Hamas yaishinikiza Israel kuwaachia huru wafungwa mashuhuri kama sehemu ya makubaliano ya Gaza

Wizara ya sheria ya Israel imechapisha majina ya wafungwa 250 watakaoachiliwa, bila kuwajumuisha wafungwa saba wenye hadhi ya juu, akiwemo Marwan Barghouti na Ahmad Saadat.

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Martha Saranga

  1. Tunakomea hapo kwa sasa. Kwaheri.

  2. Waandamanaji Madagascar wafika uwanja wa uhuru

    ,

    Waandamanaji wa Gen Z nchini Madagascar wamefanikiwa kufika Uwanja wa Uhuru maarufu Mei 13 Square kwa mara ya kwanza tangu maandamano yalipoanza wiki mbili zilizopita.

    Walikuwa wakiimba kwa sauti kubwa, kucheza dansi, na kupiga vigelegele, huku baadhi yao wakibeba bendera ya Madagascar.

    Pia walishangilia kundi la wanajeshi walioonekana kuwapa ulinzi.

    Juhudi za waandamanaji kufika eneo hilo wiki mbili zilizopita ziligonga mwamba kutokana na ulinzi mkali uliowekwa. Eneo hilo lililopo katikati ya jiji - linajulikana kama Place du 13 Mai - moja wapo ya maeneo yanayotumiwa kushinikiza mageuzi ya kisiasa nchini.

    Lilipewa jina hilo baada ya Mei 13, 1972, wakati maandamano makubwa yalipozuka na kusababisha kuanguka kwa Rais Philibert Tsiranana, na kuashiria mabadiliko katika siasa za baada ya uhuru wa Madagascar.

    Mwandamanaji mmoja aliiambia BBC kwamba wakati kitengo cha maalum cha jeshi, CAPSAT, kilipoingia uwanjani, vikosi vya usalama kutoka vitengo vingine vinavyolinda eneo hilo "vilikimbia kama panya."

    Awali kitengo maalum cha usalama kinachojulikana kama CAPSAT, kilitoa agizo kuvitaka vikosi vya usalama vilivyoko katika Ikulu za Lavoloha na Ambotsirohotra kurejea katika kambi zao.

    Rais yuko wapi?

    Kumekuwa na taarifa zinazokinzana kuhusiana na mahali alipo Rais Andry Rajoelina.

    Hapo awali, jarida moja la Ufaransa linaloangazia Afrika liliripoti kwamba rais alikuwa ameondoka katika mji mkuu, Antananarivo.

    Baadaye, taarifa hiyo ilibadilishwa na kusema hajulikani aliko.

    Mwandishi wa habari wa eneo hilo alisema aliarifiwa na chanzo cha kidiplomasia kwamba Rajoelina amekimbilia mji wa Majunga, ambako inadaiwa kuwa anasubiri kuondoka kuelekea Paris, Ufaransa.

    Bado tunaendelea kuthibitisha uhalisi wa ripoti hizi. (Na Omega Rakotomalala, wa BBC Monitoring Nairobi)

    Maelezo zaidi;

  3. Biden apokea tiba ya mionzi kukabiliana na Saratani ya kibofu

    ASD

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, anapokea tiba ya mionzi kama sehemu ya matibabu yake dhidi ya saratani ya kibofu, msemaji wake amethibitisha.

    Msemaji wake ameeleza kuwa Biden, mwenye umri wa miaka 82, anapokea matibabu ya homoni, bila kutoa ufafanuzi zaidi.

    Matibabu hayo ya mionzi yanatarajiwa kuchukua wiki tano ikiashiria hatua mpya katika matibabu yake, kwa mujibu wa chanzo kimoja kilichoiambia NBC News.

    Mnamo mwezi Mei, ofisi ya Biden ilitangaza kuwa aligunduliwa kuwa na aina kali ya saratani ya kibofu ambayo imeenea kwenye mifupa yake.

    Ugunduzi huo ulifanyika baada ya mwanasiasa huyo wa chama cha Democrat kuripoti kuhisi dalili zake kwenye njia ya mkojo, ambazo ziliwaongoza madaktari kugundua uvimbe mdogo kwenye kibofu.

    Taarifa hizo zinakuja huku maswali yakiibuliwa upya kuhusu afya ya rais huyo wa zamani alipokuwa madarakani.

    Soma Zaidi:

  4. Watu 60 wauawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani Sudan

    abc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 60 wameuawa katika shambulizi la ndege zisizo na rubani katika eneo la watu waliokimbia makazi yao huko El-Fasher, mji uliozingirwa na uliokaribu kuporomoka nchini Sudan.

    Kamati ya upinzani ya El-Fasher, inayoundwa na raia na wanaharakati wa eneo hilo, iliarifu kuwa kikosi cha Sudan (RSF) kilitekeleza mashambulizi mawili ya ndege zisizokuwa na rubani na mizinga nane.

    "Watoto, wanawake na wazee waliuawa huku wengine wakiteketea kwa moto kabisa," taarifa ya kundi hilo ilisema.

    Mashuhuda walielezea matukio hayo ya kuogofya wakati waokoaji wakiondoa miili kutoka kwenye vifusi.

    Hospitali ambazo tayari zinakabiliwa na miezi kadhaa ya kuzingirwa zimezidiwa, huku madaktari wakiwatibu majeruhi kwenye sakafu na viambaza.

    RSF imezingira El-Fasher kwa muda wa miezi 17 sasa, katika jaribio la kuchukua udhibiti wa ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan huko Darfur.

    Kwa mujibu wa kamati hiyo hali katika eneo la El-Fasher "imevuka maafa na mauaji ya halaiki".

    Sudan imekumbwa na mzozo tangu mwaka 2023, baada ya makamanda wakuu wa jeshi la RSF na Sudan kutoelewana na kuzuka mzozo mkali wa madaraka na kusababisha moja ya mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu.

    Soma zaidi:

  5. Hamas: Israel iwaachilie huru wafungwa mashuhuri kama sehemu ya makubaliano ya Gaza

    abc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Marwan Barghouti alipatikana na hatia ya mashambulizi mabaya dhidi ya raia wa Israel, lakini bado ni mmoja wa viongozi maarufu wa Palestina.

    Hamas inaishinikiza Israel kujumuisha Wapalestina mashuhuri katika orodha ya wafungwa wanaotaraji kuachiliwa ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo pia yatashuhudia mateka walioko Gaza kurejeshwa.

    Msisitizo huo wa Hamas unakuja baada ya wizara ya sheria ya Israel kuchapisha majina ya wafungwa 250 watakaoachiliwa, lakini ikiwaacha kando wafungwa saba wenye hadhi ya juu, akiwemo Marwan Barghouti na Ahmad Saadat.

    Wanaume hao ambao wanatumikia kifungo baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika na mashambulizi tofauti nchini Israel, wametazamwa kwa muda mrefu na Wapalestina kama nembo ya upinzani.

    Mateka 20 wa Israel wanatarajiwa kuachiliwa kabla ya saa 12:00 (09:00 GMT) siku ya Jumatatu kama sehemu ya makubaliano yaliyopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

    Afisa mwandamizi wa Kipalestina anayefahamu kuhusu mazungumzo hayo aliidokeza BBC kwamba mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff, aliahidi kulifikisha hoja ya kutengwa kwa wafungwa wa Kipalestina kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, lakini Israel imekataa vikali kuwajumuisha.

    Makabidhiano hayo yanatarajiwa kufanyika katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya usitishaji vita na kurejea kwa mateka, ulioidhinishwa wiki hii kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka miwili huko Gaza.

    Miili ya mateka walioaga dunia pia itarejeshwa.

    Inakadiriwa kuwa mateka 26 wamefariki, na hatima ya wengine wawili haijulikani.

    Israel pia itawaachilia wafungwa wa Kipalestina wapatao 250 wanaotumikia kifungo cha maisha katika magereza ya Israel, na Wapalestina wengine 1,700 kutoka Gaza ambao wamezuiliwa.

    Hamas ilikuwa imewasilisha orodha ya wafungwa waliotaka waachiliwe ambayo ni pamoja na Barghouti na Saadat.

    Soma Zaidi:

  6. Watu 18 hawajulikani walipo baada ya mlipuko Kiwandani Tennessee

    abc

    Watu 18 hawajulikani walipo baada ya mlipuko kutokea katika kitwanda cha silaha za kijeshi huko Tennessee siku ya Ijumaa.

    Kiongozi wa kauti ya Humphreys Chris Davis alithibitisha watu wanne au watano walipelekwa katika hospitali iliyo karibu baada ya mlipuko mkubwa uliosababisha kiwanda hicho kuporomoka kabisa.

    "Hakuna cha kuelezea, Kwisha kabisa," alisema.

    Kiwanda hicho cha Bucksnort, Tennessee kilichopo umbali wa takriban maili 56 (90km) kusini magharibi mwa Nashville kimejikita katika uzalishaji na uhifadhi wa mabomu.

    Chanzo cha mlipuko huo bado hakijafahamika.

    Video iliyorekodi kuonesha anga la kiwanda hicho inaonesha vifusi, magari yanayofuka moshi na mabaki machache ya kituo hicho kilichoteketea, ambacho kinamilikiwa na Accurate Energetic Systems.

    Sheriff Davis, alikataa kusema ni watu wangapi walikufa.

    Lakini alibaini kuwa kiwanda hicho kilikuwa kinaendelea kufanya kazi wakati mlipuko ulipotokea na kwamba milipuko iliyofuata iliwalazimu waokoaji kukimbia mbali na eneo hilo kujinusuru.

    Baadhi ya wafanyakazi ambao walikuwa wameanza majukumu yao wakati huo wanaweza kuwa hawajulikani walipo au wamekufa".

    Soma zaidi:

  7. Waisrael wawasubiri mateka kwa hamu na ghamu

    abc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Makabidhiano ya awali yalishuhudia mateka wakisafirishwa kwa ndege hadi hospitali za Israel kwa uchunguzi na kuunganishwa na familia zao.

    Waisrael wameendelea kuwa na matarajio makubwa wakati tarehe ya mwisho ya mateka kurudishwa nyumbani ikikaribia.

    Kama ambavyo tumekuwa tukiripoti, mateka 48 wanatarajiwa kurejeshwa nchini Israeli 47 kati yao walichukuliwa wakati wa mashambulizi ya Hamas mnamo 7 Oktoba 2023.

    Ishirini wanaaminika bado wangali hai.

    Shay Shimoni, ambaye mama yake aliuawa huko Kibbutz Nir Oz tarehe 7 Oktoba, anasema ni wakati wa wasiwasi na matumaini.

    "Tunajisikia msongo wa mawazo sana tunapotarajia kurejeshwa kwa mateka na kufikiwa kwa ukomo wa vita.

    Tunatumai tunaweza kuanza kupata uponyaji," anaeleza kupitia WhatsApp.

    Katika ujumbe mwingine, raia mkazi wa Kibbutz Be'eri - ambaye pia alilengwa katika mashambulizi anaeleza ana matumaini kwamba mateka watarejeshwa "leo au kesho na kwamba mambo yatakuwa mazuri".

    Moja ya hospitali zilizopangwa kuwapokea raia hao ilijiandaa kwa kufanya mazoezi ya kuwapokea na kuwapatia huduma,kwa mujibu wa NBC News.

    Daktari aliiambia NBC hatua ya kwanza itakuwa kuwaunganisha na familia zao.

    Baada ya hapo, badala ya kuingizwa moja kwa moja kwenye uchunguzi wa kimatibabu, mateka watapewa fursa ya kuchagua nini cha kufanya kama sehemu ya mchakato kisaikolojia wa kurejesha hali yao ya kawaida baada ya zaidi ya miaka miwili kifungoni.

    Soma Zaidi:

  8. UNRWA: Tuna uwezo wa kulisha Gaza kwa miezi mitatu

    axc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la misaada la Umoja wa Mataifa linasema linauwezo wa kutoa chakula cha kutosha kuwalisha wakazi wa Gaza kwa muda wa miezi mitatu.

    Katika maelezo mafupi aliyotoa mapema jumamosi, mkurugenzi wa mawasiliano wa UNRWA, Juliette Touma, anasema kuwa kusambaza msaada huo "ni hatua muhimu kabisa ili kudhibiti njaa zaidi".

    Mnamo Agosti, Shirika la usalama wa chakula linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa lilithibitisha uwepo wa njaa katika Jiji la Gaza na maeneo ya Jirani.

    Touma amerejelea wito wa kuruhusu msaada katika eneo hilo mara moja ili kudhibiti njaa iliyoenea.

    Kwa kuzingatia masharti ya awamu ya kwanza ya mpango wa Gaza, takriban msafara wa malori 600 ya misaada kwa siku yanatakiwa kuingia katika Ukanda huo kuanzia wakati wa usitishwaji wa mapigano ulipoanza kutekelezwa ambapo ilikuwa Ijumaa saa 12:00 saa za Gaza.

    Soma zaidi:

  9. Jeshi lawataka Polisi Madagascar kusitisha vurugu dhidi ya raia

    axb

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Jeshi nchini Madagascar limetoa wito kwa polisi kusitisha vurugu dhidi ya waandamanaji.

    Video iliyochapishwa katika ukurasa wa mtandao wa Facebook, kikosi hicho kimetoa wito kwa wanajeshi wenzao wanaounga mkono msimamo wao kujiunga nao katika kambi yao iliyoko Antananarivo.

    Kikosi hicho, almaarufu kama kama CAPSAT, kinaundwa hasa na maafisa wavyeo vidogo (Non-Commissioned Officers) na kujumuisha kanali mmoja kikiwa kiungo muhimu katika jeshi la Madagascar.

    Agizo hilo limevitaka vikosi vya usalama vilivyoko katika Ikulu za Lavoloha na Ambotsirohotra kurejea katika kambi zao za awali.

    Aidha mwanaharakati mmoja mjini Antananarivo anasema kuwa wanajeshi wengi wameripotiwa kuwasili katika kambi ya CAPSAT. (Tunaendelea kuthibitisha taarifa hii kwa njia huru).

    Huku wakitaka pia wanajeshi walioko katika kambi ya kijeshi ya Ivato kufunga uwanja wa ndege.

    CAPSAT imewataka wanajeshi kusaidiana, kuzifunga kambi zao, kukaidi amri kutoka kwa maafisa wa juu, na kuepuka kushiriki katika vurugu za kiraia.

    Soma zaidi:

  10. Melania Trump asema ameanzisha mfumo wa 'mawasiliano' na Putin kuhusu watoto wa Ukraine

    Melania Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump

    Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump anasema Rais wa Urusi Vladimir Putin amejibu barua aliyomuandikia kuelezea wasiwasi wake kuhusu watoto wahanga wa vita vya Urusi na Ukraine.

    Alitoa tangazo hilo siku ya Ijumaa, akisema kwamba baada ya '' mawasiliano ya wazi" na Putin, watoto wa Ukraine waliopoteleana na wazazi wao wakati wa vita wameunganishwa tena na familia zao.

    "Barua ya amani" ya Mke wa Rais iliwasilishwa kwa mkono kwa Putin wakati wa ziara yake huko Alaska mnamo mwezi Agosti.

    Rais Donald Trump aliweka sehemu za barua hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

    Katika barua hiyo, Melania Trump anamsihi Putin kuwalinda watoto, akiongeza kwamba kufanya hivyo "kutafanya hivyo sio kwa maslahi ya Urusi pekee" bali ni "kuonyesha moyo wa ubinadamu".

  11. Waziri wa mambo ya ndani wa Cameroon awaonya wagombea kutojitangaza washindi wa uchaguzi

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cameroon Paul Atanga Nji

    Chanzo cha picha, Michel Mvondo/BBC

    Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cameroon Paul Atanga Nji

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cameroon Paul Atanga Nji amewaonya wagombea wanaoshiriki uchaguzi wa rais Jumapili dhidi ya kudai ushindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa na baraza la katiba.

    Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa kabla ya upigaji kura, Nji alidai kuwa amepokea taarifa zikionyesha kwamba kuna mgombea anapanga kujitangaza mshindi japo hakumtaja mgombea huyo.

    Nji alilitaja wazo hilo kuwa “limepitwa na wakati” akitishia kumchukulia hatua yeyote atakayefanya hivyo.

    "Wale ambao watajaribu kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais au ushindi wowote wa kujitangaza wenyewe kwa kukiuka sheria za jamhuri watakuwa wamevuka mstari mwekundu," alionya.

    "Wagombea lazima watumie njia za kisheria kutetea haki zao," alisema.

    Hapo awali, waziri huyo alidai kuwa baadhi ya wagombea wa upinzani walikuwa wakipanga njama ya kuvuruga mchakato wa uchaguzi kupitia maandamano na kughushi matokeo.

    Mnamo 2018, Paul Biya alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa 2018.

    Lakini kiongozi wa upinzani Maurice Kamto alidai kura hizo ziliibiwa na kumuunga mkono mgombea aliye madarakani, akidai ndiye mshindi halali.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Hamas inawakusanya mateka 'sasa', asema Trump, Wapalestina wakirejea kaskazini mwa Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wameanza kutembea kaskazini kando ya barabara ya al-Rashid kuelekea mji wa Gaza ya mpango wa usitishaji vita na kuondoka kwa wanajeshi wa Israel kuanza kutekelezwa.

    Watakachokuwa wakirejelea ni uharibifu uliosababishwa na miaka miwili ya vita.

    "Niliiacha familia yangu nyuma na kuanza kutembea kuelekea kaskazini. Maelfu ya watu wanahangaika. Kukodisha gari kunagharimu karibu shekeli 4,000 (£924; $1,227), kiwango ambacho watu wengi hawaweza kumudu."

    Wanaorudi wanasema wanasukumwa na kukata tamaa na wala sio kujiamini kwamba watakuwa salama. Baadhi yao tayari wameambiwa kwamba nyumba zao hazipo tena.

    Kulingana na uchanganuzi wa picha za satelaiti uliotolewa mapema mwezi huu kutoka kwa watafiti katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Oregon, majengo 198,883 katika Ukanda wa Gaza yanakisiwa kuharibiwa tangu kuanza kwa vita.

    Uharibifu wa majengo unaweza kuonekana katika eneo lote, huku Jiji la Gaza likiwa mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi.

    Watafiti wanakadiria kuwa 74% ya majengo katika eneo hilo yaharibiwa tangu 7 Oktoba 2023.

    Maelezo zaidi:

  13. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.