Kwa nini Trump ni maarufu miongoni mwa Republican?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mpende au umchukie, amerudi.
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameimarisha ushawishi wake kama mgombea wa urais wa chama cha Republican 2024, kufuatia ushindi wa kishindo huko Iowa.
Ushindi uliompa kura nyingi kuliko wagombea wengine wote kwa pamoja.
Iwapo Trump atapata uteuzi wa chama chake na kushinda uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 5 Novemba, atakuwa miongoni mwa maraisi wa Marekani kutawala, kisha kushindwa na baadaye kurejea mamlakani.
Rais wa mwisho kufanya hivyo alikuwa Grover Cleveland mwaka1892.
Ni siku za awalai katika kinyang'anyiro cha kuwa rais wa 60 wa Marekani, lakini ushindi ni ishara kwamba umaarufu wake unaendelea kudumu miongoni mwa Warepublican. Je, sababu ni nini?
Uchumi

Bei ya gesi ni mada kuu miongoni mwa wapiga kura wengi wa Republican
"Ataimarisha uchumi na bei ya gesitapungua," mfuasi wa Trump huko Iowa alisema, alipoulizwa kwa nini anataka kumuona rais huyo wa zamani akirudi ofisini.
Uchumi umekuwa ujumbe muhimu katika kampeni ya Trump. Mwanawe Eric Trump aliiambia BBC, "watu wanataka ustawi na nguvu kwa nchi hii.
"Baba yangu alijenga uchumi mkubwa zaidi katika historia ya taifa hili, ukosefu wa ajira ulipungua, mfumuko wa bei ulikuwa wa chini na bei ya gesi ilikuwa chini"
Ni kweli uchumi wa Marekani ulikuwa ukifanya vizuri wakati Trump kabla ya janga la corona. Kulikuwa na nyakati ambapo uchumi ulikuwa na nguvu zaidi na ilikuwa wa wakati wa utawala wa Rais Obama wa Demokratic.
Wakati wa Rais Biden, vita vya Ukraine vilisababisha gharama za nishati kupanda na mfumuko wa bei kuwa juu, ingawa sasa umeshuka sana na uchumi umeonekana kuwa na nguvu.
Trump na Sleepy Joe

Chanzo cha picha, Getty Images
Mfuasi wa Trump, Billy Blathras anamwona Trump kama "kiongozi mahiri". Anasema: "Tuliona alichokifanya katika muhula wake wa kwanza. Tunataka arudi tena. Nchi yetu imeporomoka wakati wa Rais Biden.”
Biashara na historia ya Trump, vinatajwa. Mfuasi mwingine huko Iowa anasema: "Nchi hii haihitaji kuongozwa na mwanasiasa mwingine, ninaamini mgombea bora ni anayejua jinsi ya kuendesha biashara."
Trump anaonekana na wafuasi wengi wa Republican kuwa tofauti kabisa na wa Rais Biden, ambaye wakosoaji wake walimpachika jina la "Sleepy Joe" baada ya kunaswa na kamera akisinzia wakati wa mkutano wa tabia nchi wa COP26.
Lakini mara ya mwisho wawili hao walipopambana, Biden alishinda.
Wahamiaji na wapinzani wa Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuzuia wahamiaji na kujenga ukuta mpakani na Mexico ilikuwa sehemu muhimu ya kampeni ya awali ya Trump ya urais
Trump aliposema wahamiaji "wanatia sumu damu ya nchi yetu" wakati wa mahojiano na chombo cha habari cha mrengo wa kulia cha The National Pulse mwezi Oktoba.
Rais Biden alimshutumu kutumia maneno kama ya wakati wa Ujerumani ya Wanazi.
Trump amesema, ikiwa atarudi ofisini, atawatafuta wale wote wanaompinga na kuwatowesha.
"Inalingana na lugha ya wakati wa Ujerumani ya Wanazi miaka ya 1930," Rais Biden alisema, kulingana n White House. "Na hata si mara ya kwanza."
Wanahistoria na wataalamu ambao wamechunguza propaganda za Wanazi waliiambia BBC, ulinganisho wa Rais Biden ulikuwa sahihi.
"Siyo tu kwamba kulikuwa na lugha kama hii wakati wa Ujerumani ya Wanazi, waliyoyasema ndiyo waliyoyafanya," anasema Anne Berg, mwanahistoria wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, akitoa mmfano wa mashambulizi ya Wanazi, mara tu walipochukua mamlaka, dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Kura za maoni za CBS zinaonyesha wafuasi sugu wa chama cha Republican waliunga mkono maoni yake.
CBS iliwauliza wapiga kura wa Republican waliojiandikisha ikiwa wanakubalina au hawakubaliani na kauli ya Trump.
Nusu ya waliohojiwa waliulizwa kuhusu kauli ya "kutia damu sumu" bila ya kuihusisha na mtu yeyote, huku nusu nyingine iliambiwa Trump ndio alisema.
Asilimia 72 walikubaliana na kauli hiyo bila ya kuhusishwa na Trump, na 82% walikubaliana na kauli hiyo ilipohusishwa na Trump. Kura hiyo inaeleza msimamo wake kuhusu uhamiaji unaendelea kuwavutia wafuasi wake.
Vijana wa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, wapiga kura vijana wanaweza kumsaidia Trump kuwa rais wa Marekani mwezi Novemba?
Kura ya maoni iliyochapishwa katikati ya mwezi wa Disemba na New York Times na Chuo cha Siena ilimuonyesha Trump yuko mbele ya Joe kwa asilimia sita miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 18 hadi 29.
Na hili linatokana na sera za Biden jinsi alivyoshughulikia vita vya Israel-Hamas, baadhi ya wataalamu wanaamini hivyo.
Mary Weston, mkuu wa kundi la Iowa Young Republicans, aliiambia BBC anadhani vijana wa Republican wanavutiwa na Trump kwa uwezo wake jukwaani:
Akiwa na umri wa miaka 23, akiwa chuo anasema watu wengi "walimdhihaki na kumnyanyasa" kwa kumuunga mkono Trump.
Weston anasema "Trump anasimama kwa kile anachoamini na haogopi na ndio sababu unawavutia wapiga kura vijana.’’
Kesi dhidi ya Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump amefunguliwa mashtaka ya jinai mara nne, na atakuwa na msururu wa kesi 2024 atakapowania tena kuingia Ikulu ya White House.
Ameshtakiwa New York na kufunguliwa mashtaka Georgia, Florida, Manhattan na Washington, na waendesha mashtaka wamefungua uchunguzi dhidi yake.
Kuna kesi pia katika majimbo kadhaa wakitaka kumuondoa Trump katika kinyang'anyiro cha urais, wakisema alihusika na uasi wakati wa ghasia katika Bunge la Marekani miaka mitatu iliyopita.
"Kila alipofunguliwa mashitaka ushawishi wake uliongezeka. Kila walipomtoa kwenye kinyanganyiro - huko Maine na Colorado - idadi ya wafuasi iliongezeka,” mtafiti mkongwe Frank Lance aliiambia BBC.
Kila unapoenda kwa Donald Trump, anaitumia. Hatujawahi kuona mtu yeyote Amerika. kama yeye."
Hata hivyo, inafaa kufahamu kwamba mafanikio ya Trump huko Iowa, wengi wana maoni tofauti - kama Judy, ambaye alisema: "Hafai, anachukiza kabisa. Sielewi kwa nini watu wangempigia kura."
Ikiwa Trump atateuliwa kuwa mgombea wa Republican bado ana kazi nyingi ya kufanya.
Anatarajiwa kukabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa balozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa Nikki Haley katika kura ya mchujo ya New Hampshire wiki ijayo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












