Trump aahidi kutoa amri nyingi za kiutendaji katika siku ya kuapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati wa mkesha wa kurejea kwake White House, Rais mteule Donald Trump aliahidi kusaini amri ya utendaji katika siku yake ya kwanza kama rais, akiwaeleza wafuasi wake kwamba atasonga mbele kwa "kasi ya kihistoria na nguvu" katika saa chache baada ya kula kiapo.

Akihutubia umati mkubwa wa maelfu ya watu katika uwanja wa Washington DC waliokusanyika kwa ajili ya mkutano wa ushindi "Victory Rally", Trump alitoa hakikisho la miaka minne ijayo na kusherehekea ushindi wake wa uchaguzi wa mwezi Novemba dhidi ya Democrats.

Chama cha Republican kimeahidi kuchukua hatua bila kuhusisha chama kingine katika masuala mbalimbali, kwa kutumia mamlaka yake ya urais kuanzisha operesheni za kuwarudisha watu wengi katika nchi zao, kupunguza kanuni za mazingira na kusitisha mipango inayowahusu watu wa jamii mbali mbali.

"Tunaiweka Marekani kwanza na yote yanaanza kesho," aliuambia umati wa watu katika hafla hiyo ya kampeni, na kuongeza kusema kuwa : "Utakuwa na furaha kubwa kutazama televisheni kesho." Trump anatarajiwa kutia saini zaidi ya hatua 200 za utendaji siku ya Jumatatu.

Hii itajumuisha maagizo ya kiutendaji, ambayo yataenda kinyume na sheria, na maagizo mengine ya rais kama matangazo, ambayo kwa kwa kawaida hayatolewi.

"Kila amri ya kiutendaji yenye msimamo mkali na ya kijinga ya utawala wa Biden itafutwa ndani ya saa chache baada ya kuapishwa," rais huyo anayeingia mamlakani alisema.

Trump aliahidi kuweka amri za kiutendaji ambazo zitaimarisha mipango ya akili mnemba, kuunda Idara ya Ufanisi wa Serikali (Doge), kukusanya rekodi zinazopatikana kuhusiana na mauaji ya John F Kennedy mnamo 1963, kuelekeza jeshi kuunda ngao ya ulinzi wa makombora ya Iron Dome.

Pia aliwaambia wafuasi wake kuwa atawazuia wanawake waliobadili jinsia kushindana katika makundi ya michezo ya wanawake na kurudisha udhibiti wa elimu kwa majimbo ya Marekani.

"Utaona maagizo ya kiutendaji ambayo yatakufanya uwe na furaha sana," aliuambia umati wa watu. "Tunapaswa kuweka nchi yetu katika njia sahihi."

Marais kwa kawaida huchukua hatua za kiutendaji wanapoingia madarakani lakini kiwango cha siku moja vya amri kutoka kwa Trump kinaweza kuwa cha juu kupita watangulizi wake na amari nyingi zainatarajiwa kupingwa mahakamani.

Aliahidi kwamba utendaji wake utalenga uhamiaji haramu - suala ambalo ni kiini cha kampeni ya ushindi wa Republican ya urais.

Lakini wataalamu wanasema ahadi yake ya kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji wasio na vibali itakabiliwa na vikwazo vikubwa vya vifaa, na huenda ikagharimu makumi au mamia ya mabilioni ya dola.

Trump pia anatarajiwa kutoa msamaha kwa watu waliopatikana na hatia ya kushiriki katika ghasia za Januari 6 katika jengo la bunge la Marekani mwaka 2021 wakiongozwa na wafuasi wake.

Aliwataja waandamanaji wa Januari 6 kama "waandaaji" na kuahidi kuwa kila mtu "atafurahishwa sana" na uamuzi wake Jumatatu.

Unaweza pia kusoma:

Mkutano wa Trump ulifanyika katika uwanja wa Capital One Arena mjini Washington DC, ambao una uwezo wa kuchukua watu 20,000.

Ulianza kwa onyesho la Kid Rock na lilijumuisha hotuba kutoka kwa mytangazaji maarufu wa Televisheni Megyn Kelly, muigizaji Jon Voight na mshauri mwandamizi wa Trump Stephen Miller.

Elon Musk pia alitoa hotuba fupi baada ya Trump kutangaza kuundwa kwa Doge, shirika la ushauri ambalo bilionea huyo wa teknolojia anatarajiwa kuliongoza na Vivek Ramaswamy, mjasiriamali ambaye alijaribu kugombea uteuzi wa urais wa Republican na kushindwa lililoshindwa.

Familia ya Trump pia iliungana naye jukwaani, wakiwemo watoto wa kiume Donald Trump Jr na Eric, na mke wa Eric Lara Trump.

Wafuasi wa Trump walifurika katika mji mkuu kuonyesha Uungwaji mkono wa rais mteule katika mji mkuu wa taifa hilo mwishoni mwa wiki hii licha ya baridi kali na theluji siku ya Jumapili.

Sherehe za kuapishwa kwa rais wa Marekani zimehamishwa ndani ya jengo la Rotunda kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 40 kutokana na hali mbaya ya hewa, na hivyo kuwaacha nje maelfu ya watu ambao walikuwa na matumaini ya kushuhudia sherehe hiyo katika uwanja wa National Mall.

Viwango wa nyuzijoto vinatarajiwa kuwa karibu -6C (22F) saa sita mchana wakati wa kuapishwa kwa Trump.

Wafuasi badala yake wametakiwa kutazama tukio hilo kutoka uwanja wa Capitol One Arena, ambao pia utaandaa gwaride nje.

Trump amesema ataungana na umati wa watu baada ya kula kiapo na kutoa hotuba yake ya uzinduzi. Mada za hotuba yake zitaripotiwa kuwa umoja, nguvu na "usawa".

Franklin Graham - mtoto wa muinjilisti maarufu Billy Graham - atatoa wito huo wakati wa sherehe ya kuapishwa Jumatatu.

"Nadhani Rais Trump ni mtu tofauti sana na alivyokuwa mwaka 2017," alikiambia kipindi cha BBC Radio 4 cha Jumapili. "Nadhani Mungu amemuimarisha na amekuja kupitia huyu mtu mwenye nguvu zaidi na atakuwa rais bora zaidi kutokana na shida hizi zote alizopitia."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi