Ajali ya ndege ilisababishwa na “hitilafu za nje” juu ya anga ya Urusi kabla ya kuanguka - Azerbaijan

Haya yanajiri huku mkuu wa shirika la usafiri wa anga la Urusi akisema hali katika eneo la Grozny, ambalo ndege hiyo ilielekea, kulikuwa na "matatizo" wakati huo.

Muhtasari

  • Shirika la Ndege la Azerbaijan lasema ajali ya ndege ilisababishwa na "hitilafu za nje"
  • "Machozi ya furaha" - Msafara wa msaada wa kwanza wawasili Khartoum tangu vita vianze
  • Takriban watu 69 wafariki baada ya meli kuzama katika maji ya Morocco
  • Jeshi la Israel lawalazimisha wafanyakazi wa hospitali kaskazini mwa Gaza kuondoka
  • Chombo cha Nasa chasalamika kwa kukaribia Jua kwa ukaribu zaidi
  • 'Tunaunga mkono Slovakia kuandaa mazungumzo ya amani na Ukraine' - Urusi
  • Somaliland na Ethiopia zakubaliana kutatua kwa amani mzozo unaoendelea
  • Mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyekamatwa na Ukraine afariki dunia
  • Korea Kusini yapiga kura kumtimua kaimu rais Han Duck-soo
  • Waandamanaji wawaua polisi huku ghasia za uchaguzi zikitishia Msumbiji
  • Watu 29 bado hawajapatikana kutokana na utekaji nyara nchini Kenya - KNCHR
  • Video: Tazama hali ilivyokuwa katika uwanja wa ndege wa Yemen kufuatia shambulio la Israel
  • Ukraine yamkamata mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyejeruhiwa, yasema Seoul
  • Mkuu wa WHO ajipata katikati ya mashambulizi ya Israel huko Yemen

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Shirika la Ndege la Azerbaijan lasema ajali ya ndege ilisababishwa na “hitilafu za nje”

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shirika la Ndege la Azerbaijan limesema matokeo ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege yake nchini Kazakhstan iliyotokea mnamo tarehe 25 Desemba yanaonyesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na “hitilafu za kiufundi za nje.”

    Watu 38 walifariki dunia baada ya ndege ya Embraer kuanguka kwa kasi, ikalipuka na kuchomeka takriban kilomita 3 (maili 1.9) kabla ya kufika kwenye uwanja wa ndege wa Aktau.

    Ndege hiyo ilijaribu kutua awali kwenye uwanja wa ndege wa Grozny, kusini mwa Urusi, lakini walioshuhudia ajali hiyo wamesema kulikuwa na mlipuko kabla ya ndege hiyo kuelekezwa Kazakhstan kwa kuvuka Bahari ya Caspian.

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Anga la Urusi alieleza Ijumaa kwamba hali katika mji mkuu wa Chechnya ilikuwa “ngumu sana” na kwamba taratibu za anga zimerejeshwa.

    “Ndege zisizo na rubani za kivita za Ukraine zilikuwa zikishambulia miundombinu ya kiraia katika miji ya Grozny na Vladikavkaz,” alisema Dmitry Yadrov, mkuu wa Rosaviatsia, kwenye video aliyoichapisha kwenye shirika la habari la Urusi, Tass.

    Shirika la Ndege la Azerbaijan halikufafanua hasa ni aina gani ya hitilafu ya kiufundi kutoka nje ya ndege iliofanyika, na serikali ya Baku imeepuka kumtuhumu moja kwa moja Rais Vladimir Putin wa Urusi, labda ili kuepuka kuzua mivutano.

    Hata hivyo, wataalamu wa anga na vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali ya Azerbaijan wanaamini kuwa ndege hiyo iliharibiwa na vipande vya roketi kutoka kwa mlipuko wa kombora la ulinzi wa anga la Urusi.

    Hata hivyo, Urusi imekataa kutoa maoni kuhusu taarifa kwamba ndege ya Shirika la Ndege la Azerbaijan ilishambuliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi.

    Soma zaidi:

  3. “Machozi ya furaha” - Msafara wa msaada wa kwanza wawasili Khartoum tangu vita vianze

    .

    Chanzo cha picha, South Belt Emergency Room

    Msafara wa magari ya msaada wa chakula umefika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, kwa mara ya kwanza tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza mnamo mwezi Aprili 2023.

    Kwa sasa, nchi inakabiliana na “janga kubwa zaidi la njaa duniani,” kulingana na Umoja wa Mataifa, kutokana na mapigano kati ya jeshi na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF).

    Wakati malori yaliyosheheni msaada yalipofika Khartoum Kusini siku ya Alhamisi, walikuwa na “machozi ya furaha na kicheko,” alisema mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada Duaa Tariq alipozungumza na BBC.

    Mashirika ya misaada yamelalamika kwa muda mrefu kwamba vitisho vya kiusalama na vizuizi vya barabara - vilivyowekwa na pande zinazopigana - vimezuia usambazaji wa misaada muhimu.

    Ili kutekeleza hatua hii muhimu, mashirika ya Umoja wa Mataifa na vikundi vya jamii vya Sudan walifanya mazungumzo na jeshi la Sudan na vikosi vya RSF.

    Msafara huo ulijumuisha magari 28.

    Shirika la Unicef - ambalo lilileta magari matano kati ya hayo - lilisema liliweza kusambaza “chakula kuokoa maisha” na vifaa vya afya kwa Hospitali ya Al Bashayer na vituo vingine vya afya vilivyoko Khartoum.

    “Hapa Khartoum, [tunahitaji] msaada huu kwa dharura. Tumekuwa tukiusubiri na tumekuwa tukijaribu njia nyingi kupambana na hili, lakini njia pekee ya kupunguza athari za njaa Khartoum hivi sasa, ni kupokea msaada huu,” alisema Bi Tariq.

    Takribani nusu ya idadi ya watu - milioni 24.6 - wanahitaji msaada wa chakula kwa haraka, ilisema (IPC).

    Soma zaidi:

  4. Takriban watu 69 wafariki baada ya meli kuzama katika maji ya Morocco

    Takriban watu 69, wakiwemo raia wa Mali 25, wamefariki baada ya meli iliyokuwa inatoka Afrika Magharibi kuelekea Hispania kuzama karibu na pwani ya Morocco, mamlaka za Mali zimethibitisha.

    Meli hiyo “ya mpango wa dharura” ilikuwa na abiria takriban 80, lakini ni watu 11 pekee walioishi, ilisema taarifa kutoka kwa Wizara ya Mali Wanaoishi Nje.

    Karibu tisa kati ya waliokolewa ni kutoka Mali.

    Meli ilizama wiki iliyopita, lakini wizara ilithibitisha tukio hilo Alhamisi.

    Kitengo cha dharura kimepelekwa kufuatilia hali hiyo.

    Ukosefu wa ajira na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwenye kilimo pia kumewalazimu wengi kutafuta maisha bora Ulaya.

    Hata hivyo, njia hii ya uhamiaji inayopitia kutoka kwenye fukwe za Atlantiki za Mauritania na Morocco hadi Hispania, inachukuliwa kuwa mojawapo ya njia hatari zaidi duniani.

    Wengi wa wale wanaotumia njia hii hatari wanatoka Afrika ya Kusini mwa Sahara, wakikimbia umaskini na migogoro katika nchi zao za asili.

  5. Jeshi la Israel lawalazimisha wafanyakazi wa hospitali kaskazini mwa Gaza kuondoka

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watu waliokuwa katika hospitali ambayo ilikuwa inahudumia wakaazi wengi Gaza Kaskazini wamefurushwa baada ya mfululizo wa mashambulizi ya anga ya Israel ilioua raia kadhaa.

    Eid Sabbah, mkuu wa idara ya uuguzi katika hospitali ya Kamal Adwan, aliiambia BBC kuwa saa 07:00 za Ijumaa, jeshi liliwaambia viongozi wa hospitali kuwa wana dakika 15 tu kuhamisha wagonjwa na wafanyakazi hadi uwanja wa hospitali.

    Baada ya hapo, wanajeshi wa Israel walifika hospitalini na kuanza kuwahamisha wagonjwa waliobaki, alisema.

    Jeshi la Israel lilisema Ijumaa alasiri kwamba lilikuwa likifanya operesheni katika eneo la hospitali, ambayo iliita “ngome ya kigaidi ya Hamas.”

    Hata hivyo jeshi halikusema ni wapi wagonjwa hao wangehamishiwa, lakini mwanzoni wiki hii, afisa mmoja wa Israel alisema walikuwa na mpango wa kuhamisha wagonjwa kutoka hospitali ya Kamal Adwan kwenda hospitali ya Indonesia iliyo jirani, ambayo nayo ilihamishwa na jeshi Jumanne.

    “Ni hatari kwa sababu kuna wagonjwa wa ICU walioko kwenye koma na wanahitaji mashine za kupumua, na kuhamishwa kwao kutawaweka hatarini,” alisema Dkt. Sabbah.

    “Ikifikiwa na jeshi kuendelea kuhamisha wagonjwa hawa, watahitaji magari maalum,” aliongeza.

    Hii inajiri masaa machache baada ya mkurugenzi wa hospitali ya Kamal Adwan kusema kuwa takribani watu 50 walifariki dunia, wakiwemo wafanyakazi watano wa afya, katika mashambulizi ya anga ya Israel yaliyolenga maeneo ya karibu na hospitali hiyo.

    Soma zaidi:

  6. Chombo cha Nasa chasalamika kwa kukaribia Jua kwa ukaribu zaidi

    .

    Chanzo cha picha, NASA

    Chombo cha anga za juu cha NASA kimeweka historia kwa kunusurika kwa kurabia kwa ukaribu zaidi wa Jua.

    Wanasayansi walipokea ishara kutoka kwa chombo cha Parker Solar kabla ya saa sita usiku EST siku ya Alhamisi (05:00 GMT siku ya Ijumaa) baada ya kukosa mawasiliano kwa siku kadhaa.

    Nasa ilisema chombo hicho kiko "salama" na kinafanya kazi kama kawaida baada ya kupita maili milioni 3.8 (kilomita milioni 6.1) kutoka kwenye uso wa jua.

    Chombo hicho kiliingia kwenye anga ya nje ya nyota yetu siku ya mkesha wa Krismasi, kikistahimili halijoto na mionzi mikali katika jitihada za kuboresha uelewa wetu wa jinsi Jua linavyofanya kazi.

    Nasa kisha ikangoja ishara kwa woga, ambayo ilitarajiwa saa 05:00 GMT mnamo 28 Desemba.

    "Utafiti huu wa karibu wa Jua huruhusu chombo hicho kuchukua vipimo vinavyosaidia wanasayansi kuelewa vyema jinsi nyenzo katika eneo hili hupata joto hadi mamilioni ya digrii, kufuatilia asili ya upepo wa jua (mtiririko unaoendelea wa nyenzo zinazotoroka Jua), na ugunduzi wa jinsi chembe chembe za nishati huharakishwa hadi karibu na kasi ya mwanga," shirika hilo lilisema.

    Soma zaidi:

  7. ‘Tunaunga mkono Slovakia kuandaa mazungumzo ya amani na Ukraine’ - Urusi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema siku ya Alhamisi kwamba Urusi iko tayari kwa pendekezo la Slovakia la kuandaa mazungumzo ya amani na Ukraine ili kumaliza mzozo ambao alisema Urusi imedhamiria kuhitimisha.

    Putin, ambaye wiki hii alikuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico huko Kremlin, alisema kuwa Fico, ambaye amekuwa akipinga msaada wa kijeshi wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine, amejitolea nchi yake kama mwenyeji wa mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine.

    Putin alisema mamlaka ya Slovakia "... itakuwa yenye furaha kutoa nchi yao kama mwenyeji wa mazungumzo. Ikiwa itakuwa hivyo, Kwa nini tupinge? Kwa kuwa Slovakia ina msimamo usioegemea upande wowote."

    Slovakia inaonekana kama moja ya kambi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ya kati na mashariki yenye mashaka na uungaji mkono kwa Ukraine, na badala yake inapendelea mazungumzo na Urusi.

  8. Somaliland na Ethiopia zakubaliana kutatua kwa amani mzozo unaoendelea

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maafisa kutoka Jamhuri iliyojitangazia uhuru wake ya Somaliland na wenzao wa Ethiopia wamekubaliana kutatua kwa amani mapigano makali ambayo yametokea katika kipindi cha wiki tatu zilizopita katika kijiji cha mpakani cha Da'awaley.

    Taarifa iliyotolewa na utawala wa Somaliland na kuchapishwa na Televisheni ya Taifa ya Somaliland (SNLTV) inayomilikiwa na serikali ilisema makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo ya jana huko Jigjiga, mji mkuu wa jimbo la eneo la Somalia la Ethiopia.

    Mazungumzo hayo yalifanyika huku kukiwa na mvutano mkali kati ya Somaliland na jimbo la Somalia la Ethiopia kuhusu madai ya kuhusika kwa jeshi la polisi la Liyuu katika mapigano hayo.

    Tarehe 25 Disemba, Somaliland ilishutumu jeshi la polisi la Liyuu kwa "kuwaua" wafugaji, kukiuka haki zao za kibinadamu na kusema kuhusika kwao "kunahujumu" mfumo wa utawala katika jimbo la kikanda.

    Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakishirikisha picha za kutisha za maiti na mazishi mengi yaliyofanywa kwa waathiriwa.

    Hapo awali mapigano hayo yalichochewa na mauaji ya afisa wa usalama wa eneo hilo wa Ethiopia na walinzi wake.

    Hapo awali mapigano hayo yalichochewa na mauaji ya afisa wa usalama wa eneo hilo wa Ethiopia na walinzi wake.

    Soma zaidi:

  9. Mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyekamatwa na Ukraine afariki dunia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Idara ya kijasusi ya Korea Kusini imesema mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyekamatwa akiwa hai wakati wa mapigano kati ya Urusi na Ukraine amefariki dunia kutokana na majeraha, shirika la habari la Yonhap liliripoti.

    Mapema siku ya Ijumaa, Korea Kusini iliripoti kwamba ujasusi umethibitisha kuwa wanajeshi wa Ukraine wamemkamata mwanajeshi wa Korea Kaskazini.

    "Kupitia ubadilishanaji wa taarifa za moja kwa moja na idara ya ujasusi ya nchi washirika, imethibitishwa kuwa mwanajeshi mmoja wa Korea Kaskazini aliyejeruhiwa amekamatwa," Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya Korea Kusini ilisema katika taarifa.

    Picha ya mwanajeshi, anayedhaniwa kuwa mfungwa, ilikuwa imeonekana hapo awali kwenye mitandao ya kijamii; Mamlaka ya Ukraine haikuwa imetoa maoni rasmi juu ya habari hii.

    Chanzo cha habari cha AFP katika idara ya ujasusi ya Korea Kusini kilisema kuwa mwanajeshi huyo alikamatwa na jeshi la Ukraine, lakini ni wapi haswa hii ilitokea haijulikani.

    Soma zaidi:

  10. Habari za hivi punde, Waandamanaji wawaua polisi huku ghasia za uchaguzi zikitishia Msumbiji

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waandamanaji

    Waandamanaji katika jimbo la kaskazini la Nampula nchini Msumbiji wamewaua takriban maafisa watano wa polisi katika mji wa Namapa, tovuti inayomilikiwa na watu binafsi ya Integrity Magazine imeripoti.

    Miongoni mwa maafisa waliouawa ni mkuu wa operesheni ambaye alikuwa amehamishwa hivi majuzi kutoka mji mkuu wa Maputo.

    Mkazi mmoja aliliambia Jarida la Integrity Magazine kwamba kiwango cha vurugu kiliwalazimu watu wengi kukimbilia vichakani kwa hofu, huku msongamano wa magari ukikatizwa, na hivyo kuzuia ufikiaji wa jimbo la Cabo Delgado na jiji la Nampula.

    "Hali ni ya wasiwasi hapa. Wanajeshi na maafisa wa polisi pia walikimbia," mkazi mwingine wa Namapa alisema.

    Takriban watu 200 wanahofiwa kuuawa tangu maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi yalipoanza tarehe 21 Oktoba.

    Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo alikuwa ametangazwa kuwa rais mteule baada ya kupata asilimia 65 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa tarehe 9 Oktoba.

  11. Habari za hivi punde, Korea Kusini yapiga kura kumtimua kaimu rais Han Duck-soo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Korea Kusini imepiga kura ya kumuondoa madarakani kaimu rais wake Han Duck-soo, wiki mbili baada ya bunge kupiga kura ya kumshtaki rais wake Yoon Suk Yeol.

    Baadhi ya wabunge 192 walipiga kura ya kung'atuliwa kwake, zaidi ya kura 151 zinazohitajika ili kufanikiwa.

    Waziri Mkuu Han alichukua wadhifa huo baada ya Rais Yoon kuondolewa madarakani na bunge kufuatia jaribio lake lisilofanikiwalililogonga mwamba la kuweka sheria ya kijeshi tarehe 3 Disemba.

    Han alitakiwa kuiongoza nchi hiyo kutoka katika msukosuko wake wa kisiasa, lakini wabunge wa upinzani walidai kuwa alikuwa akikataa matakwa ya kukamilisha mchakato wa kumuondoa Yoon.

    Bunge lilikumbwa na ghasia wakati ambapo kura ilikuwa ikipigwa siku ya Ijumaa.

    Wabunge kutoka chama tawala cha Yoon na Han People Power Party (PPP) waliandamana kupinga tangazo la spika wa Bunge la Kitaifa Woo Won-shik kwamba kura 151 pekee ndizo zitahitajika ili kupitisha mswada wa kuondolewa madarakani.

    Hii ilimaanisha kuwa, tofauti na kura 200 zinazohitajika kwa kuondolewa kwa Yoon, hakuna kura kutoka kwa wabunge tawala ambazo zingehitajika wakati huu kwa Han kushtakiwa bungeni.

    Wabunge wa chama tawala walikusanyika katikati ya ukumbi wa kupigia kura wakiimba, "batili!" na "matumizi mabaya ya madaraka!" wakijibu, na kumtaka Spika aondoke madarakani. Wengi wao walisusia kura.

    Upinzani kwa mara ya kwanza uliwasilisha ombi la kumuondoa Han siku ya Alhamisi baada ya kuzuia uteuzi wa majaji watatu ambao bunge lilikuwa limewachagua kusimamia kesi ya Yoon.

    Mahakama ya Kikatiba ya Korea kwa kawaida huundwa na benchi ya watu tisa. Angalau majaji sita lazima waidhinishe mashtaka ya Yoon ili uamuzi huo uidhinishwe.

    Kwa sasa kuna majaji sita pekee kwenye benchi, ikimaanisha kukataliwa mara moja kutamuokoa Yoon kuondolewa.

    Upinzani ulikuwa na matumaini kwamba wateule watatu wa ziada wangesaidia kuboresha uwezekano wa Yoon kushtakiwa.

    Waziri wa fedha Choi Sang-mok anatarajiwa kuchukua nafasi ya Han kama kaimu rais.

    Kuondolewa kwa Han kunaweza kuzidisha msukosuko wa kisiasa na kutokuwa na uhakika ambao nchi inapambana nao kwa sasa.

  12. Watu 29 bado hawajapatikana kutokana na utekaji nyara nchini Kenya - KNCHR

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) imeibua wasiwasi kuhusu visa vya utekaji nyara vinavyoongezeka nchini huku watu 26 wakidaiwa kupotea tangu maandamano ya kuipinga serikali mwezi Juni.

    Katika taarifa ya Alhamisi, KNCHR ilisema kwamba imeona kwamba utekaji nyara huu "unaendelezwa kwa siri, na watu wasiojulikana wenye silaha".

    Imeongeza kuwa tume hiyo pia ilibaini kuwa waliotekwa nyara wamekuwa wakipinga vikali serikali kwenye mitandao ya kijamii.

    Kufikia sasa, KNCHR inasema, kuna visa vingine kumi na tatu vya utekaji nyara au kutoweka kwa watu katika muda wa miezi mitatu iliyopita na kufikisha jumla ya kesi 82 ​​tangu Juni 2024.

    "Kesi saba za utekaji nyara za hivi majuzi ziliripotiwa mwezi wa Disemba 2024 huku sita kati yao wakiwa bado hawajulikani waliko, na hivyo kufanya jumla ya watu ishirini na tisa ambao hawajapatikana tangu Juni 2024," alisema.

    Tume ilisema kuwa utekaji nyara huo uko nje ya maagizo ya Katiba na unapaswa kushughulikiwa haraka.

    "Tume inatahadharisha kwamba ikiwa tabia hizi za utekaji nyara zitaendelea, basi tutakuwa tunarejea kwa kasi katika siku za giza za historia yetu ambapo mashambulizi hayo yalikuwa yanaleta hofu kwa mtu yeyote anayeikosoa Serikali," alisema.

    KNCHR pia ilipinga taarifa iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja mnamo Desemba 26 kwamba maafisa wa polisi hawahusiki na utekaji nyara unaofuata.

    Tume hiyo ilisema kuwa jeshi la polisi linapaswa kuendelea kuwa makini katika kutekeleza jukumu lao la kulinda raia, na kuongeza kuwa watu wanapaswa kukamatwa ikizingatiwa kuwa matukio haya ya utekaji yanafanyika mchana kweupe, huku baadhi yao yakinaswa na CCTV.

  13. Video: Tazama hali ilivyokuwa katika uwanja wa ndege wa Yemen kufuatia shambulio la Israel

    Maelezo ya video, Tazama: Israeli syashambulia uwanja wa ndege wa Yemen na vituo vya umeme
  14. Ukraine yamkamata mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyejeruhiwa, yasema Seoul

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vikosi vya Ukraine vimemkamata mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyejeruhiwa ambaye alitumwa kusaidia vita vya Urusi, shirika la kijasusi la Korea Kusini lilithibitisha Ijumaa.

    Mwanajeshi huyo anaaminika kuwa mfungwa wa kwanza wa kivita wa Korea Kaskazini kukamatwa tangu mwezi Disemba, wakati Pyongyang ilipotuma vikosi vyake kusaidia vita vya Urusi nchini Ukraine.

    Uthibitisho huo unakuja baada ya picha inayodaiwa kumuonyesha askari aliyejeruhiwa kusambaa kwenye Telegram.

    Korea Kaskazini imetuma zaidi ya wanajeshi 10,000 kuisaidia Urusi, kulingana na Kyiv na Seoul - ingawa Moscow na Pyongyang hazijathibitisha wala kukanusha kuwepo kwao.

    Zaidi ya wanajeshi 3,000 wa Korea Kaskazini wamekufa au kujeruhiwa wakati wa mapigano huko Kursk, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema Jumatatu.

    Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Moscow na Pyongyang unaongeza "hatari ya eneo la mfereji wa Korea kukosa uthabiti.

  15. Mkuu wa WHO ajipata katikati ya mashambulizi ya Israel huko Yemen

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Dk Tedros alisema hakujeruhiwa baada ya shambulio hilo

    Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na wafanyakazi wengine wa Umoja wa Mataifa walikuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Yemen mjini Sanaa siku ya Alhamisi wakati wa shambulizi la anga la Israel.

    Katika chapisho la mtandao wa kijamii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema yeye na wafanyikazi walikuwa karibu kupanda ndege wakati uwanja wa ndege ulipopigwa na angani.

    "Mmoja wa wafanyakazi wa ndege yetu alijeruhiwa," aliandika, akiongeza kuwa watu wawili katika uwanja wa ndege waliuawa.

    Mashambulizi hayo - ambayo pia yamegonga vituo vya umeme na bandari - yamesababisha vifo vya watu wasiopungua watatu huku zaidi ya dazeni wakijeruhiwa, kulingana na vyombo vya habari vinavyoendeshwa na Houthi.

    Kundi la waasi linaloungwa mkono na Iran limetaja mashambulizi hayo kuwa ya kinyama baada ya Israel kudai kuhusika ..

    Haijabainika iwapo waliouawa ni raia au waasi wa Houthi.

    Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema "ndege zake za kivita zilifanya mashambulizi ya kijasusi kwenye shabaha za kijeshi za utawala wa kigaidi wa Houthi kwenye pwani ya magharibi na ndani ya Yemen".

    Ililenga "miundombinu ya kijeshi" katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa na vile vile vituo vya umeme vya Hezyaz na Ras Kanatib, na tovuti katika bandari za Al-Hudaydah, Salif na Ras Kanatib kwenye pwani ya magharibi, IDF ilisema.

    Katika maoni yake muda mfupi baada ya shambulio hilo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema "itaendelea kukata mkono wa kigaidi wa mhimili wa uovu wa Iran hadi tutakapomaliza kazi," na kuongeza "tunaanza tu na [Wahouthi]".

    Mohammed Ali al-Houthi, mkuu wa kamati kuu ya mapinduzi ya Houthis, aliita mashambulizi hayo "ya kinyama" na "uchokozi".

  16. Natumai Hujambo