Mpango wa amani wa Lebanon uko mashakani baada ya Israel na Hezbollah kushambuliana

Watu kumi wameuawa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatatu usiku, wizara ya afya imesema, baada ya Israel kufanya mashambulio

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa matangazo yetu, tukutane kesho panapo uhai.

  2. Habari za hivi punde, Rais wa Korea Kusini atangaza hali ya hatari huku jeshi likisimamisha shughuli za bunge

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol, ametangaza hali ya hatari muda mfupi uliopita, katika hotuba ya usiku wa manane.

    Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuilinda nchi kutokana na vikundi vya kikomunisti vya Korea Kaskazini na kuwaondoa watu wanaoipinga serikali. “Uamuzi huo umefanywa ili kuviondoa vikundi vinavyoiunga mkono Korea Kaskazini na kuilinda katiba.”

    Ripoti kutoka vyombo vya habari vya Korea Kusini, vinasema jeshi la nchi hiyo limetangaza kusimamisha shughuli zote za bunge. Shirika la Habari la Yonhap linasema wajumbe wa Bunge la Kitaifa wamepigwa marufuku kuingia kwenye jengo hilo.

    Kanda za video zimeanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaonyesha uwepo wa maafisa wengi wa usalama nje ya bunge. Shirika la Habari la Yonhap linaripoti kwamba kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Party cha Korea Kusini, Lee Jae-myung, amesema kutangazwa hali ya hatari ni kinyume cha katiba.

    Yonhap pia limeripoti kwamba Han Dong-hoon, mkuu wa chama tawala cha People Power Party - ambacho Rais Yoon Suk Yeol ni mwanachama - pia ameapa kulizuia tamko hilo, akielezea ni "makosa."

    Yoon amekuwa rais aliyekosa nguvu tangu uchaguzi mkuu wa hivi karibuni baada ya upinzani kushinda kwa kishindo na hakuwa na uwezo wa kupitisha sheria alizotaka.

    Yoon pia amekumbwa na kashfa kadhaa, moja ikimuhusu mkewe, ambaye anatuhumiwa kwa ufisadi. Upinzani umekuwa ukijaribu kuanzisha uchunguzi maalum dhidi yake. Wiki hii, upinzani ulizuia bajeti ambayo serikali na chama tawala ilipendekeza.

    Pia upinzani, unapanga kuwashtaki wajumbe wa baraza la mawaziri, hasa mkuu wa wakala wakaguzi wa serikali, kwa kushindwa kumchunguza mke wa rais.

  3. Mkahawa unaounga mkono Palestina wazindua kinywaji cha Gaza-Cola

    p

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Gaza-Cola zenye bendera ya Palestina

    Osama Ghasho amezindua kinywaji cha Gaza-Cola katika kitongoji cha Holborn, London tangu Novemba 2023. Anasema kuna sababu kadhaa za kufanya hivyo, lakini sababu kuu ni kususia makampuni yanayosaidia kuimarisha jeshi la Israel.

    Watu wanaoiunga mkono Palestina na wakosoaji wa Israel wamekuwa wakijaribu kukisusia kinywaji cha Coca-Cola kwa miezi kadhaa. Kiwanda cha "Tabor," ambacho ni kampuni tanzu ya Coca-Cola, hukuza zabibu zake katika ardhi inayokaliwa ya Ukingo wa Magharibi na sehemu ya Syria ya Miinuko ya Golani.

    Pia, kampuni hii inazalisha vinywaji laini katika makazi ya Wayahudi ya Atrot kaskazini mwa Jerusalem. Tovuti ya GazaCola inasema faida yote kutokana na mauzo ya kinywaji hiki itatumika kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

    Kuendelea mashambulizi ya Israel huko Gaza na maandamano ya mara kwa mara dhidi ya Israel katika miji mbalimbali ya Ulaya, imeifanya kampeni ya kususia bidhaa na huduma zinazohusishwa na Israel pia kupanuka.

  4. Mamia ya nyumba zashikiliwa Nigeria katika kesi kubwa ya ufisadi

    d

    Chanzo cha picha, EFCC

    Maelezo ya picha, Tume ya kupambana na ufisadi inasema nyumba hizo zilijengwa kwa mapato ya ufisadi

    Tume ya kupambana na ufisadi nchini Nigeria inashikilia idadi kubwa ya nyumba kuwahi kutokea, zinazodaiwa kununuliwa kwa mapato ya ufisadi.

    Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC), ilitangaza inazishikilia zaidi ya nyumba 750 katika mji mkuu, Abuja.

    EFCC iliyoanzishwa mwaka 2003 ili kupambana na rushwa, haijafichua ni nani hasa miliki wa ardhi na nyumba hizo za kifahari, lakini taarifa yake inasema ni za afisa wa zamani wa ngazi za juu serikalini.

    Nyumba hizo zilizoko nje kidogo ya Abuja, ziko kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 150,000, na mtaalamu wa mali aliyeko Abuja anakadiria zinaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya dola.

    Ufisadi ni moja wapo ya tatizo kubwa nchini Nigeria licha ya uwepo wa sera za serikali zinazoahidi kukomesha tatizo hilo.

    Nchi hiyo ni mojawapo ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi barani Afrika, lakini wakazi wake wachache tu kati ya wakazi milioni 225 ndio wamefaidika na utajiri huo.

    Kwa sasa kuna kesi kadhaa za ufisadi mahakamani zinazohusisha maafisa wa serikali wa zamani na ya sasa.

    Mei mwaka huu, aliyekuwa waziri wa usafiri wa anga, Hadi Sirika, alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa, pamoja na bintiye na mkwe wake.

    Sirika alikuwa mmoja wa mawaziri wenye nguvu katika serikali ya Rais wa zamani Muhammadu Buhari. EFCC inamshutumu kwa kutumia cheo chake kuinufaisha makampuni ya bintiye na mkwe wake.

    Watatu hao wamekana mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana.

  5. Mpango wa amani wa Lebanon uko mashakani baada ya Israel na Hezbollah kushambuliana

    erfd

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mashambulio mabaya ya anga ya Israel na shambulio la Hezbollah yameibua hofu kwamba huenda usitishaji mapigano nchini Lebanon ukasambaratika.

    Watu kumi wameuawa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatatu usiku, wizara ya afya imesema, baada ya Israel kufanya mashambulio makubwa zaidi ya anga tangu pande zote mbili zilikubali wiki iliyopita kumaliza mzozo wa miezi 13.

    Jeshi la Israel lilisema liliwashambulia wapiganaji wa Hezbollah, maeneo ya kurushia makombora na miundombinu na kuitaka serikali ya Lebanon kuzuia kile ilichokiita "shughuli za uhasama" za kundi hilo.

    Hezbollah imerusha makombora mawili kwenye kambi ya jeshi la Israel katika eneo la mpakani linalozozaniwa, ikisema ni onyo juu ya kile ilichokiona kama "ukiukaji wa mara kwa mara" wa mapatano kwa upande wa Israel. Hakuna majeruhi walioripotiwa.

    Marekani, ambayo pamoja na Ufaransa ilipitisha makubaliano hayo na inafuatili, inasema "kwa kiasi kikubwa" usitishaji mapigano ulikuwa ukiendelea licha ya ghasia.

    Mzozo huo ulianza tarehe 8 Oktoba 2023, pale Hezbollah iliporusha makombora kaskazini mwa Israel kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza siku moja baada ya shambulio baya la mshirika wake Hamas katika eneo la kusini mwa Israel.

    Israel ilianzisha mashambulizi makali ya anga na uvamizi wa ardhini dhidi ya kundi hilo. Mamlaka za Lebanon zinasema zaidi ya watu 3,960 waliuawa, wengi wao wakiwa raia.

    Mamlaka ya Israel inasema zaidi ya wanajeshi 80 wa Israel na raia 47 waliuawa.

  6. Idadi ya waliofariki katika maporomoko ya udongo Uganda yafikia 28

    fdc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Watu wamekusanyika katika eneo la maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyozika nyumba nyingi katika vijiji kadhaa wilayani Bulambuli, Uganda Novemba 29, 2024.

    Miili ya wavulana wawili wenye umri wa miaka mitatu ni miongoni mwa iliyotolewa kwenye tope mashariki mwa Uganda, na kufanya idadi ya waliokufa kuongezeka hadi 28 kutokana na maporomoko ya ardhi wiki iliyopita, polisi wamesema.

    Maporomoko hayo yalivikumba vijiji kadhaa huku makumi ya watu bado hawajulikani walipo.

    Zaidi ya watu 100 wanahofiwa kupotea, kwenye miteremko ya Mlima Elgon, kwenye mpaka na Kenya, yapata kilomita 300 (maili 190) mashariki mwa mji mkuu, Kampala.

    Tangu Oktoba, mvua kubwa isiyo ya kawaida imesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya Uganda, huku Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda likilaumu mabadiliko ya tabia nchi.

    Eneo lililo karibu na eneo la mkasa wa wiki jana limekumbwa na maporomoko ya udongo yaliyosababisha vifo vya watu wengi mwaka 2010, takribani watu 80 walikufa.

    Juhudi za hapo awali za serikali za kuwashawishi wakaazi wa maeneo yanayokumbwa na majanga hayo kuhamia maeneo salama zimepata mafanikio madogo kwani wengi wao ni maskini na hawana uwezo wa kufanya hivyo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Aliyemgonga bibi harusi na kumuua akiwa amelewa akiri makosa

    c

    Chanzo cha picha, Annette Hutchinson/GoFundMe

    Maelezo ya picha, Samantha Miller alifariki, na mumewe mpya Aric Hutchinson alijeruhiwa, saa chache baada ya kufunga ndoa mwaka jana.

    Mwanamke mmoja nchini Marekani amekiri mashtaka ya kuendesha gari akiwa amelewa katika tukio ambalo alimuua bibi harusi aliyekuwa akisafiria kwenye kigari cha gofu usiku wa harusi yake.

    Jamie Lee Komoroski amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kutokana na ajali iliyotokea South Carolina mwaka jana na kumuua Samantha Miller akiwa bado amevalia vazi lake la harusi.

    Mume wa marehemu, Aric Hutchinson, alikuwa miongoni mwa watu wengine watatu waliojeruhiwa, pamoja na wanafamilia wake wawili ambao pia walikuwa kwenye gari hiyo.

    Ajali hiyo ilitokea katika jiji la Folly Beach mwezi Aprili 2023, wakati wana ndoa hao wapya walipokuwa wakirudishwa kwenye makao yao saa chache baada ya sherehe yao.

    Komoroski alishtakiwa na waendesha mashtaka kwa kunywa pombe kwenye baa kadhaa na kisha kuendesha gari kwa mwendo wa kasi ya kilomita 104 kwa saa katika eneo la chini ya spidi 25. Gari lake liliigonga gari ya gofu iliyokuwa imewabeba wanandoa hao.

    Uchunguzi wa damu ulionyesha alikunywa mara tatu juu ya juu ya kiwango kinachoruhusiwa, kulingana na ripoti iliyotolewa na maafisa wa serikali baada ya ajali hiyo. Hapo awali alikataa kuwapa maafisa sampuli za pumzi zake, ripoti ya polisi ilisema.

    Katika Mahakama ya Kaunti ya Charleston siku ya Jumatatu, Komoroski alikubali makosa ikiwa ni pamoja na kusababisha kifo.

  8. Ukraine yasisitiza kujiunga na NATO

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bendera za Ukraine na NATO zilionekana wakati wa mkutano wa London, Uingereza, Julai 10, 2024.

    Katika mkesha wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO huko Belgium, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine Andriy Sybiha, amesema dhamana pekee ya usalama wa nchi hiyo ni kuwa uanachama kamili wa NATO.

    "Hatutakubali njia zozote mbadala, zaidi ya Ukraine kuwa mwanachama kamili katika NATO," alisema Sybiha.

    "Ninawaomba muidhinishe uamuzi wa kuialika Ukraine kujiunga na Muungano kama mojawapo ya matokeo ya Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NATO wa Desemba 3-4."

    Kwa upande wake msemaji wa NATO, Farah Dakhlallah, ameiambia BBC kuwa Mawaziri wa mambo ya nje watabadilishana mawazo kuhusu hali ya Ukraine na kuthibitisha uungaji mkono wetu usioyumbayumba kwa Ukraine

    Muungano huo unatarajiwa kuwa katika mkutano wa Desemba 3-4, wa kwanza chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu mpya, Mark Rutte.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Malipo ya dola bilioni 56 kwa Elon Musk yakataliwa tena mahakamani

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Elon Musk

    Jaji katika mahakama moja nchini Marekani, aliamua siku ya Jumatatu kwamba mtendaji mkuu wa kampuni ya magari ya umeme Tesla, Elon Musk hana haki ya kupokea fidia ya dola za kimarekani bilioni 56, licha ya wanahisa wa kampuni hiyo kupiga kura ya kukubali malipo hayo yafanyike miezi sita iliyopita.

    Uamuzi wa jaji Kathaleen McCormick katika jimbo la Delaware, unafuatia uamuzi wake wa Januari 2024 ambapo aliita fidia hiyo kuwa ni malipo makubwa kupita kiasi.

    Uamuzi huo ulileta sintofahamu juu ya mustakabali wa Musk kama mtengenezaji wa magari. Bodi ya Tesla ilisema mpango huo wa malipo ulikuwa muhimu ili kumfanya Musk ajihusishe na kampuni hiyo, hoja ambayo bilionea huyo, ambaye tayari ni mtu tajiri zaidi duniani, aliiunga mkono.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Bingwa wa dunia Dubois kuzichapa na Parker nchini Saudi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Muingereza Daniel Dubois atatetea taji lake la uzito wa juu duniani dhidi ya bingwa wa zamani Joseph Parker nchini Saudi Arabia mnamo tarehe 22 Februari.

    Dubois, 27, alitetea mkanda wake wa kwanza wa IBF kwa kuzichapa na Anthony Joshua mnamo mwezi Septemba.

    Parker wa New Zealand, 32, alishikilia taji la WBO kati ya 2016 na 2018 kabla ya kupoteza kwa Joshua.

    Pia huko mjini Riyadh, Artur Beterbiev atatetea taji lake la uzito wa light-heavy katika pambano la marudiano na Mrusi mwenzake Dmitry Bivol.

    Mchezaji wa London ambaye hajashindwa Hamzah Sheeraz atatetea taji lake la kwanza la dunia dhidi ya bingwa wa uzito wa kati wa WBC Carlos Adames, huku Waingereza wa uzani wa light-heavy, Joshua Buatsi na Callum Smith wakizichapa ulingoni kuwania taji la muda la WBO la Buatsi.

    Shakur Stevenson atatetea mkanda wake wa WBC uzani mwepesi dhidi ya Floyd Schofield huku Zhilei Zhang akipambana na Agit Kabayel kuwania taji la muda la WBC uzani wa juu.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Namibia kupata rais wa kwanza Mwanamke

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Namibia inajiandaa kupata rais wake wa kwanza mwanamke huku thuluthi mbili ya kura za uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita zikihesabiwa mapema hii leo na kumuweka mgombea wa chama tawala cha SWAPO kifua mbele katika uchaguzi ambao upinzani mkuu tayari umeupinga wakidai umekumbwa na udanganyifu.

    Makamu wa rais Netumbo Nandi-Ndaitwah kutoka chama tawala ambacho kimeiongoza taifa hilo tangu ipate uhuru miaka 34 iliyopita, alikuwa amepata zaidi ya asilimia 54 ya kura, kulingana na hesabu ya tume ya uchaguzi ni karibu asilimia 66 ya kura zilizopigwa.

    Kiongozi wa upinzani Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for change (IPC), ameachwa mbali na asilimia 28 ya kura.

    Itula, mwenye umri wa miaka 67, amesema kulikuwa na “mapungufu mengi” na kwamba haijalishi matokeo yatakuwaje, “IPC haitakubali matokeo ya uchaguzi huu.”

    Alisema, “Sheria ya utawala imeshindwa kabisa na hatuwezi kuita uchaguzi huu kuwa huru, haki, na wa halali kwa vyovyote vile.”

    Uchaguzi wa tarehe 27 Novemba ulilazimika kuahirishwa mara mbili kutokana na matatizo ya kiufundi na ya usafiri, ikiwa ni pamoja na upungufu wa karatasi za kupigia kura, hali iliyosababisha foleni ndefu ambapo baadhi ya wapiga kura walilazimika kukata tamaa baada ya kusubiri kwa saa 12.

    Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 72, anaweza kulazimika kwenda kwenye duru ya pili ya uchaguzi ikiwa hatapata zaidi ya asilimia 50 ya kura wakati matokeo yote yatakapotangazwa.

    Ikiwa atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hii yenye watu takribani milioni tatu, inayojulikana kwa ukame na mazingira ya hali ya hewa ya jangwa.

    Matokeo yaliyotangazwa mapema Jumanne yalikuwa ya majimbo 79 kati ya 121, ikiwa ni pamoja na karibu majimbo yote ya mji mkuu Windhoek. Kwa jumla, wapiga kura milioni 1.5 walisajiliwa, asilimia 73 walipiga kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.

    Netumbo Nandi-Ndaitwah akitangazwa mshindi rasmi wa urais atakuwa rais wa tatu mwanamke barani Afrika.

  12. Guinea yaanza siku tatu za maombolezo ya kitaifa

    Maelezo ya video, Mashabiki wakipanda juu ya kuta kwa hofu baada ya mechi ya soka

    Raia wa Guinea leo wataanza kuadhimisha siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kufuatia vifo vya takriban watu 56 katika mkanyagano uliotokea uwanjani kwenye mji wa N'Zerekore Kusini-mashariki.

    Waziri Mkuu Amadou Oury Bah ambaye alitembelea eneo la tukio Jumatatu jioni, alisema bendera za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kuashiria kipindi cha maombolezo rasmi.

    Mvutano ulizuka wakati wa mechi ya kandanda Jumapili, kufuatia uamuzi wa kutatanisha wa mwamuzi.

    Walioshuhudia walisema mashabiki walio na ghadhabu walirusha mawe, na kusababisha hofu na msongamano na mkanyagano katika uwanja huo.

    Mashindano ya kandanda yaliandaliwa kwa heshima ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Mamady Doumbouya, lakini upinzani ulikashifu serikali ya kijeshi kwa kutumia michezo kisiasa.

    Walidai kuwa mashindano hayo yalikuwa ni mbinu ya kupendelea uwezekano wa Jenerali Doumbouya kugombea wakati wa uchaguzi ambao haujatangazwa.

    Katika taarifa yake Rais alitangaza kuwa uchunguzi utaanzishwa ili kubaini chanzo cha mkasa huo huku akiwataka wananchi kuwa watulivu.

    Soma zaidi:

    .

    Chanzo cha picha, Nimba Sports Zaly/AP

  13. Gari jipya la Jaguar linalotumia umeme lazua gumzo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kampuni ya kutengeneza magari ya kifahari ya Jaguar imezindua gari lake jipya la umeme, chini ya wiki mbili baada ya kutolewa kwa video ya kuwatia hamu iliyozua mjada mkali mtandaoni.

    Kuzinduliwa kwa gari aina ya Type 00 kulizua hisia tofauti kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku wengine wakishangilia muundo wake na wengine wakikejeli uzinduzi huo.

    Mwezi uliopita, wakosoaji wengi walisema kuwa video ya matangazo ya modeli hiyo mpya haifanani na gari halisi - lakini kampuni hiyo pia ilisifiwa na wengine kwa ujasiri wake.

    Wakati wa hafla ya uzinduzi huko Miami, Mkurugenzi Mtendaji wa Ubunifu wa Jaguar, Gerry McGovern, alisema anafurahi kuona mwelekeo mpya wa kampuni unavyoibua hisia mseto.

    Aliandika kwa mtandao wa kijamii, “Jaguar haitaki kupendwa na kila mtu,” alisema.

    Hata hivyo, mchambuzi Karl Brauer, alikuwa na mashaka kuhusu utambulisho mpya wa kampuni akihoji ikiwa kweli itafanikiwa.

    “Kampuni ya Jaguar inaonekana “kuachana na malengo ya zamani kwa matumaini ya kupata mafanikio siku za usoni," aliambia BBC.

    "Sidhani kama hatua hii waliochukua itafanikiwa".

    Soma zaidi:

  14. Rais wa Marekani Joe Biden kukutana na mwenzake wa Angola

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Joe Biden anatazamiwa kukutana na rais wa Angola, Joao Lourenco, leo Jumanne ikiwa ni ziara yake ya kwanza na ya pekee barani Afrika kama rais wa Marekani.

    Anatarajiwa kuzungumzia mkopo wa Marekani kwa mradi wa reli mpya ya kilomita elfu moja na mia tatu.

    Mradi huo unaonekana kama jaribio la kushindana na China ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kanda hiyo - hasa katika sekta ya madini.

    Beijing ilitia saini makubaliano na Tanzania na Zambia mwezi Septemba kwenye mradi wa reli kuelekea pwani ya mashariki ya Afrika.

    Hii ni ziara ya kwanza kabisa nchini Angola kufanywa na rais wa Marekani. Wakati wa vita baridi, ilikuwa mshirika wa Urusi na Cuba.

    Hata hivyo, kwa sasa Angola ina washirika mbalimbali ikiwa ni pamoja na wapinzani kama Marekani na China.

    Makampuni ya mafuta ya Marekani yamekuwa Angola kwa miaka mingi lakini sasa Joe Biden anawekeza katika reli kusaidia kuuza nje madini yanayohitajika ikiwa ni mabaadiliko kutoka kwa fueli ya visukuku.

    Jambo ambalo bado halijajulikana ni iwapo Donald Trump ataupa kipaumbele mradi huo huo au atajiondoa huku China ikiongeza ushawishi wake katika eneo hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Ikulu ya Marekani yatetea msamaha wa Biden kwa mwanawe

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Ikulu ya White House imetetea msamaha wa Rais Joe Biden kwa mtoto wake, Hunter, baada ya kusisitiza mara kwa mara kwamba hana mpango wa kutoa huruma kama hiyo.

    Waziri wa habari Karine Jean-Pierre alisema Biden amemsamehe mtoto wake wa kiume, ambaye alikuwa akikabiliwa na hukumu baadaye mwezi huu katika kesi mbili, ili kumkinga dhidi ya mateso yanayoweza kutokea kutoka kwa maadui wa kisiasa wa rais anayeondoka.

    Msamaha huo wa wigo mpana unahusu uhalifu wowote ambao Hunter mwenye umri wa miaka 54 anaweza kuwa alifanya katika kipindi cha muongo mmoja.

    Warepublican wameshutumu hatua hiyo, huku rais mteule Donald Trump akiutaja kuwa "unyanyasaji na upotovu wa haki".

    Rais wa chama cha Democratic alitoa msamaha huo Jumapili jioni kabla ya kuanza safari rasmi kuelekea barani Afrika.

    Bi Jean-Pierre alizungumza na waandishi wa habari: "Anaamini katika mfumo wa haki, lakini pia anaamini kwamba siasa mbaya ziliathiri mchakato huo na kusababisha kukosekana kwa haki."

    Soma zaidi:

  16. Tajiri wa Vietnam apoteza rufaa dhidi ya hukumu ya kifo kwa ulaghai mkubwa zaidi wa benki duniani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tajiri wa Vietnam Truong My Lan amepoteza rufaa yake dhidi ya hukumu ya kifo aliyopewa kwa kupanga ulaghai mkubwa zaidi wa benki duniani.

    Tajiri huyo mwenye umri wa miaka 68 sasa yuko kwenye harakati za kuokoa maisha yake kwa sababu sheria nchini Vietnam inasema kwamba ikiwa anaweza kulipa 75% ya kile alichochukua, hukumu yake itabadilishwa na kuwa kifungo cha maisha.

    Ukiwa ni uamuzi ambao ni nadra sana kutolewa na wa kushangaza - ni mmoja wa wanawake wachache nchini Vietnam waliohukumiwa kifo kwa uhalifu wa kujinufaisha kibiashara.

    Katika kesi ya Aprili, mahakama ilibaini kwamba alikuwa akisimamia kwa siri Benki ya Biashara ya Saigon, ambayo ni ya tano kwa ukubwa nchini humo, na alichukua mikopo na pesa kupitia kampuni hewa kwa zaidi ya muongo mmoja, ikiwa ni jumla ya dola bilioni 44.

    Waendesha mashtaka walisema kwamba dola bilioni 27 zilikuwa zimepotea katika hali tatanishi, na dola bilioni 12 zilisemekana kuwa zimefujwa, kosa kubwa zaidi la kifedha ambalo ndio sababu ya kuhukumiwa kifo.

    Hata hivyo, mawakili wake wameweka wazi kuwa mteja wao yuko mbioni kutafuta pesa ili aweze kulipa deni la dola bilioni 9 lakini imekuwa kibarua kigumu kuuza mali yake.

    Truong My Lan alizaliwa katika familia ya Wasino-Vietnamese katika Jiji la Ho Chi Minh, na alianza kama mchuuzi wa soko, akiuza vipodozi na mama yake.

    Alianza kununua ardhi na mali baada ya Chama cha Kikomunisti kuanzisha mageuzi ya kiuchumi mwaka wa 1986. Kufikia miaka ya 1990, alikuwa anamiliki sehemu kubwa ya hoteli na mikahawa.

    Vietnam inachukulia adhabu ya kifo kama siri ya serikali na huwa haichapishi ni watu wangapi wanaosubiri kunyongwa, ingawa mashirika ya haki za binadamu yanasema kuna zaidi ya 1,000 na kwamba Vietnam ni mojawapo ya nchi zenye kutoa hukumu ya kunyongwa kwa kiasi kikukubwa zaidi duniani.

    Ikiwa Truong My Lan atafanikiwa kurejesha fedha hizo kwa wakati unaofaa, huenda maisha yake yakasalimika.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Israel yaishambulia Lebanon huku Hezbollah ikilenga kituo cha kijeshi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Israel imesema ililenga shabaha nchini Lebanon Jumatatu jioni baada ya kuapa kulipiza kisasi kwa shambulio la Hezbollah kwenye kituo cha kijeshi, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa kukiuka usitishaji vita wa wiki iliyopita.

    Takriban watu tisa waliuawa na mashambulizi ya Israel katika vijiji viwili vya kusini mwa Lebanon, kulingana na wizara ya afya ya umma ya nchi hiyo.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema lilifikia maeneo lengwa ya Hezbollah na miundombinu "Lebanon nzima", huku likirejelea kujitolea kwake kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Hezbollah ilisema ilikuwa ikijibu "ukiukaji" wa Israel na kuongeza kuwa ilifanya shambulizi la "kujilinda kama onyo", ikifyatua risasi kwenye kituo cha jeshi la Israel katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel.

    Israel ilisema hakukuwa na majeruhi katika mashambulizi ya Hezbollah kwenye eneo la Mlima Dov - linalozozaniwa kwenye mpaka wa Israel-Lebanon linalojulikana kimataifa kama Mashamba ya Shebaa.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alielezea shambulio la Hezbollah kama "ukiukaji mkubwa wa usitishaji mapigano", na kuapa kuwa Israel "itajibu vikali".

    Wakati makubaliano ya kusitisha mapigano yalipotangazwa kwa mara ya kwanza, Netanyahu alisema nchi yake haitasita kufanya mashambulizi ikiwa Hezbollah itavunja masharti.

    Ghasia za Jumatatu ni dalili ya jinsi usitishaji vita uliokubaliwa hivi karibuni unavyoyumba, ambao unaolenga kumaliza mzozo wa miezi 13 kati ya Israel na Hezbollah.

    Soma zaidi:

  18. Natumai umzima wa afya msomaji wetu. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 03/12/2024.