Habari za hivi punde, Maandamano Kenya: Afisi ya jinai yatoa video za wahalifu wakati wa Maandamano
Afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imetoa onyo kali kwa vyombo vya uhalifu vinavyotumia maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali kama kisingizio cha kufanya uhalifu.
Katika taarifa kwenye X siku ya Jumanne, DCI ilichapisha kanda za video zikionyesha wizi huo wa mchana, zikiangazia magenge ya wahalifu waliojihami wanaoendeleza uhalifu huo.
"Maafisa wa afisi hiyo sasa wameagizwa kuwafuata wafuasi wa magenge waliorekodiwa na wananchi wanaohusika wakiwaibia Wakenya wasio na hatia barabarani, huku wakichukua fursa ya maandamano yanayoendelea," ilisema afisi ya DCI.
Wakati huohuo Mfanyabiashara mmoja mjini Mombasa aliyeripotiwa kuwatimua waandamanaji katika eneo la Ganjoni wakati wa maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali amekamatwa.
Afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), katika taarifa iliyotolewa Jumanne, imesema mmiliki wa Hoteli moja mjini Mombasa aliwapiga risasi na kuwajeruhi watu wawili mwendo wa mchana.
Mfanyabiashara huyo alikuwa akijaribu kulinda biashara zake dhidi ya waandamanaji
Afisi ya DCI imesema kuwa mtu huyo kwa sasa anazuiliwa na maafisa wa polisi.




























