Shambulio la angani lamuua afisa mkuu wa Hamas huko Gaza

Shambulizi la anga la Israel katika mji wa kusini wa Khan Younis huko Gaza limemuua kiongozi mkuu wa chama cha Hamas Salah al-Bardaweel, afisa wa Hamas aliambia BBC mapema Jumapili.

Muhtasari

  • Dereva Muingereza Elfyn Evans aibuka mshindi wa mbio za magari za Safari Rally nchini Kenya.
  • Watu 3 wauawa katika shambulio la Urusi mjini Kyiv, Zelensky akitoa wito wa shinikizo dhidi ya Moscow
  • Video: Tazama papa Francis akiwasalimia waumini wake kutoka katika dirisha la hospitali
  • Papa Francis kuondoka hospitalini leo
  • M23 yaondoka Walikale siku chache baada ya kuuteka mji huo wa Kivu Kusini
  • Mjumbe wa Trump apuuza mpango wa waziri mkuu wa Uingereza kuhusu Ukraine
  • Hereni zenye thamani ya $769,500 zapatikana na polisi baada ya anayedaiwa kuwa mwizi kuzimeza
  • Shambulio la angani lamuua afisa mkuu wa Hamas huko Gaza

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu na Leila Mohammed

  1. Habari za hivi punde, , Urusi na Ukraine zakubali kusitisha mashambulizi ya kijeshi katika Bahari Nyeusi - Marekani

    Ikulu ya White House inasema Urusi na Ukraine zimekubali kuhakikisha kupita kwa usalama kwa meli za kibiashara na kusitisha mashambulizi ya kijeshi katika Bahari Nyeusi.

    Marekani inasema Urusi ilikubali kuendeleza hatua za kutekeleza marufuku ya mashambulizi dhidi ya vituo vya nishati nchini Ukraine na Urusi

  2. Rwanda yaunga mkono kuondoka kwa M23 mjini Walikale DR Congo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Serikali ya Rwanda imepokea vyema hatua ya kundi la waasi la M23 kujiondoa kwenye mji wa Walikale ambao waliuteka siku moja baada ya Rais Paula Kagame na Felix Tsishekdi kutia Saini mkataba wa makubaliano kusitisha vita mashariki mwa DRC bila ya kuweka masharti.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumapili Machi 23, msemaji wa serikali Yolande Makolo alisema kwamba wamepokea vyema habari kwamba shughuli za kijeshi za jeshi la FARDC na kundi la Wazalendo linalowaunga mkono yatasitishwa pia.

    M23 imesema kwamba imechukuwa hatua hiyo kwa ajili ya kuheshimu mkataba wa makubaliano ya kusitisha amani uliafikiwa mwezi Februari mwaka 2025.

    Kwa Upande wake, Rwanda imesema kwamba: “ Serikali iko tayari kushirikiana na pande zote kuhakikisha kwamba maafikiano yaliyotiwa Saini yanadumishwa na kwamba wote wanaheshimu maagizo yaliyowekwa na marais wa jumuiya za EAC na SADC kwa pamoja na kuweka njia ya kupatikana kwa suluhu ya kudumu kurejesha usalama katika eneo hilo.”

  3. Dereva Muingereza Elfyn Evans aibuka mshindi wa mbio za magari za Safari Rally nchini Kenya.

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Dereva Elfyn Evans kutoka Uingereza ndiye mshindi wa mashindano ya mbio za magari ya Safar Rally ambazo zimekamilika mchana wa Jumapili hii, katika mji wa Naivasha nchini Kenya.

    Evans mwenye umri wa miaka 36 ameshinda awamu hii ya tatu ya mashindano ya magari ulimwenguni WRC ambayo inatarajiwa kukamilika nchini Saudi Arabia mwezi Novemba, mwishoni mwa msimu wa 2025.

    Evans na mwongoza njia wake waliongoza mashindano haya kuanzia siku ya pili hadi kukamilika kwa mashindano hayo kwenye mbuga ya Wanyama ya Hells Gate mjini Naivasha mwendo was saa tisa.

    Rais wa Kenya William Ruto mbali na kuwapongeza madereva walioshiriki katika Makala ya mwaka huu ya Safari Rally, amesema kwamba; “ Kulingana na tunayoyasikia kwa walioshiriki ni kwamba mashindano ya mwaka huu yalikuwa makubwa zaidi na yaliwavutia madereva na mashabiki wengi katika eneo la mashindano,”

    Mashindano ya Safari Rally Kenya , yalirejea kwenye msururu wa WRC miaka mitano iliyopita baada ya kuondolewa katika miaka ya tisini kwa ajili ya ukosefu wa maandalizi mema.

    Huku Elfyn akifurahia ushindi wake wa kwanza kwenye Safari Rally, dereva mwenzake katika timu ya TOYOTA GAZOO WRT na mshindi mara mbili wa Safari Rally Kalle Rovapena, alilazimika kujiondoa kwenye mashindano katika kiwango cha 17- eneo la Olnegsengoni kwa ajili ya matatizo ya kiufundi kwenye gari lake.

    Dereva wa Japani Takamoto Katsuta alipata ajali katika siku ya mwisho ambapo gari lake lilibingirika na japo aliweza kulirejesha barabarani na kukamilisha mashindano, hakuweza kujumuishwa katika orodha ya madereva kumi bora kwenye mashindano hayo.

    Awali alikuwa na matumaini makubwa kuibuka mshindi .

    Mashindano ya mwaka huu yalianza Alhamisi Machi 20th na Kukamilika Jumapili Machi 23 , muda yakiongezwa kwa siku moja ili kuwapa madereva muda wa kushiriki vyema.

  4. Watu 3 wauawa katika shambulio la Urusi mjini Kyiv, Zelensky akitoa wito wa shinikizo dhidi ya Moscow

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine usiku wa kuamkia leo yamesababisha vifo vya watu watatu mjini Kyiv na wengine kadhaa kujeruhiwa, maafisa wa eneo hilo wamesema.

    Shahidi mmoja amesema "kila mtu alianza kupiga mayowe na kukimbia" huku vifusi vikigonga jengo la ghorofa.

    Jeshi la anga la Ukraine limesema kuwa limeangusha ndege 97 kati ya 147 zilizorushwa nchini humo.

    Wakati huo huo, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema ilizidungua takriban ndege 60 za Ukraine zisizo na rubani na kusema mtu mmoja aliuawa baada ya gari kushika moto kufuatia shambulio.

    Kufuatia mashambulizi katika mji mkuu wa taifa lake, Rais wa Ukraine Zelensky ametoa wito wa shinikizo mpya dhidi ya Urusi.

    Inakuja wakati Ikulu ya Kremlin ikisema kwamba wako karibu na mkutano wa ana kwa ana kati ya Trump na Putin - lakini msemaji anasema mazungumzo "magumu" ya kiufundi yanahitaji kufanywa kabla ya hii kuendelea.

    Wajumbe wa Marekani na Ukraine watakutana nchini Saudi Arabia siku ya Jumapili, wakati Washington ikitaka kujadiliana ili kumaliza mzozo huo. Siku ya Jumatatu, Marekani inatarajiwa kukutana na wenzao wa Urusi.

    Putin amekataa wito wa pamoja wa Marekani na Ukraine wa kusitishwa kwa siku 30 za vita kamili na mara moja, na kupendekeza badala yake kusitisha mashambulizi kwenye vituo vya nishati pekee.

  5. Video: Tazama papa Francis akiwasalimia waumini wake kutoka katika dirisha la hospitali

    Maelezo ya video, Wakati papa Francis alipowasalimia waumini kutoka kwa dirisha la hospitali
  6. Meya wa Istanbul ambaye ni mpinzani mkuu wa rais Erdogan akamatwa kwa shutuma za ufisadi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Imamoglu alikamatwa alipokuwa akijiandaa kusajiliwa kuwania Urais dhdidi ya Rais wa sasa Erdogan.

    Meya wa mji wa Istanbul huko uturuki, Ekrem Imamoglu amekamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi.

    Imamoglu ambaye ni mpinzani mkali wa Rais Recep Tayyip Erdogan, alizuiliwa siku ya Jumatano wiki iliyopita, siku chache kabla ya kupokea uteuzi wa chama chake kuwa mgombea Urais na kujiandaa kwa Kinyang’anyiro cha 2028.

    Kukamatwa kwakwe kumezua maandamalo jijini Istanbul Jumaposi na Jumapili ambapo polisi wamekabiliana na waandamanaji waliofika kulalamikia hali anayokumbana nayo kiongozi huyo.

    Imamoglu mwenyewe anakanusha madai hayo dhidi yake, na amelalamikia kuzuliliwa kwake .

    Maandamano ya kumuunga mkono ni mojawapo ya makubwa yaliyoandaliwa nchini Uturuki katika muongo mmoja uliopita.

    Rais Erdogan amelaani ghasia zilizoshuhudiwa katika maadamano hayo, akisema kwamba Imamoglu na chama chake cha Republican Peopl’s party CHP wanajaribu kutatiza usalama wan chi na kuwachochea raia wan chi hiyo.

    Mamia ya waandamanaji waliofika nje ya ofisi ya Meya , walikamatwa na polisi, hata kabla ya maandamano hayo kuanza rasmi. Polisi walirusha vitoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji hao usiku wa Jumamosi.

    Na japo ilikuwa vigumu kwa wengi kupumua chini ya moshi mkali wa mabomu ya kutoa machozi, waliokuwa hapo kuandamana waliimba na kusema ‘ tunataka haki, sheria na haki kutendeka kwa mujibu wa sheria.’

    Katika miji ya Ankara na Ismir, polisi walitumia magari ya kurusha maji kutawanya makundi ya watu yaliyokusanyika kuandamana.

    Maanddamano hayo yaliyoanza siku tano zilizopita, yamekuwa yenye utulivu hadi usiku wa Jumamosi ambapo ghasia zimeshuhudiwa.

    Yalisambaa hadi miji mingine ya Ankara na Izmir huku ikisemekana kwamba yangesambaa kote nchini Uturuki.

    Mamalaka nchini humo zimeseka kwamba hadi sasa watu 343 wanazuliiwa na polisi baada ya kukamatwa usiku wa Ijumaa.

    Imamoglu anaonekana kama mojawapo ya wapinzani wakubwa wa Rais Erdogan na ndiye mgombea wa pekee wa chama cha CHP, ambacho kilikuwa kimuidhinishe kuwania Urais Jumapili hii.

    Hata hivyo, Jumatano wiki hii , alikuwa miongoni maw watu 111, wakiwemo wanasiasa wengine, wanahabari na wafanyabisahara ambao walikamatwa na kuzuiliwa katika msako ambao mamlaka inasema ni wa kuchunguza visa vya ufisadi.

  7. Papa Francis kuondoka hospitalini leo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kuwa hospitalini kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja. Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibu katika hospitali ya Gemeli, mjini Roma Papa ataondoka hospitalini baadaye leo, na kurejea katika makazi yake rasmi huko Vatican ambapo atatarajiwa kuwa ndani kwa ndani kwa muda wa miezi miwili.

    Mwandishi wa BBC Bethany Bell ambaye yuko nje ya hospitali hiyo mjini Rome, amesema kwamba Papa ataonekana hadharani kwa mara ya kwanza saa nane saa za Afrika Mashariki ambazo ni sawa na saa sita mchana saa za Roma.

    Anaatarajiwa kuonekana kwenye dirisha la wodi ambayo alikuwa amelazwa, kwa muda huo wote.

    Atawabariki waumini waliokusanyika nje ya hospitali hiyo kumuombea apate afueni, kisha ataondoka kuelekea kwenye makazi yake ambapo ataangaliwa kwa ukaribu na madaktari wake.

    Hatoweza kutangamana na watu wengi, kwa muda wa miezi miwili hadi pale afya yake itakapohakikishwa kuwa salama kabisa,’ alisema mwandishi Bell.

    Kiongozi huyo wa madhehebu ya wakatoliki ya dini la Kikristo , alilazwa mnamo February 14 akiwa na changamoto za mfumo wa kupumua na vile vile akiuguwa nimonia ama kichomi.

    Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 amekuwa hospitalini kwa wiki tano hivi, na katika muda huo alikabiliwa na changamoto zaidi za kiafya mara mbili ambapo madaktari wanasema maisha yake yalikuwa hatarini.

    Daktari Sergio Alfieri , ambaye ni mmoja wa madaktari wanaomtibu Papa Francis amesema kwamba wamefurahia hali ya kwamba Papa atarejea nyumbani.

    Aidha amefafanua kwamba, ‘ wagonjwa wanaouguwa hali mbaya ya nimonia hupoteza sauti hasa wakiwa wenye umri mkubwa , kwa hivyo itachukuwa muda kwa sauti ya mgonjwa kurejea hali ya kawaida.’

    Siku ya Ijumaa, Kadinali Victor Fernandez aliambia wanahabari kwamba Papa alipokezwa hewa ya Oksijeni mara kwa mara na idadi kubwa ya hewa hiyo hukausha viungo mwilini hasa kwenye koo, na kwa sababu ya hilo Papa atalazimika kujifunza kuzungumza upya,’

    Wengi wanafuraha kwamba Papa amehisi vyema na kwamba anarea nyumbani ila haijulikani kwa wakati huu ikiwa ataweza kuongoza misa ya Pasaka kama ilivyokuwa kawaida yake.

    Wiki chache zilizopita Wakristo waliadhimisha Jumatano ya Majivu kwa ibada maalum, ambapo Papa hakuhudhuria kwa ajili ya hali yake ya kiafya.

  8. M23 yaondoka Walikale siku chache baada ya kuuteka mji huo wa Kivu Kusini

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wapiganaji wa M23

    Kundi la waasi la M23 ambalo limekuwa likipiga hatua ya kuteka miji kadhaa katika majimbo ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini Mashariki mwa DRC, sasa linasema kwamba litaondoa wapiganaji wake katika mji wa Walikale ambao ulitekwa mapema wiki hii.

    Kwa mujibu wa taarifa walioitoa usiku wa Jumamosi Machi 22, kundi hilo limesema kwamba hatua hiyo imefanyika kwa ajili ya , ‘kuheshimu mkataba wa makubaliano wa kusitisha vita uliotiwa sanini mwezi februari 2025.’

    ‘AFC/M23 imesalia na msimamo wake kwamba tuko tayari kuhakikisha kwamba mzozo huu unaoendelea unapata suluhu ya kudumu na vile vile lengo letu ni kulinda maisha na mali ya raia katika eneo hili, ‘ ilisema taarifa hiyo iliyotiwa Saini na Lawrence Kanyuka, ambaye ni msemaji wa muungano wa Congo River Alliance.

    Hata hivyo kundi hilo limeshikilia msimamo wa awali kwamba wakihisi kwamba wanachokozwa kwa kushambuliwa upya na jeshi la FARDC, hali ambayo inatishia maisha ya raia, basi watabatilisha uamuzi wao kuondoka mji wa Walikale na viunga vyake na kurejea huko mara moja.

    Walikale, ni mji ambao upo kwenye makutano ya barabara kuu inayounganisha mji wa Bukavu ambao ni makao makuu ya Kivu Kusini na mji wa Goma ambao ni makao makuu ya Kivu Kaskazini. Aidha, Walikale sio mbali na mji wa Kisangani ambao ndio njia ya kuunganisha mashariki mwa DRC na mji mkuu wa Kinshasa uliopo kusini magharibi mwa taifa hilo.

    Wachambuzi Godwing Gonde na Nicodemus Minde katika mahojiano na BBC Swahili mapema wiki hii walisema kwamba hatua ya kundi hilo kuuteka mji wa Walikale ni ishara kwamba azimio lao la kuingia tena Kinshasa bado lipo.

    “Mnamo 1997 waliingia Kinshasa ila hawakukaa kwa muda, na sasa wanavyotekeleza mipangilio yao ya kuteka miji mikuu katika eneo la msahariki mwa DRC, inaonekana wazi kwamba wana lengo moja tu,’ alisema Dkt. Nicodemus Minde ambaye ni mtafiti katika taasisi ya utafiti wa usalama wa kimataifa ISS.

    Kwa upande wake, Gonde ambaye ni mhadhiri wa Diplomasia na mchambuzi wa masuala ya usalama wa Kikanda, anahisi kwamba; ‘ hali ya kuendelea kuteka miji katika eneo la mashariki mwa DRC inaathiri hali ya maisha ya kila siku kwa raia ambao hawana huduma muhimu kama vile ya benki ambazo zilifungwa tangu mapigano yaanze mashariki mwa DRC, na hali inatatizika pakubwa kwa kuwa viwanja vikuu vya ndege katika eneo hilo vimekaliwa na wapiganaji wa M23 na kuzuia huduma muhimu kama dawa na chakula kuwafikia waathiriwa.’

    Jumanne Machi 18, kundi hilo lilijiondoa kwenye mkutano uliopangwa na Rais wa Angola , kuwaleta pamoja viongozi wakuu wa M23 na wawakilishi wa serikali ya DRC ambapo pia ilitarajiwa kwamba Rais Felix Tsishekedi angehudhuria.

    Japo M23 ilituma ujumbe wa watu tano, kiongozi wa CRA Corneille Nangaa, wala Sultani Makenga wa M23 hawakusafiri hadi Luanda, huku kundi lililotumwa Angola likisema kwamba vikwazo dhidi ya maafisa wao wakuu ni dhuluma dhidi yao ambayo hawakufurahia.

    Huku wakisema kwamba hatua yao ya kuondoka Walikela ni ya kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa katika eneo hilo, kundi hilo pia limesema kwamba linasubiri kuona ikiwa jeshi la FARDC litazingira mji huo ama litachukuwa hatua gani.

    Upande wa serikali ya DRC imesema kwamba wao pia wanasubiri kuona ikiwa M23 itaondoa wapiganaji wao kutoka kwa mji huo kama walivyoahidi.

  9. Mjumbe wa Trump apuuza mpango wa waziri mkuu wa Uingereza kuhusu Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer

    Mpango wa waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer kwa kikosi cha kimataifa kusaidia usitishaji vita nchini Ukraine umepuuziliwa mbali na mjumbe maalum wa Donald Trump.

    Steve Witkoff alisema wazo hilo lilitokana na dhana "rahisi" ya waziri mkuu wa Uingereza na viongozi wengine wa Ulaya wanaofikiri "sote lazima tuwe kama Winston Churchill".

    Katika mahojiano na mwandishi wa habari anayemuunga mkono Trump Tucker Carlson, Witkoff alimsifu Vladimir Putin, akisema "alimpenda" rais wa Urusi. "Simchukulii Putin kama mtu mbaya," alisema.

    "Yeye ni mwerevu sana." Witkoff, ambaye alikutana na Putin siku kumi zilizopita, alisema rais huyo wa Urusi alikuwa na "neema" za "moja kwa moja" naye.

    Putin alimwambia, kwamba alikuwa amemuombea Trump baada ya jaribio la mauaji dhidi yake mwaka jana.

    Pia alisema Putin alitengeneza picha ya rais wa Marekani kama zawadi na Trump "aliguswa na hatua hiyo ".

    Wakati wa mahojiano, Witkoff alirudia hoja mbalimbali za Kirusi, ikiwa ni pamoja na kwamba Ukraine ilikuwa "nchi ya uongo" na kuuliza ni lini ulimwengu ungetambua eneo la Ukraine linalokaliwa na Urusi.

    Witkoff anaongoza mazungumzo ya Marekani ya kusitisha mapigano na Urusi na Ukraine lakini hakuweza kutaja mikoa mitano ya Ukraine iliyotwaliwa au inayokaliwa kwa kiasi fulani na majeshi ya Urusi.

    Alisema: "Suala kubwa katika mgogoro huo ni mikoa minne, kwa majina ya Donbas, Crimea,." Mikoa mitano - au oblasts - ni Luhansk, Donetsk, Zaporizhzhia, Kherson na Crimea.

    Donbas ni eneo la viwanda mashariki ambalo linajumuisha sehemu kubwa ya Luhansk na Donetsk. Witkoff alitoa madai kadhaa ambayo si ya kweli au yanabishaniwa

  10. Hereni zenye thamani ya $769,500 zapatikana na polisi baada ya anayedaiwa kuwa mwizi kuzimeza

    .

    Chanzo cha picha, Orlando police

    Polisi wa Orlando wamepata hereni mbili za almasi zenye thamani ya $769,500 (£597,000) baada ya anayedaiwa kuwa mwizi kuzimeza zaidi ya wiki mbili zilizopita.

    Jaythan Gilder, 32, alimeza hereni hizo za Tiffany & Co. wakati alipowekwa kizuizini tarehe 26 Februari, polisi walisema.

    Bw Gilder alifuatiliwa na wapelelezi katika hospitali ya Orlando kwa "zaidi ya siku kumi na mbili" kabla ya hereni hizo kutolewa tumboni, kulingana na Idara ya Polisi ya Orlando.

    Bw Gilder anakabiliwa na mashtaka ya wizi kwa kutumia barakoa na wizi mkubwa wa kiwango cha kwanza. Kampuni ya Tiffany imesafisha hereni hizo tangu wakati huo.

    Polisi wanadai kuwa Bw Gilder alijifanya msaidizi wa mchezaji wa mpira wa vikapu NBA ili aweze kuonyeshwa "vito vya hali ya juu" katika chumba cha watu mashuhuri katika duka la Tiffany & Co. huko Orlando, Florida mnamo 26 Februari.

    Bw Gilder alidaiwa kuwachanganya wafanyikazi wa duka hilo, kisha akakimbia kutoka dukani akiwa na hereni mbili za almasi.

    Inaelekea mshukiwa pia alidondosha hereni ya almasi yenye thamani ya $587,000 alipokuwa akitoroka dukani.

    Maafisa walipomkamata baadaye siku hiyo, waliona Bw Gilder "akimeza vitu kadhaa vinavyoaminika kuwa hereni zilizoibwa," polisi walisema. Maafisa waliomsafirisha Bw Gilder hadi jela inadaiwa walimsikia akisema, "Nilipaswa kuzitupa nje ya dirisha," CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani, iliripoti.

    Katika jela, Bw Gilder alidaiwa kuwauliza wafanyakazi, "Je, nitashtakiwa kwa kile kilicho tumboni mwangu?"

  11. Shambulio la angani lamuua afisa mkuu wa Hamas huko Gaza

    ..

    Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

    Maelezo ya picha, Mhusika mkuu wa Hamas Salah al-Bardaweel, aliyeonyeshwa hapa kwenye picha mwaka wa 2015, aliuawa huko Khan Younis.

    Shambulizi la anga la Israel katika mji wa kusini wa Khan Younis huko Gaza limemuua kiongozi mkuu wa chama cha Hamas Salah al-Bardaweel, afisa wa Hamas aliambia BBC mapema Jumapili.

    Wenyeji wanasema shambulizi hilo la anga liliua wote wawili Bardaweel, mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo, na mkewe.

    Maafisa wa Israel hawakuwa na maoni ya mara moja.

    Jeshi la Israel lilianza tena mashambulizi makubwa dhidi ya Gaza siku ya Jumanne, likiilaumu Hamas, na kuacha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza tarehe 19 Januari na kuhitimisha takriban miezi miwili ya utulivu.

    Hamas ilikanusha shutuma hizo za Israel na kuishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalitiwa saini na kuratibiwa na Qatar, Misri na Marekani.

  12. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja