Jinsi rais muinjilisti wa Kenya alivyokosana na makanisa

Chanzo cha picha, William Ruto/X
Imani ya Kikristo ya William Ruto imekuwa msingi wa maisha yake binafsi na safari yake ya kisiasa.
William Ruto, ambaye alikua rais wa Kenya miaka miwili iliyopita akipata kura nyingi za Wakristo, ameonekana kushtushwa na kugundua kuwa katika miezi michache iliyopita viongozi wa makanisa ya imani zote wanapoteza imani naye – wakimfananisha na mtoza ushuru fisadi aliyeandikwa kwenye biblia.
Katika kuelekea ushindi wake, baadhi ya wafuasi wake wa kiinjili tiifu walimwita "Daudi", jina la mvulana mchungaji katika Biblia ambaye aliibuka na kuwa mfalme.
Upinzani ulikuwa umembatiza "naibu Yesu", wakimtuhumu kutumia Ukristo kupata mtaji wa kisiasa alipokuwa akihudhuria ibada za kanisa kuanzia kwenye umati wa Kikatoliki hadi mikusanyiko ya madhehebu yasiyojulikana.
Alivalia mavazi yanayoendana na dini husika kimpangilio, nyakati fulani akipiga magoti katika dua na mara kwa mara alibubujikwa na machozi ibadani.
Baadaye, alimtukuza Mungu kwa mafanikio yake katika uchaguzi, na akaendeleza utaratibu huu wa kuzunguka nchi nzima ili kuhudhuria makanisa tofauti kila Jumapili.
Lakini kufuatia upinzani mkubwa kufuatia nyongeza ya kodi iliyowekwa na serikali yake, ya rais huyo mwenye umri wa miaka 57 alipatiwa jina jipya la utani: "Zakayo" - ambalo ni Kiswahili cha Zakayo, mtoza ushuru tajiri na asiyependwa na watu wa Yeriko anayetajwa katika Biblia.
Rais amekuwa akisisitiza kuwa ikiwa watu wanataka huduma bora za umma na kupunguzwa kwa mzigo wa deni la nchi, lazima walipe.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa muda wa miaka miwili iliyopita, kodi inayokatwa kwenye mishahara imepanda, ushuru wa mauzo ya mafuta umeongezeka maradufu na watu pia wanalipa ushuru mpya wa nyumba na ushuru wa bima ya afya ambayo bado haijawafaidi Wakenya wengi.
Wakati maandamano makubwa ya kupinga ushuru yalipozuka mwezi Juni, yakiongozwa na vijana maarufu kama Gen Zs, pia walitoa angalizo kwa makanisa kwa kuwa karibu sana na wanasiasa na kuwaruhusu kuhubiri kwenye mimbari zao.
Hasira zao ziliilazimu serikali kubatilisha muswada tata wa fedha ambao ulikuwa umejumuisha nyongeza zaidi ya ushuru - na iliamsha makanisa, ambayo makasisi walianza kumkosoa Ruto na sera zake waziwazi.
Haya pia yalikuwa maendeleo makubwa kwani uchumi unaotokana na imani ni biashara kubwa katika nchi ambayo zaidi ya 80% ya watu ni Wakristo - na dini itakayoweza kufanya harambee ya uchangishaji wa pesa kwa kutumia mwanasiasa sahihi inaweza kubahatika kuneemeka.
Mwezi uliopita, Teresia Wairimu, mwanzilishi wa kanisa la Faith Evangelistic Ministries (Fem), katika mji mkuu, Nairobi, ambako Ruto na familia yake wamekuwa wakiabudu mara kwa mara, alipendekeza kuwa Mfalme wao Daudi alikuwa akirejea shambani ambako ufugaji wa kondoo ulifanyika.
"Kama mpiga kura, nina aibu," alisema katika mahubiri yake.
Mahubiri mengine ya Kasisi Tony Kiama wa Kanisa la River of God yalisambaa hivi karibuni baada ya kuitaka serikali ya Ruto kuwa "haitumikii kusudi la Mungu bali uovu", akitaja mauaji wakati wa maandamano ya hivi karibuni , kupanda kwa gharama ya maisha na rushwa.
Ukosoaji mkali zaidi ulikuwa kauli ya wiki iliyopita kutoka kwa maaskofu wa Kikatoliki, ambao wana uzito zaidi kwa sababu ya heshima na ushawishi wao nchini Kenya.
Walishutumu serikali ya Ruto kwa kuendeleza "utamaduni wa uongo", wakitaja ahadi ambazo hazijatekelezwa wakati wa kampeni.
"Kimsingi, inaonekana kwamba ukweli haupo, na kama upo, ni kile tu ambacho serikali inasema," Mkutano wa Maaskofu wa Kikatoliki wa Kenya ulisema, pia ukipinga ufisadi, ulafi na kutozwa ushuru kupita kiasi wakiutaja kudumaza uchumi.
Askofu mmoja aliitaja Kenya kuwa nchi ya "Orwellian dystopian authoritarian", ambapo upinzani ulikabiliwa "kwa vitisho, utekaji nyara au hata mauaji".
Hii ilikuwa rejea ya watu 60 waliokufa na wengine 1,300 waliokamatwa wakati wa maandamano ya kupinga ushuru.
Watu wengine 74 wametekwa nyara na 26 wameripotiwa kutoweka katika muda wa miezi mitano iliyopita, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kauli hiyo kali ya maaskofu ilifuatiwa na kukataliwa na kanisa kwa mchango wa $40,000 (£32,000) uliotolewa na Ruto alipohudhuria Kanisa Katoliki la Soweto jijini Nairobi Jumapili iliyopita - huku Askofu Mkuu wa Nairobi akitaja "maswala ya kimaadili na hitaji la kulinda Kanisa lisitumike kwa madhumuni ya kisiasa."
Wakristo wengi wa Kenya ni Wakatoliki - takriban watu milioni 10, au 20% ya watu wote, kulingana na takwimu za serikali.
Wakristo wengine ni wa makanisa mbalimbali ya kiinjilisti na madhehebu mengine, ikiwa ni pamoja na Kanisa la Anglikana la Kenya na Kanisa la Presbyterian.
Na ushawishi wa Kanisa Katoliki nchini Kenya unazidi waumini wake kutokana na uwekezaji wake mkubwa katika elimu, huduma za afya na programu nyingine za kijamii.
Pia limekasirishwa na mabadiliko ya mkanganyiko kwenye mpango mpya wa bima ya afya ya jamii, huku serikali ikidaiwa mamilioni ya dola na hospitali za kidini.
Tathmini ya maaskofu kwa uwazi kuhusu hali ya taifa imewakumbusha Wakenya jukumu la viongozi wa makanisa waliposhinikiza kurejea kwa demokrasia ya vyama vingi katika miaka ya 1990.
Makasisi shupavu kama vile Ndingi Mwana a’Nzeki wa Kanisa Katoliki, Alexander Muge, Henry Okullu na David Gitari wa Kanisa la Kianglikana na Timothy Njoya wa Kanisa la Presbyterian walipinga bila woga utawala wa ukandamizaji na wa chama kimoja cha Rais wa wakati huo Daniel arap Moi.
Lakini wachambuzi wanasema chini ya warithi wa Moi - Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, wote Wakatoliki - makasisi walipoteza sauti zao.
"Chini ya Rais William Ruto, mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi kwa sababu washiriki muhimu wa kanisa walionekana kuingizwa kwenye chumba cha kulia chakula," mwandishi wa habari mkongwe Macharia Gaitho aliandika katika gazeti la Daily Nation la Kenya wiki hii, akimaanisha "makanisa yalihongwa ili kunyamaza" .
Msimamo wa maaskofu wa Kikatoliki umepata kuungwa mkono na madhehebu mengine, pamoja na wahubiri wa Kiislamu - licha ya uungwaji mkono ulioenea wa kidini ambao Ruto aliufurahia hapo awali kwa msimamo wake mkali kuhusu haki za mashoga na maoni yake ya kihafidhina kuhusu uavyaji mimba.
Taarifa ya pamoja ya baadhi ya viongozi wa Kipentekoste na makanisa iliwapongeza maaskofu kwa ushujaa wao na pia kwa "kufanya jambo ambalo halikudhaniwa"hasa kwa kukataa pesa za Ruto.
Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Kenya Askofu Jackson Ole Sapit, ambaye aliongoza maombi ya kitaifa siku ambayo Ruto alitangazwa mshindi wa kinyang'anyiro cha urais, aliungana na maaskofu wa Kikatoliki kulaani kile alichokitaja kuwa "kukithiri kwa utawala mbovu, kutokujali na ukiukaji mkubwa wa haki".
"Katika hali hiyo, hatupaswi kukunja mikono tu na kuomba miujiza," Ole Sapit alisema, akiongeza kuwa maaskofu wa Kikatoliki walionyesha hisia za Wakenya wengi.
Kasisi wa Baptist Daniel Wambua aliongeza kuwa viongozi wa kidini sasa wameazimia kukomesha "uhusiano wa miamala ya fedha na serikali.
Lakini wadadisi wanasema Ruto, ambaye mara kwa mara hutumia maandiko kujibu wakosoaji, anafaa kuwa makini na makabiliano ya moja kwa moja kwani hata makanisa madogo yanaweza kuwa na maelfu ya wafuasi ambao wanaweza kuathiri vibaya azma yake ya kuchaguliwa tena.
Rais tayari anakabiliwa na uasi katika sehemu za ngome zake za kisiasa za 2022 baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mwezi uliopita.
Walitofautiana kuhusu namna maandamano ya kupinga ushuru yalivyoendeshwa, ambayo yametikisa utawala wa Ruto.
Mshirika wa karibu wa rais, mbunge Oscar Sudi, ameandika katika ukurasa wa mtandao wa X akikiri kuwa wamekosea na akiwaomba msamaha maaskofu wa Kikatoliki kwa niaba ya serikali.
Ruto mwenyewe tangu wakati huo ameonekana kulegeza jibu lake kwa ukosoaji unaozidi kuongezeka, akisema amewasikia viongozi wa dini na yuko tayari kushirikiana nao.
"Tumefanya maendeleo yasiyopingika katika nchi yetu. Hata hivyo, bado kuna mengi ya kufanywa. Lazima tuendelee kufanya kazi pamoja ili kuharakisha utekelezwaji wa ahadi zetu na kubadilisha Kenya," alichapisha katika mtandao wa X siku ya alhamisi.
Kile ambacho rais wa kwanza wa kiinjilisti nchini Kenya analazimika kukubali ni kwamba makanisa aliyotumia kwa mafanikio kupata mamlaka ya serikali yanaweza kusaidia kumng'oa katika uchaguzi ujao.
"Anajua hawezi kupigana na kanisa," alisema Bw Gaitho.

Chanzo cha picha, AFP
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












