ya kijeshi siku ya Jumanne.

    Hoja hiyo bado itahitaji kujadiliwa kabla ya kupiga kura, labda baadaye wiki hii.

    Pindi mswada wa kumuondoa madarakani utakapopendekezwa, takriban theluthi mbili ya Wabunge katika Bunge la Kitaifa lenye wajumbe 300 la Korea Kusini lazima wapige kura ili kupitisha hoja hiyo ya kutokuwa na imani na Yoon - ambayo ina maana ya angalau kura 200.

    Kura lazima ifanyike ndani ya saa 72.

    Hatua inayofuata sasa, ni kwa Spika wa Bunge Woo Won-sik kuitisha kikao ili hoja hiyo ijadiliwe - ambayo inaweza kutokea pengine baada ya siku mbili.

    Soma zaidi:

  17. Wanawake wa Afghanistan 'wapigwa marufuku kufanya kozi za wakunga'

    .

    Chanzo cha picha, HANDOUT

    Wanawake wanaopata mafunzo ya kuwa wakunga na wauguzi nchini Afghanistan wameiambia BBC kuwa waliamriwa wasirudi masomoni asubuhi - na hivyo kutamatisha ndoto yao ya kupata elimu zaidi nchini humo.

    Taasisi tano tofauti kote Afghanistan pia zimeithibitishia BBC kwamba Taliban walikuwa wameziagiza zifunge hadi ilani nyingine itakapotolewa, huku video zinazosambazwa mtandaoni zikionyesha wanafunzi wakilia baada ya kutapa taarifa hiyo.

    BBC bado haijathibitisha agizo hilo rasmi na wizara ya afya ya serikali ya Taliban.

    Hata hivyo, kufungwa kwa taasisi hizo kunaonekana kuambatana na sera pana kuhusu elimu ya wanawake, ambayo imesababisha wasichana vijana wasipate elimu ya sekondari na ya juu tangu Agosti 2021.

    Taliban wameahidi mara kwa mara kwamba wataruhusiwa kurejea shuleni mara tu masuala kadhaa yatakapotatuliwa - ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mtaala ni wa "Kiislam".

    Hili bado halijafanyika.

    Moja ya njia chache ambazo bado ziko wazi kwa wanawake wanaotafuta elimu ilikuwa kupitia vyuo vya elimu ya juu, ambapo wangeweza kujifunza uuguzi au kuwa wakunga.

    Ukunga na uuguzi pia ni mojawapo ya kazi pekee ambazo wanawake wanaweza kufanya chini ya vikwazo vya serikali ya Taliban kwa wanawake – ambayo ni muhimu, kwani madaktari wa kiume hawaruhusiwi kuwatibu wanawake isipokuwa mlezi wa kiume awepo.

    Miezi mitatu tu iliyopita, BBC ilipewa fursa ya kufikia kituo kimoja cha mafunzo ya wakunga kinachoendeshwa na Taliban, ambapo zaidi ya wanawake kumi na wawili katika miaka yao ya 20 walikuwa wakijifunza jinsi ya kusaidia kina mama kujifungua.

    Soma zaidi:

  18. Madaktari nchini Kenya watishia kugoma wakilalamikia hadaa za serikali

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Muungano wa madaktari nchini Kenya umetoa ilani ya mgomo ya siku 21, itakayoanza rasmi tarehe 22 mwezi Desemba, ikiwa serikali haitotekeleza makubaliano ya utendakazi ya 2017.

    Takriban madaktari kutoka hospitali za umma nchini Kenya 4000 walifanya mgomo mnamo mwezi Machi tarehe 14, mapema mwaka huu wakilalamikia serikali kujikokota kuwapatia kazi madaktari matarajali na mazingira mazuri ya kazi na mafunzo ya kitaaluma.

    Mgomo huo ulisitishwa baada ya siku 56 walipoafikiana matakwa yao Mei, 8.

    Hata hivyo, hadi kufikia sasa serikali haijatekeleza maafikiano waliofikia ya kurejea kazini kama walivyoahidiwa.

    Madaktari wamatajali ambao huhitajika kuhudumu kwa mwaka mmoja kabla ya kupata leseni, wamelalamikia dhiki wakiwa kazini na kufanyakazi kwa saa nyingi bila kutolipwa mishahara yao.

    Soma zaidi:

  19. Trump atishia Hamas akiwaonya kuwa 'watalipia vikali' juu ya mateka

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais mteule wa Marekani Donald Trump ametoa onyo kwa Hamas, akitishia kuwa "watalipia vikali " ikiwa mateka waliozuiliwa huko Gaza hawatakuwa wameachiliwa kufikia wakati atakaporejea Ikulu mnamo tarehe 20 Januari, 2025.

    Makumi ya watu waliochukuliwa wakati wa shambulio la Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 bado hawajulikani waliko.

    Siku ya Jumatatu, jeshi la Israel lilisema mwanajeshi wa Israel na Marekani ambaye inaaminika kuwa mateka aliuawa Oktoba mwaka jana.

    Jumatatu wiki hii, jeshi la Israel lilitangaza kuwa mwanajeshi wa Israel mwenye asili ya Marekani ambaye anadaiwa kuwa mateka anayejulikana kama Omer Neutra aliuawa mwezi Oktoba.

    Bila ya kutamka jina Hamas, Trump aliandika ujumbe mtandaoni siku hiyo nikinukuu: "Wale waliohusika wataadhibiwa vikali kuliko mtu yeyote aliyewahi kuadhibiwa katika historia ya Marekani".

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimshukuru Trump kwa "msimamo wake mkali".

    Hata hivyo Trump amekuwa akizungumza kwa mapana juu ya kumaliza mizozo katika nchi za kigeni, na kupunguza ushiriki wa Marekani katika masuala kama hayo.

    Alijiweka kama mfuasi mkubwa wa Israeli wakati wa kampeni zake huko Gaza, lakini amemtaka mshirika huyo wa Marekani kusitisha operesheni yake ya kijeshi.

    Israel ilianzisha kampeni ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika eneo la kusini mwa Israel mwaka 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

    Zaidi ya watu 44,000 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayosimamiwa na Hamas. Makumi ya maelfu ya wengine wamejeruhiwa na sehemu kubwa ya eneo la Palestina limeharibiwa.

    Soma zaidi:

  20. Rais wa Korea Kusini aondoa sheria ya kijeshi baada ya wabunge kupiga kura kuizuia

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol ametangaza Jumatano asubuhi kwamba ameondoa sheria ya kijeshi nchini Korea Kusini, saa chache baada ya kuitangaza.

    Hatua hiyo inawadia baada ya wabunge 190 waliokuwepo Bungeni mjini Seoul kwa kauli moja kuzuia hatua hiyo.

    Rais wa Korea Kusini alisema: "Baada ya Bunge la Kitaifa kutaka kuondoa sheria za kijeshi, wanajeshi wa sheria za kijeshi wameondolewa.

    "Nitakubali ombi la Bunge la Kitaifa na kuondoa sheria ya kijeshi kupitia mkutano wa baraza la mawaziri."

    Wakati huo huo, chama kikuu cha upinzani nchini Korea Kusini kimemtaka rais wa taifa hilo, Yoon Suk Yeol kujiuzulu ama apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye kutokana na hatua yake ya kutangaza sheria ya kijeshi katika taifa linaloamini demokrasia.

    Mmoja wa wanachama waandamizi wa chama cha upinzani cha Democratic Party amesema ilibainika tangu awali kwamba Yoon hawezi kuendesha nchi hiyo kwa njia za kawaida.

    Katika hotuba yake Jumanne usiku, alielezea majaribio ya upinzani wa kisiasa kuhujumu serikali yake kabla ya kusema kwamba ametangaza sheria ya kijeshi "kukandamiza vikosi vinavyopinga serikali ambavyo vimekuwa vikisababisha uharibifu".

    Baadhi ya watu waliozungumzia kutangazwa kwa sheria hiyo walielezea namna walivyochanganyikiwa na tangazo hilo.

    Soma zaidi: