Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rwanda yakubaliana na Marekani kuchukua wahamiaji 250
Makubaliano yalioripotiwa kwa mara ya kwanza na Reuters, yalitiwa saini na maafisa wa Marekani na Rwanda mjini Kigali mwezi Juni, alisema afisa wa Rwanda, akitoa sharti la kutotajwa jina.
Muhtasari
- Wakaazi wa jiji la Sudan liliozingirwa wanakabiliwa na njaa, Umoja wa Mataifa waonya
- Nasa kuweka kinu cha nyuklia mwezini ifikapo 2030 - vyombo vya habari vya Marekani
- Netanyahu kuwasilisha mpango wa Israel kuiteka Gaza - Ripoti
- Maandamano yalipuka China kupinga unyanyasaji shuleni
- Mchezaji Thomas Partey anayekabiliwa na tuhuma za ubakaji aachiwa kwa dhamana
- Marekani yasitisha utoaji wa viza kwa raia wa Burundi juu ya 'ukiukaji wa mara kadhaa'
- Al-Shabab yadai kuwaua wanajeshi kadhaa wa Uganda nchini Somalia
- India yasema tishio la Trump juu ya mafuta ya Urusi 'sio halali'
- Uchafuzi wa plastiki kwa mazingira ni hatari kubwa inayoongezeka - Wataalamu wa afya waonya
- Marekani yashtumu kifungo cha nyumbani cha aliyekuwa rais wa Brazil
- Kupunguzwa kwa misaada kutatumbukiza Wanigeria kwenye mtego wa Boko Haram, UN yaonya
- 'Amesalia mifupa ya binadamu tu' kaka wa mateka wa Gaza ameiambia BBC
- Rwanda yafikia makubaliano na Marekani kuchukua hadi wahamiaji 250, Reuters inaripoti
Moja kwa moja
Ambia Hirsi & Asha Juma
Baraza la Katiba lathibitisha kuondolewa kwa kiongozi wa upinzani wa Cameroon kwenye uchaguzi wa rais
Baraza la Katiba la Cameroon limethibitisha kuenguliwa kwa kiongozi wa upinzani Maurice Kamto katika uchaguzi ujao wa rais, kwa kukataa ombi lake la kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kumuondoa kwenye orodha ya wagombea.
Uamuzi wa baraza hilo ambao ukitolewa muathiriwa hawezi kukata rufaa umetolewa leo, katika hatua muhimu kuelekea kampeni za uchaguzi.
"Uamuzi uliotolewa una uzito zaidi kwa upande wa kisiasa kuliko upande wa kisheria," alisema Hyppolyte Tiakouang, mmoja wa mawakili wanaomwakilisha Maurice Kamto.
Tume ya uchaguzi Elecam ilikuwa ilimuondoa kwenye orodha ya wagombea Kamto ambaye aliidhinishwa na chama cha MANIDEM, juu ya "wingi wa wagombea."
Mgombea mwingine kutoka upande unaopingana na chama hicho naye aliwasilisha ombi lake, jambo lililozua wasiwasi kuhusu uhalali wa uongozi wa chama hicho.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, Kamto aliyeonekana kusikitishwa na uamuzi huo aliondoka eneo hilo bila kuzungumza na waandishi wa habari.
Mawakili wake ambao walikataa kutoa maoni yao juu ya hatua yake inayofuata walisema mzee huyo wa miaka 71 ataamua jinsi ya kusonga mbele.
Wakaazi wa jiji la Sudan liliozingirwa wanakabiliwa na njaa, Umoja wa Mataifa waonya
Shirika maalum la chakula la Umoja wa Mataifa linasema família zilizokwama katika mji wa El Fasher nchini zinakabiliwa na baa la njaa.
Shirika la Chakula Duniani WFP linasema halijafanikiwa kupeleka chakula cha msaada mjini humo kwa zaidi ya mwaka mmoja , huku njia za biashara zikikatizwa na njia za msaada kuzuiwa.
Taarifa hii ya WFP imejiri siku chache tu baada ya mashirika ya kijamii kuripoti vifo vya watu kutokana na baa la njaa mwaka mmoja tangu wapiganaji wa Rapid Support forces kuuteka mji huo mkuu wa jimbo la Darfu ya Kaskazini.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa katika kanda ya afrika mashariki na kusini Eric Perdison, amesema watu wote wanaoishi mjini El Fashir wanakabiliwa na changamoto ya kuishi kutokana na baa la njaa.
