'Hakuna mahali salama' - Raia waliokwama kati ya waasi na wanajeshi

- Author, Nick Ericsson
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ngabi Dora Tue, akiwa na huzuni, jeneza la mumewe, Johnson Mabia, linapita katikati ya umati wa waombolezaji huko Limbe katika eneo la Kusini-Magharibi mwa Cameroon - eneo ambalo limeshuhudia matukio kama haya mara nyingi.
Akiwa katika safari ya kikazi, Johnson - mtumishi wa umma anayezungumza Kiingereza - na wenzake watano walikamatwa na watu wenye silaha wanaotaka kujitenga.
Wanamgambo hao wanapigania uhuru wa mikoa miwili inayozungumza lugha ya Kiengereza katika nchi ambayo wengi wao wanazungumza lugha ya kifaransa. Mzozo wa takriban muongo mmoja umesababisha maelfu ya vifo na kudumaa kwa maisha katika eneo hilo.
Alipotekwa nyara miaka minne iliyopita, Dora alijitahidi kumfuatilia Johnson. Hatimaye wanamgambo wanaotaka kujitenga, waliomba fidia ya zaidi ya dola za kimarekani 55,000 (£41,500) ilipwe ndani ya saa 24 ili kuachiliwa kwake.
Kisha Dora akapokea simu nyingine kutoka kwa jamaa mmoja wa Johnson. "Alisema ... ‘niwatunze watoto. Mume wangu hayupo tena. Sikujua hata la kufanya. Alitekwa Jumanne alipokuwa akisafiri. Ijumaa aliuawa," anasema Dora.
Wanamgambo hao hawakumuua tu bali walimkata kichwa, na kuuacha mwili wake barabarani
Kutaka kujitenga

Chanzo cha picha, AFP
Mapambano ya kutaka kujitenga yanatokana na malalamiko ya muda mrefu ambayo yanaanzia wakati wa uhuru mwaka 1961, na kuundwa kwa taifa moja la Cameroon mwaka 1972 kutoka maeneo ya zamani ya Uingereza na Ufaransa.
Tangu wakati huo watu wanaozungumza Kiingereza wamehisi kutopewa haki na serikali kuu. Johnson alikuwa mpita njia asiye na hatia, alijikuta katikati ya vita vya kikatili vya kutaka kujitawala na mapambano ya serikali ya kukomesha uasi huo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wimbi la sasa la vurugu lilianza karibu muongo mmoja uliopita.
Mwishoni mwa mwaka 2016, maandamano ya amani yalianza dhidi ya kile kilichoonekana kama kuondoa matumizi ya Kiengereza katika mfumo wa sheria katika vyumba vya mahakama vya eneo hilo. Sehemu zinazozungumza Kifaransa na Kiingereza hutumia mifumo tofauti ya mahakama.
Maandamano hayo yalienea kwa kasi, na kusababisha kufungwa kwa maduka na taasisi.
Majibu ya vikosi vya usalama yalikuwa ya haraka na makali - watu walipigwa, kutishwa na wengi kukamatwa. Umoja wa Afrika uliita "matumizi mabaya ya nguvu na yasiyo na uwiano."
Wizara ya ulinzi ya Cameroon haikujibu maswali ya BBC kuhusu jambo hili au masuala mengine katika makala haya.
Vikundi vyenye silaha vilianzishwa. Mwishoni mwa 2017 mvutano ulipozidi, viongozi wanaotaka kujitenga walitangaza uhuru kwa kile walichokiita Jamhuri ya Shirikisho ya Ambazonia.
Hadi sasa, Wacameroon milioni tano wanaozungumza Kiingereza wamejikuta katika mzozo huo. Takriban watu 6,000 wameuawa na maelfu kulazimishwa kukimbia makazi yao.

"Tulikuwa tukiamka asubuhi na kuona maiti zikiwa barabarani," anasema Blaise Eyong, mwandishi wa habari kutoka Kumba katika eneo linalozungumza Kiingereza la Kusini-Magharibi mwa Cameroon.
"Au unasikia nyumba imechomwa moto. Au unasikia kuna mtu ametekwa. Viungo vya mwili vya watu vimekatwa. Unaishije katika jiji ambalo kila kukicha unakuwa na wasiwasi ikiwa jamaa zako watakuwa salama?"
Kusuluhisha mzozo
Kumekuwa na majaribio kadhaa ya kitaifa na kimataifa kusuluhisha mzozo huo, pamoja na kile ambacho serikali ilikiita "mazungumzo makubwa ya kitaifa" 2019.
Ingawa mazungumzo hayo yalitoa hadhi maalum kwa mikoa hiyo miwili inayozungumza lugha ya Kiingereza, lakini ni mambo machache sana ambayo yalitatuliwa kwa vitendo.
Felix Agbor Nkongho - wakili ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa maandamano ya 2016 na baadaye kukamatwa - anasema pande zote mbili sasa zinafanya zitakavyo, msingi wa maadili umetoweka.
"Kuna wakati… ambapo watu wengi walihisi, kama watahitaji usalama, watakawenda kwa wanaotaka kujitenga," aliambia BBC.
"Lakini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, sidhani kama kuna mtu yeyote mwenye akili timamu anawaza kwamba wanaotaka kujitenga ndio watawalinda.”

Serikali yashutumiwa
Lakini sio wale wanaotaka kujitenga tu wanaoshutumiwa kwa uhalifu.
Mashirika kama vile Human Rights Watch yamerekodi matukio ya kikatili ya vikosi vya usalama dhidi ya wanaodai uhuru. Kuchomwa kwa vijiji na mateso, kukamatwa kinyume cha sheria na mauaji ya watu kinyume cha sheria katika mgogoro ambao kwa kiasi kikubwa haujaonekana na ulimwengu wa nje.
John (sio jina lake halisi) na rafiki yake wa karibu waliwekwa chini ya ulinzi na vikosi vya jeshi la Cameroon, wakituhumiwa kununua silaha kwa ajili ya kundi linalotaka kujitenga.
John anakumbuka baada ya kuwekwa mahabusu, walipewa hati ambayo waliambiwa watie saini bila kupewa nafasi ya kuisoma. Walipokataa, mateso yalianza.
“Hapo ndipo walipotutenganisha katika vyumba tofauti,” anasema John. "Walimtesa [rafiki yangu]. Nilisikia wakimchapa viboko kila mahali. Baadaye waliniambia alikubali na kutia saini na wakamruhusu kuondoka."
Lakini huo haukuwa ukweli.
Mwezi mmoja baada ya kukamatwa, mwanaume mwingine aliingia katika seli ya John. Alimwambia rafiki yake alikufa katika chumba alichokuwa amewekwa na kuteswa. Miezi kadhaa baadaye kesi ya John ilifutwa na kuachiliwa bila kufunguliwa mashtaka.
Mbinu za waasi

Sehemu ya mkakati wa wanaotaka kujitenga kudhoofisha serikali na vyombo vyake vya usalama ni kushinikiza kupigwa marufuku kwa elimu ambayo wanasema ni chombo cha propaganda za serikali.
Oktoba 2020, shule moja huko Kumba ilishambuliwa. Hakuna aliyedai kuhusika na ukatili huo lakini serikali ililaumu wanaotaka kujitenga. Wanaume waliokuwa na mapanga na bunduki waliwaua takribani watoto saba.
Tukio hilo lilizua, hasira ya kimataifa na kulaaniwa kwa muda mfupi.
"Takribani nusu ya shule katika eneo hili zimefungwa," anasema mwanahabari Eyong.
"Watoto wanakosa elimu. Hebu fikiria athari kwa jamii zetu na pia kwa nchi yetu."
Mbali na ghasia kati ya vikosi vya serikali na vikundi vinavyotaka kujitenga, pia kuna ghasia nyingine. Makundi ya wapiganaji katika maeneo yanayotaka kujitenga yamejitokeza kupambana na Waambazonia katika juhudi za kudumisha umoja wa Cameroon.
Kiongozi wa mojawapo ya vikundi hivi, John Ewome (anayejulikana kama Moja Moja), aliongoza doria mara kwa mara katika mji wa Buea kutafuta watu wanaotaka kujitenga hadi alipokamatwa Mei 2024.
Yeye pia ameshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu, udhalilishaji na kuwatesa raia wasio na silaha wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa makundi ya wanaoaka kujitenga. Anakanusha tuhuma hizo.
"Sijawahi kuweka mikono yangu juu ya raia yeyote. Nawashika Waambazoni tu. Na ninaamini miungu ya nchi hii iko pamoja nami," aliambia BBC.
Wakati huo huo, utekaji nyara na mauaji unaendelea. Na kwa Ngabi Dora Tue, akiwa ameketi na mtoto wake mdogo mapajani mwake, maisha yanamwelemea.
"Nina madeni ninayopaswa kuyalipa hata sijui jinsi ya kuyalipa," anasema.
"Nilifikiria kujiingiza kwenye ukahaba. Kisha niliona aibu ambayo itakuja baadaye, ilinibidi nimeze magumu na kusonga mbele. Ni mdogo sana kuwa mjane."
BBC imeomba majibu kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Ambazonia (ADF). Limejibu kwamba kuna makundi mengi ya wapiganaji wanaotaka kujitenga katika eneo hilo.
ADF imesema inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na haishambuli wafanyakazi wa serikali, shule, waandishi wa habari au raia.
Inawaumu watu binafsi na makundi madogo madogo ambayo si wanachama wa ADF kwa mashambulizi haya.
Kundi hilo pia linashutumu serikali kwa kufanya ukatili huku wakidai kuwa ni wapiganaji wa Ambazonia ili kuwafanya wakazi wa eneo hilo kupinga mapambano ya ukombozi.















