Somalia inayaita makubaliano ya Ethiopia-Somaliland kuwa kitendo cha uchokozi

Chanzo cha picha, SOMALIA GOVERNMENT
Somalia imeyataja makubaliano yaliyofikiwa kati ya Ethiopia na eneo la Somaliland kuhusu ufikiaji wa bahari kama kitendo cha "uchokozi".
Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini haitambuliki kimataifa.
Somalia ilisema kuwa Ethiopia ilikubali kutambua uhuru wa eneo hilo wakati fulani katika siku zijazo ili kubadilishana kijeshi kuingia pwani.
Ethiopia haijathibitisha kipengele hiki cha makubaliano yenye utata yaliyofikiwa Jumatatu.
Badala yake, ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ilisema ilitia saini kile kinachojulikana kama mkataba wa maelewano (MoU) "ili kupata ufikiaji wa baharini na kupanua ufikiaji wake wa bandari".
Bw Abiy hapo awali alielezea upatikanaji wa bahari kama "suala lililopo" kwa nchi yake. Mshauri wake wa usalama wa taifa, Redwan Hussein, pia alisema kwenye X kwamba mpango huo unaweza kuiwezesha Ethiopia kufikia "kambi ya kijeshi iliyokodishwa" baharini, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Makubaliano ya Maelewano yanazingatiwa kama taarifa ya dhamira na inaweza kusababisha mkataba wa kisheria.
Matukio hayo yanaonyeshwa na pande zote mbili kama hatua kuu ya kidiplomasia. Somalia, hata hivyo, imejibu kwa hasira MoU hiyo kwani inaiona Somaliland kama sehemu ya ardhi yake.
Ilisema inamwita nyumbani balozi wake nchini Ethiopia.
Serikali ilisema makubaliano hayo ni "batili " na ukiukaji wa uhuru wake.
Katika taarifa yake iliongeza kuwa "inachukulia hatua hii kama uchokozi na... ni kikwazo kwa ujirani mwema, amani na utulivu wa eneo ambalo [tayari] linakabiliwa na changamoto nyingi".
Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Bare aliwataka watu kuwa watulivu.
"Nataka niwahakikishie kuwa tumejitolea kulinda nchi. Sehemu ya ardhi yetu, bahari yetu na anga yetu haiwezi kukiukwa na nitaitetea kwa kila njia ya kisheria," alisema katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa kwa dharura.
Somalia pia imesema ilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kujadili suala hilo.

Maelezo kamili ya makubaliano ya Jumatatu ambayo yalitiwa saini na Waziri Mkuu Abiy na Rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, hayajulikani.
Bw Abdi alisema makubaliano hayo yanajumuisha sehemu inayosema kwamba wakati fulani Ethiopia itaitambua Somaliland kama nchi huru.
Wizara ya mambo ya nje ya Somaliland ilisema katika taarifa baadaye kwamba "makubaliano ya kihistoria yanahakikisha ufikiaji wa Ethiopia baharini kwa vikosi vyao vya wanamaji, unaorudiwa kwa utambuzi rasmi wa Jamhuri ya Somaliland, na kuashiria hii kama hatua muhimu ya kidiplomasia kwa nchi yetu".
Ilimnukuu rais akisema kwamba kutambuliwa kutakuwa katika "mabadilishano ya kilomita 20 (maili 12) kufikia bahari kwa vikosi vya wanamaji vya Ethiopia, vilivyokodishwa kwa muda wa miaka 50".
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Lizzy Masinga












