Biden awahakikishia wafadhili kuwa bado anaweza kushinda uchaguzi

Rais Biden awaahidi wafadhili kuwa atashinda uchaguzi, na "atapambana zaidi" baada ya mjadala wake usio na mvuto.

Muhtasari

  • Uchaguzi wa Ufaransa: Idadi kubwa ya raia wajitokeza kupiga kura
  • Mvulana, 13, aliyepigwa risasi na polisi Marekani alikuwa na mfano wa bunduki
  • Kikosi cha mpito cha Umoja wa Afrika chakabidhi kambi ya jeshi kwa Somalia
  • Kimiminika walichodhani ni pombe chawaua mabaharia wanne
  • Zelensky atoa wito wa kutaka apewe silaha za masafa marefu baada ya shambulio
  • Takriban watu 18 wameuawa katika milipuko kaskazini mwa Nigeria
  • Biden awahakikishia wafadhili kuwa bado anaweza kushinda uchaguzi

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Uchaguzi wa Ufaransa: Idadi kubwa ya raia wajitokeza kupiga kura huku mrengo wa kulia ukitafuta ushindi wa kihistoria

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wapiga kura wa Ufaransa wakipanga foleni kupiga kura

    Ufaransa inapiga kura katika uchaguzi wa ubunge ambao unaweza kuweka historia, huku mrengo wa kulia ukitarajia kupata ushindi baada ya Rais Emmanuel Macron kuitisha uchaguzi wa mapema kufuatia matokeo mabaya katika uchaguzi wa hivi karibuni wa Ulaya.

    Hadi kufikia sasa, idadi kubwa ya wapiga kura wamejitokeza na kutarajiwa kuweka historia ikilinganishwa na upigaji kura wa hivi karibuni.

    Shughuli ya upigaji kura katika maeneo ya mijini itafungwa saa 20:00 saa za eneo.

    Kufikia saa 17:00 saa za eneo, 59.39% ya wapiga kura walikuwa tayari wamepiga kura, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.

    Mnamo 2022 wakati kama huo, waliojitokeza walikuwa 39.4%.

  3. Kiungo wa kati wa Villa Luiz ajiunga na Juventus kwa mkataba wa £42.35m

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Juventus ya Italia imekamilisha usajili wa kiungo wa Aston Villa Douglas Luiz kwa pauni milioni 42.35 (Euro milioni 50).

    Mbrazil huyo, 26, amesaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo ya Serie A na kutamatisha uwepo wake huko Villa Park.

    Luiz, ambaye amechezeshwa mara 15 na taifa lake, alifunga mabao 22 katika mechi 204 akiwa na Villa, ambayo ilimsajili kutoka Manchester City mnamo 2019.

    Kiungo huyo kwa sasa yuko Marekani na timu ya taifa ya Brazil kwenye michuano ya Copa America ambako alikamilisha vipimo vyake vya afya vya Juventus.

    "Nina furaha sana kuwa Bianconero," alisema Luiz kwenye video katika mtandao wa kijamii.

    "Siwezi kusubiri kucheza katika Uwanja wa Allianz. Tutaonana hivi karibuni na Forza Juve!"

    Luiz alifunga mabao tisa katika mechi 35 za Ligi ya Primia msimu uliopita Villa ikifuzu kwa Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza kwa kumaliza nafasi ya nne.

    Lakini hitaji kubwa la Villa la kufuata Sheria za Faida na Uendelevu yaani Profit and Sustainability Rules (PSR) lilimaanisha kuwa walilazimika kumnunua mmoja wa wachezaji wao muhimu.

    Sheria za PSR huruhusu hasara ya hadi £105m kwa miaka mitatu kwa vilabu vya Ligi ya Primia.

    Villa tayari wamemuuza kiungo Tim Iroegbunam, 21, kwa Everton kwa kitita cha pauni milioni 9, wakati Chelsea wamekamilisha uhamisho wa pauni milioni 19 kwa kiungo wao mshambuliaji Omari Kellyman, 18.

    Soma zaidi:

  4. Mvulana, 13, aliyepigwa risasi na polisi Marekani alikuwa na mfano wa bunduki - mamlaka

    .

    Chanzo cha picha, Utica police

    Polisi katika jimbo la New York wamempiga risasi na kumuua mvulana wa miaka 13 baada ya kuwakimbia polisi huku akiwa ameshikilia mfano halisi wa bunduki, mamlaka ilisema.

    Maafisa waliwasimamisha Nyah Mway na kijana mwingine mwenye umri wa miaka 13 siku ya Ijumaa usiku walipokuwa wakilinganisha maelezo ya washukiwa waliokuwa wakisakwa kwa wizi wa hivi majuzi huko Utica, polisi walisema.

    Maafisa hao walipokuwa wakiwahoji wavulana hao, Nyah Mway alikimbia kwa miguu na msako ukafuata. Mkuu wa Polisi wa Utica Mark Williams alisema polisi waliona kile "kilichoonekana kama bastola".

    Afisa mmoja kisha akapigana mweleka na mvulana huyo hadi sakafuni. "Wakati wa mapambano ya ardhini", afisa mwingine alifyatua risasi moja ambayo ilimpiga kijana huyo kifuani, mkuu wa polisi alisema.

    Alipewa huduma ya kwanza katika eneo la tukio lakini baadaye alifariki katika Hospitali ya Wynn.

    Polisi walitoa dakika kadhaa za picha za kamera za mwili wa kijana huyo Jumamosi usiku, kutoka kwa kamera zote za maafisa.

    Hilo lilitokea muda mfupi baada ya watu waliokasirishwa na tukio hilo kumzomea mkuu wa polisi wa Utica katika mkutano na waandishi wa habari, ambao ulihudhuriwa na familia ya mvulana huyo.

    Meya wa Utica Michael Galime alitoa wito wa utulivu, akisema: "Tunaelewa uzito wa hali hii na tunataka kuhakikisha kuwa kila kipande cha hili kinaeleweka."

    Kanda hiyo inaonekana kuonyesha kijana huyo akionyesha kile polisi wanasema ilikuwa silaha ya mfano, wakati akikimbia. Maafisa hao wanaweza kusikika wakipiga kelele "bunduki!" kwa kila mmoja.

    Maafisa hao waliamini kuwa wameona bunduki halisi, polisi walisema - lakini baadaye iliamuliwa kuwa mfano wa silaha ya Glock 17.

    Soma zaidi:

  5. Kikosi cha mpito cha Umoja wa Afrika chakabidhi kambi ya jeshi kwa Wanajeshi wa Kitaifa wa Somalia

    .

    Chanzo cha picha, ATMIS

    Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimekabidhi kambi ya jeshi ya Abdalla Birolle kwa Wanajeshi wa Kitaifa wa Somalia (SNAF).

    Kambi hiyo ya kijeshi, ambayo hapo awali ilikuwa chini ya Wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya wa ATMIS (KDF), ni ya nne kukabidhiwa kama sehemu ya mchakato uliopangwa.

    Naibu Mwakilishi Maalum ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (DSRCC), Siyuvile Bam, aliongoza tukio la kukabidhiwa kwa kambi hiyo ya kijeshi.

    Katika tukio hilo, miongoni mwa walikuwapo ni wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN) na maafisa wa Jimbo la Jubaland.

    "Somalia iliwahi kutoa hifadhi kwa wapigania uhuru kutoka nchi nyingine za Afrika wakati wa harakati zao za kutafuta uhuru. Ni wajibu wetu kurudisha uungwaji mkono na kujitolea kwa watu wa Somalia kwa ajili ya uhuru wa nchi zetu," alisema Bw. Bam.

    Aliongeza kuwa, "Ingawa tunakabidhi majukumu ya usalama, Umoja wa Afrika hautaitelekeza Somalia na utaendelea kuunga mkono mchakato wa amani na usalama unaoongozwa na Somalia."

