Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni makundi gani ya waasi yanayotafuta kuishambulia Uganda?
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi
Takriban wanafunzi 40 katika shule moja huko Kasese, magharibi mwa Uganda wameuawa katika shambulio la Ijumaa usiku na watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa Allied Democratic Forces.
Wengine wanane katika Shule ya Sekondari ya Lhubiriha, iliyoko chini ya kilomita mbili kutoka mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini, kwa mujibu wa Polisi wa Uganda.
Pia makumi ya wengine wanahofiwa kutekwa nyara na polisi wanasema jeshi linawafuatilia wapiganaji hao waliokuwa wamevuka kutoka DRC.
Lakini ni makundi gani ya waasi yanayotafuta kuishambulia Uganda?
Wakati wa vita na mivutano ya kuwania madaraka baada ya uhuru, Uganda ilizalisha makundi mengi ya waasi. Mengi ya makundi hayo kwa sasa hayako hai. Na yale yaliyo hai hayafanyi shughuli zao nchini Uganda ama sio kitisho cha moja kwa moja kwa utawala wa Yoweri Kaguta Museveni. Ila yapo machache yamebaki kuwa mwiba.
Shambulio la sasa hivi ni hilo la tkriban wanafunzi 40 katika shule moja huko Kasese, na inashukiwa kuwa waasi wa Allied Democratic Forces ndio waliotekeleza unyama huo.
Shambulio la Oktoba 24, 2021 katika baa liliacha vifo vya watu wawili na wengine wakijeruhiwa kwa mujibu wa Polisi ya Uganda. Na lile la Oktoba 25 katika basi limesababisha kifo cha mtu mmoja, mlipuaji mwenyewe wa kujitoa muhanga. Ingawa aliacha majeruhi kadhaa.
Mashambulizi haya yamekuja siku chache tangu Ubalozi wa Uingereza nchini humo October 14, kuonya uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi. Sanjari na Ufaransa kuonya raia wake wasitembee katika mikusanyiko ya watu.
Hii si mara ya kwanza Uganda kuonywa. Mei 2014 na Machi 2015, Ubalozi wa Marekani nchini humo ulitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mashambulio ya kigaidi ya kujitoa muhanga.
Licha ya mashambulio yaliyohofiwa kutotokea katika miaka hiyo. Uganda imebaki katika tahadhari kubwa tangu 2010. Swali ni: Je, ni makundi gani yenye uadui na Uganda, yanatafuta kuishambulia?
ADF
Allied Democratic Forces (ADF), ni kundi la Kiislamu la siasa kali lililozaliwa Uganda. Katikati ya miaka ya 90 lilahamia Magharibi mwa taifa hilo, kabla ya kutokomea katika misitu ya Mashariki mwa Congo mwishoni mwa miaka ya 90.
Kundi hili limefanya mashambulizi mengi zaidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuliko Uganda lilikotokea. Tangu wakati lilipoingia Congo limehusika na mauaji, kushambulia vijiji na utekaji. Likidaiwa pia kushirikiana na makundi mengine katika misitu hiyo.
Kwa miaka mingi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) limefanikiwa kuendesha operesheni zilizouwa wapiganaji wengi wa ADF katika mpaka wake na Congo. Na kulifanya kundi hilo kutokuwa na nguvu ya kuingia na kuishambulia Uganda moja kwa moja.
Agosti mwaka huu, vikosi vya usalama vilimkamata mtu mmoja kwa tuhuma za kutaka kujitoa muhanga katika mazishi ya Meja Jenerali Paul Lockech. Aliyewahi kuwa kamanda wa kikosi cha Jeshi la Uganda katika AMISOM, nchini Somalia.
Taifa hilo lilitupa lawama kwa kundi la ADF, kwa madai ndio liko nyuma ya shambulio hilo lililotibuliwa. Miezi michache baadae mashambulizi ya Oktoba 24 na 25 yakafuata. Uganda imeilaumu ADF vilevile.
Kwanini Dola la Kiislamu linadai kuhusika?
Kundi la Dola la Kiislamu limejikita zaidi Mashariki ya Kati. Liliibuka wakati wa ghasia za machipuo ya kiarabu (Arab Spring). Baada ya vita vikali hatimae utawala wao wa Khilafa ulianza kudondoshwa kuanzia 2016 katika nchi ya Iraq na Syria.
Kwa sasa linatekeleza mashambulizi ya kulipua mabomu katika mataifa ya Mashariki ya kati na nje ya hapo. Katika mataifa ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kundi hilo limekita kambi katika ukanda wa Sahel.
Ingawa Uganda haina uadui wa moja kwa moja na magaidi hao. Baada ya shambulio la Oktoba 24 lililouwa katika baa, Dola la Kiislamu liliibuka na kudai kuhusika na tukio hilo.
Serikali ya Uganda kwa upande wake kupitia Jeshi la Polisi imelinyooshea kidole kundi la ADF. Kwanini Uganda inalaumu ADF na sio Dola la Kiislamu?
Tangu 2017, ADF ilianza kuwa na ushirikiano na Dola la Kiislamu na kutangaza utiifu kwa kundi hilo miaka michache baadae. Kwa sasa ADF linajuulikana pia kama Dola la Kiislamu la Afrika ya Kati (ISCAP).
Utiifu huu ndio uliosukuma Dola la Kiislamu kudai kuhusika na mashambulio yaliyotokea katika baa na basi siku chache zilizopita.
Septemba 18, mwaka huu, taifa la Congo lilimkamata raia wa Jordan kwa tuhuma za kuwa mfuasi wa Dola la Kiislamu. Alikamatwa katika eneo la Makisabo karibu na mji wa Beni, jimboni Kivu ya Kaskazini ambako ADF wanaendesha shughuli zao.
Taarifa zinaeleza huyo ndio mtu wa kwanza asiye Muafrika kukamatwa Congo kwa tuhuma za kuhusika na Dola la Kiislamu. Tangu wakati huo hadi sasa bado serikali ya Congo haijatoa taarifa za ziada kumhusu.
Al-Shabaab
Somalia iko katika machafuko kwa miongo mitatu sasa. Umoja wa Afrika (AU) ulipoamua kupeleka kikosi cha walinda amani mwaka 2007, kijuulikanacho kama AMISOM. Uganda ikawa mchangiaji katika kikosi hicho.
Mataifa mengine yaliyo katika AMISOM ni Burundi, Ethiopia, Nigeria, Djibouti, Kenya, Ghana, kuyataja kwa uchache. Mataifa haya yote yanatazamwa na Al-Shabaab kwa jicho la uadui.
Licha ya kuwa vita dhidi ya Al-Shabaab havijafikia hata mwanzo wa mwisho. Vikosi vya AMISOM vimefanikiwa pakubwa kulikata makali kundi hilo na kulitoa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na miji mengine.
Tarehe 11, Julai 2010, Al-Shabaab ilikiri kuhusika na shambulio nchin Uganda kwenye uwanja uliofurika mashabiki waliokuwa wakifuatilia fainali ya kombe la dunia iliyochezwa Afrika Kusini. Watu zaidi ya 70 waliuwawa na wengine wakijeruhiwa
UHLM/F
Uganda Homeland Liberation Movement /Force (UHLM/F), ni kundi la waasi lililoanza mashambulizi 2016 kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Polisi la Uganda. Ripoti hiyo inaeleza kundi hili limetekeleza mashambulizi matano tangu 2016 hadi 2021, wakilenga kambi za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).
Mashambulizi yote yalizimwa na wanajeshi. Katika baadhi ya mashambulizi waasi walifanikiwa kuua wanajeshi kadhaa. Huku wanajeshi wakifanikiwa kuuwa waasi na kuwakamata baadhi yao. Kundi hili linatokea Uganda ingawa linajificha katika misitu ya Congo.
Ukubwa wa tishio ukoje?
Siku moja baada ya shambulio katika basi. Akizungumza na vyombo vya habari, msemaji wa Jeshi la Polisi (UPF), Fred Enaga alieleza, "ADF limeunda kundi la kufanya mashambulizi Uganda. Limesajiliwa na kupewa mafunzo ya kulipua mabomu na kushambulia maeneo mbalimbali."
Mkurugenzi wa Polisi ya Kimataifa, upande wa Uganda, (Interpol), Charles Birungi ameliambia gazeti la Daily Monitor siku ya Jumatatu Oktoba 25, "lililowazi ni kuwa kumekuwa na ongezeko la kitisho cha ugaidi, kutoka Dola la Kiislamu, al-Shabaab, ADF na Ansar al-Sunna ama al-Shabaab wa Mozambique."
Wakati Polisi ya Uganda ikikiri ADF kusajili na kutoa mafunzo ya kulipua. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Polisi ya Kimataifa ametoa onyo kwa vijana wa Kiganda wasio na ajira wasikubali kurubuniwa na makundi hayo pindi yakija kwa lengo la kutaka kuwaajiri.