Kundi la waasi la M23 ambalo limekuwa likipiga hatua ya kuteka miji kadhaa katika majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini Mashariki mwa DRC, sasa linasema kwamba litaondoa wapiganaji wake katika mji wa Walikale ambao ulitekwa mapema wiki hii.
Kwa mujibu wa taarifa walioitoa usiku wa Jumamosi Machi 22, kundi hilo limesema kwamba hatua hiyo imefanyika kwa ajili ya , ‘kuheshimu mkataba wa makubaliano wa kusitisha vita uliotiwa sanini mwezi februari 2025.’
‘AFC/M23 imesalia na msimamo wake kwamba tuko tayari kuhakikisha kwamba mzozo huu unaoendelea unapata suluhu ya kudumu na vile vile lengo letu ni kulinda maisha na mali ya raia katika eneo hili, ‘ ilisema taarifa hiyo iliyotiwa Saini na Lawrence Kanyuka, ambaye ni msemaji wa muungano wa Congo River Alliance.
Hata hivyo kundi hilo limeshikilia msimamo wa awali kwamba wakihisi kwamba wanachokozwa kwa kushambuliwa upya na jeshi la FARDC, hali ambayo inatishia maisha ya raia, basi watabatilisha uamuzi wao kuondoka mji wa Walikale na viunga vyake na kurejea huko mara moja.
Walikale, ni mji ambao upo kwenye makutano ya barabara kuu inayounganisha mji wa Bukavu ambao ni makao makuu ya Kivu Kusini na mji wa Goma ambao ni makao makuu ya Kivu Kaskazini. Aidha, Walikale sio mbali na mji wa Kisangani ambao ndio njia ya kuunganisha mashariki mwa DRC na mji mkuu wa Kinshasa uliopo kusini magharibi mwa taifa hilo.
Wachambuzi Godwing Gonde na Nicodemus Minde katika mahojiano na BBC Swahili mapema wiki hii walisema kwamba hatua ya kundi hilo kuuteka mji wa Walikale ni ishara kwamba azimio lao la kuingia tena Kinshasa bado lipo.
“Mnamo 1997 waliingia Kinshasa ila hawakukaa kwa muda, na sasa wanavyotekeleza mipangilio yao ya kuteka miji mikuu katika eneo la msahariki mwa DRC, inaonekana wazi kwamba wana lengo moja tu,’ alisema Dkt. Nicodemus Minde ambaye ni mtafiti katika taasisi ya utafiti wa usalama wa kimataifa ISS.
Kwa upande wake, Gonde ambaye ni mhadhiri wa Diplomasia na mchambuzi wa masuala ya usalama wa Kikanda, anahisi kwamba; ‘ hali ya kuendelea kuteka miji katika eneo la mashariki mwa DRC inaathiri hali ya maisha ya kila siku kwa raia ambao hawana huduma muhimu kama vile ya benki ambazo zilifungwa tangu mapigano yaanze mashariki mwa DRC, na hali inatatizika pakubwa kwa kuwa viwanja vikuu vya ndege katika eneo hilo vimekaliwa na wapiganaji wa M23 na kuzuia huduma muhimu kama dawa na chakula kuwafikia waathiriwa.’
Jumanne Machi 18, kundi hilo lilijiondoa kwenye mkutano uliopangwa na Rais wa Angola , kuwaleta pamoja viongozi wakuu wa M23 na wawakilishi wa serikali ya DRC ambapo pia ilitarajiwa kwamba Rais Felix Tsishekedi angehudhuria.
Japo M23 ilituma ujumbe wa watu tano, kiongozi wa CRA Corneille Nangaa, wala Sultani Makenga wa M23 hawakusafiri hadi Luanda, huku kundi lililotumwa Angola likisema kwamba vikwazo dhidi ya maafisa wao wakuu ni dhuluma dhidi yao ambayo hawakufurahia.
Huku wakisema kwamba hatua yao ya kuondoka Walikela ni ya kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa katika eneo hilo, kundi hilo pia limesema kwamba linasubiri kuona ikiwa jeshi la FARDC litazingira mji huo ama litachukuwa hatua gani.
Upande wa serikali ya DRC imesema kwamba wao pia wanasubiri kuona ikiwa M23 itaondoa wapiganaji wao kutoka kwa mji huo kama walivyoahidi.