Uganda yakanusha kupeleka wanajeshi zaidi mashariki mwa DRC

Msemaji wa Naibu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda ameiambia BBC kwamba jeshi la Uganda linadumisha tu wanajeshi waliopelekwa DRC chini ya operesheni ya pamoja na vikosi vya Congo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Kiongozi wa zamani wa Kenya azungumza juu ya mkwamo wa kutafuta amani DR Congo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa ukosefu wa nia njema ya kisiasa kumekwamisha mazungumzo ya amani kushughulikia mzozo wa DR Congo.

    Bwana Kenyatta, mpatanishi wa mchakato unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema kwamba kuna haja ya kufanya mazungumzo kati ya pande zinazozozana.

    Katika taarifa yake Alhamisi, rais huyo wa zamani anasisitiza kwamba michakato ya amani ya Nairobi na Luanda ina ahadi kubwa kwa azimio la mzozo huo.

    Yakiwa yalianzishwa mnamo mwezi Aprili 2022, mchakato wa Nairobi unatafuta kuwashirikisha wadau ikiwa ni pamoja na serikali ya DR Congo, makundi yenye silaha, asasi za kiraia, na jamii ya kimataifa katika kupata azimio la amani kupitia mazungumzo.

    Mchakato wa Luanda ulianzishwa mnamo mwaka 2022 lakini mapigano kati ya kikundi cha waasi cha M23 na Jeshi la Congo (FARDC) mnamo mwezi Oktoba 2023 kulisababisha mkwamo.

    Kulingana na Bwana Kenyatta, michakato hiyo miwili ya amani ilikuwa imewekwa kando baada ya uchaguzi wa Desemba 2023 huko DR Congo.

    Soma zaidi:

  3. Jeshi la Sudan lafanikiwa kukomboa baadhi ya maeneo

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Jeshi la Sudan linasema limefanikiwa kusonga mbele katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum wakati linaendelea kupigana na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF).

    Madai hayo hayajathibitishwa kwa uhuru lakini ripoti kadhaa zinaonyesha kuwa katika wiki za hivi karibuni, vikosi vya jeshi vimesonga mbele katika sehemu za jiji hilo.

    Msemaji wa jeshi alisema vikosi vya jeshi la Sudan vilikuwa vimewarudisha nyuma wapiganaji wa RSF na kuchukua baadhi ya maeneo huko Khartoum, pamoja na sehemu ya viwandani.

    Hili linawadia karibu wiki mbili baada ya jeshi kutangaza kuwa limefanikiwa kuingia katika makao makuu ya mji huo, ambao ulikuwa umezingirwa na vikosi vya RSF tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2023.

    Hata hivyo, kwasababu imekuwa vigumu kuingia ndani ya mji huo sio rahisi kuthibitisha madai ya jeshi.

    Mapigano makali yamekuwa yakiriporiwa katika wiki za hivi karibuni huko Khartoum na sehemu zingine za Sudan.

    Mapigano hayo yanaendelea kuhatarisha mgogoro wa kibinadamu ambao umesababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    Soma zaidi:

  4. Korea Kusini yaamuru viwanja vya ndege kuweka kamera za kutambua ndege wa angani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Viwanja vyote vya ndege vya Korea Kusini vitahitajika kuweka kamera za kutambua ndege wa angani kwenye rada, baada ya ajali ya ndege iliyotokea mnamo mwezi Desemba mwaka jana na kuua watu 179.

    Kutumika kwa kamera hizo kunatarajiwa kuanza mwaka 2026.

    Wachunguzi walisema wiki iliyopita kwamba walipata ushahidi wa ndege wa angani ileingia kwenye injini ya ndege ya Boeing 737-800 - manyoya na matone ya damu pia yalipatikana kwenye injini zote mbili za ndege.

    Uchunguzi wa ajali hiyo - mbaya zaidi kutokea kwenye ardhi ya Korea Kusini - bado unaendelea lakini utajikita zaidi ndege wa angani na muundo wa zege mwishoni mwa barabara ya kuruka ndege, ambayo ndege hiyo iligonga baada ya kutua kwa dharura.

    Soma zaidi:

  5. Waasi wa M23 wamefanya mkutano wao wa kwanza Goma

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wamefanya mkutano wao wa kwanza katika mji wa Goma nchini ya DR Congo tangu kuuteka wiki iliyopita.

    Umati mkubwa ulizuia barabara karibu na Unity stadium na kulikuwa na ripoti za kusikika kwa milio ya risasi huku watu wengine wakikimbilia usalama wao.

    Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya kikundi cha waasi cha M23 kuanzisha mapigano mapya, na kuuteka mji wa madini wa Nyabibwe.

    Nyabibwe ni karibu km 100 kutoka Bukavu-mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa DR Congo ambao waasi wanalenga.

    Mapema wiki hii, walikuwa wametangaza kusitisha mapigano kwa misingi ya kibinadamu.

    UN inasema karibu watu elfu tatu wameuawa tangu mapigano kuanza.

    Viongozi kutoka jamii ya maendeleo ya Afrika Kusini na jamii ya Afrika Mashariki watakutana nchini Tanzania kuanzia Ijumaa, kujadili jinsi ya kutatua mzozo huo.

    Soma zaidi:

  6. Panama yakanusha madai ya Marekani kupita kwenye mfereji huo bila malipo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Panama imekanusha kuwa imefanya mabadiliko ya kuruhusu meli za serikali ya Marekani kupita kwenye Mfereji wa Panama bila malipo, kufuatia madai ya Ikulu ya White House kuwa imekubali hatua hiyo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ilisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X kwamba meli za serikali "sasa zinaweza kuvuka Mfereji wa Panama bila malipo, na kuokoa serikali ya Marekani mamilioni ya dola kwa mwaka".

    Ikijibu maoni hayo, Mamlaka ya Mfereji wa Panama (ACP) ilisema "imepewa uwezo wa kuweka ushuru na ada nyinginezo za kuwezesha kupita mfereji huo," na kuongeza kuwa "haijafanya marekebisho yoyote kwao".

    Rais wa Marekani Donald Trump amerudia kueleza nia yake ya kutaka kudhibiti tena njia hiyo ya maji, ambayo ni muhimu kwa biashara ya kimataifa.

    Mfereji wa Panama wenye urefu wa maili 51 (km 82) upo katika taifa la Amerika ya Kati na ndio kiunganishi kikuu kati ya bahari ya Atlantiki na Pasifiki.

    Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, ambaye amekuwa ziarani katika nchi za Amerika Kusini wiki hii, aliitaka Panama kufanya "mabadiliko ya haraka" kwa kile anachokiita "ushawishi na udhibiti" wa China juu ya mfereji huo.

    Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani alisema Panama ilibidi ichukue hatua la sivyo Marekani itachukua hatua zinazohitajika kulinda haki zake chini ya mkataba kati ya nchi hizo mbili.

    Soma zaidi:

  7. Uganda yakanusha kupeleka wanajeshi zaidi mashariki mwa DRC

    .

    Chanzo cha picha, Ugandan army

    Uganda yakanusha kupeleka wanajeshi zaidi mashariki mwa DRC

    Jeshi la Uganda limekanusha madai kwamba limepeleka wanajeshi wake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambapo vikosi vya Congo vinapigana na waasi wa M23.

    Awali, ripoti zinaonyesha vyanzo vya kidiplomasia vya UN vilidai kwamba nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilikuwa imetuma wanajeshi zaidi ya 1,000 Mashariki mwa Congo karibu na maeneo ambayo mapigano yanaendelea kati ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na wanajeshi wa Congo, huku hofu ikiongeza juu ya kugeuza mzozo huo kuwa wa kikanda.

    Hata hivyo, Kanali Deo Akiiki, msemaji wa Naibu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda ameiambia BBC kwamba jeshi la Uganda linadumisha tu wanajeshi waliopelekwa DRC chini ya operesheni ya pamoja na vikosi vya Congo dhidi ya wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF).

    "Habari kwamba tumepeleka vikosi vipya DRC sio kweli," alisema.

    "Tumebadilisha sehemu tuliyokuwa tu kama tulivyofahamisha ulimwengu hivi karibuni kuimarisha misingi yetu ya ushirikiano ili kuzuia kutanuka kwa mzozo huo katika eneo letu la pamoja la kufanya kazi na vikosi vya DRC."

    Tangu mwaka 2021, vikosi vya Uganda vimekuwa vikifanya mashambulizi ya kijeshi ya pamoja na vikosi vya Congo dhidi ya ADF katika maeneo ya Kivu na Ituri.

    Wataalam wa UN hapo awali walishutumu Uganda na Rwanda kwa kuunga mkono M23, madai ambayo nchi zote mbili zimekanusha mara kwa mara.

    Tangu kutekwa kwa mji wa Goma, waasi wa M23 wamekuwa wakitafuta kuteka maeneo ya Kivu Kusini, haswa mji mkuu wa Bukavu.

    Viongozi wa DRC pia walisema mashambulizi mapya yameanza kuchukua tena mkoa wenye utajiri wa madini, siku mbili tu baada ya waasi kutangaza kusitisha mapigano.

    UN ilisema karibu watu 3,000 waliuawa wakati wa mashambulizi ya M23 ya kuuteka mji wa Goma.

    Soma zaidi:

  8. Trump apiga marufuku wanamichezo wa kike waliobadili jinsia kushindana mashindano ya wanawake

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo linalozuia wanawake waliobadili jinsia kushindana katika michezo ya wanawake.

    "Kuanzia sasa, michezo ya wanawake itakuwa ya wanawake tu," Trump alisema, akizungukwa na wanariadha wanawake na wasichana kabla ya kusaini agizo hilo huko White House. "Kwa agizo hili, vita juu ya michezo ya wanawake imekwisha."

    Kulingana na yeye, Marekani itakataza visa wanamichezo waliobadili jinsia.

    Agizo hilo ambalo linaanza kutumika mara moja linatoa mwongozo, kanuni na tafsiri za kisheria, na litaorodhesha Idara ya Elimu kuchunguza shule za upili zinazodhaniwa kutofuata sheria.

    Warepublican wanasema hatua hiyo inarejesha usawa katika michezo lakini wanaotetea haki za LGBT na mashirika ya haki za binadamu yameielezea kama ya kibaguzi.

    Afisa wa utawala alisema kuwa agizo hilo litabadilisha msimamo wa utawala wa Biden ambao mnamo mwezi Aprili mwaka jana ulisema kwamba wanafunzi wa LGBT watalindwa na sheria ya shirikisho, ingawa haikutoa mwongozo maalum kwa wanariadha waliobadilisha jinsia.

    Rais Trump alibainisha kuwa agizo hilo litajumuisha Michezo ya Olimpiki ya 2028 huko Los Angeles.

    Siku ya kwanza ya Trump madarakani tarehe 20 Januari, alitia saini agizo tofauti akitaka serikali ya shirikisho ifafanue rasmi jinsia kuwa ni mwanamume au mwanamke.

    Soma zaidi:

  9. Kuhama kwa Wagaza itakuwa kwa muda tu - Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuwapa makazi mapya wakazi wa Gaza litakuwa la muda tu, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio amesema.

    Hilo inafuatia pendekezo la Trump kwamba Marekani inaweza "kuchukua" Gaza na kuwapa makazi mamilioni ya Wapalestina wanaoishi huko - wazo ambalo limeleta ukosoaji kutoka kwa Umoja wa Mataifa, mashirika ya haki za binadamu na viongozi wa Kiarabu.

    Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt alifafanua zaidi maoni ya Trump, akisema kuwa Marekani haina mpango wa "kujikita" katika eneo hilo.

    Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz amesema Wagaza "wanapaswa kupewa uhuru wa kutoka na kuingia", lakini alitoa maelezo machache juu ya jinsi hili litafanyaka.

    Akiwa safarini Guatemala, Marco Rubio alisema pendekezo la Trump si la "chuki", bali kitendo cha "ukarimu", inayoonyesha "nia ya Marekani kuwajibika kwa ujenzi wa eneo hilo".

    Alisema wazo lilikuwa Wagaza kuondoka katika eneo hilo kwa kipindi cha "muda" wakati vifusi vinaondolewa na ujenzi upya unafanyika.

    Trump alisema Jumanne kwamba uhamisho huo utakuwa wa kudumu.

    Maoni yake yanawadia baada ya Donald Trump kupendekeza kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza na kuijenga upya kuwa "eneo la kitalii la Mashariki ya Kati".

    Soma zaidi:

  10. Karibu kwenye muendelezo wa matangazo yetu ya moja kwa moja mchana huu ukiwa nami Asha Juma.

  11. Israel yaamuru jeshi kuandaa mpango wa kuwaruhusu wakazi wa Gaza kuondoka

    vc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wapalestina ambao walihamishwa na kupelekwa kusini kwa amri ya Israel wakirejea makwao kaskazini mwa Gaza

    Siku ya Alhamisi Waziri wa ulinzi wa Israel ameliamuru jeshi kuandaa mpango wa kuruhusu "kuondoka kwa hiari" wakaazi wa Gaza, vimeripoti vyombo vya habari vya Israel.

    Maagizo hayo yanakuja kufuatia tangazo la Trump kwamba Marekani inapanga kuichukua Gaza, na kuwapeleka Wapalestina wanaoishi huko sehemu nyingine na kulibadilisha eneo hilo kuwa "kivutio cha Mashariki ya Kati."

    Ninakaribisha mpango wa Rais Trump, wakaazi wa Gaza wanapaswa kuruhusiwa kwa hiari kuondoka na kuhama," Channel 12 ya Israel imemnukuu Katz.

    Alipoulizwa ni nani atawachukua Wapalestina hao, Waziri huyo amesema, “zinapaswa kuwa ni nchi ambazo zinapinga operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza.”

    "Nchi kama Uhispania, Ireland, Norway, na zingine, ambazo zimetoa shutuma na madai ya uwongo dhidi ya Israel juu ya operesheni yake huko Gaza, zina wajibu wa kisheria kuruhusu mkaazi yeyote wa Gaza kuingia katika maeneo yao," amesema.

    “Unafiki wao utafichuka kama watakataa kufanya hivyo. Kuna nchi kama Canada, ambayo ina mpango wa kupokea wahamiaji, ambayo hapo awali imeonyesha nia ya kuwapokea wakazi wa Gaza."

    Mpango wa Katz utajumuisha kuchagua kuondoka kupitia vivuko vya ardhini, pamoja na mipangilio maalumu wa kuondoka kupitia baharini na angani, imeripoti Channel 12.

    Wazo tata la Trump, ambalo limezua hasira katika eneo la Mashariki ya Kati, linakuja wakati Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas wakitarajiwa kuanza mazungumzo juu ya duru ya pili ya mpango wa kusitisha mapigano ili kumaliza karibu miezi 16 ya mapigano huko Gaza.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mzozo wa DRC 'Muda wa kuwazika waliouawa wazidi kuyoyoma'

    Maelezo ya video, Mzozo wa DRC 'Muda wa kuwazika waliouawa wayoyoma'

    Vyumba vya kuhifadhi maiti vilivyofurika na uhaba wa ardhi ya kuwazika waliofariki inatishia kuzuka kwa magonjwa wakati mzozo ukiendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Karibu watu 3,000 wameripotiwa kuuawa katika makabiliano kati ya waasi wa kundi la M23 na wanajeshi wa Congo mashariki mwa nchi hiyo.

    Mashirika ya kutoa misaada yanasema miili ya watu waliouawa inastahili kuzikwa haraka iwezekanavyo kwasababu vyumba cha kuhifadhi maiti viimefurika.

    Yanasema hali hiyo inahatarisha maisha ya watu wanaoishi katika kambi ya wakimbizi na jamii zinazoishi karibu na kambi hizo.

  13. Usitishaji mapigano Congo uko mashakani baada ya waasi kuteka mji mwingine

    d

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mtu akikagua gari lililoungua wakati wa mapigano katika mji wa Goma ambao umeangukia mikononi mwa waasi wa M23, Februari 5, 2025.

    Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa wenye madini katika jimbo la Kivu Kusini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, vyanzo nane vimesema siku ya Jumatano.

    Shirika la habari ya Reuters limeripoti kuwa huo utakuwa ni ukiukaji wa usitishaji mapigano ambao waasi hao walitanganza wiki hii. M23 ilitangaza kusitisha mapigano siku ya Jumatatu.

    Kutekwa kwa mji wa Nyabibwe kwenye Ziwa Kivu kunawapeleka waasi karibu na mji mkuu wa jimbo la Bukavu kilomita 70 kusini, mji ambao waasi walisema wiki iliyopita kwamba hawana na nia ya kuuteka.

    Watu wanane, wakiwemo viongozi wa eneo hilo, mwakilishi wa mashirika ya kiraia, waasi na chanzo kutoka usalama wa taifa, wameithibitishia Reuters kuwa Nyabibwe iko mikononi mwa waasi.

    "Kumekuwa na mapigano na mji uliangukia mikononi mwa waasi. Wako katikati mwa mji kwa sasa," alisema kiongozi huyo wa mashirika ya kiraia, ambaye kama vyanzo vingine alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

    Nyabibwe, kuna migodi ambayo huzalisha dhahabu, coltan na metali, ni kitovu cha biashara kati ya Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini ambao waasi waliuchukua wiki iliyopita, na Bukavu.

    Waziri wa Mawasiliano wa Congo, Patrick Muyaya ameliambia shirika la habari la Reuters, waasi walikiuka usitishaji mapigano na wameingia katika mapambano na wanajeshi wa Congo karibu na Nyabibwe.

    Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa waasi wa Congo River Alliance unaojumuisha M23, alithibitisha kuwa kundi hilo limekwenda Nyabibwe. "Walitushambulia na tukajilinda," ameiambia Reuters.

    Kwa upande mwingine, mahakama ya kijeshi ya Congo imetoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Nangaa siku ya Jumanne ikimtuhumu kwa uhalifu wa kivita na uhaini.

    Kutekwa kwa mji wa Goma, ulio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kumesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kuzua hofu ya kutokea kwa vita vya kikanda.

    Congo inaishutumu Rwanda kwa kutumia M23 kupora madini. Rwanda imekana madai hayo na inasema inajilinda na kulinda kabila la Watutsi

    Pia unaweza kusoma:

  14. Binti wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ashtakiwa

    c

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Duduzile Zuma, binti wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma

    Duduzile Zuma-Sambudla, binti wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amefikishwa mahakamani siku ya Alhamisi baada ya kushtakiwa kwa kuchochea ghasia wakati wa vurugu za mwaka 2021 ambapo zaidi ya watu 300 waliuawa.

    Waendesha mashtaka wanadai kuwa Zuma-Sambudla alichochea watu wengine kufanya vurugu kupitia machapisho kwenye mitandao ya kijamii Julai 2021, baada ya babake kukamatwa kwa kutotii amri ya mahakama ya kutoa ushahidi katika uchunguzi wa rushwa.

    Hasira juu ya kufungwa kwa Zuma ziligeuka kuwa ghasia, na kusababisha uporaji wa maelfu ya maduka, uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umma na vifo vya takriban watu 350.

    Jacob Zuma alikwenda na Zuma-Sambudla hadi katika mahakama ya Durban. Atarudi tena mahakamani mwezi Machi.

    Baada ya hukumu yake ya kudharau mahakama kumalizika mwaka 2022 Zuma aliunga mkono chama kipya cha siasa cha Umkhonto we Sizwe (MK).

    MK kilishinda viti 58 vya ubunge. Zuma-Sambudla ni mmoja wa wabunge wa MK katika baraza la chini la bunge

    Pia unaweza kusoma:

  15. Palestina na mataifa ya Kiarabu yakataa mpango wa Trump wa kuikalia Gaza

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Idadi kubwa ya wakazi milioni 2.1 wa Gaza wamekimbia makazi yao kutokana na vita vya miezi 15 kati ya Israel na Hamas.

    Rais wa Palestina amekataa vikali pendekezo la Rais Donald Trump la Marekani kuitwaa Gaza na kuwahamisha wakazi wa Wapalestina milioni 2.1 wanaoishi huko.

    "Hatutaruhusu haki za watu wetu, kukiukwa," amesema Mahmoud Abbas, akionya kwamba Gaza ni "sehemu muhimu ya jimbo la Palestina" na kuwahamisha watu kwa nguvu utakuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

    Wazo la Trump limekataliwa na nchi nyingine katika eneo hilo kama vile Jordan na Misri, ambao ni washirika wakuu wa Marekani, huku Umoja wa Mataifa ukitoa onyo dhidi ya "aina yoyote ya kuwafukuza watu kwa nguvu."

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Gaza ni sehemu muhimu ya taifa la baadaye la Palestina. Amesema huko New York kwamba haki za Wapalestina kuishi kama binadamu katika ardhi yao zinazidi kukiukwa.

    Saudi Arabia imesema Wapalestina "hawatahama" kutoka katika ardhi yao na haitarekebisha uhusiano na Israel bila kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema pendekezo la Trump linaweza "kubadilisha historia" na "linastahili kuzingatiwa".

    Baadaye siku ya Jumatano, Ikulu ya White House ilifafanua pendekezo hilo la Rais Trump, na msemaji wake Karoline Leavitt akiwaambia waandishi wa habari kuwa rais amejitolea kuijenga upya Gaza na kuwahamisha kwa muda wakaazi wake. Lakini Trump alisema siku ya Jumanne uhamisho huo utakuwa wa kudumu.

    Kauli ya Trump inakuja wiki mbili baada ya kuanza kwa usitishaji vita huko Gaza, ambapo Hamas imewaachia huru baadhi ya mateka wa Israel inaowashikilia ili kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walio katika jela za Israel.

    Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu shambulio la kuvuka mpaka tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na 251 walichukuliwa mateka.

    Zaidi ya watu 47,540 wameuawa na 111,600 kujeruhiwa huko Gaza tangu mashambulizi hayo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

    Idadi kubwa ya wakazi wa Gaza pia wamelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa, karibu 70% ya majengo yameharibiwa na huduma za afya, maji, usafi wa mazingira zimetatizika, na kuna uhaba wa chakula, mafuta, dawa na makazi.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Prince Rahim Al-Hussaini ateuliwa kuwa Aga Khan mpya

    d

    Chanzo cha picha, X/Aga Khan Development Network

    Maelezo ya picha, Prince Rahim Al-Hussaini ni Aga Khan wa 50

    Prince Rahim Al-Hussaini ametangazwa kuwa Aga Khan mpya, kiongozi wa kiroho wa mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ya Ismailia.

    Atachukua nafasi hiyo kutoka kwa babake Prince Karim Aga Khan, aliyefariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 88.

    Uteuzi huo ulifanywa baada ya wasia wa Prince Karim kufichuliwa, imesema taarifa ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan.

    Prince Rahim Al-Hussaini Aga Khan V atakuwa Imamu wa 50 wa Waislamu wa Ismailia, ambao wanasema wao ni kizazi cha moja kwa moja cha Mtume Muhammad.

    Ismaili ni madhehebu ya Waislamu wa Shia ambao ni wafuasi wa Maimamu kadhaa, akiwemo Imam Ismail, aliyefariki mwaka AD765.

    Idadi yao duniani kote inafika milioni 15, wapatao 500,000 wakiwa nchini Pakistani. Pia kuna idadi kubwa ya wafuasi nchini India, Afghanistan na sehemu za Afrika.

    Prince Karim Aga Khan alimrithi babu yake kama Imamu wa Waislamu wa Ismailia mwaka 1957 akiwa na umri wa miaka 20.

    Alikufa akiwa amezungukwa na familia huko Lisbon, Ureno, ambako ndio makao ya Maimamu wa Ismailia. Mazishi yatafanyika huko siku zijazo.

    Wakati akiwa kiongozi wa kiroho wa jumuiya ya Kiislamu ya Ismailia, marehemu Aga Khan alisaidia kuundwa shirika la hisani lenye jukumu la kuendesha mamia ya hospitali, miradi ya elimu na kitamaduni, haswa katika ulimwengu unaoendelea.

    Aga Khan mpya ndiye mtoto wa kwanza wa babake marehemu na mamake Begum Salimah, mwanamitindo wa zamani wa Uingereza ambaye alisilimu na kubadili jina lake kutoka Sarah Croker Poole.

    Prince Rahim ana watoto wawili wa kiume kupitia ndoa yake na mwanamitindo wa zamani wa Marekani Kendra Spears.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Wamarekani wenye asili ya Palestina wakasirishwa na mpango wa Trump wa kuitwaa Gaza

    dx

    Chanzo cha picha, Laila El-Haddad

    Maelezo ya picha, Laila El-Haddad, Mmarekani mwenye asili ya Palestina, anasema "mpaka ukiwa wazi, tunataka kurejea" Gaza.

    Wapalestina ambao ni Wamarekani wameelezea kukerwa na pendekezo la Donald Trump la "kuchukua" udhibiti wa Gaza, mahali ambapo wengi wao bado wanapaona ni nyumbani.

    "Haki yetu ya kurudi, ni jambo ambalo tunalifikiria katika maisha yetu yote," anasema Iman Kishawi, aliyezaliwa Gaza lakini sasa anaishi Los Angeles.

    Anasema amekerwa sana na kile kilichosemwa na Rais Trump, akiuliza: "Wewe ni nani kumiliki ardhi hiyo?"

    Alipokutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne, Trump alipendekeza kwamba Wapalestina watahamishwa kupelekwa mahali pengine huku Marekani ikichukua eneo hilo na kuligeuza kuwa "kivutio cha Mashariki ya Kati."

    Katika mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, Netanyahu, kiongozi wa kwanza wa kimataifa kuzuru Ikulu ya White House tangu kuapishwa kwa Trump, alisema: "Marekani itachukua Ukanda wa Gaza, na tutafanya nao kazi pamoja."

    Laila El-Haddad, mwandishi na mwanaharakati wa Marekani mwenye asili ya Palestina, anasema "alipigwa na butwaa."

    "Inaonyesha tu aina ya dharau na kutojali maisha ya Wapalestina na ubinadamu wa Palestina na hadhi ya Wapalestina.”

    Baadhi ya Warepublican wamemtetea Trump au kutaka kufafanua matamshi yake, huku wengine wakilieleza pendekezo hilo kwa mashaka na mkanganyiko.

    Tariq Luthun, Mmarekani mwenye asili ya Palestina anayeishi Michigan, ameiambia BBC, "kila siku ninapoamka, huangalia ikiwa familia yangu iko hai," anasema "nilishitushwa na matamshi ya Trump.”

    Anasema pendekezo la Trump kuwa ni mwendelezo wa "sera ya ubeberu wa Marekani."

    Pia unaweza kusoma:

  18. Rais wa Malawi aagiza wanajeshi wake kujiandaa kuondoka Mashariki mwa DRC

    Chakwera

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera

    Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amemuagiza kamanda wa jeshi la nchi hiyo kujiandaa kuondoa majeshi ya Malawi kutoka eneo la Mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kulingana na taarifa Televisheni ya serikali.

    Taarifa hiyo ilisema uamuzi wa rais unalenga "kuheshimu tangazo la kusitisha mapigano kati ya pande zinazozana," ingawa uamuzi wa kusitisha mapigano ulikuwa ni mpango wa waasi wa M23 ambao ulitibuka baada ya kundi hilo kushambulia Nyabibwe katika Jimbo la Kivu Kusini mwa DRC.

    Kuondolewa kwa wanajeshi wa Malawi "kutatoa nafasi mazungumzo yaliyopangwa kuelekea amani ya kudumu," iliongeza taarifa hiyo.

    Rais Lazarus Chakwera amekuwa chini ya shinikizo la kuondoa majeshi ya nchi yake Mashariki mwa DRC baada ya wanajeshi watatu wa Malawi kuuawa katika mashambulizi ya M23 mjini Goma.

    Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Kusini mwa Afrika uliotumwa na SADC kusaidia mamlaka ya Congo kukabiliana na makundi yenye silaha katika eneo la mashariki linalokabiliwa na mzozo.

    Kufuatia M23 kuuteka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, wamekuwa wakitafuta kuteka maeneo ya Kivu Kusini, hasa mji mkuu Bukavu. Kundi hilo limeteua maafisa wakuu akiwemo gavana wa Kivu Kaskazini, kusimamia eneo hilo.

    Umoja wa Mataifa unasema karibu watu 3000 waliuawa wakati wa makabiliano makali ya M23 ya kuiteka Goma.

    Kuna hofu kwamba magonjwa kama Mpox na kipindupindu yanaweza kuenea nje ya jiji.

    Pia unaweza kusoma:

  19. Maelfu ya wafanyakazi wa USAID wataondolewa kazini kuanzia Ijumaa

    rd

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelfu ya wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) wataondolewa kazini kwa muda kuanzia Ijumaa usiku, limesema shirika hilo.

    Taarifa ya USAID inasema agizo hilo litaathiri "wafanyakazi wa kuajiriwa moja kwa moja" isipokuwa wale walio kwenye "kazi muhimu, uongozi na programu maalumu."

    Haijulikani ni kazi zipi hasa zimeathirika. Taarifa hiyo iliyotumwa kwenye tovuti ya shirika hilo, inasema wafanyakazi watajuulishwa kufikia Alhamisi mchana.

    Utawala wa Trump umesema USAID inafuja pesa na inahitaji kuundwa ili kuendana na vipaumbele vya sera za rais.

    Wafanyakazi wa shirika hilo, wakiungwa mkono na wabunge wa chama cha Democratic, wameandamana kupinga kuondolewa kazini, wakisema hilo litaweka maisha hatarini na kutatiza usalama wa taifa.

    Katika taarifa kwenye tovuti yake siku ya Jumanne, USAID inasema itashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kupanga na kulipia usafiri wa kurejea kwa wafanyakazi waliotumwa nje ya Marekani ndani ya siku 30.

    Shirika hilo linalotoa misaada ya kibinadamu kwa zaidi ya nchi 100, limeajiri watu 10,000 duniani kote. Theluthi mbili ya watu hao wanafanya kazi nje ya nchi, kulingana na Congress.

    USAID, iliyoanzishwa mwaka 1961, ina bajeti ya karibu dola bilioni 40 kwa mwaka, kiasi cha takriban 0.6% ya matumizi ya serikali, kulingana na takwimu rasmi.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Wanasayansi wazalisha kiinitete cha kwanza cha kangaroo kupitia upandikizaji

    dx

    Chanzo cha picha, Queensland

    Maelezo ya picha, Patricio Palacios alikuwa mmoja wa wanasayansi waliohusika katika utafiti huo

    Wanasayansi wa Australia wamezalisha kiinitete cha kwanza cha kangaroo duniani kupitia upandikizaji mimba (IVF), mafanikio ambayo wanasema yanaweza kusaidia kuokoa viumbe vingine ambao wako hatariki kutokweka.

    Watafiti walifanikiwa kudunga seli moja ya mbegu kwenye yai, lakini wanasema kufikia kiini tete hicho kutunga mtoto na kuzaliwa akiwa hai kutahitaji kazi kubwa na "maendeleo ya kiufundi."

    “Kazi hiyo inaweza kusaidia juhudi za kuboresha aina mbalimbali za viumbe vilivyo hatarini kutoweka,” anasema, mtafiti mkuu Andres Gambini.

    Australia ina idadi kubwa ya kangaruu, lakini pia ina kiwango cha juu zaidi cha kutoweka kwa mamalia hao.

    Utafiti huo wa Chuo Kikuu cha Queensland uliangalia ukuaji wa mayai ya kangaruu na manii katika mazingira ya maabara kabla ya kuunda viinitete kwa kutumia njia ya kudunga sindano.

    Ni mbinu, ambayo tayari inatumiwa kwa wanadamu na baadhi ya wanyama wa kufugwa, lakini ilikuwa mara ya kwanza kujaribiwa kwa kwa kangaruu.

    Upandikizaji inatumika kama njia ya kujaribu na kuhifadhi spishi zilizo hatarini ulimwenguni kote.

    Mwaka jana, wanasayansi walipata mimba ya kwanza ya faru kupitia upandikizaji, kwa kufanikiwa kuhamisha kiinitete cha kifaru kilichoundwa katika maabara hadi kwa mama faru nchini Kenya.

    Mwaka 2018, upandikizaji pia ulitumiwa kuunda kiinitete cha kwanza cha punda ulimwenguni.