Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer amesema yuko "radhi na tayari" kupeleka wanajeshi wa Uingereza nchini Ukraine kusaidia kuhakikisha usalama wake kama sehemu ya makubaliano ya amani.
Sir Keir amesema amani ya kudumu nchini Ukraine ni "muhimu ikiwa tunataka kumzuia Putin asiendelee na uchokozi zaidi siku zijazo".
Kabla ya kuhudhuria mkutano wa dharura wa viongozi wa Ulaya mjini Paris leo Jumatatu, Sir Keir alisema Uingereza iko tayari kuchangia katika dhamana za usalama wa Ukraine kwa "kupeleka wanajeshi wetu nchini humo ikiwa itahitajika".
"Siwezi kusema hivyo kirahisi," aliandika katika gazeti la Daily Telegraph. "Ninawajibika inapokuja uwezekano wa kuwaweka wanajeshi wa Uingereza katika hatari."
Waziri Mkuu aliongeza: "Lakini jukumu lolote la kusaidia kuhakikisha usalama wa Ukraine ni kusaidia kuhakikisha usalama wa bara letu na usalama wa nchi hii."
Wanajeshi wa Uingereza wanaweza kupelekwa kandokando ya mpaka kati ya maeneo yanayoshikiliwa na Ukraine na yale yanayoshikiliwa na Russia, wakiungana na wanajeshi kutoka mataifa mengine ya Ulaya.
Tangazo la Sir Keir linakuja baada ya aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Uingereza, Lord Dannatt, kusema katika mahojiano na BBC kwamba jeshi la Uingereza "limepunguzwa sana" na haliwezi kuongoza ujumbe wowote wa amani wa siku zijazo nchini Ukraine.
Waziri Mkuu anatarajiwa kumtembelea Rais Donald Trump mjini Washington baadaye mwezi huu na amesema "dhamana ya usalama kutoka Marekani ni muhimu kwa amani ya kudumu, kwa sababu ni Marekani pekee inayoweza kumzuia Putin asishambulie tena".
Sir Keir anakutana na viongozi wengine wa Ulaya kutokana na wasiwasi kwamba Marekani inasonga mbele katika mazungumzo ya amani na Russia bila kushirikisha mataifa ya Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, anapanga kukutana na maafisa wa Urusi nchini Saudi Arabia katika siku zijazo, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani.
Jumamosi, mjumbe maalum wa Marekani kwa Ukraine, Keith Kellogg, alisema viongozi wa Ulaya watahusishwa tu kwa mashauriano na hawatashiriki katika mazungumzo kati ya Marekani na Urusi.
Chanzo kimoja cha juu serikalini Ukraine kiliiambia BBC siku ya Jumapili kwamba Kyiv haijaalikwa kwenye mazungumzo hayo kati ya Marekani na Urusi.