Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mkutano wa Ulaya kuhusu Ukraine umeanza huko Paris

Waziri Mkuu wa Poland amesema ikiwa Ulaya itashindwa "kutumia kiasi kikubwa kwa ulinzi wake sasa, watalazimika kutumia mara 10 zaidi wakati wa vita.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu & Asha Juma

  1. Ulaya inahitaji kufikia Urusi katika ulinzi - Waziri Mkuu wa Poland anasema

    Waziri Mkuu wa Poland amezungumza na waandishi wa habari mapema, na kusema kuwa atawahimiza viongozi wa Ulaya katika mkutano wa leo mjini Paris kuimarisha ulinzi wa Ulaya "mara moja".

    Hii ni kwa sababu Ulaya "haina uwezo wa kukabiliana na uwezo wa kijeshi wa Urusi" na wanahitaji "kujitahidi", Tusk alisema.

    "Hatutaweza kuisaidia Ukraine ipasavyo ikiwa hatutachukua hatua za kivitendo mara moja kuhusu uwezo wetu wa kiulinzi," Tusk aliwaambia waandishi wa habari, kabla ya kuelekea Paris.

    Katika ujumbe mtandaoni baada ya maoni yake, Tusk aliandika kwamba ikiwa Ulaya itashindwa kutumia zaidi kwenye ulinzi hivi sasa, "italazimika kutumia mara 10 zaidi wakati wa vita".

  2. Jaji wa UN alilazimisha mwanamke kufanya kazi kama mtumwa, mahakama yaambiwa

    Jaji wa Umoja wa Mataifa alimhadaa mwanamke kijana kuja Uingereza kufanya kazi kama mtumwa wake alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Oxford, mahakama imearifiwa.

    Lydia Mugambe anatuhumiwa kutumia "mamlaka yake vibaya" dhidi ya anayedaiwa kuwa mwathiriwa katika "njia mbaya zaidi".

    Inadaiwa alimzuia msichana huyo wa Uganda kutafuta kazi ya kumuwezesha kujimudu na kumlazimisha kufanya kazi kama mjakazi wake na kutoa huduma ya watoto bure.

    Bi Mugambe amekanusha mashtaka manne dhidi yake.

    Waendesha mashtaka wanadai kuwa tangu awali, Bi Mugambe, ambaye pia ni jaji wa Mahakama Kuu nchini Uganda, alikuwa na nia ya "kupata mtu wa kurahisisha maisha yake na kwa gharama anayoweza yeye".

    Anashutumiwa kwa kujihusisha na "uhalifu" na naibu kamishna mkuu wa Uganda John Leonard Mugerwa ambaye walikula njama naye ya kumleta msichana huyo Uingereza.

    Wawili hao wanadaiwa kushiriki katika biashara "isiyo ya uaminifu", ambapo Bw Mugerwa alidaiwa kupanga Ubalozi wa Uganda kufadhili mwanamke huyo kuingia Uingereza.

    Bi Mugambe pia anashtakiwa kwa kupanga safari ya mwathiriwa anayedaiwa "kwa nia ya kuwa adhuluiwe", na kujaribu "kumtisha" mwathiriwa ili kufuta kesi.

    Mahakama ya Oxford iliyosikiliza kesi ya mshtakiwa hapo awali aliwaambia polisi kuwa ana "kinga ya kidiplomasia" na hangeweza kukamatwa kutokana na kazi yake kama jaji nchini Uganda na katika Umoja wa Mataifa.

  3. Papa hayuko katika "hali nzuri kiafya', Vatican inasema

    Papa Francis anatibiwa kutokana na kwamba hayuko katika "hali nzuri kiafya" na atasilia hospitalini kadiri na kutakavyokuwa na ulazima wa kufanya hivyo, Vatican imesema.

    Papa mwenye umri wa miaka 88 alilazwa katika Hospitali ya Gemelli huko Roma siku ya Ijumaa ili kupata matibabu na kufanyiwa vipimo vya matatizo ya kupumua.

    Katika taarifa zilizotolewa siku ya Jumatatu, Vatikani ilisema Papa ana "maambukizi yanayosababishwa na mchanganyiko wa virusi, bakteria na vimelea" katika njia yake ya kupumua, ambayo yanahitaji matibabu mengine.

    Kabla ya kulazwa wiki iliyopita, Papa alikuwa na dalili za ugonjwa wa kupumua kwa siku kadhaa na alikuwa amewakabidhi maafisa kusoma hotuba zilizoandaliwa kwenye hafla.

    Msemaji wa Vatican Matteo Bruni aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba Papa alikuwa katika hali nzuri.

    Taarifa fupi kuhusu hali yake ilisema: "Vipimo vyote vilivyofanywa hadi sasa vinaonyesha hali yake sio ya kuridhisha na itahitaji alazwe hospitalini kupata matibabu mwafaka."

    Hadhira ya maombi ya kila wiki ya Papa - ambayo kawaida hufanyika kila Jumatano - imeahirishwa kwa wiki hii, taarifa hiyo iliongeza.

    Taarifa zaidi kuhusu hali ya Papa itatolewa baadaye Jumatatu, Bw Bruni aliongeza.

    Papa mwenye asili ya Argentina ametumia karibu miaka 12 kama kiongozi wa Kanisa Katoliki la Roma.

    Mnamo mwezi Machi 2023, aliwahi kulazwa katika hospitali hiyo hiyo kwa siku tatu na kupata matibabu ya matatizo kupumua.

    Mnamo Desemba mwaka huo huo, alilazimika kukatisha safari yake ya kwenda Falme za Kiarabu kwa mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 kwa sababu ya ugonjwa mwingine.

    Amekuwa akikabiliwa na matatizo kadhaa ya kiafya katika maisha yake yote, ikiwa ni pamoja na kuondolewa sehemu ya pafu lake akiwa na umri wa miaka 21.

  4. Bobi Wine wa Uganda akatazwa kumuona kiongozi wa upinzani Kizza Besigye

    Kiongozi mkuu wa upinzaji wa Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amekatazwa kumuona Kizza Besigye ambaye ni mgonjwa.

    Akiwa katika mgomo wa kula, Besigye ameshikiliwa katika gereza kubwa mjini Kampala, na afya yake inazidi kuibua wasiwasi nchini humo huku upande wa upinzani na familia yake ikitaka kuachiliwa kwake kwa misingi ya kupata matibabu.

    Bobi Wine, pamoja na wanasiasa wengine wa upinzaji na wanaharakati wa haki za kibinadamu walikuwa wakimtembelea Besigye lakini wakaarifiwa na maafisa wa gereza kwamba Besigye ni dhaifu sana na kwamba haweza kukutana nao.

    Alipowasiliana na BBC, Frank Baine msemaji wa Magereza ya Uganda aliiambia BBC kwamba, "Nimesema sina maoni, hiyo inatosha"

    Jana, Besigye mkosoaji wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, alikimbizwa hospitalini na baadaye akarudi gerezani.

    Vikosi vya usalama vilipelekwa karibu na kituo hicho.

    Mwanasiasa huyo maarufu alianza mgomo wa kukataa kula chakula kushinikiza kuzuiliwa kwake baada ya mahakama kuu ya nchi humo kuamuru kuachiliwa kwake kutoka kizuizi cha kijeshi.

    Soma zaidi

  5. Ukraine haitashiriki katika mazungumzo ya Marekani na Urusi nchini Saudi Arabia - Zelensky

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anasema Kyiv haitashiriki katika mkutano kati ya maafisa wa Marekani na Urusi nchini Saudi Arabia siku ya Jumanne, wakati akijiandaa kuelekea nchini humo kwa ziara iliyopangwa kwa muda mrefu.

    "Ukraine inazingatia mazungumzo yoyote kuhusu Ukraine bila Ukraine kama vile ambayo hayana matokeo; na hatuwezi kuyatambua...makubaliano kuhusu sisi bila sisi," Zelensky anawaambia waandishi wa habari wakati wa ziara ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Pia anasema safari zake katika UAE na baadaye Saudi Arabia zilipangwa kabla, na kupendekeza kuwa hazihusiani na mazungumzo ya Marekani na Urusi.

    Soma zaidi:

  6. Marekani: Takriban 10 wafariki dunia kwa mafuriko na mvua kubwa

    Takriban watu 10 wamefariki kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa juma katika sehemu za kusini-mashariki mwa Marekani, na kusababisha barabara na nyumba kuzama.

    Gavana wa Kentucky Andy Beshear alisema watu tisa wamefariki katika jimbo lake, baada ya kutangaza hali ya dharura.

    Karibu watu 1,000 waliokwama kwenye maji ya mafuriko waliokolewa, alisema pia Jumapili.

    Maeneo hayo sasa yanaweza kuathiriwa na hali kavu lakini baridi pia, na ipo katika hatari ya kuwa na theluji, barafu na usumbufu mkubwa - kulingana na mtabiri wa BBC John Hutchinson.

  7. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi na msaidizi mkuu wa Putin wasafiri kuelekea Saudi Arabia

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na msaidizi wa Rais Vladimir Putin, Yuriy Ushakov, wanasafiri kwa ndege kuelekea Saudi Arabia kukutana na maafisa wa Marekani, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimeripoti.

    Awali, tulisema kwamba waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, pia alitakiwa kuwepo katika mji mkuu, Riyadh, kukutana na maafisa kutoka Moscow na kuanza mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine.

    Rubio anaungana na Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani Mike Waltz na mjumbe maalum katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff.

  8. Korea Kusini yaondoa programu ya Deepseek kutoka App Store kwa wasiwasi wa faragha

    Korea Kusini imepiga marufuku upakuaji mpya wa programu ya China ya akili mnemba Deepseek, kulingana na walinzi wa data binafsi.

    Shirika la serikali lilisema programu hiyo itapatikana tena kwa watumiaji wa Korea Kusini wakati "maboresho na masuluhisho" yatakapofanywa ili kuhakikisha kuwa inatii sheria za ulinzi wa data za kibinafsi za nchi hiyo.

    Wiki moja baada ya kugonga vichwa vya habari kimataifa, DeepSeek ilipata umaarufu mkubwa nchini Korea Kusini ikiwa na watumiaji zaidi ya milioni moja kwa wiki.

    Lakini kuongezeka kwa umaarufu wa programu hiyo pia kulivutia uchunguzi kutoka kwa nchi mbali mbali kote ulimwenguni ambazo zimeweka masharti kwa programu hiyo juu ya maswala ya faragha na usalama wa kitaifa.

    Hatua hii inawadia baada ya mashirika kadhaa ya serikali ya Korea Kusini kuwapiga marufuku wafanyikazi wao kupakua programu hiyo kwenye vifaa vyao vya kazi.

    Kaimu rais wa Korea Kusini Choi Sang-mok ameelezea Deepseek kama "mshtuko", ambao unaweza kuathiri viwanda vya nchi hiyo, zaidi ya AI.

    Licha ya kusitishwa kwa upakuaji mpya, watu ambao tayari wanayo kwenye simu zao wataweza kuendelea kuitumia au wanaweza kuipata kupitia tovuti ya DeepSeek.

    Soma zaidi:

  9. Wanajeshi 46,000 wa Ukraine wauawa vitani tangu uvamizi wa Urusi

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema zaidi ya wanajeshi 46,000 wa Ukraine wameuawa tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza kwa kiwango kikubwa mnamo Februari 2022, huku "makumi ya maelfu wengine wakiwa hawajulikani walipo au wakiwa mateka".

    Akizungumza na NBC News Jumapili, Zelensky alisema wale waliotangazwa hawajulikani walipo huenda wamefariki au wako kizuizini nchini Urusi.

    Wiki moja na nusu iliyopita (tarehe 6 Februari), Zelensky alisema wanajeshi wa Ukraine waliouawa walifikia 45,100, huku takriban 390,000 wakijeruhiwa. Hata hivyo, wataalamu wa kijeshi wa Ukraine na Magharibi wanaamini idadi halisi inaweza kuwa juu zaidi.

    Pia, Zelensky alisema kuwa watoto wa Ukraine wapatao 19,500 wamepelekwa kwa lazima nchini Urusi.

    Urusi haijawahi kutangaza idadi ya wanajeshi wake waliopoteza maisha katika vita vya Ukraine, lakini ripoti ya Ujasusi wa Ulinzi nchini Uingereza mnamo Desemba ilikadiria kuwa wastani wa wanajeshi 1,523 wa Urusi wanauawa au kujeruhiwa kila siku.

    Zelensky anadai kuwa hadi sasa wanajeshi 350,000 wa Urusi wameuawa, ingawa ripoti nyingine zinasema kuwa idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi.

  10. Trump akata rufaa dhidi ya mfanyakazi aliyemfikisha mahakamani

    Rais Donald Trump amepeleka ombi la dharura katika Mahakama ya Juu ya Marekani ili iamue ikiwa ana mamlaka ya kumfukuza kazi mmoja wa viongozi waandamizi serikalini, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.

    Hampton Dellinger, mtendaji Mkuu wa Ofisi ya mwanasheria maalumu, amemshtaki Trump baada ya kufutwa kazi kupitia barua pepe mwezi huu.

    Trump pia amewafukuza wakaguzi wakuu kadhaa katika mashirika mbalimbali ya serikali pamoja na maelfu ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani.

    Bw. Dellinger, aliyeteuliwa na rais wa zamani Joe Biden, anasema kufutwa kwake kunakiuka sheria inayowalinda viongozi wa mashirika huru dhidi ya kufutwa kazi na rais, "isipokuwa katika kesi za uzembe wa kazi, matumizi mabaya ya madaraka, au kutoendana na majukumu yao".

    Jaji wa shirikisho mjini Washington DC alitoa amri ya muda Jumatano inayomruhusu Dellinger kuendelea na kazi yake huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.

    Juhudi za Trump kupunguza na kurekebisha mfumo wa utawala wa kiraia wa wafanyakazi wa serikali takriban milioni 2.3 ziliendelea mwishoni mwa wiki.

    Wafanyakazi katika mashirika mbalimbali ya afya waliokuwa bado kwenye kipindi cha majaribio walipokea barua Jumamosi usiku wakifahamishwa kuwa watafutwa kazi, kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyozungumza na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Trump tayari amefukuza wafanyakazi wasiopungua 9,500 katika wizara za Afya na huduma za binadamu, nishati, masuala ya wanajeshi wastaafu, mambo ya ndani, na Kilimo.

    Aidha, wafanyakazi wengine wapatao 75,000 wamepokea ofa ya kuondoka kwa hiari yao kwa kupewa malipo maalum, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.

    Mpango huu wa kupunguza gharama unapendekezwa na Idara ya Ufanisi wa Serikali (Department of Government Efficiency), au kwa kifupi Doge, kikosi kazi kinachoongozwa na Elon Musk.

  11. Imamu wa kwanza duniani aliyejitangaza kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja auawa

    Muhsin Hendricks, mtu mashuhuri aliyejulikana kama imamu wa kwanza duniani aliyejitangaza hadharani kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, ameuwa kwa risasi nchini Afrika Kusini.

    Kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 57 alikuwa anaongoza msikiti mmoja katika jijini la Cape Town uliolenga kuwa mahali salama na kimbilio kwa waumini wa kiislamu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wale waliotengwa na jamii.

    Alipigwa risasi Jumamosi asubuhi baada ya gari alilokuwa akisafiria karibu na jiji la kusini la Gqeberha kushambuliwa.

    "Washukiwa wawili wasiojulikana wakiwa wamefunika nyuso zao walitoka kwenye gari ingine na kuanza kulimiminia risasi nyingi gari hilo," polisi walisema katika taarifa yao.

    Habari za kifo cha Hendricks zimeleta mshtuko mkubwa katika jamii ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ+ ) na kwingineko, huku kukitolewa salamu nyingi za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

    Julia Ehrt, mkurugenzi mtendaji wa shirika la International Lesbian, Gay, Bisexual, Trans and Intersex Association (ILGA), ametoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi wa kina juu ya kile kinachohofiwa kuwa "huenda ni uhalifu unaohusisha chuki".

    "Aliwasaidia na kuwaelekeza watu wengi nchini Afrika Kusini na duniani kote katika safari yao ya kiimani, na maisha yake yalikuwa mfano wa uponyaji unaotokana na mshikamano wa jamii mbalimbali," alisema.

    Hendricks aliuawa baada ya kuripotiwa kufungisha ndoa ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, ingawa hili halijathibitishwa rasmi.

    Taarifa za tukio hilo zilifichuliwa kupitia picha za video za CCTV zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

    Video hiyo inaonyesha gari likisimama na kuziba njia ya gari alilokuwamo Hendricks kabla ya kuanza kushambuliwa.

    Kwa mujibu wa Polisi, imamu huyo alikuwa amekaa kwenye kiti cha nyuma.

  12. Kizza Besigye amerejeshwa gerezani kutoka hospitalini Uganda

    Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amerejeshwa gerezani baada ya kulazwa katika hospitali moja mjini Kampala kwa muda mfupi alipougua kutokana na hatua yake ya kususia chakula.

    Awali, wafuasi wa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye walifichua kwamba mwanasiasa huyo alikimbizwa kwenye hospitali moja huko Bugolobi jana.

    Kupitia mtandao wa kijamii wa x mbunge wa Buhweju nchini Uganda, Francis Mwijukye alifafanua kwamba Besigye aliyekuwa akitumia kiti cha magurudumu alipelekwa kwenye hospitali iliyoko kwenye jengo la kibiashara linaloitwa Bugolobi village Mall.

    Haya yanajiri baada ya familia ya Besigye kuibua wasiwasi kufuatia kupokea ujumbe kutoka idara ya magereza ya Uganda iikiitaka familia hiyo itume daktari binafsi wa Besigye.

    Familia ya Besigye imeahidi kumwajibisha kiongozi wa taifa la Uganda Yoweri Museveni,kwa chochote kitakachomfika Besigye.

    Mwanasiasa huyu alikuwa amewekwa gerezani baada ya kusomewa mashtaka ya kumiliki silaha katika mahakama ya kijeshi ya Uganda.

    Besigye, aliyekuwa daktari wa binafsi wa Rais Yoweri Museveni, alikamatwa katika mazingira ya kutatanisha mwezi Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale.

    Wawili hao baadaye walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Kampala, ambapo walishtakiwa kwa kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria, mashtaka ambayo wanapinga.

    Katika uamuzi wa kihistoria mwezi uliopita, Mahakama ya Juu ya Uganda ilitangaza kuwa ni kinyume cha katiba kwa mahakama za kijeshi kuwahukumu raia, na kuamuru kesi zote hizo kuhamishiwa katika mahakama za kiraia.

    Uamuzi huo ulimkasirisha Rais Museveni, ambaye alipuuzilia mbali na kuutaja kuwa "uamuzi usio sahihi" na kuapa kuupinga.

    Siku ya ijumaa wiki jana, Besigye, mgombea urais mara nne nchini Uganda alifika mahakamani akionekana kudhoofika kiafya.

    Raia wengi wa Uganda ikiwemo mpinzani mwenza Bobi Wine aliandika kwa mtandao wa kijamii kushurutisha Besigye aachiliwe huru na aruhusiwe kupata huduma za matibabu.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Uingereza yawakataa makomando 2000 wa Afghanistan

    Maafisa wa Vikosi Maalum vya Uingereza walikataa maombi ya kutaka kuhifadhiwa kutoka kwa zaidi ya makomando 2,000 wa Afghanistan waliowasilisha ushahidi wa kuaminika wa kuhudumu katika vikosi vilivyopigana bega kwa bega na SAS na SBS, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza (MoD) imethibitisha kwa mara ya kwanza.

    Inaelezwa kuwa maafisa wa Vikosi Maalum vya Uingereza walikataa kila ombi kutoka kwa aliyekuwa komando wa Afghanistan yaliyowasilishwa kwao kwa ajili ya udhamini, licha ya kwamba vikosi hivyo vya Afghanistan vilipigana pamoja na Waingereza katika operesheni hatari dhidi ya Taliban.

    Hapo awali, MoD ilikanusha kuwa kulikuwa na sera ya jumla ya kukataa wanachama wa vikosi hivyo – vinavyojulikana kama Triples – lakini BBC haijapata ushahidi wowote unaoonyesha kuwa Vikosi Maalum vya Uingereza (UKSF) viliunga mkono maombi yoyote ya makazi.

    MoD ilipoulizwa ikiwa UKSF iliunga mkono au kukubali maombi yoyote, ilikataa kujibu swali hilo. Vikosi vya Triples vilivyopewa majina ya CF 333 na ATF 444, viliundwa, kupewa mafunzo, na kulipwa na Vikosi Maalum vya Uingereza, na vilisaidia SAS na SBS kwenye operesheni nchini Afghanistan.

    Wakati nchi hiyo iliangukia mikononi mwa Taliban mnamo 2021, walitajwa kuwa katika hatari kubwa ya kulipiziwa kisasi na walistahili kuomba makazi na kuhifadhiwa nchini Uingereza.

    Kukataliwa kwa maombi yao kulizua utata kwa sababu kulitokea wakati ambapo uchunguzi wa umma nchini Uingereza ulikuwa ukiendelea kuchunguza madai kwamba Vikosi Maalum vilitekeleza uhalifu wa kivita katika operesheni nchini Afghanistan ambapo vikosi vya Triples vilikuwepo.

  14. Baada ya kichapo dhidi ya Spurs, kocha wa United akiri: "Nina matatizo mengi"

    Meneja wa Manchester United Ruben Amorim amesema kazi yake "ni ngumu" baada ya klabu hiyo kuchapwa na Tottenham, na kuiacha timu hiyo ikiwa katika nafasi ya 15 kweney msimamo wa ligi kuu ya England.

    Mreno huyo ameshuhudia timu yake ikichapwa michezo 8 kati ya 12, kufuatia goli la dakika ya 13 la James Maddison kuipa Spurs ushindi.

    Kwa mara nyingine mashetani hao wekundu wameendelea kusuasua, Amorim akiwa na majeruhi 12, na kumfanya kocha huyo kutumia wachezaji wa timu ya vijana kwenye benchi lake.

    Tangu amejiunga na klabu hiyo Amorim, 40, amekuwa muwazi kwenye mazungumzo yake na wanahabari hasa baada ya mechi. Akifanya hivyo tena baada ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Spurs.

    "Nina matatizo mengi," aliiambia Sky Sports. "Kazi yangu ni ngumu, lakini niko hapa kuendelea na kazi yangu kuelekea wiki ijayo nikiamini nitajaribu kushinda tena."

    Licha ya timu yake kuwa nyuma kwa zaidi ya dadika 70, Amorim hakufanya mabadiliko yoyote, mpaka dakika za majeruhi, alipomuingiza kinda wa miaka 17 Chido Obi.

    Mshambuliaji hiyo kinda alikuwa miongoni mwa makinda nane yaliyokuwa kwenye benchi la Amori jana.

  15. Uingereza iko tayari' kupeleka jeshi nchini Ukraine kulinda amani

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer amesema yuko "radhi na tayari" kupeleka wanajeshi wa Uingereza nchini Ukraine kusaidia kuhakikisha usalama wake kama sehemu ya makubaliano ya amani.

    Sir Keir amesema amani ya kudumu nchini Ukraine ni "muhimu ikiwa tunataka kumzuia Putin asiendelee na uchokozi zaidi siku zijazo".

    Kabla ya kuhudhuria mkutano wa dharura wa viongozi wa Ulaya mjini Paris leo Jumatatu, Sir Keir alisema Uingereza iko tayari kuchangia katika dhamana za usalama wa Ukraine kwa "kupeleka wanajeshi wetu nchini humo ikiwa itahitajika".

    "Siwezi kusema hivyo kirahisi," aliandika katika gazeti la Daily Telegraph. "Ninawajibika inapokuja uwezekano wa kuwaweka wanajeshi wa Uingereza katika hatari."

    Waziri Mkuu aliongeza: "Lakini jukumu lolote la kusaidia kuhakikisha usalama wa Ukraine ni kusaidia kuhakikisha usalama wa bara letu na usalama wa nchi hii."

    Wanajeshi wa Uingereza wanaweza kupelekwa kandokando ya mpaka kati ya maeneo yanayoshikiliwa na Ukraine na yale yanayoshikiliwa na Russia, wakiungana na wanajeshi kutoka mataifa mengine ya Ulaya.

