Ni nini kinachosababisha wimbi la vurugu nchini Msumbiji?

th

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 5

BBC Africa Digital

BBC News

Wanajeshi na polisi wanashika doria katika barabara za mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, huku wafuasi wa upinzani wakipinga matokeo yenye utata ya uchaguzi wa mwezi uliopita .

Polisi walirusha mabomu ya machozi katika umati wa waandamanaji na makabiliano yalizuka siku ya Alhamisi.

Takriban waandamanaji kumi na wanane na polisi mmoja wameuawa katika majuma kadhaa ya ghasia nchini kote, kufuatia uchaguzi wa Oktoba 9.

Chama cha Frelimo (Frente de Libertação Moçambique), ambacho kimekuwa madarakani kwa karibu miaka hamsini, kilitangazwa kuwa mshindi lakini vyama vya upinzani vimedai kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika uchaguzi.

Maandamano ya Alhamisi yalikusudiwa kuwa kilele cha maandamano yanayoendelea mitaani dhidi ya Daniel Chapo wa Frelimo, ambaye alitangazwa kuwa rais mteule kwa kupata zaidi ya 70% ya kura.

Maandamano hayo yalipaswa kuongozwa na kiongozi wa upinzani Venâncio Mondlane ambaye aliibuka wa pili kwa asilimia 20 ya kura. Ameliambia shirika la habari la Agence France Presse kwamba kulikuwa na mazingira ya kimapinduzi, na taifa hilo lilikuwa kwenye ukingo wa mpito wa kihistoria wa kisiasa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, kwa sasa Mondlane yuko mafichoni nchini Afrika Kusini baada ya kile anachodai kuwa ni jaribio la kumuua. Hakutoa ushahidi wowote kuunga mkono dai hili na mamlaka ya Msumbiji haijatoa maoni yoyote.

Bila yeye kuwepo, haijulikani jinsi maandamano ya leo yatakavyofanikishwa au kuenea.

Ingawa Alex Vines, Mkurugenzi wa programu ya Afrika katika kituo cha ushauri chenye makao yake makuu London, Chatham House, anasema hata kama maandamano hayatakuwa makubwa kama inavyotarajiwa, machafuko yanaweza kuendelea.

"Uchaguzi ulikuwa tetemeko la kisiasa kwa Msumbiji kwa sababu umevunja muundo wa kisiasa ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka thelathini," anasema.

"Venâncio Mondlane amechochea maandamano katika Frelimo - dhidi ya hali ya kuridhika na kujiamini kwa chama ambacho kimetawala kwa miaka 50. Wananchi wa Msumbiji wanataka mabadiliko.”

Kwa nini matokeo ya uchaguzi mkuu wa Msumbiji yamepingwa?

Takriban watu milioni 17 walipiga kura katika uchaguzi mkuu wa Msumbiji tarehe 9 Oktoba.

Upigaji kura kwa kiasi kikubwa ulikuwa wa amani, lakini waangalizi wengi na wafuasi wa upinzani waliripoti kasoro nyingi ikiwa ni pamoja na kujazwakwa masanduku ya kura na matumizi ya rasilimali za serikali kufanya kampeni kwa ajili ya chama tawala kilichokuwa madarakani cha Frelimo.

Idadi ya wapiga kura ilikuwa karibu 43% na hasa chini katika majimbo ya kaskazini, ikiwa ni pamoja na 28% katika eneo la Nampula.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walisema walizuiwa kutazama shughuli ya uigaji kura katika baadhi ya wilaya na majimbo, na pia katika ngazi ya kitaifa. Kundi la waangalizi wa EU pia liliripoti hitilafu wakati wa kuhesabu kura katika kituo cha kupigia kura na ngazi ya wilaya.

Tarehe 24 Oktoba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza ushindi wa Daniel Chapo wa Frelimo katika uchaguzi wa rais wa Msumbiji.

Hata hivyo, vyama vya upinzani vimedai udanganyifu mkubwa katika uchaguzi. Madai yao yanazingatiwa na Baraza la Katiba la Msumbiji ambalo linatazamiwa kutoa matokeo yake ya mwisho mwishoni mwa mwezi huu.

Unaweza Pia Kusoma
th

Chanzo cha picha, Reuters

Nini kimetokea tangu kutangazwa kwa matokeo uchaguzi?

Kiongozi wa upinzani Venâncio Mondlane aliungwa mkono katika azma yake ya kuwa rais na The Optimistic People for the Development of Mozambique (PODEMOS). Podemos ni chama kipya cha kisiasa nchini Msumbiji, kilichoanzishwa mwaka wa 2019.

Mondlane mwenyewe ni mchungaji mwenye mvuto ambaye amekuwa akishirikiana na vyama kadhaa vya upinzani. Amejenga ufuasi mkubwa wa vijana kwenye mitandao ya kijamii.

"Yeye ni mtu maarufu na ameshikamana na tawi la Upentekoste - kuna hali hii ya ujio wa hatima ya kimasihi," anasema Alex Vines wa Chatham House.

Baada ya matokeo kutangazwa, Mondlane na vyama vingine vya upinzani vilikusanyika pamoja ili kuitisha maandamano ya wiki moja.

Wakili na mgombea kutoka timu ya Mondlane wote waliuawa walipokuwa wakijiandaa kupinga matokeo. Elvino Dias na Paulo Guambe walipigwa risasi katika mji mkuu.

Takriban watu 18 wameuawa katika maandamano hayo kufikia sasa, kwa mujibu wa Human Rights Watch. Mashirika yasiyo ya kiserikali yameripoti vifo vya takribani watu tisa katika mapigano na polisi katika majimbo ya Nampula na Zambézia.

Ikifikiriwa kuwa sehemu ya mkakati wa kupunguza maandamano, pia kumekuwa na siku nyingi za kukatwa kwa huduma za mtandao na mitandao ya kijamii, kulingana na mfuatiliaji wa udhibiti wa mtandao kutoka Surfshark, mtoa huduma wa mtandao wa kibinafsi.

Hannah Danzinger da Silva, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Search for Common Ground lenye makao yake makuu mjini Maputo, Hannah Danzinger da Silva, alisema kwamba mara tu maandamano yalipotangazwa, huduma za data za simu za mkononi, “hasa WhatsApp na Facebook yaani, kila kitu cha Meta kimezimwa, kisha kwa muda mfupi. kurejeshwa lakini kumekuwa na hitilafu kadhaa."

th

Chanzo cha picha, LUISA NHANTUMBO/EPA-EFE/REX/Shutterstock

Nini kinachoweza kutokea baadaye?

Mapema wiki hii Waziri wa Ulinzi Cristóvão Chume alitishia kupeleka jeshi kabla ya maandamano ya kitaifa ya Alhamisi.

Rais anayemaliza muda wake Filipe Nyusi amekanusha habari kwamba wanajeshi wa Rwanda wametumwa katika mji mkuu Maputo kukandamiza maandamano.

Wakati huo huo, siku ya Jumatano Afrika Kusini ilifunga kwa muda mfupi moja ya vivuko vyake vyenye shughuli nyingi zaidi mpaka na Msumbiji kufuatia ghasia hizo.

Siku ya Alhamisi Reuters na mashirika ya habari ya AFP yaliripoti kwamba kuongezeka kwa mvutano kumesababisha kusimamishwa kwa shughuli za bandari na vituo vya usafiri nchini Msumbiji.

Wakati nchi ikisubiri matokeo ya mwisho kutoka kwa Baraza la Katiba, Chama cha Wanasheria wa Msumbiji kimemtaka Rais Filipe Nyusi "kuanzisha mazungumzo ya kweli" na wote wanaohusika akiwemo Venâncio Mondlane.

Msumbiji si nchi tajiri kwa hivyo waandamanaji hawawezi kudumisha shinikizo la aina hii kwa muda usiojulikana, "anasema Alex Vines.

"Wakati ujao wa shughuli za hali ya juu ya msukosuko utakuwa karibu na takwimu yoyote rasmi ambayo Baraza la Katiba litatoa."

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi