Tanzania yawafutia mashtaka washukiwa 600 wa maandamano

Chanzo cha picha, Reuters
Tanzania yawamefuta mashtaka dhidi ya watu 607 waliokamatwa wakati wa msako wa baada ya uchaguzi wa Oktoba, wengi wao wakishtakiwa kwa uhaini kufuatia maandamano mabaya.
Katika taarifa ya video, Waziri wa Masuala ya Sheria, Juma Homera amesema watu 2,045 kote nchini walikamatwa na kushtakiwa kuhusiana na machafuko hayo.
Homera amesema zaidi ya watu 1,400 wanaendelea kushikiliwa huku kesi zao zikipitiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
"Watu 607 tayari wameachiliwa huru kufikia Jumanne... Baadhi wataachiliwa huru siku zijazo na huku wengine wakitarajiwa kubaki kizuizini kwa tathmini zaidi, na kuachiliwa huru zaidi kutategemea matokeo ya DPP," anasema Homera.
Uamuzi wa kuondoa mashtaka unafuatia agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu wakati wa ufunguzi wa Bunge Novemba 14, likimuagiza DPP na vyombo vya usalama kupitia kesi hizo na kuwaachilia wale ambao hawakuwa katikati ya ghasia za baada ya uchaguzi.
Maandamano ya wiki nzima, yaliyosababishwa wakati wa uchaguzi wa Oktoba, yalishuhudia vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji.
Kulingana na vyanzo mbalimbali, mamia ya watu waliuawa.
Uhaini una adhabu ya kifo nchini Tanzania, ingawa hukumu nyingi za kifo baadaye hubadilishwa kuwa kifungo cha maisha.
Utekelezaji wa mwisho nchini wa hukumu ya kifo ni katika miaka ya 1990.


















