Je, nchi hii itafuata nyayo za Tanzania kumpata Rais wake wa kwanza mwanamke?

Netumbo Nandi-Ndaitwah amekuwa mwanachama sugu wa chama tawala tangu awe na umri wa miaka 14

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Netumbo Nandi-Ndaitwah amekuwa mwanachama sugu wa chama tawala tangu awe na umri wa miaka 14
    • Author, Frauke Jensen
    • Nafasi, BBC News, Windhoek
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Iwapo siasa za Nambia zinazoendelea kuchacha na matumaini ya chama tawala yatazaa matunda, taifa hilo litachagua rais wa kike wa kwanza wiki hii.

Hata hivyo, hisia za kutokuwa na imani na harakati za ukombozi kusini mwa Afrika, pamoja na hisia za kupinga watawala zilizozidi katika sehemu nyingi za dunia, huenda zikaleta tishio kwa mafanikio haya ya kihistoria.

Naibu wa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 72, ndiye mgombea wa chama cha Swapo, ambacho kimeiongoza Namibia tangu uhuru kutoka Afrika Kusini ya ubaguzi wa rangi mwaka 1990.

Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ndiye rais pekee mwanamke barani Afrika kwa sasa, hivyo kama Nandi-Ndaitwah atashinda, atajiunga na kikosi cha kipekee.

Chama chake, ambacho kimekuwa na nguvu kubwa kwa miongo mitatu, kiliona upungufu mkubwa wa msaada katika uchaguzi mkuu uliopita.

Sasa kinakwenda kwenye uchaguzi wa Jumatano huku kukiwa na kiwango cha ukosefu wa ajira cha asilimia 19 – kama kilivyokuwa miaka 30 iliyopita - changamoto za kifedha serikalini, maswali kuhusu rushwa na viwango vikubwa vya ukosefu wa usawa.

Anayemtia tumbo joto Nandi-Ndaitwah ni mpinzani wake mkuu kati ya wagombea 14 wengine – Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for Change (IPC).

Pia anakutana na tamaduni za kisiasa za kiasili na zinazotawaliwa na taasubi za kiume nchini humo.

Hata hivyo, yeye ni kiongozi anayeaminika katika nchi hii yenye idadi ndogo ya watu na amani, akiwa amehudumu katika nyadhifa za juu serikalini kwa robo ya karne.

“Daima nimekuwa nikiamini katika kazi ya pamoja, na hiyo ndiyo iliyoniwezesha kufikia nilikofikia,” amesema.

Akitambulika kwa mtindo wake wa uongozi wa vitendo, makamu wa rais pia ni mtiifu sana kwa chama, ambacho alijiunga nacho akiwa mtoto wa kike.

Alikuwa na umri wa miaka 14 alipokuwa sehemu ya harakati za kupinga utawala kutoka Afrika Kusini, ambayo ilikuwa imetawala nchi hiyo – iliyojulikana wakati huo kama South West Africa – tangu kumalizika kwa Vita vikuu vya Kwanza vya Dunia na baadaye kuanzisha mfumo wa siasa za ubaguzi wa rangi.

Panduleni Itula alifanya kazi kama daktari wa meno Uingereza kabla ya kurejea Namibia 2013

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Panduleni Itula alifanya kazi kama daktari wa meno Uingereza kabla ya kurejea Namibia 2013
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alitambuliwa kwa ukakamavu wake na talanta ya shirika kama kiongozi wa Ligi ya Vijana ya Swapo, ambayo ikawa hatua ya maendeleo yake ya kisiasa, ambayo imejumuisha majukumu ya mawaziri katika mambo ya nje, utalii, ustawi wa watoto na habari.

Amepata maarifa na uzoefu mwingi ambao utamweka katika nafasi nzuri ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa Namibia.

"Anaonekana kuwa mwenye busara na mkarimu, hata kwa jinsi anavyojaribu kusema kila kitu kwa njia ambayo hata kama mimi nitaelewa," Laimi, mpiga kura anayetarajiwa, aliiambia BBC katika mji mkuu, Windhoek.

"Itula ni kama kipande kipya cha vito na miwani yake, suti yake nadhifu na kutembea kwake kwa ujasiri, lakini labda anakupofusha kwa kung'aa kwake," rafiki yake Maria alisema.

Wapiga kura hawa wawili ni vijana ambao hawajaweza kupata kazi.

Daktari wa meno aliyeidhinishwa, Itula, mwenye umri wa miaka 67, alikuwa mfuasi mkereketwa wa Swapo lakini alitimuliwa kutoka kwa chama mnamo 2020 baada ya kuwania kama mgombeaji huru dhidi ya Rais Hage Geingob katika kura ya maoni ya 2019.

Pia alikuwa kiongozi wa vijana na alikaa gerezani kwa muda kabla ya kwenda uhamishoni nchini Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 1980. Alirejea Namibia mwaka 2013.

Miaka sita baadaye, alikuja kwa kishindo katika safu ya mbele ya siasa za Namibia, akimpinga Geingob katika uchaguzi wa rais baada ya kusema mchakato wa Swapo wa kuchagua mgombea wake ulikuwa na dosari.

Kuingilia kati kwa Itula katika uchaguzi huo kulipelekea Swapo kupata mgao wake wa chini zaidi kuwahi kutokea - 56% - katika uchaguzi wa rais na pia kupoteza thuluthi mbili ya wingi wake bungeni.

Kama mtu ambaye alikuwa na maisha ya taaluma kando na siasa,anavutia asilimia 50% ya wapiga kura milioni 1.5 walio chini ya umri wa miaka 35,wengi wao wakitaka mabadiliko ya kiuchumi,ajira au mifumo ya kuboresha kipato chao.

Mtindo wake wa kijasiri na ukakamavu, kukataa matamshi ya kisiasa ya Nandi-Ndaitwah, umemfanya apate kuungwa mkono na wafanyabiashara na wasomi wanaoongezeka mijini.

Lakini wakati Itula anajulikana kama mcheshi na mfasaha, makamu wa rais anachagua maneno yake kwa busara, na kuzungumza kwa utaratibu na pia kwa ustaarabu.

Wapiga kura wako kwa njia panda wachague chama kilichozoeleka au chama ambacho kimeundwa hivi majuzi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wapiga kura wako kwa njia panda wachague chama kilichozoeleka au chama ambacho kimeundwa hivi majuzi

Nandi-Ndaitwah anatafuta maelewano na kazi ya pamoja, akisisitiza ushirikiano wa kijamii, na kutiririka hadi mashinani.

Na akiwa mwanamke wa kwanza mwenye nafasi ya kuwa rais wa nchi, anabeba matumaini ya baadhi ya wanawake wanaotaka mabadiliko kutoka kwa jamii ya mfumo dume.

Hata hivyo, Nandi-Ndaitwah anawakilisha chama cha zamani "kilichojaribiwa na kuaminiwa" ya mapambano ya ukombozi ya Namibia, wakati Itula anawakilisha uwezekano wa "wimbi la mabadiliko" katika mazingira ya kisiasa yanayohitaji kurekebishwa.

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Henning Melber, ushindani wa karibu kati ya wagombea hawa wawili wakuu unaweza kumaanisha kuwa uchaguzi wa rais utaingia katika awamu ya pili ya uchaguzi ambayo haijawahi kutokea, ambayo inahitajika ikiwa hakuna mgombea atakayepata zaidi ya nusu ya idadi ya kura zilizopigwa.

Katika nchi jirani ya Afrika Kusini, chama cha African National Congress, kilichokuwa madarakani tangu 1994, kililazimishwa kuingia katika muungano kufuatia uchaguzi mkuu wa mwezi Mei. Nikiwa Botswana - mashariki mwa Botswana - Chama cha Demokrasia cha Botswana, kilichotawala kwa takriban miongo sita, kilipata kushindwa kwa kufedhehesha mwishoni mwa mwezi uliopita.

Swapo inataka kuepuka hatima sawia ,Melber asema.

Mshindi Jumatano atakuwa mgombea ambaye anaweza kuaminiwa zaidi katika masuala kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana, rushwa, huduma za afya, elimu na uboreshaji wa miundombinu, huku pia akiwa na uwezo wa kuimarisha uchumi.

Hili likihitajika kuafikia maendeleo hayo bila kushurutika kuuza maliasili za nchi kwa wawekezaji wa kigeni - kama vile gesi ya pwani pamoja na lithiamu na metali nyingine muhimu.

Chama cha IPC cha Itula hakikuwa sehemu ya uchaguzi wa 2019, lakini kimefanya vyema katika chaguzi za mitaa tangu wakati huo na ina mwonekano wa mbadala wa kisiasa unaoaminika. Imepata sifa kwa jinsi ilivyoendesha baadhi ya serikali za mitaa.

Sifa kubwa ya Nandi-Ndaitwah inaweza kuwa kwamba yeye, kama mwanadiplomasia wa Namibia Tuliameni Kalomoh alivyowahi kusema, anaonekana kama mtu mwenye maadili na mtunza mali za umma".

Soma zaidi mada inayofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla