Jeshi la DRC 'ladungua ndege zisizo na rubani' za Rwanda

Msemaji wa jeshi alisema waasi wa M23 walikuwa wakiwatumia vijana waliovalia sare za kijeshi za Rwanda katika maeneo ya vita.

Muhtasari

  • Waandishi wa habari Gaza wauawa katika shambulizi la Israel
  • Urusi yatoa onyo juu ya "propaganda" baada ya ajali ya ndege ya Azerbaijan
  • Morocco kuwapa wanawake haki zaidi
  • Wanakijiji wauawa kwa mashambulio ya anga siku ya Krismasi Nigeria
  • Ethiopia 'yafunga mpaka na Somaliland' huku mapigano ya kiukoo yakiendelea
  • Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo 'ladungua ndege zisizo na rubani' za Rwanda
  • Makumi wamenusurika katika ajali ya ndege ya abiria ya Kazakhstan
  • Polisi hawahusika na utekaji nyara wowote - Afisa Mkuu wa polisi Kenya
  • Papa ahimiza mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine na Urusi
  • Man City wanaweza kukosa kushiriki ligi ya mabingwa - Guardiola
  • Mwili wapatikana kwenye gurudumu la ndege ya United Airlines baada ya kutua Hawaii
  • Mamia watoroka jela ya Msumbiji kufuatia maandamano ya uchaguzi
  • Syria yasema maafisa 14 wa usalama waliuawa kwa shambulio la 'kuviziwa' na wafuasi watiifu wa Assad

Moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu & Asha Juma

  1. Waandishi wa habari Gaza wauawa katika shambulizi la Israel

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kituo cha televisheni cha Palestina kimesema waandishi wa habari watano kutoka kituo hicho wameuawa katika shambulizi la Israeli katika Ukanda wa Gaza katikati.

    Walikuwa katika gari la Quds Today lililokuwa limeegeshwa nje ya hospitali ya al-Awda, ambapo mke wa mmoja wa waandishi alikuwa katika pilka pilka za kujifungua, katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.

    Kituo hicho kilichapisha video iliyoonyesha gari lililokuwa likichomeka lenye maandishi “press” kwenye milango ya nyuma.

    Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vimesema vililenga “watekelezaji wa Islamic Jihad waliokuwa wakijifanya waandishi wa habari” na kwamba hatua zilichukuliwa ili kuepuka kuumiza raia.

    Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) imesema ilikuwa “imevunjika moyo” na taarifa hizo. “Waandishi wa habari ni raia na lazima walindwe kila wakati,” ilisema CPJ.

    Kituo hicho kinakadiriwa kupokea ufadhili kutoka kwa kundi hilo.

    Jeshi la Israeli lilitaja majina ya waandishi watano waliouawa kama Ibrahim Jamal Ibrahim Al-Sheikh Ali; Faisal Abdallah Muhammad Abu Qamsan; Mohammed Ayad Khamis al-Ladaa; Ayman Nihad Abd Alrahman Jadi; na Fadi Ihab Muhammad Ramadan Hassouna. Walidai “habari kutoka vyanzo vingi vilithibitisha” kwamba wote walikuwa watekelezaji wa PIJ.

    Kufikia tarehe 20 Desemba, angalau waandishi wa habari 133 wa Palestina walikuwa wameuawa tangu vita vilipoanza, na CPJ inasema kwamba vita hivi vimekuwa janga kubwa zaidi kwa waandishi wa habari.

    Soma zaidi:

  2. Urusi yatoa onyo juu ya “propaganda” baada ya ajali ya ndege ya Azerbaijan

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Serikali ya Urusi imeonya dhidi ya kuanzisha propaganda kuhusu sababu ya ajali ya ndege ya abiria iliyokuwa ikienda Urusi na kuua watu 38 nchini Kazakhstan Jumatano.

    Picha za ndege iliyoharibika zilionyesha vipande vya chuma vya ndege, na baadhi ya wataalamu wa anga walidokeza kuwa ndege ya Azerbaijan Airlines inaweza kuwa imeshambuliwa na mifumo ya ulinzi wa anga juu ya Jamhuri ya Chechnya ya Urusi.

    Ndege hiyo ilielekezwa kuelekea bahari ya Caspian kutoka Chechnya hadi Kazakhstan magharibi kabla ya kudondoka karibu na jiji la Aktau nchini Kazakhstan.

    Abiria 29 kati ya 67 walinusurika, na Azerbaijan ilitangaza siku ya maombolezo kwa waathiriwa wa ajali hiyo.

    Rais Ilham Aliyev alisema, “Hili ni janga kubwa ambalo limesababisha huzuni kubwa kwa watu wa Azerbaijan.”

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisisitiza, “Itakuwa makosa kueneza propaganda kabla ya hitimisho la uchunguzi. Hatutafanya hivyo, na hakuna mtu anayeweza kufanya hivyo. Tunahitaji kusubiri uchunguzi ukamilike.”

    Ndege ya Embraer 190 iliondoka kutoka Baku asubuhi ya Jumatano ikielekea Grozny, lakini ilielekezwa kwa sababu ya ukungu mzito.

    Abiria mmoja aliyepona alisema rubani alijaribu kutua mara mbili kabla ya mlipuko kutokea.

    Ndege ilielekezwa uwanja wa ndege wa Aktau, kilomita 450 mashariki, na video inaonyesha ndege ikianguka kwa kasi kabla ya kulipuka.

    Mamlaka ya Kazakhstan zimepata rekodi za data za ndege na uchunguzi unaendelea. Awali, baadhi ya ripoti zilieleza kuwa ajali ilitokana na mgongano na kundi la ndege, lakini wataalamu walieleza kuwa hili halingeweza kusababisha ndege kutoka nje ya njia.

    Soma zaidi:

  3. Morocco kuwapa wanawake haki zaidi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Morocco inalenga kuwapa wanawake haki zaidi ya malezi pamoja na kupinga ndoa za wake wengi, katika mapitio ya kwanza ya kanuni za familia katika kipindi cha miaka 20, mawaziri wa haki na masuala ya Kiislamu walisema Jumanne.

    Wanaharakati wa kutetea haki za wanawake wamekuwa wakishinikiza kupitiwa tena kanuni zinazosimamia haki za wanawake na watoto ndani ya familia nchini Morocco, ambako Uislamu ni dini ya serikali.

    Rasimu ya kanuni inapendekeza zaidi ya marekebisho 100, hasa kuruhusu wanawake kupinga ndoa za wake wengi, waziri wa sheria Abdellatif Ouahbi aliwaambia waandishi wa habari.

    Pia inalenga kurahisisha taratibu za talaka, inazingatia ulezi wa mtoto kuwa ni haki ya pamoja kati ya wanandoa na inampa kila mwanandoa haki ya kuhifadhi nyumba ya ndoa endapo mwenzake atafariki, alisema.

    Wanawake walioachwa wataruhusiwa uendelea kutunza mtoto baada ya kuolewa tena.

  4. Wanakijiji wauawa kwa mashambulio ya anga siku ya Krismasi Nigeria

    Mamlaka katika jimbo la Sokoto Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria wanasema wanachunguza shambulio la mabomu katika vijiji viwili yaliyoua takriban watu kumi siku ya Krismasi.

    Ndege ya kivita iliyoripotiwa kulenga kundi jipya la wanamgambo wa Kiislamu - Lakurawa, ilisababisha moto katika jamii hizo mbili kwenye eneo la Serikali ya Mtaa ya Silame jimboni humo.

    Takriban watu sita ambao walijeruhiwa vibaya bado wamelazwa hospitalini.

    Wakaazi wa Gidan Sama na Rumtuwa, waliamka kwa hofu ya mashambulizi ya mabomu kutoka kwa vikosi vya ardhini na anga mnamo tarehe 25 Disemba.

    Baadhi ya wanakijiji wanasema waliona jamaa zao wakiteketea kwa moto lakini hawakuwa na uwezo wa kutoa msaada wowote. Jamii zote ziko karibu na Msitu wa Surame, maficho yanayojulikana ya vikundi vya kigaidi na majambazi.

    Pia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Silame, Abubakar Muhammad aliambia BBC Hausa kuwa yeye na gavana ni miongoni mwa waliozika watu waliopoteza maisha wakati wa shambulio hilo.

    “Nilipigiwa simu na kuambiwa kuna tukio la bomu kulipuka. Nilifuatilia na kuthibitisha kuwa ni kweli limefanyika. Ndege mbili zilionekana zikirusha mabomu kwenye vijiji hivyo,” alisema.

    Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Jeshi la Nigeria ilisema kwamba maeneo yaliyolengwa ya Gidan Sama na Rumtuwa yametambuliwa kuhusishwa na kundi la wanamgambo wa Lakurawa.

  5. Ethiopia 'yafunga mpaka na Somaliland' huku mapigano ya kiukoo yakiendelea

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ethiopia imeripotiwa kufunga mpaka wake na Jamhuri iliyojitangaza ya Somaliland jana baada ya siku kadhaa za mapigano yaliyoigharimu pakubwa katika maeneo ya mpakani ambayo yamezua mvutano na Hargeisa.

    Mapigano hayo yamekuwa yakitokea ndani na karibu na kijiji cha Dawa'ley katika Wilaya ya Harshin nchini Ethiopia na yameripotiwa kuua zaidi ya watu 100 kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo.

    Awali ilihusisha koo zinazohasimiana kutoka Ethiopia na Somaliland, lakini uingiliaji kati wa moja kwa moja wa Polisi wa Liyu - kitengo maalum cha polisi katika Mkoa wa Somalia wa Ethiopia - umeibua hisia na kukasirisha serikali ya Somaliland.

    Wizara ya usalama wa ndani ya Somaliland jana ilitoa taarifa ikiwashutumu Polisi wa Liyu kwa kufanya "mauaji" dhidi ya raia na kufichua kuwa Somaliland iliwasilisha malalamishi kwa serikali ya Ethiopia.

    Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti kwamba mapigano mapya yaliyodumu kwa saa moja yalizuka tena katika eneo hilo hapo jana.

    Mzozo huo unatishia kuharibu uhusiano wa karibu kati ya Ethiopia na Somaliland wakati ambapo hatima ya makubaliano muhimu ya baharini ambayo pande hizo mbili zilitia saini Januari 2024 iko mashakani.

    Soma zaidi:

  6. Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo 'ladungua ndege zisizo na rubani' za Rwanda

    ,

    Chanzo cha picha, AFP

    Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo 'limedungua' ndege sita zisizo na rubani za Kamikaze za jeshi la Rwanda katika mji wa Mambasa eneo la Lubero katika Mkoa wa Nord Kivu, tovuti ya Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa iliripoti jana.

    Msemaji wa jeshi Lt Kanali Mak Hazukay alisema waasi wa M23 walikuwa wakiwatumia vijana waliovalia sare za kijeshi za Rwanda kama "wale wa ziada" katika maeneo ya vita.

    "Jeshi linatoa wito kwa raia wanaotumiwa kama ngao kusalimisha silaha zao, na linawataka wakazi wa maeneo yanayokaliwa kuondoka kwenye kwa usalama wao," Hazukay alisema.

    Lubero imekuwa kitovu cha mapigano mapya kati ya waasi na vikosi vya usalama baada ya mazungumzo kati ya DR Congo na Rwanda hivi karibuni kushindikana.

    Jeshi la Congo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wamekuwa wakishambulizi mara kwa mara lakini Rwanda imekuwa ikikanusha kuunga mkono waasi wa M23 na kuishtumu serikali ya Congo kushirikiana na waasi wa Rwanda wa FDLR shutuma ambazo pia Congo inakanusha.

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Soma zaidi:

  7. Makumi wamenusurika katika ajali ya ndege ya abiria ya Kazakhstan

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Makumi ya watu wamenusurika katika ajali iliyohusisha ndege iliyobeba watu 67 huko Kazakhstan, maafisa wa eneo hilo wanasema.

    Mamlaka ya Kazakh ilisema watu 38 waliuawa katika ajali hiyo.

    Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Grozny nchini Urusi lakini ikaelekezwa kwengineko kwa sababu ya ukungu, shirika hilo la ndege liliambia BBC.

    Ndege ya shirika la ndege la Azerbaijan J2-8243 ilishika moto ilipokuwa ikijaribu kutua kwa dharura karibu na mji wa Kazakh wa Aktau.

    Picha zinaonyesha ndege ilikuwa kwa mwendo wa kasi huku gia yake ya kutua ikiwa chini, kabla ya kuwaka moto ilipokuwa ikitua.

    Shirika hilo la ndege lilisema kuwa ndege hiyo "ilitua kwa dharura" yapata kilomita 3 kutoka Aktau.

    Soma zaidi:

  8. Polisi hawahusika na utekaji nyara wowote - Afisa Mkuu wa polisi Kenya

    .

    Chanzo cha picha, KNA

    Maelezo ya picha, Inspekta jenerali wa Polisi nchini Kenya Douglas Kanja

    Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya Douglas Kanja amekanusha madai yoyote yanayohusisha polisi katika visa vya utekaji nyara vinavyoendelea nchini.

    Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Kanja alisema kuwa hakuna kituo cha polisi nchini ambacho kwa sasa kinawashikilia watu walioripotiwa kutekwa nyara.

    "Ili kuepusha shaka, Huduma ya Kitaifa ya Polisi haihusiki na utekaji nyara wowote, na hakuna kituo cha polisi nchini ambacho kinawashikilia watu walioripotiwa kutekwa," alisema.

    IG aliongeza kuwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) itachunguza utekaji nyara huo, kwani alitoa wito kwa umma wenye taarifa zozote muhimu kuhusu watu waliopotea kuripoti katika vituo vya polisi vilivyo karibu.

    "Suala linalozungumziwa linapaswa kuchunguzwa na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi na chombo kingine chochote kilicho huru. Tunatoa wito kwa mtu yeyote aliye na taarifa muhimu kuhusu mtu yeyote aliyepotea kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu nawe.”

    Kauli ya Inspekta Jenerali inafuatia kilio cha umma kuhusu visa vya utekaji nyara vinavyoongezeka, haswa miongoni mwa vijana Kenya, siku chache zilizopita.

  9. Papa ahimiza mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine na Urusi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Papa Francis ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi ili kumaliza vita vilivyochochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.

    Katika hotuba yake Siku ya Krismasi, Papa alisema "ujasiri [ulihitajika} kufungua mlango" wa mazungumzo "ili kufikia amani ya haki na ya kudumu" kati ya pande hizo mbili.

    Ombi lake linafuatia shambulio kubwa la Urusi siku ya Krismasi kwenye vituo vya kawi vya Ukraine, ambalo Ukraine ilisema lilihusisha angalau makombora 184 na ndege zisizo na rubani.

    Mapema mwaka huu, Ukraine ilikataa vikali wito wa papa wa kufanya mazungumzo ya kusitisha vita na kuwa na "ujasiri wa kuinua bendera nyeupe".

    Ujumbe wake wa Urbi et Orbi (kwa jiji na ulimwengu) pia uligusa migogoro mingine.

    Akizungumza na maelfu ya watu waliokusanyika katika uwanja wa St Peter's Square, Papa huyo mwenye umri wa miaka 88 alitangaza: "Milio ya risasi inyamaze katika Ukraine iliyokumbwa na vita," na kwingineko.

    "Ninamwalika kila mtu binafsi, na watu wote wa mataifa yote... kuwa mahujaji wa matumaini, kunyamazisha sauti za risasi na kuondokana na migawanyiko," alisema.

  10. Man City wanaweza kukosa kushiriki ligi ya mabingwa - Guardiola

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kocha wa Manchester City Pep Guardiola anasema klabu hiyo iko katika hatari ya kukosa nafasi ya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

    City kwa sasa wako katika msimu wao wa 14 mfululizo katika mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya.

    Ni Arsenal pekee kati ya 1998 na 2017, na Manchester United kati ya 1996 na 2014, ambazo ndizo zilizo na rekodi ndefu zaidi ya kufuzu kati ya vilabu vya Uingereza.

    City wamo katika nafasi ya saba kwenye Ligi ya Premia baada ya mechi 17, pointi nne nyuma ya Nottingham Forest iliyo nafasi ya nne na pointi moja nyuma ya Bournemouth iliyo nafasi ya tano.

    England kwa sasa wako kileleni mwa jedwali la Uefa la Uropa na wako katika nafasi nzuri ya kupata nafasi ya tano kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao, ingawa City bado hawatafuzu kwenye msimamo wa sasa.

    "Niliposema hapo awali, watu walicheka," alisema Guardiola. "Walisema, 'kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa sio mafanikio makubwa'.

    "Lakini najua kwa sababu inatokea kwa vilabu katika nchi hii. Walitawala kwa miaka mingi na baada ya miaka mingi wakashindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa."

  11. Mwili wapatikana kwenye gurudumu la ndege ya United Airlines baada ya kutua Hawaii

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ndege ya kampuni ya United Airlines

    Mwili umepatikana katika sehemu gurudumu, la ndege ya United Airlines baada ya kutua Hawaii usiku wa mkesha wa Krismasi, kampuni hiyo ilisema.

    Ndege aina ya Flight 202 iliondoka kwenye uwanja wa ndege wa Chicago wa O'Hare Jumanne asubuhi na kutua katika uwanja wa ndege wa Kahului wa Maui alasiri.

    Shirika la ndege la United Airlines lilisema bado haijafahamika ni lini mtu huyo aliingia kwenye eneo hilo, ambalo ilisema linaweza kufikiwa tu kutoka nje ya ndege ya Boeing 787-10.

    Kampuni hiyo ilisema inashirikiana na mamlaka ya kutekeleza sheria katika uchunguzi.

    Marehemu bado hajatambuliwa

    Katika taarifa, idara ya polisi iliiambia Hawaii News Now kwamba ilikuwa ikifanya uchunguzi "kuhusu mtu aliyefariki aliyegunduliwa kwenye ndege iiliowasili kutoka bara leo mchana. Kwa wakati huu, hakuna maelezo zaidi yanayopatikana".

    BBC imewasiliana na Idara ya Polisi ya Maui kwa maoni.

    .

  12. Mamia watoroka jela ya Msumbiji kufuatia maandamano ya uchaguzi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waandamanaji wamepambana na polisi katika mji mkuu Maputo, kama katika eneo hili kuanzia Jumatatu

    Zaidi ya wafungwa 1,500 wametoroka katika gereza moja nchini Msumbiji, wakitumia fursa ya machafuko ya kisiasa yanayoendelea yaliyochochewa na matokeo ya uchaguzi yenye utata, polisi wamesema.

    Watu 33 waliuawa na 15 kujeruhiwa katika mapigano na walinzi, mkuu wa polisi Bernardino Rafael aliambia mkutano na waandishi wa habari.

    Takriban watoro 150 zaidi wamekamatwa tena, aliongeza.

    Maandamano yalizuka siku ya Jumatatu kujibu mahakama ya juu zaidi ya Msumbiji ikithibitisha kwamba chama tawala cha Frelimo, kilichokuwa madarakani tangu mwaka 1975, kilishinda uchaguzi wa rais wa Oktoba.

    Bw Rafael alisema makundi ya waandamanaji wanaoipinga serikali yalikaribia gereza hilo katika mji mkuu Maputo siku ya Jumatano. Wafungwa walitumia machafuko hayo kuangusha ukuta na kutoroka, alisema.

    Msumbiji imekumbwa na machafuko tangu uchaguzi uliozozaniwa mwezi Oktoba. Matokeo rasmi yalionyesha mgombea urais wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo, akishinda.

    Maandamano mapya yalizuka siku ya Jumatatu, wakati mahakama ya kikatiba ilipoamua kuwa Chapo alishinda uchaguzi huo, huku ikirekebisha tofauti yake ya ushindi.

    Matokeo ya awali ya mwezi Oktoba yalisema Daniel Chapo alipata asilimia 71 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Venâncio Mondlane aliyepata 20%. Mahakama sasa imeamua kwamba alishinda 65% dhidi ya 24% ya Mondlane.

  13. Syria yasema maafisa 14 wa usalama waliuawa kwa shambulio la 'kuviziwa' na wafuasi watiifu wa Assad

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamlaka mpya inayoongozwa na waasi nchini Syria imesema maafisa 14 wa wizara ya mambo ya ndani wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulizi la kuvizia lililofanywa na vikosi vinavyomtii Rais aliyepinduliwa Bashar al-Assad magharibi mwa nchi hiyo.

    Wanasema mapigano hayo yalifanyika karibu na bandari ya Mediterranean ya Tartous siku ya Jumanne.

    Ripoti zinasema kuwa vikosi vya usalama vilivamiwa wakati vikijaribu kumkamata afisa wa zamani kuhusiana na jukumu lake katika gereza maarufu la Saydnaya, karibu na mji mkuu Damascus.

    Zaidi ya wiki mbili zilizopita, urais wa Assad ulipinduliwa na vikosi vya waasi vinavyoongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS).

    Shirika la Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) lenye makao yake nchini Uingereza limesema wanamgambo watatu pia waliuawa katika mapigano hayo.

    SOHR iliongeza kuwa vikosi vya usalama baadaye viliweka usalama.

    Kwengineko , mamlaka ya Syria iliweka amri ya kutotoka nje usiku kucha katika mji wa kati wa Homs, vyombo vya habari vya serikali viliripoti.

    Ripoti zinasema kuwa hii ilifuatia machafuko baada ya video inayodaiwa kuonyesha shambulio kwenye hekalu la Alawite.

    Wizara ya mambo ya ndani ya Syria ilisema ni video ya zamani, iliyoanzia kwenye mashambulizi ya waasi huko Aleppo mwishoni mwa mwezi Novemba, na ghasia hizo zilitekelezwa na makundi yasiyojulikana.

    SOHR ilisema mtu mmoja aliyekuwa akiandamana aliuawa na watano kujeruhiwa huko Homs.

    Maandamano pia yaliripotiwa katika maeneo yakiwemo miji ya Tartous na Latakia, na mji alikozaliwa Assad wa Qardaha.

    Alawites ni madhehebu ya wachache ambayo familia ya Assad inatoka, na ambayo wengi wa wasomi wa kisiasa na kijeshi wa utawala wa zamani walitoka.

    Mashambulizi makali yaliyoongozwa na HTS ambayo yalianza kutoka kaskazini-mashariki mwa Syria na kuenea nchi nzima yalihitimisha utawala wa zaidi ya miaka 50 wa familia ya Assad.

  14. Natumai hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja leo ikiwa siku ya Boxing Day