Mtu mmoja afariki baada ya ndege ya Singapore kukumbwa na msukosuko
Ndege hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 211 na wafanyakazi 18, shirika hilo la ndege lilisema katika taarifa yake.
Muhtasari
- Ndege ilipata 'msukosuko wa ghafla', shirika la ndege la Singapore lasema
- Wapalestina saba wauawa katika uvamizi wa Israel Ukingo wa Magharibi
- Euro 2024: Rashford & Henderson waachwa nje ya kikosi cha England
- Mali: Profesa afungwa jela kwa kukosoa utawala wa kijeshi
- Salah adokeza kusalia Liverpool baada ya uteuzi wa Slot
- 'Alikuwa mvulana asiyejua alichokuwa akifanya na kumfuata tu babake' - Mama wa mtoto wa Christian Malanga
- Mtu mmoja afariki baada ya ndege ya Singapore Airlines kukumbwa na msukosuko
- Mahakama yaahidi kukabiliana na wanaotoa matusi mtandaoni dhidi ya rais wa Iran
- Kesi ya kundi la Ujerumani linalotuhumiwa kupanga mapinduzi yaendelea kusikilizwa
- Yatakayotokea ndani ya siku tano za maombolezo nchini Iran
- Waziri Mkuu Uingereza aahidi kulipa fidia waathiriwa wa sakata ya damu yenye maambukizi
- Kijana muuaji aliyenunua mapanga 79 mtandaoni atajwa jina lake
- Korea Kusini yapiga marufuku wimbo wa 'kumtukuza' Kim Jong Un
- Iran yatangaza siku tano za maombolezo ya kifo cha rais wake
- Netanyahu ashutumu ombi la kumkamata juu ya vita vya Gaza
Moja kwa moja
Asha Juma & Ambia Hirsi
Ndege ilipata 'msukosuko wa ghafla', shirika la ndege la Singapore lasema
Shirika la ndege la Singapore limetoa taarifa zaidi kuhusu idadi ya abiria waliojeruhiwa.
Inasema safari ya ndege kutoka Singapore kwenda London ilikumbana na "msukosuko mkubwa wa ghafla" kwenye Bonde la Irrawaddy (Myanmar) kwa umbali wa futi 37,000 (11,300m) takriban saa 10 baada ya kuondoka.
Rubani alitangaza dharura ya matibabu na kuelekeza ndege hiyo hadi Bangkok.
Kufikia 19:50 saa za Singapore (11:50 GMT), watu 30 tunapokea matibabu hospitalini Bangkok.
Abiria na wafanyakazi waliosalia walikuwa wakichunguzwa na kupewa matibabu, inapobidi, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Suvarnabhumi, shirika la ndege lilisema.
"Shirika la ndege la Singapore linatoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu.
Tunaomba radhi kwa hali ngumu iliyowakumba abiria na wafanyakazi wetu kwenye safari hii ya ndege.
Tunatoa usaidizi wote muhimu katika wakati huu mgumu," inaongeza
Wapalestina saba wauawa katika uvamizi wa Israel Ukingo wa Magharibi

Chanzo cha picha, afp
Wapalestina saba, akiwemo daktari, wameuawa na wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni huko Jenin kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, wizara ya afya ya Palestina imesema.
Dk Aseed Jabareen, daktari wa upasuaji mwenye umri wa miaka 50 katika Hospitali ya Serikali ya Jenin, aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa njiani kuelekea kazini, kulingana na wizara hiyo.
Vyombo vya habari vya Palestina pia vilisema kijana mdogo aliuawa akiwa anaendesha baiskeli. Jeshi la Israel limesema linachunguza ripoti hizo.
Hapo awali, ilitangaza kuwa imeanza operesheni ya kukabiliana na ugaidi huko Jenin - na kwamba watu wenye silaha walikuwa wamepigwa risasi.
Kumekuwa na ongezeko la ghasia katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, vilivyochochewa na shambulio baya la Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba.
Umoja wa Mataifa unasema takriban Wapalestina 480 - wanachama wa makundi yenye silaha, washambuliaji na raia - wameuawa katika matukio yanayohusiana na migogoro katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki.
Waisraeli kumi, wakiwemo maafisa sita wa vikosi vya usalama, pia wameuawa katika Ukingo wa Magharibi.
Wizara ya afya ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi ilisema watu saba wameuawa na tisa kujeruhiwa, wawili kati yao vibaya, na moto wa Israeli wakati wa operesheni ya Jumanne asubuhi huko Jenin.
Majeruhi pekee iliyomtaja ni Dk Jabareen, ambaye ilisema vikosi vya Israel vilimpiga risasi alipokuwa akisafiri kwenda kazini katika Hospitali ya Serikali ya Jenin, ambako alikuwa daktari wa upasuaji.
Wizara hiyo ilishutumu vikosi vya Israel kwa kumuua daktari huyo kimakusudi.
Shirika rasmi la habari la Palestina Wafa liliripoti kwamba mvulana wa shule katika darasa la 9, Mahmoud Hamadna, aliuawa alipokuwa akiendesha baiskeli kupitia Jenin.
Pia unaweza kusoma:
Euro 2024: Rashford & Henderson waachwa nje ya kikosi cha England

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Marcus Rashford (kushoto) na Jordan Henderson wamekuwa tegemeo katika kikosi cha England kwa miaka mingi Marcus Rashford na Jordan Henderson wameachwa nje ya kikosi cha muda cha wachezaji 33 cha England kilichoteuliwa na kocha Gareth Southgate kwa ajili ya michuano ya Euro 2024.
Rashford, 26, mshambuliaji wa klabu ya Manchester United amekuwa na wakati mgumu katika kuwa na kiwango kizuri msimu huu, akifunga mabao saba na kusimamia mabao mawili katika mechi 33 za ligi.
Rashford alicheza katika mechi saba za England msimu huu kabla ya kuachwa nje dhidi ya Ubelgiji mwezi Machi, na sasa ameondolewa kwenye kikosi cha mazoezi cha Southgate.
Henderson alijiunga na Al-Ettifaq ya Saudi Arabia akitokea Liverpool majira ya kiangazi mwaka jana lakini aliwaacha na kujiunga na Ajax ambayo ilikuwa na matatizo mwezi Januari
Southgate aliendelea kumjumuisha katika timu ya taifa ha baada ya kuhamia ligi kuu ya Saudia, ingawa alizomewa na baadhi ya mashabiki wa England kwenye mchezo wake wa kwanza kurejea nchini, dhidi ya Australia katika Uwanja wa Wembley mwezi Oktoba, jambo ambalo meneja huyo wa Uingereza alisema wakati huo "halikuwa na msingi".
Henderson alikuwepo kwenye kikosi kilichocheza mechi za kirafiki mwezi Machi dhidi ya Brazil na Ubelgiji lakini hakucheza.
Pia soma:
Mali: Profesa afungwa jela kwa kukosoa utawala wa kijeshi

Chanzo cha picha, AFP
Mwanauchumi na profesa maarufu wa Mali amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, kwa ukosoaji wake dhidi ya utawala wa kijeshi.
Étienne Fakaba Sissoko pia aliamriwa kulipa faini ya dola 4,900 za Kimarekani.
Msomi huyo mwenye umri wa miaka 41, ambaye amekuwa kizuizini tangu Machi, alishtakiwa kwa kukashifu na kuharibu sifa ya serikali kwa kusambaza habari ghushi.
Mashtaka hayo yanahusiana na kitabu alichochapisha mwaka jana, ambacho alikitetea mahakamani, akisema kazi hiyo ilitokana na ukweli.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kesi yake ni ya hivi punde zaidi katika ukandamizaji ulioenea dhidi ya wakosoaji na wapinzani wa kisiasa wa watawala hao wa kijeshi.
Waliingia madarakani mnamo Agosti 2020 wakati Rais wa wakati huo Ibrahim Boubacar Keïta alipoondolewa katika mapinduzi baada ya maandamano makubwa ya kuipinga serikali kuhusu jinsi alivyoshughulikia machafuko ya wanajihadi.
Salah adokeza kusalia Liverpool baada ya uteuzi wa Slot

Chanzo cha picha, Getty Images
Nahodha wa timu ya taifa ya Misri Mohamed Salah amedokeza kuwa atasalia Liverpool msimu ujao baada ya kuteuliwa kwa Arne Slot kama meneja mpya wa klabu hiyo.
Liverpool ilikataa ofa ya pauni milioni 150 kutoka kwa Al-Ittihad kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 Septemba mwaka jana, na mshambuliaji huyo tena amehusishwa na kuhamia Saudi Arabia.
Salah alifunga mabao 25 katika mechi 44 katika mashindano yote msimu huu lakini zawadi pekee ambayo timu hiyo ya Anfield ilipata kwenye kampeni ya mwisho ya Jurgen Klopp kuinoa ilikuwa Kombe la Ligi.
"Tunajua kwamba mataji ndiyo yanayotegemewa na tutafanya kila tuwezalo kufanya hivyo msimu ujao," Salah aliandika kwenye X.
"Mashabiki wetu wanastahili na tutapigana kama kuzimu."
Salah amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Liverpool na, baada ya ofa ya Al-Ittihad kukataliwa mwaka jana, mkurugenzi wa soka wa Saudi Pro League Michael Emenalo alisema mlango haujafungwa kwa Mmisri huyo.
Cristiano Ronaldo, Neymar, Karim Benzema na Riyad Mahrez ni miongoni mwa wachezaji mashuhuri ambao wamehamia Saudi Arabia katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.
Salah pia alituma ujumbe wa shukrani kwa Klopp, ambaye aliwaongoza The Reds kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia la Vilabu mnamo 2019 na taji la Ligi Kuu mnamo 2019-20.
"Ilikuwa nzuri kushiriki nawe makombe hayo yote na uzoefu katika kipindi cha miaka saba iliyopita," Salah alisema
"Nakutakia kila la heri na natumai tutakutana tena." Salah alitofautiana hadharani na Klopp wakati akijiandaa kuingia kama mchezaji wa akiba wakati wa droo yao dhidi ya West Ham mwezi uliopita, lakini Mjerumani huyo alisema hoja hiyo "ilitatuliwa" mwanzoni mwa Mei.
Liverpool walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi ya Premia msimu huu, pointi tisa nyuma ya mabingwa Manchester City, na Salah alifunga mabao 18 kwenye ligi hiyo ilikuwa chini yake tangu ajiunge na Roma mwaka 2017.
'Alikuwa mvulana asiyejua alichokuwa akifanya na kumfuata tu babake' - Mama wa mtoto wa Christian Malanga

Chanzo cha picha, MARCEL MALANGA/FACEBOOK
Familia ya Christian Malanga inaendelea kueleza hisia zao baada ya shambulio la siku ya Jumapili ambalo alifichua kuwa lilikuwa ni jaribio la 'kuvuruga mamlaka' nchini DR Congo, ambapo alimtambua mwanawe Marcel Malanga kuhusika katika shambulio hilo.
Brittney Sawyer, mamake Marcel Malanga, alitangaza kwenye Facebook kwamba anasikitika kwa wale wanaomtumia picha za mwanawe.
Jeshi la DR Congo lilitangaza kuwa Christian Malanga alipigwa risasi na kuuawa katika ofisi ya mkuu wa nchi baada ya kukataa kujisalimisha kwa vikosi vya usalama.
Marcel Malanga ni miongoni mwa takriban watu 50 waliokamatwa na jeshi, wakiwemo Wamarekani watatu, na raia mmoja wa Uingereza, kulingana na msemaji wa jeshi Brigedia Jenerali Sylavin Ekenge.
Duru za habari zinasema kuwa wale waliokamatwa kwenye Mto Kongo mjini Kinshasa walivua sare zao za kijeshi na kutaka kuvuka mto huo ili watoke DR Congo.
Video mbalimbali zinamuonyesha Marcel Malanga akiwa na mmoja wa Wamarekani hao na wengine waliotekwa na askari waliowatoa kwenye kile kinachoonekana kuwa kinamasi.
Hawa wanatuhumiwa kujaribu kupindua serikali katika shambulio walilofanya mapema Jumapili, shambulio la Christian Malanga 'Live' kwenye 'ukurasa' wake wa Facebook walipokuwa wakiteka ofisi ya rais wa DR Congo mjini Kinshasa.
Brittney Sawyer, Mmarekani ambaye ana watoto - ikiwa ni pamoja na Marcel - na Christian Malanga, aliandika: "Huyu alikuwa mvulana ambaye hakujua alichokuwa akifanya na alimfuata baba yake." Anaongeza: “Nimechoshwa na picha zinazosambazwa na wanazonitumia. Mungu atawasimamia!...”
Soma pia:
Habari za hivi punde, Mtu mmoja afariki baada ya ndege ya Singapore Airlines kukumbwa na msukosuko

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya maktaba ya Boeing 777-300ER Abiria mmoja amefariki na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa baada ya ndege ya shirika la ndege la Singapore kutoka London kuelekea Singapore kukumbwa na msukosuko mkubwa.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777-300ER iliyokuwa inaenda Singapore ilielekezwa Bangkok na kutua saa kumi kasoro robo kwa saa za ndani (08:00 GMT).
Ndege hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 211 na wafanyakazi 18, shirika hilo la ndege lilisema katika taarifa yake.
"Singapore Airlines inatoa rambirambi zake za dhati kwa familia ya marehemu," ilisema.
Shirika hilo la ndege liliongeza kuwa linashirikiana na mamlaka ya Thailand kutoa usaidizi wa kimatibabu kwa abiria, na lilikuwa linatuma timu Bangkok kutoa usaidizi wowote wa ziada unaohitajika
Mamlaka ya Thailand imetuma ambulensi na timu za dharura kwenye Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi.
Waziri wa Uchukuzi wa Singapore Chee Hong Tat alisema serikali itatoa msaada kwa abiria na familia zao.
"Nimehuzunishwa sana na tukio kwenye ndege ya Singapore Airlines SQ321 kutoka London Heathrow hadi Singapore," alichapisha taarifa kwenye mtandao wa Facebook.
Bado haijabainika ni nini hasa kilitokea kwenye ndege hiyo.
Mahakama yaahidi kukabiliana na wanaotoa matusi mtandaoni dhidi ya rais wa Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Magazeti ya Iran yenye picha za hayati Rais wa Iran Ebrahim Raisi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Iran, Mohammad Kazem Movahhed Azad, ameamuru kuchukuliwa hatua kali dhidi ya watumiaji wa mtandao wanaochapisha "matusi" dhidi ya marehemu rais na wengine waliofariki katika ajali ya helikopta.
Azad alianza kutoa wito wa kukamatwa kwa watu hao siku ya Jumatatu, muda mfupi baada ya rais Ebrahim Raisi kuthibitishwa kufariki.
Wakati watumiaji wanaounga mkono taasisi hizo wamekuwa wakisambaza ujumbe wa maombolezo kwenye mitandao ya kijamii, vile vile kumekuwa na wale wanaorusha cheche za matusi wakisisitiza madai ya kuwa Raisi alihusika katika mauaji ya maelfu ya wafungwa wa kisiasa katika miaka ya 1980 na kukandamiza kwa nguvu maandamano ya kuipinga serikali, huku baadhi wakieleza furaha yao juu ya kifo chake.
Muda mfupi baada ya habari za kuanguka kwa helikopta hiyo kuanza kuripotiwa Jumapili usiku, baadhi ya watumiaji mtandaoni walianza kusambaza video za fataki nchini Iran, wakionekana kusherehekea kifo cha rais kabla ya kuthibitishwa.
Wengine walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kushangilia timu ya uokoaji ikikabiliwa na hali ngumu wakati wakitafuta eneo la ajali.
Soma zaidi:
Kesi ya kundi la Ujerumani linalotuhumiwa kupanga mapinduzi yaendelea kusikilizwa

Chanzo cha picha, Reuters
Kesi ya kundi moja nchini Ujerumani linalodaiwa kupanga njama ya mapinduzi inaendelea kusikilizwa.
Kundi hilo linadaiwa kuwa na uhusiano na kile kinachoitwa vuguvugu la Reichsbürger na wale wanaoshutumiwa kuwa viongozi wakitarajiwa kufika mbele ya majaji.
Watu hao wanasemekana kupanga njama ya kupindua serikali ya Ujerumani kwa nguvu.
Wachunguzi wanadai kwamba watu hao waliamini kuwa nchi hiyo ilikuwa inaongozwa na "mfumo fulani wa kisiri".
Kesi hiyo itakayosikilizwa mjini Frankfurt siku ya Jumanne ndiyo inayoongoza katika kesi tatu kufuatia uvamizi wa kitaifa mnamo 2022.
Kesi hiyo inaonekana kuwa muhimu sana kwa sababu ya ukubwa wake na maelezo ambayo inaweza kutoa kwenye mitandao ya mrengo wa kulia.
Reichsbürger, ni kundi linakanusha uhalali wa serikali ya kisasa ya Ujerumani - hata kudai kuwa iliwekwa na Washirika wenye nguvu baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Ujasusi wa ndani umekadiria kuwa karibu watu 23,000 wanafuata vuguvugu hilo ambalo linaonyesha "mitazamo ya chuki" na "uhusiano wa juu" wa silaha.
Yatakayotokea ndani ya siku tano za maombolezo nchini Iran

Chanzo cha picha, EPA
Iran inapanga kufanya misafara kadhaa ya maombi kwa ajili ya Rais Ebrahim Raisi na maafisa wengine waliofariki katika ajali ya helikopta.
Msafara wa kwanza umeanza leo saa 09:30 kwa saa za huko (06:00 GMT) katika jiji la kaskazini-magharibi la Tabriz.
Makamu wa Rais wa Masuala ya Utendaji Mohsen Mansouri alieleza katika mahojiano na IRINN kwamba mwili wa Raisi kisha utahamishwa hadi katika mji wa kidini wa Qom, ambako raia watakuwa na fursa ya kuuaga saa 16:30 kwa saa za huko (13:00 GMT).
Miili hiyo itapelekwa katika mji mkuu wa Tehran, Mansouri anasema, akiongeza kuwa ibada itafanyika huko siku ya Jumatano, huku Kiongozi Mkuu Khamenei akiongoza maombi ya jamaa kwa Raisi na wengine.
Jumatano pia imetangazwa kuwa siku ya mapumziko nchini Iran.
Kwa mujibu wa Mansouri, mwili wa Raisi baadaye utahamishwa Alhamisi asubuhi hadi Birjand, mji mkuu wa jimbo la Khorasan Kusini, ambako rais alikuwa amechaguliwa tena kuwa mwakilishi wa baraza la waangalizi wa uongozi Bunge la Wataalamu.
Ibada ya mazishi ya Raisi itafanyika katika mji wa kaskazini-mashariki wa Mashhad, katika makaburi ya Imamu wa nane wa Shia Reza siku ya Alhamisi jioni.
Soma zaidi:
Waziri Mkuu Uingereza aahidi kulipa fidia waathiriwa wa sakata ya damu yenye maambukizi

Chanzo cha picha, PA Media
Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ameahidi kulipa "fidia" kwa watu walioathiriwa na kashfa ya damu yenye maambukizi.
Waziri mkuu alisema serikali italipa "chochote itakachogharimu" kufuatia ripoti juu ya kashfa hiyo, ambayo watu 30,000 wameambukizwa.
Uchunguzi wa umma uligundua kuwa mamlaka iliwaweka waathirika katika hatari isiyokubalika na kuficha maafa makubwa ya matibabu katika Huduma ya Afya ya Taifa.
Serikali itaweka maelezo ya fidia siku ya Jumanne.
Serikali itaweka maelezo ya fidia siku ya Jumanne.
Mawaziri wameripotiwa kutenga karibu £10bn kwa kifurushi cha fidia.
Uchunguzi wa damu Iliyoambukizwa ilishutumu madaktari, serikali na Huduma ya Afya ya Taifa kwa kuruhusu wagonjwa kuambukizwa virusi vya ukimwi na homa ya ini walipokuwa wakipokea huduma ya Huduma ya Afya ya Taifa kati ya miaka ya 1970 na 1990.
Takriban 3,000 wamefariki na vifo zaidi vitaendelea kutokea kutokana na Sakata hiyo.
Kijana muuaji aliyenunua mapanga 79 mtandaoni atajwa jina lake

Chanzo cha picha, Polisi wa Bedfordshire
Jaji wa Mahakama ya Juu ameamua kuwa umma unafaa kuambiwa jina la kijana mfanyabiashara wa dawa za kulevya ambaye alinunua visu 79 na mapanga katika miezi kadhaa kabla ya kumdunga mtu na kumuua.
Bi Justice Foster ameondoa amri ambayo iliwazuia wanahabari kufichua utambulisho wa Rayis Nibeel mwenye umri wa miaka 17, ambaye amepatikana na hatia ya kumuua Omar Khan mwenye umri wa miaka 38 huko Luton.
Amri ilikuwa imetolewa chini ya sheria iliyolenga kuwalinda watoto na vijana wanaohusika katika kesi mahakamani.
Lakini jaji ameondoa amri hiyo baada ya BBC kuhoji kuwa kufichua jina la Nibeel ni kwa manufaa ya umma.
Mapema mwaka huu majaji walikuwa wamempata Nibeel na kijana mwingine, Umer Choudhury mwenye umri wa miaka 18, na hatia ya kumuua Bw Khan, ambaye alishambuliwa kwa kisu cha cha inchi 15 (sentimita 37.5).
Walikuwa wamesikia jinsi Bw Khan, wa Leicester Road, Luton, alivyofariki katika eneo la shambulio katika eneo la Sundon Park eneo la Luton mnamo Septemba 16, 2023, baada ya kuzuka kwa mzozo wa dawa za kulevya.
Bi Justice Foster aliwafunga vijana wote wawili siku ya Ijumaa wakati wa kusikilizwa kwa hukumu katika Mahakama ya St Albans Crown.
Alisema Nibeel, wa Butely Road, Luton, atatumikia kifungo kisichopungua miaka 20 na Choudhury, wa Tulip Close, Luton, kifungo kisichopungua miaka 18.
Pia unaweza kusoma:
Korea Kusini yapiga marufuku wimbo wa 'kumtukuza' Kim Jong Un

Chanzo cha picha, Reuters
Korea Kusini imesema itapiga marufuku wimbo wa propaganda wa Korea Kaskazini unaomsifu dikteta wa Pyongyang Kim Jong Un kama "baba rafiki" na "kiongozi mkuu".
Mdhibiti wa vyombo vya habari wa Seoul alisema video hiyo ya muziki, ambayo imekuwa maarufu kwenye TikTok tangu ilipotolewa Aprili, ni ukiukaji wa Sheria ya Usalama wa Kitaifa ya nchi hiyo.
"[Wimbo huo] unamsifu na kumtukuza Kim Jong Un," Tume ya Mawasiliano ya kuangazia Ubora ya Seoul ilisema katika taarifa siku ya Jumatatu.
Sheria ya Usalama inazuia ufikiaji wa tovuti na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini, na inaadhibu tabia na hotuba zinazopendelea utawala huo.
Toleo la 29 la video ya wimbo wa Baba Rafiki itazuiwa, tume ilisema, lakini haikufafanua jinsi hilo lingetekelezwa. Uamuzi huo ulichochewa na ombi kutoka Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi ya Korea Kusini, iliongeza.
"Video hiyo ni maudhui ya kawaida yanayohusishwa na vita vya kisaikolojia dhidi ya Korea Kusini, na ilichapishwa kwenye kituo kinachoendeshwa ili kufahamika kwenye ulimwengu wa nje na inalenga zaidi kumtukuza Kim," mdhibiti alisema.
Soma zaidi:
Iran yatangaza siku tano za maombolezo ya kifo cha rais wake

Chanzo cha picha, Reuters
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ametangaza siku tano za maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa nchi hiyo, Ebrahim Raisi.
Bw Raisi alifariki dunia katika ajali ya helikopta eneo la milima kaskazini-magharibi mwa Iran, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian.
Vyombo vya habari vya serikali vilithibitisha kuwa alifariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka siku ya Jumapili.
Ayatullah Khamenei alisema ametoa rambirambi zake "kwa watu wapenzi wa Iran".
Bw Raisi, mwenye umri wa miaka 63, alikuwa ametajwa kuwa mrithi wa kiongozi mkuu.
Vyombo vya habari vya serikali vilisema uchaguzi utafanyika tarehe 28 Juni ili kuchagua rais mpya.
Wakati huo huo, makamu wa Rais Mohammad Mokhber ameteuliwa kushika madaraka ya muda.
Baraza la mawaziri la Iran pia limemteua naibu waziri wa mambo ya nje Ali Bagheri Kani kuwa kaimu waziri wa mambo ya nje.
Soma zaidi:
Netanyahu ashutumu ombi la kumkamata juu ya vita vya Gaza

Chanzo cha picha, EPA
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemkashifu kwa hasira mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kutafuta hati ya kukamatwa kwake pamoja na viongozi wa Hamas kuhusu madai ya uhalifu wa kivita katika mzozo wa Gaza.
Bw Netanyahu alisema alikataa kwa kuchukizwa na kwamba "Israel ya kidemokrasia" imelinganishwa na kile alichokiita "wauaji wa halaiki".
Maoni ya Bw Netanyahu yameungwa mkono na Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye alisema hakuna usawa kati ya Israel na Hamas.
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Karim Khan, alisema kuna sababu za kuridhisha za kuamini kuwa Bw Netanyahu na Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant waliwajibika kwa uhalifu katika uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
ICC pia inatafuta kibali cha kukamatwa kwa kiongozi wa Hamas huko Gaza, Yahya Sinwar, kwa uhalifu wa kivita.
Israel na Marekani, mshirika wake mkuu, si wanachama wa ICC, ambayo ilianzishwa mwaka 2002.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 21/05/2024
