'Serikali na dunia wameisahau Chibok'

    • Author, Azeezat Olaoluwo
    • Nafasi, BBC reporter
    • Akiripoti kutoka, Chibok, Nigeria

Mnamo Aprili 2014, mji wa kaskazini-mashariki wa Nigeria wa Chibok ulipata umaarufu duniani baada ya kutekwa nyara kwa wasichana 276 wa shule na kampeni ya #bringbackourgirls iliyohusisha watu maarufu duniani .

Miaka kumi baadaye, tishio linaloendelea linaloletwa na makundi yenye vurugu bado linadhuru maisha ya watu wengi katika mji huo.

Huku akifuta machozi, Esther Yakubu anakumbuka jinsi maisha yalivyokuwa magumu bila binti yake Dorcas.

''Imepita miaka 10 tangu binti yangu awe mateka na Boko Haram. Haijawahi kuwa rahisi. Watu watasema niendelee, kwamba nina watoto wengine, lakini ninapokuwa peke yangu, ninamfikiria yeye.''

Kuona vitu vya Dorcas nyumbani kwake kulikuwa kukimrudishia kumbukumbu zenye uchungu kila mara na hakumruhusu kusonga mbele kutokana na huzuni yake. Esther aliamua kuachana nazo, isipokuwa picha chache tu.

''Nilitoa vitu vyake vyote kwa watu wanaoishi nje ya Chibok ili nisiwe karibu navyo. Sikutaka kuviona.''

Usiku wa tarehe 14 Aprili 2014, kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram liliwateka nyara wasichana 276 wa shule ya bweni katika mji uliokuwa haujulikani sana wa Chibok.

Utekaji nyara huo uliibua kampeni ya kimataifa ya mitandao ya kijamii #BringBackOurGirls, iliyohusisha mke wa rais wa zamani wa Marekani Michelle Obama, Mshindi wa Tuzo ya Nobel Malala Yusufzai, na watu wengine mashuhuri.

Miaka kumi baadaye, wasichana wengi wameokolewa au kufanikiwa kutoroka. Hata hivyo, 87 kati ya hao 276 bado wanashikiliwa mateka na hawajulikani waliko. Dorcas ni mmoja wa wasichana waliopotea ambaye alikuwa na umri wa miaka 16 tu wakati wa kutekwa nyara kwake.

Kwa mama yake Esther, kutokuwa na uhakika wa kutojua kuhusu hatima yake kunafanya iwe vigumu kuendelea na maisha yetu. ''Ninataka serikali kuwaacha wasichana wetu kuwa huru na warudi nyumbani. Tunataka kuwaona walio hai ili angalau tuwe na furaha. Wale ambao hawapo hai, tujulishwe ili tuweze kukata tamaa.''

Esther hajapata taarifa rasmi kuhusu sehemu ambapo binti yake anazuiliwa , lakini alionekana kwenye video ya 'kuthibitisha uhai' ya watekaji nyara mnamo 2016. Katika video hiyo, Dorcas alijitambulisha kwa jina la Maida, jina jipya alilopewa na waliomteka.''Kama Dorcas angeweza kunisikia sasa, ningemwambia mimi niko hai na mji wa Chibok bado upo, ili awe na hamu ya kurudi nyumbani kutuona.''

Kufika Chibok

Kusimulia hadithi kutoka sehemu hii ya mbali ya kaskazini-mashariki mwa Nigeria ni safari ndefu na ngumu yenyewe. Barabara ya kuelekea Chibok inaanzia jimbo jirani la Adamawa. Ni mwendo mrefu kupitia mandhari kavu na wazi.

Tunaendesha gari kupita mnara ulioanguka wa mawasiliano. Mwenyeji wetu anatuambia kuwa inashukiwa kuwa Boko Haram waliangusha mnara huo ili kutatiza mawasiliano. Je, watu wanaoishi hapa wanawezaje kuomba msaada?

Kikundi hicho bado kinahudumu katika eneo hilo.

Tunapita takribani nusu dazeni za vituo vya ukaguzi vya kijeshi kabla ya kufika tunakoenda.

Chibok yenyewe ni mji wa kijeshi na uwepo mkubwa wa wanajeshi wa serikali. Jeshi limeweka vizuizi vingine viwili pamoja na amri kali ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri.

Shule mpya

Shule ya Sekondari ya Serikali huko Chibok ina sura mpya. Ilijengwa upya mnamo 2021, na kuna daalili chache za matukio yaliyotokea hapa usiku huo wa kutisha.

Bweni ambalo wasichana hao walitekwa nyara limebomolewa. Hakuna dalili ya kile kilichotokea hapa muongo mmoja uliopita .

Ijapokuwa ni mpya, mchoro wa rangi ya krimu kwenye baadhi ya majengo ya shule tayari unabambuka, labda kutokana na hali ya joto, ambayo imepauka nyasi mbele ya jengo la utawala hadi rangi ya dhahabu-kahawia.

Muhammad Chiroma aliteuliwa kuwa mkuu mpya shule ilipofunguliwa tena 2021. Alisema kumekuwa na kuboreka kwa usalama tangu aanze kazi.

''Karibu kila sehemu ya shule, ndani na nje, imezingirwa na wanajeshi. Tuna ulinzi mkali sana. Ukiingia humu, utajisikia tu kama uko nyumbani''.

''Wazazi waliopeleka watoto wao katika shule nyingine sasa wanawarudisha. Tumekuwa tukipokea wanafunzi wapya wanaohamishwa kutoka shule zingine ili kujiunga nasi,'' anatuambia.

Chibok ina chaguo chache za shule, shule ya msingi na ya upili ya serikali.

Bwana Chiroma ananiambia kuwa anaamini kuwa jamii iko salama, na ana imani na jeshi linalowalinda. Hata hivyo, kumekuwa na angalau mashambulizi mawili ya hivi karibuni ya waasi wa Boko Haram kama hivi karibuni kama Desemba 2023 na Januari 2024. Watu wenye silaha waliua takriban watu 14 na kuiba vyakula.

Changamoto zilizopo

Manase Allen alizaliwa na kukulia Chibok na kuhamia mji mkuu wa Abuja miezi minane tu baada ya wasichana hao wa shule kutekwa nyara. Leo, anafanya kampeni huko kwa niaba ya wakazi wa mji wake wa asili na huwatembelea mara kwa mara kuwaona wazazi wake wagonjwa.

''Kuna mambo mengi ambayo hayajabadilika huko Chibok, hata shuleni. Ndio, miundo imekuja, lakini hakuna vifaa vya ICT, hakuna maabara, hakuna maktaba, hakuna maji, hakuna chochote.

''Kuna utawala mdogo hapa. Hakukuwa na umeme kwa miaka 10 iliyopita; wale wanaofanya biashara inayohitaji mwanga hawawezi kufanya kazi vizuri," anasema.

''Kabla ya 2014, nilikuwa nikifanya kilimo ufugaji wa kuku, na uvuvi. Nilikuwa mmoja wa waajiri wa juu wa sekta ya kibinafsi wa wafanyikazi huko Chibok.''

Mwanaharakati na mwanasiasa huyo alisema biashara yake ya shamba iliharibiwa wakati Boko Haram walipofanya fujo.

''Tulipoteza kila kitu, kila kitu kiliteketezwa, baadhi ya madereva wetu waliuawa hata kwenye barabara kuu. Tumepoteza magari; tulipoteza kila kitu kwa Boko Haram.''

Manase anaamini kuwa hakuna maendeleo yoyote tangu alipohama.

''Nafikiri serikali na dunia imeiacha Chibok,'' Manase ananiambia.

Mahali pekee ambapo kuna shamra shamra na shughuli nyingi zaidi ni soko kuu la Chibok. Hassan Usman anauza vifaa vya ujenzi huko na ananikaribisha katika duka lake, anapenda kuzungumza kuhusu biashara huko Chibok.

''Usalama katika Chibok hapa umeathiri biashara zetu pakubwa, hasa zangu. Ninauza vifaa vya ujenzi. Hakuna mtu aliye tayari kuja kujenga nyumba yake au kukarabati nyumba yake tena.''

''Baadhi wamehama kutoka katika jamii hii tangu 2014, wakati utekaji nyara wa shule ulipofanyika. Lakini hali ya usalama inarejea taratibu,'' alisema.

Tangu kutekwa nyara kwa wasichana wa shule ya Chibok mwaka wa 2014, zaidi ya wanafunzi 1,400 wametekwa nyara katika takriban mashambulizi 10 ya shule. Katika visa viwili vya mwezi Machi, zaidi ya wanafunzi 300 walitekwa nyara.

Juhudi Zinazoendelea

Katika mji mkuu wa Abuja, ninakutana na Seneta Muhammad Ali Ndume ambaye ni mbunge wa kitaifa kutoka Wilaya ya Seneta ya Borno Kusini, ambako Chibok iko, kwa chama tawala cha APC.

''Serikali inafanya jambo na serikali ina wasiwasi,'' ananiambia. "Nitawaomba wazazi waendelee kuwa wavumilivu na kuendelea kuwaombea mabinti zao warudi."

Anasema malipo ya fidia wakati wa utawala uliopita, wakati zaidi ya wasichana 100 wa Chibok waliachiliwa kufuatia mazungumzo, yamezidisha tatizo.

''Ni Mungu pekee anayejua kiasi cha pesa kilicholipwa. Nadhani ni kuanzia hapo ndipo watu wanaamini ukichukua mtu unaweza kupata pesa nyingi sana.

''Hilo lilikuwa kosa ambalo lilifungua nafasi kwa hali hii ya usalama sasa.''

Serikali wakati huo ilikuwa imekanusha ripoti kwamba ililipa fidia kwa ajili ya kuachiliwa kwa wasichana 21 wa Chibok mwaka wa 2016. Lakini mwaka uliofuata, maafisa walikiri kufanikisha kuachiliwa kwa wasichana wengine 82 wa Chibok waliobadilishana na washukiwa waliokuwa kizuizini wa Boko Haram.

Seneta Ndume anakanusha ukosoaji kwamba amekosa kuwahudumia ifaavyo watu wa Chibok na anaendelea kuitaka serikali ichukue hatua kuwaokoa wasichana waliosalia na wengine wanaoshikiliwa na Boko Haram.

''Seneti itaanza tena tarehe 16 Aprili ambayo itakuwa siku mbili baada ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kutekwa nyara kwa wasichana wa Chibok," asema.

“Ninaahidi kutoa hoja ya kuitaka serikali kuweka juhudi zaidi kuzuia utekaji nyara na kufanya shule kuwa salama,’’ Seneta Ndume ananiambia.

Matumaini ya wazazi wa wasichana 87 waliotoweka wa shule ya Chibok kwamba watarejesha binti zao huenda yanafifia, lakini kwa Esther, hakati tamaa.

''Ninajua kwamba Mungu yuko pamoja naye huko na nina matumaini kwamba siku moja nitamuona tena.''

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah