Je, Trump anaweza kugombea urais baada ya kukutwa na hatia?

Trump

Chanzo cha picha, Reuters

Donald Trump amekuwa rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kutiwa hatiani kwa mashtaka ya jinai, baada ya jopo maalum la mahakama mjini New York kumpata na hatia katika mashtaka yote 34 dhidi yake.

Mashtaka hayo yote yanahusiana na kughushi rekodi za biashara yake ili kuficha malipo aliyolipwa nyota wa zamani wa filamu za ngono Stormy Daniels ili kumshurutisha kutosema lolote kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2016.

Sasa ni nini kitafuata baada ya uamuzi huu?

Haya hapa ni baadhi ya masuala muhimu ya kuzingatia.

Bado anaweza kugombea urais?

Ndio. Katiba ya Marekani inaweka masharti machache ya kustahiki kwa wagombeaji urais: lazima wawe na angalau miaka 35, wawe raia wa Marekani "wazaliwa asili" na wameishi Marekani kwa angalau miaka 14. Hakuna sheria zinazozuia wagombea walio na rekodi za uhalifu.

Lakini uamuzi huu wa hatia bado unaweza kuathiri uchaguzi wa urais wa Novemba. Kura ya maoni kutoka kwa Bloomberg na Morning Consult mapema mwaka huu iligundua kuwa 53% ya wapiga kura katika majimbo muhimu yanayoweza kuamua mshindi wa uchaguzi wangekataa kumpigia kura mgombea wa Republican ikiwa atapatikana na hatia.

Kura nyingine ya maoni, kutoka Chuo Kikuu cha Quinnipiac mwezi huu, ilionyesha 6% ya wapiga kura wa Trump wangekuwa na uwezekano mdogo wa kumpigia kura - hatua ambayo itaathiri matokeo katika kinyang'anyiro kikali kama hicho.

Soma pia:

Trump atafanya nini sasa?

Trump amekuwa huru kwa dhamana wakati wote wa kesi na hili halikubadilika baada ya hukumu kusomwa siku ya Alhamisi - Mrepublican huyo aliachiliwa kwa kujitambua kwake.

Atarejea kortini tarehe 11 Julai - tarehe ambayo Hakimu Juan Merchan amepanga kusikilizwa kwa hukumu.

Jaji atakuwa na mambo kadhaa ya kuzingatia katika hukumu, ikiwa ni pamoja na umri wa Trump.

Hukumu hiyo inaweza kuhusisha faini, muda wa majaribio au usimamizi, au pengine kifungo.

Stormy Daniels

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mawakili wa Trump wanaweza kutumia ushahidi wa Stormy Daniels kama msingi wa kukata rufaa

Trump, ambaye aliita uamuzi huo kuwa wa "fedheha", bila shaka atakata rufaa, mchakato ambao unaweza kuchukua miezi kadhaa au hata zaidi.

Mawakiliwake watakabiliana na Kitengo cha Rufaa huko Manhattan, na ikiwezekana Mahakama ya Rufaa.

Hii yote ina maana kwamba hata baada ya kuhukumiwa itakuwa vigumu sana Trump aondoke mahakamani akiwa amefungwa pingu, kwani angetarajiwa kusalia huru kwa dhamana huku akikata rufaa.

Je, Trump anaweza kutumia hoja gani kukata rufaa?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ushahidi wa nyota wa filamu za ngono, Bi Stormy Daniels, ambaye madai yake ya kujamiiana na Trump yalikuwa ndiyo msingi wa kesi hiyo, unaweza kuwa miongoni mwa hoja za rufaa.

"Kiwango cha undani wa maelezo yaliyotolewa [na Bi Daniels] hakikuwa cha lazima kufikiwa katika kueleza kile kilichotokea," ameeleza Anna Cominsky, profesa katika Shule Kuu ya Sheria ya New York.

"Kwa upande mmoja, maelezo yake yanamfanya aaminike na ukiwa kama mwendesha mashtaka, unataka shahidi wako atoe maelezo ya kutosha ili baraza la wazee la mahakama liweze kuamini anachosema. Kwa upande mwingine, maelezo hayo yanaweza kuvuka mstari, na kuonekana kupoteza maana na yenye kuchochewa na chuki."

Mawakili wa utetezi ya Trump mara mbili walitoa hoja za kutupiliwa mbali kwa mashtaka wakati Bi Daniels akitoa ushahidi, hoja ambazo zilikataliwa na Jaji.

Zaidi ya hayo, mkakati mpya wa kisheria uliotumiwa na chukuliwa na Mwendesha Mashtaka katika kesi hii unaweza pia kutoa mwanya wa kukata rufaa.

Kughushi rekodi za biashara kunaweza kuwa kosa la kiwango cha chini katika jimbo la New York, lakini Trump alikabiliwa na mashtaka mazito zaidi kwa sababu ya madai ya kosa lengine la uhalifu unaodaiwa kuwa ni jaribio haramu la kushawishi uchaguzi wa 2016.

Waendesha mashtaka walidai kwa ujumla wake kwamba ukiukaji wa sheria za uchaguzi za nchi na jimbo, pamoja na ulaghai wa kodi, ulikuwa sehemu ya mashtaka katika kesi hii. Lakini hawakuwaelezea wazee wa baraza wa mahakama ni jambo lipi haswa lililokiukwa.

Wataalamu wa sheria wanasema kuna maswali kuhusu upeo na matumizi ya sheria ya serikali ya shirikisho ambayo yanaweza kuunda msingi wa kukata rufaa. Haikuwahi kutokea huko nyuma ambapo mwendesha mashtaka wa jimbo, kujenga kesi yake kwa kutumia mashtaka ambayo hayajawahi kushtakiwa chini ya sheria za shirikisho. Kuna swali pia kama Mwendesha mashtaka wa wilaya ya Manhattan alikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.

Je, Trump anaweza kufungwa gerezani?

Inawezekana kwa mujibu wa sheria, ingawa kiuhalisia hakuna uwezekano kumuona Trump akitumikia kifungo gerezani.

Mashtaka yote 34 aliyokabiliwa nayo ni ya daraja la E kwa sheria za jimbo la New York, ambalo ndio daraja la chini zaidi. Kila shtaka hubeba kifungo cha juu cha miaka minne.

Kuna sababu kadhaa ambazo Jaji Merchan anaweza kuchagua kwa nini ampe Trump adhabu ndogo, ikiwa ni pamoja na umri wake mkubwa, kutokuwa na makosa mengine ya uhalifu, na uhalisia kuwa mashtaka yake yanahusisha uhalifu usiotumia mabavu.

Inawezekana pia kwamba jaji ataangazia uhalisia wa kihistoria unaozunguka kesi hii ambao haujawahi kushuhudiwa hapo awali, na hivyo kuamua kukwepa kumfunga rais wa zamani na mgombea urais wa sasa.

Pia kuna swali la uhalisia wa kifungo kitakuwaje. Trump, kama marais wote wa zamani, ana haki ya kulindwa maisha yote na makachero wa idara ya Secret Service. Hii ina maana kwamba, akifungwa , baadhi ya makachero watahitajika kumlinda ndani ya gereza.

Hata hivyo, itakuwa vigumu sana kuendesha mfumo wa magereza na rais wa zamani kama mfungwa. Itakuwa hatari kubwa ya usalama na gharama kubwa kumweka salama.

"Mifumo ya magereza inajali mambo mawili makuu: usalama wa taasisi na kupunguza gharama za uendeshaji," amesema Justin Paperny, mkurugenzi wa kampuni ya ushauri ya magereza ya White Collar Advice.

Kuwa na Trump gerezani, "itakuwa onesho la kutisha ... hakuna askari jela ambaye angeruhusu tukio hilo kutokea", alisema.

Je, Trump anaweza kupiga kura?

Kuna uwezekano mkubwa kwamba Trump atapiga kura baadae mwezi Novemba mwaka huu.

Sheria katika jimbo la Florida – ambapo Trump anaishi – zinamzuia mtu aliyekutwa na hatia katika jimbo lengine kupiga kura endapo, "ikiwa hatia hiyo ingemfanya mtu huyo kutostahili kupiga kura katika jimbo ambalo mtu huyo alitiwa hatiani".

Trump amepatikana na hatia jimboni New York, ambako wahalifu wanaruhusiwa kupiga kura mradi tu hawajafungwa gerezani.

Hii inamaanisha kuwa, endapo Trump hatakuwa gerezani siku ya Novemba 5, basi atakuwa hajapoteza sifa ya mpiga kura.

Je, anaweza 'kujisamehe'?

Hapana. Marais wa Marekani wanaweza kutoa msamaha kwa watu waliokutwa na hatia ya kufanya makosa yaliyo chini ya sheria za serikali ya shirikisho. Tuhuma ambazo Trump amekutwa na hatia zilikuwa katika kesi ya jimbo la New York. Hivyo hata akishinda urais baadae mwaka huu hatakuwa na mamlaka yoyote na tuhuma hizo.

Hali hiyo pia itamkumba katika kesi yake ya uchaguzi huko jimboni Georgia, ambako ameshutumiwa kwa kula njama ya kihalifu ya kupindua matokeo ya kushindwa kwake na Rais Joe Biden katika jimbo hilo wakati wa uchaguzi wa 2020. Kesi hii kwa sasa ipo katika hatua za rufani.

Matumizi ya mamlaka yake ya kutoa msamaha kwa wahalifu yatajaribiwa katika kesi mbili za shirikisho zinazomkabili. Mosi ni madai ya kuvunja sheria ya kuhifadhi nyaraka za siri za serikali na pili kula njama ya kutengua uchaguzi wa 2020.

Katika kesi ya kwanza, jaji aliyeteuliwa na Trump huko Florida ameahirisha kesi hiyo kwa muda usiojulikana, akisema kuweka tarehe ya kusikilizwa kesi kabla ya kusuluhisha maswali kuhusu ushahidi itakuwa "si busara".

Kesi ya pili ambayo ni ya uchaguzi nayo imecheleweshwa ili kupisha kusikilizwa kwa rufaa iliyowasilishwa na Trump.

Hakuna uwezekano wa kesi yeyote katika hizo mbili kusikilizwa na kuamuliwa kabla ya uchaguzi wa Novemba, lakini hata kama hilo lingetokea, wataalamu wa katiba hawakubaliani ikiwa mamlaka ya msamaha ya rais yanajumuisha kujisamehe yeye mwenyewe. Trump anaweza kuwa wa kwanza kujaribu kujisamehe.

Pia unaweza kusoma:

Mhariri: Athman Mtulya