Perdison amesema raia wa eneo hilo wamechoshwa na vita vilivyodumu kwa miaka miwili na kuongeza kuwa maisha yao yamo hatarini ikiwa hatua za dharura hazitachuliwa ili kuwapa misaada.
Mapigano kati ya RSF na jeshi la Sudan yameongezeka katika siku ya hivi karibuni hasa baada ya RSF kutimuliwa kutoka mji mkuu wa Khartoum.
Takwimu za Umoja wa Mataifa mwezi uliopita zilionyesha kuwa asilimia 38 ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano wanaoishi katika kambi za wakimbizi wa ndani mjini el fashir na viunga vyake wanakabiliwa na utapia mlo.
Shirika la WFP limesema vikwazo vya Usafiri vimesababisha bei ya vyakula kupanda maradufu katika masoko na kuwa bei ya bidhaa muhimu kama vile mtama na ngano imepanda kwa asilimia 500 nchini Sudan,
WFP imesema kuwa malori yake iliyosheheni vyakula na misaada mingine yako tayari kwenda katika eneo hilo ikiwa watahakikishiwa usalama wao.
Maelezo zaidi:
Nasa kuweka kinu cha nyuklia Mwezini ifikapo 2030 - vyombo vya habari vya Marekani
Shirika la anga za juu la Marekani Nasa litaharakisha mipango ya kujenga kinu cha nyuklia Mwezini ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani.
Ni ndoto ya Marekani kujenga makao ya kudumu kwa wanadamu kuishi kwenye uso wa mwezi.
Kulingana na Politico, kaimu mkuu wa Nasa alitaja mipango kama hiyo inayofanywa na China na Urusi na kusema nchi hizo mbili "zinaweza kuweka vikwazo" vya ufikiaji wa neo hilo la Mwezini.
Hata hiyo maswali yameibuka ikiwa ndoto ya Nasa itafikiwa ikizingatiwa hatua ya Marekani kuipunguzia bajeti yake, huku baadhi ya wanasayansi wakiwa na wasiwasi mpango huo unaendeshwa kwa lengo la kisiasa.
Mataifa yakiwemo Marekani, China, Urusi, India na Japan yako mbioni kuanzisha miradi Mwezi, huku baadhi yakipanga makazi ya kudumu ya watu.
Netanyahu kuwasilisha mpango wa Israel kuiteka Gaza - Ripoti
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kuwasilisha pendekezo la kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza atakapokutana na baraza lake la mawaziri la usalama, vyombo vya habari vya Israel vinasema.
"Uamuzi umefikiwa. Tunaenda kuuteka Ukanda wa Gaza - na kuwashinda Hamas," waandishi wa habari wa eneo hilo waliandika wakimnukuu afisa mkuu serikalini.
Akijibu ripoti kwamba mkuu wa jeshi na viongozi wengine wa kijeshi wanapinga mpango huo, afisa huyo ambaye hakutajwa jina alisema: "Ikiwa hilo halitafanyaka mkuu wa majeshi, anapaswa kujiuzulu."
Familia za mateka zinahofia mipango kama hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya wapendwa wao, huku 20 kati ya 50 wakiaminika kuwa hai huko Gaza, ,
Kura za maoni zinaonyesha kuwa watatu kati ya Waisraili wanne wanapendelea makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwarudisha mateka.
Washirika wa karibu wa Israel pia wanapinga hatua hiyo huku wakishinikiza kusitishwa kwa vita kama hatua ya kupunguza mzozo wa kibinadamu.
Ndani ya Israel kwenyewe, mamia ya maafisa wa usalama waliostaafu, wakiwemo wakuu wa zamani wa mashirika ya kijasusi, wametoa wito wa pamoja kwa Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatatu, kumuomba amshinikize Netanyahu amalize vita vya Gaza.
Pia unaweza kusoma:
Maandamano yalipuka China kupinga unyanyasaji shuleni
Tukio la unyanyasaji shuleni kusini mwa China limezua msururu wa maandamano kushinikiza adhabu kali kuchukuliwa dhidi ya wanafunzi walioonekana wakimshambulia mwenzao mwenye umri wa miaka 14.
Video inayomuonyesha msichana akizabwa kofi, kupegwa teke na kulazimishwa kupiga magoti na wanafunzi wenzake watatu ilisambaa katika mji wa Jiangyou katika mkoa wa Sichuan wiki iliyopita.
Polisi wanasema washukiwa watatu wote wasichana, wenye umri wa miaka 13, 14 na 15 - wawili kati yao walikuwa wamepelekwa "shule maalum ya urekebishaji tabia".
Hata hivyo taarifa za tukio hilo zimeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watu wakilalamika kuwa adhabu iliyotolewa kwa wasichana hao ni nyepesi - hasa baada ya madai kuibuka kwamba msichana huyo alionewa kwa muda.
Katika mfululizo wa video, zilizorekodiwa na washambuliai hao, mwathiriwa anasikika akisema atapiga ripoti polisi baada ya kupigwa viboko mara kwa mara huki mmoja wa wasichana wanaomshambulia akasema hawakuogopi.
Mwingine alisema ashawahi kufikishwa kituo cha polisi zaidi ya mara 10, na kudai kuwa aliachiliwa kwa chini ya dakika 20.
Kauli hizo zimewagusa baadhi ya Wachina ambao wanahofia semi kama hizo zinaendeleza visa vya unyanyasaji na uonevu nchini.
Tukio hilo limezusha wimbi la hasira za umma mtandaoni na maandamano yalizuka nje ya ofisi za serikali ya mtaa huko Jiangyou.
Zaidi ya watu 1,000 walikusanyika barabarani tarehe Agosti 4 na kusalia mitaani hadi usiku wa manane, kulingana na wamiliki wa maduka ya ndani.
Mmoja wao aliiambia BBC kwamba "vurugu zilizuka'' baada ya polisi kutumia fimbo na vifaa vya umeme kudhibiti umati.
Mchezaji Thomas Partey anayekabiliwa na tuhuma za ubakaji aachiwa kwa dhamana
Mchezaji wa zamani wa klabu ya soka ya Arsenal Thomas Partey amepewa dhamana ya masharti baada ya kushtakiwa kwa makosa matano ya ubakaji na moja la unyanyasaji wa kingono.
Partey mwenye umri wa miaka 32 alifikishwa katika Mahakama ya Westminster siku ya Jumanne.
Makosa hayo yanayodaiwa kulifanyika kati ya 2021 na 2022 alipokuwa akiichezea Arsenal huko London kaskazini.
Alishtakiwa siku nne baada ya kuondoka Arsenal wakati mkataba wake ulipomalizika mwishoni mwa Juni.
Partey alikuwa amevalia mavazi ya rangi nyeusi alipoiingia mahakamani.
Mashtaka hayo yanafuatia uchunguzi wa wapelelezi, ambao ulianza Februari 2022 baada ya polisi kupokea ripoti ya ubakaji dhidi yake kwa mara ya kwanza.
Wakili wa Partey Jenny Wiltshire awali alisema "anakanusha mashtaka yote dhidi yake", akiongeza kuwa anakaribisha "fursa ya hatimaye kusafisha jina lake.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yasitisha utoaji wa viza kwa raia wa Burundi juu ya 'ukiukaji wa mara kadhaa'
Ubalozi wa Marekani nchini Burundi hapo jana ulitangaza kusimamishwa kwa "kwa muda" kwa utoaji wa viza kwa raia wa nchi hiyo ya Afrika kwa sababu ya "ukiukaji wa mara kwa mara" na wasiwasi juu ya viwango vya juu vya raia wake kukaa nchini Marekani zaidi ya muda uliowekwa, tovuti ya habari ya SOS Medias inayoendeshwa na kampuni binafsi iliripoti.
"Kila Mburundi anayesafiri huwa na matumaini ya familia na jamii yake. Kuheshimu sheria za viza sio jambo la kibinafsi tu, ni la kitaifa", ubalozi uliandika kwenye mtandao wa Facebook.
"Cha kusikitisha, kwa sababu ya ukiukwaji wa mara kwa mara, viza ya Marekani kwa Waburundi imepigwa marufuku kwa muda. Tutekeleze sheria, kwa sababu kitendo cha mtu mmoja kinaweza kufungia taifa zima," iliongeza.
Kulingana na SOS Medias, Waburundi wana rekodi ya juu ya kukaa zaidi ya muda wao huko Marekani, na nchi hiyo ilikuwa moja ya mataifa kadhaa yaliozuiwa katika vikwazo vilivyotangazwa na Rais Trump mnamo mwezi Juni.
Marufuku hiyo haiathiri uhalali wa viza ambazo tayari zimetolewa.
Hatua hii inawadia licha ya juhudi za serikali ya Burundi kushirikiana na mamlaka ya Marekani ili kuimarisha uthibitisho wa utambulisho na "data ya ubalozi", SOS Medias iliripoti.
Nchi ambazo zinashindwa kushirikiana na Marekani juu ya uhamishaji iko katika hatari ya kukabiliwa na masharti mapya ya viza, vikwazo vya kibiashara au kupunguzwa kwa misaada.
Soma zaidi:
Al-Shabab yadai kuwaua wanajeshi kadhaa wa Uganda nchini Somalia
Kundi la wanamgambo la Al-Shabab limesema hapo jana kuwa liliwaua wanajeshi 47 wa Uganda wanaofanya kazi chini ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Kusaidia na Kudumisha Utulivu nchini Somalia (Aussom) katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga karibu na mji wa kilimo wa Barire.
Al-Shabab ilitoa taarifa ikidai kuwa pia walijeruhi wengine 31 na kuharibu magari tisa ya kijeshi.
Redio ya jeshi la Somalia ilisema jana kwamba vikosi vya Somalia na Aussom vilikamata na kuharibu magari mawili yaliyojaa mabomu kabla ya kushambulia kambi ya jeshi karibu na Barire.
Mji huo, ulioko kusini mwa Somalia katika eneo la Lower Shabelle, ulitekwa na al-Shabab wakati wa shambulio lililofanyika mwezi wa Ramadhani mnamo mwezi Machi.
Tarehe 3 Agosti Aussom ilitangaza kwamba imeanzisha shambulizi kubwa la kuuchukua mji wa Barire na kukanusha ripoti za vyombo vya habari zinazodai kuwa idadi kubwa ya wanajeshi wake wamejeruhiwa.
Mji huo uko umbali wa kilomita 50 kusini magharibi mwa Mogadishu na hutumika kama kituo cha mashambulizi ya wanamgambo, ikiwa ni pamoja na mji mkuu.
Soma zaidi:
India yasema tishio la Trump juu ya mafuta ya Urusi 'sio halali'
India imezungumzia tishio la Donald Trump la ushuru wa juu kwa sababu ya ununuzi wake wa mafuta kutoka Urusi ikisema "hiyo sio halali".
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social, rais wa Marekani alionya kuwa ataongeza ushuru kwa India na kwamba "haijali ni watu wangapi nchini Ukraine wanauawa kwa vita vya Urusi".
India kwa sasa ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Urusi.
Limekuwa soko muhimu la kuuza nje kwa Moscow baada ya nchi kadhaa za Ulaya kupunguza biashara na Urusi tangu ilipoanza uvamizi wake nchini Ukraine mnamo 2022.
Trump hakusema ushuru huo mpya ungekuwa wa asilimia ngapi, lakini hili linajitokeza siku chache baada ya kuiwekea India ushuru mkubwa wa 25%.
Soma zaidi:
Uchafuzi wa plastiki kwa mazingira ni hatari kubwa inayoongezeka - Wataalamu wa afya waonya
Watalaam wa afya wanaonya kuwa uchafuzi wa plastiki kwa mazingira ni hatari kubwa inayoongezeka pasi na kutambulika kama hatari kwa afya inayogharimu dunia takriban dolla trilioni moja na nusu kwa mwaka.
Katika tathmini inayoambatana na mazungumzo ya Geneve, wanasema plastiki husababisha magonjwa na vifo kutoka utotoni hadi uzeeni.
Pia wameangazia chembe chembe za plastiki zisizoonekana ambazo kwa sasa zipo kwenye mazingira na miili ya wanadamau.
Dunia inazalisha takriban tani nusu bilioni ya plastiki kwa mwaka.
Idadi hii inakadiriwa kuongezeka mara tatu kufikia mwaka wa 2060.
Watalaam wanatoa wito kwa Geneva kukubaliana kwa mkataba baada ya mikataba ya awali kutofaulu.
Soma zaidi:
Marekani yashtumu kifungo cha nyumbani cha aliyekuwa rais wa Brazil
Mahakama ya Juu Zaidi nchini Brazil imeamuru kuwa Rais wa zamani wa mrengo wa kulia Jair Bolsonaro awekwe chini ya kifungo cha nyumbani.
Ameshtakiwa kwa tuhuma za kupanga mapinduzi, madai ambayo anakanusha.
Jaji anayesimamia kesi ya Bolsonaro, Alexandre de Moraes, alisema uamuzi huo ni kwa sababu Bolsonaro hakufuata maagizo ya zuio aliyopewa mwezi uliopita.
Akijibu agizo hilo, timu ya wanasheria ya Bolsonaro ilikanusha kukiuka agizo lolote la zuio na kusema kwamba watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema "inalaani" amri ya mahakama na "itawawajibisha wale wote wanaosaidia na kuunga mkono vikwazo vilivyoidhinishwa".
Donald Trump amesema kesi ya Bolsonaro ni "hila", huku akiitumia kuhalalisha ushuru wa 50% kwa baadhi ya bidhaa za Brazil licha ya Marekani kuwa na ziada ya biashara na nchi hiyo.
Bw Moraes, ambaye Marekani pia imemuwekea vikwazo, alisema Bolsonaro ametumia mitandao ya kijamii ya washirika wake wakiwemo wanawe kueneza jumbe zinazohimiza mashambulizi dhidi ya Mahakama ya Juu Zaidi na uingiliaji kati wa kigeni katika mahakama ya Brazil.
Soma zaidi:
Kupunguzwa kwa misaada kutatumbukiza Wanigeria kwenye mtego wa Boko Haram, UN yaonya
Kupunguzwa kwa misaada ya kibinadamu kaskazini-mashariki mwa Nigeria kunaweza kufaidi moja ya vikundi vya wapiganaji hatari zaidi ulimwenguni, Boko Haram, mashirika ya misaada yameonya.
Kupungua kwa ufadhili katika miezi ya hivi karibuni kumelilazimisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupunguza msaada wake, na sasa halina kabisa cha kutoa.
"Itakuwa rahisi zaidi kwa wanamgambo kuwarubuni vijana kujiunga nao na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo lote," Trust Mlambo, mkuu wa operesheni katika eneo la WFP, aliiambia BBC.
Kundi hilo ambalo linafahamika duniani kote kwa kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule kutoka mji wa Chibok zaidi ya muongo mmoja uliopita, Boko Haram wameteka maelfu ya watu wakati wa uvamizi wao na kuwalazimisha zaidi ya milioni moja kuhama kwenye makazi yao vijijini.
Awali, Boko Haram lilikuwa kundi la Kiislamu la kidini lililoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambalo lilikuwa linapinga elimu ya Magharibi.
Iliendelea kuzindua operesheni za kijeshi mwaka 2009 kwa lengo la kisiasa la kuunda dola ya Kiislamu, na kusababisha ghasia katika eneo lote - ikiwa ni pamoja na katika nchi jirani kama vile Cameroon, Chad na Niger.
Kundi hilo limeorodheshwa kuwa mojawapo ya makundi mabaya zaidi ya wanajihadi duniani.
Aisha Abubakar amepoteza zaidi ya nusu ya familia yake kwa sababu ya mashambulizi katika kijiji chake jimbo la Borno na ugonjwa.
"Mume wangu na watoto sita waliuawa msituni," mama huyo mwenye umri wa miaka 40 aliambia BBC.
Watoto wake wanne walinusurika, akiwemo mmoja aliyeokolewa hivi majuzi kutoka utumwani baada ya kutekwa nyara na waasi.
Mama huyo alikimbilia Gwoza, magharibi mwa Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno.
"Siwezi kamwe kurudi kijijini," alisema Bi Abubakar. "Maisha ya kijijini yalikuwa magumu sana, tulikuwa tunatoroka kila wakati."
Amekuwa akijaribu kujenga upya maisha yake na amepata mume mwingine katika kambi ya Gwoza ya wakimbizi wa ndani na wamejaaliwa na mtoto wa miezi saba.
Soma zaidi:
‘Amesalia mifupa ya binadamu tu’ kaka wa mateka wa Gaza ameimbia BBC
Kaka wa mateka Muisraeli anayeshikiliwa katika Ukanda wa Gaza ameambia BBC kwamba video ya Hamas inayomuonyesha kaka yake akiwa amedhoofika na dhaifu ni "aina mpya ya ukatili" ambayo imewaacha wazazi wake katika hali mbaya.
Hamas ilitoa picha za Evyatar David, 24, siku ya Jumamosi, akishtumu vikali Israel na viongozi wa Magharibi.
"Amesalia mifupa ya binadamu tu. Amekabiliwa na njaa kiasi kwamba anaweza kufa wakati wowote, na anateseka sana. Hawezi kuzungumza, hawezi kusonga," kaka yake David Ilay alisema katika mahojiano Jumatatu.
Katika video, Evyatar anasema: "Sijala kwa siku kadhaa... ni nadra sana kupata maji ya kunywa." Anaonekana akichimba anachosema litakuwa kaburi lake mwenyewe.
Familia za mateka zimemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kulipa suala la kuachiliwa mateka kipaumbele kwani ripoti zinaonyesha kuwa anaweza kuongeza operesheni za kijeshi.
Picha ya Evyatar ilitolewa baada ya Wanajihad wa Kiislamu wa Palestina kuweka video ya mateka mwingine, Rom Braslavski, ambaye amekonda na alikuwa akilia.
Wanaume wote wawili walitekwa nyara kutoka kwa tamasha la muziki la Nova wakati wa shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023.
Ni miongoni mwa mateka 50 ambao bado wanazuiliwa huko Gaza, 20 kati yao wakiaminika kuwa hai.
Ilay David alisema babake hakutambua sauti ya mwanawe Evyatar mara moja kwenye video iliyotolewa na ameshindwa hata kupata lepe la usingizi. Aliongeza kuwa mama yake naye analia tu kila wakati.
"Kuona picha hizo za kaka yangu akiwa amesalia mifupa ya binadamu tu, huu ni ukatili wa aina mpya," Bw David alisema. "Ni kitu kibaya zaidi anachoweza kupitia."
Alitoa wito kwa viongozi wa dunia kuungana ili kumwokoa yeye na mateka wengine "kutoka kwa mikono ya mkatili…".
"Kwa hiyo tunapaswa kuzingatia sana kuwasilisha ujumbe, ambao ni, Evyatar anakufa, tunahitaji kumpa dawa, kumpa chakula, chakula sahihi, na anahitaji kupata matibabu haya sasa hivi, vinginevyo atakufa."
Hamas imekanusha kuwanyima chakula wafungwa kwa makusudi, ikisema kuwa mateka wanakula kile ambacho wapiganaji wao na watu wa Gaza wanakula.
Soma zaidi:
Rwanda yafikia makubaliano na Marekani kuchukua hadi wahamiaji 250, Reuters inaripoti
Marekani na Rwanda zimekubaliana kuwa nchi hiyo ya Afrika itapokea hadi wahamiaji 250 waliofukuzwa kutoka Marekani, msemaji wa serikali ya Rwanda na afisa mmoja aliliambia shirika la Reuters, huku utawala wa Rais Donald Trump ukichukua mkondo mkali juu ya wahamiaji.
Makubaliano yalioripotiwa kwa mara ya kwanza na Reuters, yalitiwa saini na maafisa wa Marekani na Rwanda mjini Kigali mwezi Juni, alisema afisa wa Rwanda, akitoa sharti la kutotajwa jina, na kuongeza kuwa Marekani tayari imetuma orodha ya awali ya watu 10 kuchunguzwa.
"Rwanda imekubaliana na Marekani kupokea hadi wahamiaji 250, kwa kiasi fulani kwa sababu karibu kila familia ya Rwanda imepitia magumu ya kuhama, na maadili yetu ya kijamii yamejengwa kuunganisha na kurekebisha," alisema msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo.
"Chini ya makubaliano hayo, Rwanda ina uwezo wa kuidhinisha kila mtu aliyependekezwa kwa ajili ya makazi mapya. Wale walioidhinishwa watapewa mafunzo ya wafanyakazi, huduma za afya, na msaada wa malazi ili kuanza maisha yao nchini Rwanda, na kuwapa fursa ya kuchangia moja ya uchumi unaokua kwa kasi zaidi duniani katika muongo mmoja uliopita."
Ikulu ya White House na Wizara ya Mambo ya Nje haikutoa maoni mara moja huku Idara ya Usalama wa Taifa ilielekeza maswali yaulizwe kwa Wizara ya Mambo ya Nje.
Rais Donald Trump analenga kuwafurusha mamilioni ya wahamiaji nchini Marekani na utawala wake umetafuta njia za kuwahamisha katika nchi zingine, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka wahalifu waliopatikana na hatia nchini Sudan Kusini na Eswatini.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Terehe ni 05/08/2025. Mimi ni Asha Juma