    "Kiutendaji, tumepata mafanikio makubwa, na kuwa na athari kubwa kwa usalama huko Kismayo. Kambi ya jeshi ya Abdalla Birolle inatumika kama eneo lisilo na vita uwanja wa ndege wa Kismayo na hivyo kwa wenzetu wanaochukua nafasi hii, tunawatakia kila la kheri. Tutaendelea kuwepo kwa mashauriano na msaada kama inavyohitajika," Brig Rashid alisema.

    Akiwakilisha kikosi cha wanajeshi wa kitaifa wa Somalia, Meja Muhudin, alishukuru kikosi cha ATMIS, KDF kwa kujitolea kwao kuhakikisha usalama wa Somalia.

    "Wanajeshi wa Jeshi la Kenya wamejitolea wakati muhimu kupigania ukombozi na usalama wa Somalia, na kuchangia katika mchakato wa amani. Hakuna anayehatarisha maisha yake isipokuwa kwa sababu muhimu," alisema Meja Muhudin.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mabaharia wanne wafariki baada ya kunywa kimiminika kilichokuwa kwenye chupa walizozipata baharini

    ,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wavuvi wanne kutoka Sri Lanka wamefariki dunia na wengine wawili wakiwa wagonjwa mahututi baada ya kutumia kimiminika kisichojulikana kutoka kwenye chupa walizozipata wakiwa baharini, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini humo.

    Mabaharia hao walisemekana kuwa katika safari ya kuvua samaki walipopata chupa hizo takriban maili 320 kutoka eneo la Tangalle, mji ulio kwenye pwani ya kusini ya kisiwa hicho.

    Jeshi la Wanamaji la Sri Lanka liliwaambia wanahabari wavuvi hao walikuwa wamekunywa kimiminika kutoka kwenye chupa hizo wakidhani zilikuwa na pombe.

    Jeshi la wanamaji liliambia vyombo vya habari vya ndani kwamba chombo walichokuwa wakitumia kilivutwa kurudi ufuoni na meli nyingine.

    Mamlaka sasa inachunguza kilichomo kwenye chupa hizo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Zelensky atoa wito upya wa kutaka apewe silaha za masafa marefu baada ya shambulio

    ,

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito upya wa kutaka silaha zaidi za masafa marefu na ulinzi wa anga baada ya shambulio la kombora kuuwa watu saba wakiwemo watoto wawili.

    Shambulio la Urusi katika mji wa Vilniansk, karibu na mji wa kusini-mashariki wa Zaporizhzhia, pia limejeruhi wengine 31, maafisa wa Ukraine walisema.

    Kwa jumla, takriban raia 11 waliuawa na wengine 37 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora kote Ukraine siku ya Jumamosi, Reuters iliripoti.

    "Miji na jamii zetu huteseka kila siku kutokana na mashambulizi kama hayo ya Urusi," Bw Zelensky aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegram.

    Lakini aliongeza kuwa kuna "njia za kuondokana na hili", ikiwa ni pamoja na "kuharibu vyombo vya kurushia makombora vya Urusi, kuyashambulia kwa uwezo halisi wa masafa marefu na kuongeza idadi ya mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga".

    Alichapisha picha za eneo la Vilniansk zinazoonyesha shimo kubwa karibu na jengo linalofuka moshi, pamoja na miili kadhaa iliyowekwa chini.

    Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ukraine Andriy Kostin alisema makombora mawili yalishambulia mji huo, na kuharibu miundombinu, duka na majengo ya makazi.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi haijatoa maoni yoyote hadharani kuhusu shambulio hilo.

    Soma zaidi:

  8. Takriban watu 18 wameuawa katika milipuko kaskazini mwa Nigeria

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban watu 18 wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa katika msururu wa milipuko mibaya katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, maafisa wamesema.

    Moja ya shambulizi linashukiwa kusababisha vifo vya watu sita na kuwajeruhi wengine katika sherehe ya harusi siku ya Jumamosi.

    Shirika la usimamizi wa dharura katika jimbo hilo lilisema kuwa watu wanaoshukiwa kujitoa mhanga walishambulia harusi, mazishi na hospitali katika mji wa Gwoza.

    Jimbo la Borno limekuwa kitovu cha uasi wa miaka 15 wa wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram, ambao umesababisha zaidi ya watu milioni mbili kuyahama makazi yao na kuua zaidi ya 40,000.

    Boko Haram walipata sifa mbaya kimataifa mwaka 2014 walipowateka nyara zaidi ya wasichana 270 wa shule kutoka mji wa Chibok, pia katika jimbo la Borno.

    Mamlaka ilisema vifo 18 vimethibitishwa Jumamosi, idadi iliyojumuisha watoto, watu wazima na wanawake wajawazito.

    Baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimeripoti idadi kubwa zaidi ya vifo - magazeti ya Vanguard ya Nigeria na This Day yalisema kuwa takriban 30 wameuawa katika milipuko hiyo.

    Amri ya kutotoka nje imewekwa na jeshi.

    Hakuna aliyedai kuhusika na mashambulizi hayo.

    Gwoza alitekwa na Boko Haram mwaka 2014, na kutwaliwa tena na vikosi vya Nigeria mwaka 2015 - lakini kundi hilo tangu wakati huo limeendelea kufanya mashambulizi na utekaji nyara karibu na mji huo.

    Mwezi Novemba mwaka jana, watu 20 waliuawa na waasi wa Boko Haram walipokuwa wakirejea kutoka katika ibada ya mazishi katika jimbo jirani la Yobe.

    Shambulio hilo lilitokea siku moja baada ya wanamgambo kuua watu 17 katika uvamizi kwenye kijiji cha Gurokayeya, baada ya wanakijiji kukataa kulipa kile kinachoitwa ushuru wa mavuno, polisi walisema.

    Soma zaidi:

  9. Biden awahakikishia wafadhili kuwa bado anaweza kushinda uchaguzi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Joe Biden amewahakikishia wafadhili wa chama cha Democrat kwamba bado anaweza kushinda uchaguzi wa urais dhidi ya Donald Trump, baada ya utendaji mbovu wa mdahalo uliozua wasiwasi kuhusu kugombea kwake.

    Rais, 81, alihudhuria mfululizo wa hafla za kuchangisha pesa huko New York na New Jersey siku ya Jumamosi, na alitetea utendaji wake katika Mjadala wa Urais wa CNN.

    Akizungumza katika moja ya hafla hizo, Bw Biden alikiri "Sikuwa na usiku mwanana, lakini hata Trump naye pia hakuwa na furaha” siku ya Alhamisi.

    “Nawaahidi tutashinda uchaguzi huu,” alisema.

    Rais baadaye alisema anaelewa wasiwasi uliopo kuhusu utendakazi wake katika mjadala wa Alhamisi, lakini akaahidi kupambana zaidi.

    Gavana wa chama cha Democratic mjini New Jersey, Phil Murphy alihudhuria hafla hiyo pamoja na Bw Biden na mkewe - na kumwambia Bw Biden kwamba "sote tuko pamoja nawe 1,000%.

    Kampeni ya Biden ilikubali kwamba mdahalo haukuenda kama walivyotarajia, lakini walisema hatajitoa kumpisha mteule mwingine.

    Rais wa zamani Barack Obama, rafiki wa karibu wa Bw Biden, alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba "usiku wa mijadala mbaya hutokea".

    "Uchaguzi huu bado ni chaguo kati ya mtu ambaye alipigania watu wa kawaida maisha yake yote na mtu anayejijali yeye tu," Bw Obama aliandika.

    Saa chache tu baada ya mjadala huo, Bw Trump aliwaambia wafuasi wake kwamba aliuchukulia mjadala huo kama "ushindi mkubwa" kwa kampeni yake, na akasema Bw Biden "hakuwa na uwezo kabisa."

    "Tatizo la Joe Biden sio umri wake," Trump mwenye umri wa miaka 78 alisema.

    Soma zaidi:

  10. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 30/06/2024