    Tangazo la Sir Keir linakuja baada ya aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Uingereza, Lord Dannatt, kusema katika mahojiano na BBC kwamba jeshi la Uingereza "limepunguzwa sana" na haliwezi kuongoza ujumbe wowote wa amani wa siku zijazo nchini Ukraine.

    Waziri Mkuu anatarajiwa kumtembelea Rais Donald Trump mjini Washington baadaye mwezi huu na amesema "dhamana ya usalama kutoka Marekani ni muhimu kwa amani ya kudumu, kwa sababu ni Marekani pekee inayoweza kumzuia Putin asishambulie tena".

    Sir Keir anakutana na viongozi wengine wa Ulaya kutokana na wasiwasi kwamba Marekani inasonga mbele katika mazungumzo ya amani na Russia bila kushirikisha mataifa ya Ulaya.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anapanga kukutana na maafisa wa Urusi nchini Saudi Arabia katika siku zijazo, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani.

    Jumamosi, mjumbe maalum wa Marekani kwa Ukraine, Keith Kellogg, alisema viongozi wa Ulaya watahusishwa tu kwa mashauriano na hawatashiriki katika mazungumzo kati ya Marekani na Urusi.

    Chanzo kimoja cha juu serikalini Ukraine kiliiambia BBC siku ya Jumapili kwamba Kyiv haijaalikwa kwenye mazungumzo hayo kati ya Marekani na Urusi.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Ukraine yatengwa kwenye mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Urusi

    Kyiv haijaalikwa kwenye mazungumzo kati ya Marekani na Urusi yenye lengo la kumaliza vita nchini Ukraine, chanzo kikuu kutoka serikali ya Ukraine kimeiambia BBC.

    Mjumbe maalum wa Marekani nchini Ukraine, Keith Kellogg, alisema kwamba Kyiv ingehusika katika mazungumzo ya Jumatatu nchini Saudi Arabia, lakini chanzo hicho kimesema hakuna mwakilishi wa Kyiv atakayehudhuria.

    Viongozi wa Ulaya pia hawajaalikwa kujiunga na majadiliano hayo, na badala yake wanatarajiwa kukutana Jumatatu hii mjini Paris katika mkutano wa kilele ulioandaliwa kwa dharura na rais wa Ufaransa, huku hofu ikiongezeka kwamba bara hilo linatengwa kwenye mazungumzo hayo.

    Mikutano hiyo tofauti inafuatia wiki yenye msukosuko ambapo Washington imeashiria mabadiliko makubwa katika mbinu yake kuhusu vita nchini Ukraine.

    Mjumbe wa Ikulu ya Marekani anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, amethibitisha kwamba alikuwa safarini Saudi Arabia Jumapili jioni kwa mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana kati ya Marekani na Urusi kuelekea kumaliza mgogoro huo.

    Rais wa Marekani alifichua Jumapili kwamba Witkoff alikuwa amekutana na Putin tayari "kwa mazungumzo marefu, kama masaa matatu hivi".

    Witkoff, bilionea na rafiki wa Trump, alikuwa Moscow wiki hii ili kuhakikisha kuachiliwa kwa mwalimu wa Marekani aliyefungwa kwa mashtaka ya kukutwa na bangi.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na mshauri wa usalama wa taifa pia wanatarajiwa kukutana na wajumbe wa Urusi nchini Saudi Arabia, chini ya wiki moja baada ya Trump kufanya mazungumzo kwa simu na kiongozi wa Urusi, Vladimir Putin.

    Simu hiyo ya Jumatano ilimaliza kipindi cha miaka mitatu cha kutokuwepo na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Moscow na Washington.

    Kwa upande wake Rais wa Ukraine, Zelensky amekuwa akikataa mara kwa mara kukubali makubaliano ya amani yaliyojadiliwa bila Ukraine kushirikishwa, akiiambai televisheni ya Marekani ya NBC Jumapili kwamba "hatutakubali kamwe maamuzi yoyote kati ya Marekani na Urusi kuhusu Ukraine, kamwe".

    Maelezo zaidi:

  17. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.