Biashara, misaada, usalama: Utawala mpya wa Trump una maana gani kwa Afrika?
Wedaeli Chibelushi
BBC News

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump anapojiandaa kula kiapo cha kuiongoza Marekani kwa awamu ya pili bara la Afrika linafuatilia kwa karibu uongozi wake nchini Marekani na Afrika inajiuliza utawala huu mpya wa Trump utakuwa na manufaa kwa bara hilo?
Wakati wa uongozi wake wa kwanza katika Ikulu ya White House wakosoaji walimshtumu kwa kuipuuza Afrika, baada ya kupunguza baadhi ya ufadhili, kuzuia uhamiaji na inasemekana alitaja baadhi ya mataifa yake kama "nchi duni".
Hata hivyo, pia alianzisha mipango ya kuongeza uwekezaji barani Afrika - miradi ambayo inaendelea kufanya kazi miaka mitatu baada ya kuondoka madarakani.
Lakini anawezaje kuifikia Afrika katika hali hii mpya ?
Biashara na uwekezaji
Utawala unaoondoka wa Joe Biden "ulijaribu sana kujenga hisia kwamba Afrika ilikuwa mshirika wa thamani na muhimu," W Gyude Moore, mshirika katika Kituo cha Maendeleo ya Dunia na waziri wa zamani wa Liberia, anaiambia BBC.
Biden alijitahidi kupatanisha shauku hii na mikataba na ushirikiano mkubwa, Bw Moore anasema, lakini hiyo haimaanishi kuwa mkakati wake wa Afrika haukuwa na matunda.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mfano, Marekani ilisifiwa kwa kuwekeza katika Ukanda wa Lobito - njia ya reli inayopitia Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Zambia ambayo itatumika kusafirisha malighafi muhimu.
Mnamo 2023,Marekani ilisema imewekeza zaidi ya $22bn tangu Biden aingie madarakani.
Lakini kuna wasiwasi kwamba Trump anaweza kuondoa uwekezaji na biashara hii. Rais wa hivi karibuni ana mtazamo wa kulinda zaidi maslahi ya nchi yake, usio wa kawaida kuliko Biden - moja ya kauli mbiu za muhula wake wa kwanza ilikuwa "Amerika Kwanza".
Mkataba wa Ukuaji na Fursa ya Afŕika (Agoa), ambao umewezesha nchi zinazostahiki za Afŕika kuuza nje baadhi ya mazao yao kwenda Maŕekani bila kulipa kodi tangu mwaka 2000, ni chanzo kikuu cha wasiwasi.
Wakati wa utawala wake uliopita, Trump alisema mpango huo hautaongezwa muda wakati utakapoisha mnamo 2025.
Na wakati wa kampeni yake ya 2024 aliahidi kutekeleza ushuru wa mapato wa 10% kwa bidhaa zote zinazotengenezwa na nchi za kigeni. Hii itafanya bidhaa zinazoagizwa kuwa ghali zaidi, na hivyo wauzaji nje ya Afrika watakuwa na uwezekano wa kuuza mazao yao kidogo katika soko kubwa la Marekani.
Wachambuzi wengi nchini Afrika Kusini - mmoja wa wauzaji bidhaa nje wakubwa chini ya mkataba wa Agoa - wametabiri kuwa kukata mkataba wa Agoa kunaweza kuwa na athari kubwa katika uchumi.
Hata hivyo, taasisi ya ushauri ya Marekani ya Brookings inatabiri kuwa Pato la Taifa la Afrika Kusini litapungua kwa "asilimia 0.06 pekee". Hii kwa kiasi fulani ni kutokana na kwamba bidhaa nyingi ambazo Afŕika Kusini inauza nje kwenda Maŕekani – kama vile madini na chuma – hazifaidiki na Agoa, ilisema.
Ingawa Trump hakutaka Agoa, alitambua kwamba ikiwa Marekani itakabiliana na ongezeko la ushawishi wa kiuchumi wa China barani Afrika, ilihitaji kudumisha kiwango fulani cha ushirikiano.
Mwaka 2018 utawala wa Trump ulizindua Prosper Africa - mpango ambao unasaidia makampuni ya Marekani yanayotaka kuwekeza Afrika - na Shirika la Fedha la Maendeleo (DFC), ambalo linafadhili miradi ya maendeleo barani Afrika na duniani kote. Biden aliendelea kuuendesha baada ya kuchukua wadhifa wake na DFC inasema hadi sasa imewekeza zaidi ya $10bn (£8bn) barani Afrika.
Ikizingatiwa kuwa China bado ina nguvu kubwa barani Afrika na kwamba Trump alianzisha sera hizi mwenyewe, kuna uwezekano mkubwa wa kufikiria mara mbili kabla ya kuzipunguza.
Misaada
Afrika inapata misaada yake mingi kutoka kwa Marekani, ambayo ilisema imetoa karibu $3.7bn katika mwaka huu wa kifedha.
Lakini utawala wa mwisho wa Trump ulirudia mara kwa mara mapendekezo ya kupunguza misaada ya kigeni duniani kote, kulingana na ripoti. Congress - ambapo misaada ya kigeni ilikuwa na uungwaji mkono kutoka pande mbili - ilikataa punguzo hili.
Kama upunguzaji huo ungetekelezwa, "sera za jadi za Marekani kuhusiana na afya, ukuzaji wa demokrasia, na usaidizi wa usalama barani Afrika zingefutiliwa mbali," lilisema Baraza la Mahusiano ya Kigeni, taasisi ya ushauri ya Washington.
Kunaweza kuwa na msukumo mdogo wa kupunguzwa kwa misaada ikiwa Warepublican watashinda kura nyingi katika Congress kufuatia uchaguzi wa Jumanne, hata hivyo. Chama hicho tayari kimeshinda wingi wa viti katika Seneti - na kwa sasa kina wabunge wengi katika baraza la chini - Baraza la Wawakilishi.
Pia kuna wasiwasi kwamba Trump anaweza kufunga Pepfar, mpango wa muda mrefu wa Marekani ambao umetumia pesa nyingi katika kupambana na VVU barani Afrika.
Mwaka jana, wabunge wa chama cha Republican walipinga kwa kiasi kikubwa Pepfar, kwa madai kuwa mpango huo ulikuwa unakuza huduma za utoaji mimba. Ilipewa nyongeza ya muda mfupi hadi Machi mwaka ujao, lakini Trump - anayejulikana kwa kupinga uavyaji mimba - anaweza kufunga mlango wa ahueni hii
Uhamiaji
Maoni ya Trump kuhusu uhamiaji haramu yako wazi - wakati wa kampeni yake ya 2024 aliahidi kuwafukuza watu milioni moja ambao hawana kibali cha kisheria kuwa nchini Marekani .
Hii inahusu Afrika kwani mnamo 2022, karibu wahamiaji 13,000 wa Kiafrika walisajiliwa kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, kulingana na data ya Forodha ya Amerika na ulinzi wa Mipaka. Kufikia 2023, idadi hii ilikuwa imeongezeka mara nne hadi 58,000. Baadhi ya wahamiaji hawa wanazungumza juu ya kukimbia vita, mateso na umaskini.
Hii haitakuwa sera yake ya kwanza ya kupinga uhamiaji. Katika muhula wake wa kwanza, Trump alianzisha hatua zilizozuia uhamiaji kutoka nchi kadhaa za Afrika, zikiwemo Nigeria, Eritrea, Sudan na Tanzania.
Tovuti ya habari ya Kenya ya Taifo Leo iliripoti kwamba wahamiaji kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki, ambao idadi yao ni takriban 160,000, wana wasiwasi kwamba watakabiliwa na ubaguzi huku Trump akiwa rais.
Usalama na migogoro
Wakati Trump amekuwa nje ya madaraka, Urusi imeongeza uwepo wake barani Afrika.
Mojawapo ya njia kuu ambayo imefanya hivyo ni kwa kutoa wanajeshi na silaha kwa nchi zilizokumbwa na wanamgambo wa kijihadi, kama vile Mali, Niger na Burkina Faso.
Msimamo wa Urusi umeitia wasiwasi Marekani - wawili hao ni wapinzani wa kihistoria.
Je, Trump atatoa msaada kwa nchi za Kiafrika katika jaribio la kuiondoa Urusi?
"Ingawa muundo wa usalama wa taifa nchini Marekani unaiona Urusi kuwa tishio, Trump binafsi hajafanya kana kwamba anaona Urusi kuwa tishio," Bw Moore anaambia BBC.
Kuna uvumi kwamba Trump ana uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuliko anavyoonyesha.
Hata hivyo, Trump katika siku za nyuma alijitokeza kuisaidia Nigeria kupambana na Boko Haram, kundi la wapiganaji wa Kiislamu ambalo limeisumbua nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa miaka 15.
"Wakati wa [Rais wa zamani, Barack] Obama, Wanigeria-Wamarekani walimtetea bila kuchoka, lakini alikataa ombi la Nigeria la silaha. Wakati jumuiya zetu za kaskazini mwa Nigeria zilipokuwa zikishambuliwa na Boko Haram, ni Trump ambaye hatimaye aliidhinisha ununuzi wa ndege za Tucano , kuturuhusu kuimarisha ulinzi wetu," mbunge wa zamani Ehiozuwa Johnson Agbonayinmma aliambia chombo cha habari cha Nigeria Vanguard.
Pia kuna suala la vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, ambavyo vimeendelea kwa muda wa miezi 18 na kuua makumi ya maelfu ya watu.
"Trump anafanya shughuli nyingi," Bw Moore alisema. "Nina shaka kuwa utawala wa Trump utajali zaidi kile kinachotokea Sudan kuliko, tuseme, utawala wa Biden ulivyofanya."
Lakini mwishowe, hakuna njia ya kuwa na uhakika kabisa ni nini Trump ataweka malengo yake mara tu atakapokuwa ofisini.
Kama Bw Moore anavyosema: "Trump si wa kawaida sana katika jinsi anavyofanya kila kitu. Kwa hivyo mtu anapaswa kuwa wazi kwa mambo mapya, si lazima mambo mazuri, lakini mambo mapya yanayotokea."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












