Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Viongozi wa CHADEMA wasimulia adha waliyokutana nayo mikononi mwa polisi Tanzania
Viongozi wakuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, wameeleza masaibu yaliyowapata walipokamatwa na polisi jijini Mbeya, kusini mwa Tanzania.
Muhtasari
- Watu laghai wadukua nambari ya WhatsApp ya Gavana nchini Nigeria
- Wafadhili wa New Zealand wasambaza peremende zenye vichocheo hatari
- Marekani yaidhinisha mauzo ya silaha ya dola bilioni 20 kwa Israel
- Ukraine yadungua ndege 17 za Urusi zisizo na rubani
- Uvamizi wa Ukraine nchini Urusi: Tunachojua kufikia sasa
- Urusi: Hali katika eneo la Belgorod 'ni tete', - Gavana
- Marekani: Polisi ashtakiwa kwa kumpiga risasi mwanamke mjamzito
- Mwanajeshi wa Marekani akiri kosa la kuuza siri za kijeshi kwa China
- Marekani yasema inalenga 'kupunguza joto' huko Mashariki ya Kati
- Rukia Bulle wa Kenya ashinda Tuzo ya BBC Komla Dumor 2024
- Waziri wa Israeli ashutumiwa kwa kufanya maombi ya Wayahudi eneo takatifu la Jerusalem
- Mapacha waliozaliwa tu wauawa baba yao akiwa ameenda kuwasajili huko Gaza
Moja kwa moja
Asha Juma
Maandamano Kenya: Mahakama yawapiga marufuku polisi kutofunika nyuso zao wakati wa maandamano
Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Kenya ameagizwa kuhakikisha kuwa maafisa waliovalia kiraia hawafuniki nyuso zao wanapokabiliana na waandamanaji wakati wa maandamano.
Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alisema Inspekta Jenerali anapaswa kuhakikisha zaidi kuwa maafisa wake hawafichi kitambulisho au usajili wa gari lolote linalotumiwa wakati wa kushughulika na watu wanaoandamana.
Jaji alitoa maagizo hayo kufuatia ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini Kenya LSK.
LSK kupitia kwa wakili Dudley Ochiel iliambia mahakama kutumwa kwa maafisa waliovalia mavazi ya kiraia kila mara kunaleta hali ya sintofahamu ambayo hatimaye inazuia haki ya watu kuandamana.
"Maafisa hawa ambao hawajatambuliwa hawawezi kuwajibika kwa matendo yao. Matokeo yake wanaishia kutumia nguvu kupita kiasi. Hawawezi kuwajibika kwa sababu hawajulikani," alisema Ochiel.
Alimwambia Jaji kwamba isipokuwa mahakama kuingilia kati na mwelekeo huo kukomeshwa, Wakenya wana hatari ya kifo na kunyimwa haki zao kwa mujibu wa katiba.
Jaji Bahati ambaye aliidhinisha suala la LSK kuwa la dharura aliagiza IG kuhakikisha kuwa kuna utiifu kamili katika suala la kuhakikisha kwamba maafisa wote waliovalia sare wataweka majina yao katika sare walizovalia kila wakati au nambari ya huduma inayotambulika.
Viongozi wa CHADEMA wasimulia 'masaibu' waliyokutana nayo mikononi mwa polisi Tanzania,
Viongozi wakuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, wameeleza masaibu yaliyowapata walipokamatwa na polisi jijini Mbeya, kusini mwa Tanzania.
Wameeleza hayo hii leo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao walikumbwa na misukosuko hiyo baada ya kukamatwa na polisi wakiwa katika ofisi za kanda ya Nyasa, jijini Mbeya, walikokwenda kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Hata hivyo maadhimisho hayo hayakufanyika, baada ya kuzuiliwa na polisi na zaidi ya viongozi na wanachama wa Chadema 520, pamoja na waandishi wa habari kushikiliwa.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, John Mnyika na Joseph Mbilinyi.
Akizungumza na waandishi wa Habari Makamu mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lisu anasema Polisi waliwapiga viongozi hao akiwemo Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika na Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu.
Lissu anasema viongozi hao walikamatwa, kupigwa na kuwanyima haki za msingi hasa haki ya kuwasiliana na mawakili wao pamoja familia.
Jopo la mawakili wanatarajiwa kukaa kuanzia Kesho ili kujadili hoja za msingi za kufungua mashtaka hayo " Tutaenda kuwashtaki viongozi hao kama wao miongoni mwa sababu za kuwashtaki ni kutukamata kinyume na Sheria, kutupiga na kuzuia kufanya kongamano ambalo lengo letu kilikuwa kuadhimisha siku ya vijana kimataifa".Alisema Lissu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wa CHADEMA Freeman Mbowe ametaka ametaka Serikali pamoja na Jeshi la polisi kuheshimu demokrasia hasa katika kipindi ambacho Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwezi October na uchaguzi mkuu hapo mwakani
''Sisi kama Chama tunachukua jambo hili kwa uzito mkubwa sana na tunaamini jambo hili ni mkakati wa makusudi uliotengenezwa na serikali, vyombo vyake vya ulinzi na usalama likiwemo jeshi la polisi''. Alisema Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe.
Mbowe amesema kuwa chama chake hakijawahi kuwa cha kigaidi. Amesema tuhuma za msajili msaidizi wa vyama vya siasa hizina msingi.
" Tunalaani vitendo vilivyofanywa na Jeshi la polisi tunataka Serikali ijue hatutaruhusu matendo haya yaendelee tukieleke uchaguzi CHADEMA tunajiandaa kuchukua nchi kupitia maboksi ya kupigia Kura"
Hayo yakiendelea Ubalozi wa Marekani umelaani tukio la Polisi kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa kuwakamata viongozi wa CHADEMA
" Tunaunga mkono wito wa mashirika ya kiraia ya Tanzania na tunahimiza Serikali ya Tanzania kuheshimu katiba yake,na kuhakikisha mazingira salama ya wazi ya kisiasa ambapo sauti zote zinakuwa huru kusikika".lilisema tamko lake.
Kenya: Bei ya mafuta yasalia ilivyo katika tangazo jipya la EPRA
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini Kenya (Epra) imetangaza bei za mafuta kuanzia tarehe 15 Agosti 2024 hadi Septemba 14, 2024.
Bei za mafuta zimesalia bila kubadilika katika tangazo jipya la bei za bidhaa hiyo muhimu.
Mafuta ya petroli yatauzwa kwa Sh188.84, dizeli Sh171.60 huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh161.75 jijini Nairobi kuanzia saa sita usiku.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 101(y) cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2019 na notisi ya kisheria nambari 192 ya mwaka 2022, hatujabadilisha bei za juu zaidi za rejareja za mafuta ya petroli, ambazo zitaanza kutumika kuanzia Agosti 15, 2024 hadi Septemba 14, 2024. ," Epra ilisema katika taarifa.
"Katika kipindi kinachoangaziwa, bei ya juu inayoruhusiwa ya petroli, dizeli na mafuta ya taa bado haijabadilika."
Epra ilisema kuwa bei hizo ni pamoja na kodi ya Ongezeko la Thamani ya asilimia 16 (VAT) kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Fedha ya 2023, Sheria ya Kodi ya Sheria ya 2020 na viwango vilivyorekebishwa vya Ushuru wa bidhaa.
Mke wa rais wa zamani wa Zambia Maureen Mwanawasa aaga dunia
Mke wa Rais wa zamani wa Zambia Maureen Mwanawasa amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 61.
Alifariki Jumanne jioni baada ya kuugua kwa muda mfupi katika hospitali moja katika mji mkuu, Lusaka, familia yake ilisema.
Mke huyo wa zamani aliolewa na Rais wa tatu wa nchi hiyo, Levy Mwanawasa, ambaye alihudumu kuanzia 2002 hadi kifo chake mwaka 2008.
Rais Hakainde Hichilema alielezea kifo chake kama "mshtuko mkubwa".
Akiwa wakili, Bi. Mwanawasa alikuwa mtetezi mahiri wa haki, maendeleo ya jamii na masuala ya afya ya umma.
Alimiliki kampuni ya mawakili pamoja na mumewe hadi alipoingia kwenye siasa na alihusika kikamilifu katika azma ya mafanikio ya mumewe ya urais mwaka wa 2001.
Kabla ya kifo cha mume wake mnamo 2008, alionekana kuwa mgombea anayeweza kumrithi lakini baada ya kifo chake, hakutaka kugombea.
Mwaka 2016, Bi Mwanawasa aligombea nafasi ya meya wa Lusaka bila mafanikio.
Haijabainika kama alikuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa kabla ya kifo chake.
Alikuwa mwanachama mwanzilishi na rais wa zamani wa Shirika la Wake wa Marais wa Afrika dhidi ya VVU/UKIMWI, ambalo kwa sasa linajulikana kama Shirika la Wanawake wa Marais wa Afrika kwa Maendeleo.
Juhudi zake katika maendeleo ya jamii zilimletea tuzo kadhaa, ikiwa ni pamoja na tuzo la Kimataifa la Matumaini kutoka kwa World Vision 2006.
Kwanini Urusi bado haijaweza kuviondoa vikosi vya Ukraine?
Mashambulizi ya Kiukreni yameingia katika siku yake ya tisa, na Urusi sio tu inajitahidi kuirudisha Ukraine nyuma, lakini inaonekana haina uwezo wa kusimamisha mapigano mapema.
Televisheni ya serikali inaonesha picha za mizinga ya Urusi ikipakiwa kutumwa eneo la Kursk.
Lakini wachambuzi wanasema jeshi la Urusi halina akiba ya kutosha kwa ajili ya operesheni hiyo.
Akina mama wa askari wa jeshi la Urusi wanawaambia waandishi wa habari kwamba watoto wao watatumwa katika eneo hilo hivi karibuni, sio kikosi cha wasomi kinachohitajika kuwafukuza wanajeshi wa Ukraine walio na vita kali.
Katika miezi michache iliyopita, Moscow imekuwa ikifanya mashambulizi yake mashariki mwa Ukraine,ikifanya mashambulizi dhidi ya safu za ulinzi za Ukraine ili kudhibiti kilomita chache za eneo.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema Urusi ilipoteza wanajeshi 70,000 ndani ya miezi miwili tu, wastani wa karibu 1,000 kwa siku.
Urusi, inaonekana, ina akiba chache zilizobaki. Wataalamu wa kijeshi wanasema Ukraine ina ujasusi bora zaidi, ikijumuisha kutoka kwa washirika wa Magharibi, na wanajeshi waliofunzwa vyema.
Unaweza kusoma;
Kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine adai kudhibiti mji wa mpakani wa Sudzha, Urusi
Kamanda mkuu wa Ukraine amedai kuwa wanajeshi wa Ukraine sasa wanadhibiti kikamilifu mji wa mpakani wa Urusi wa Sudzha.
Katika video iliyochapishwa kwenye mtandaio wa Telegram, Oleksandr Syrskyi anaonekana akimwambia Rais Volodymyr Zelensky kwamba majeshi ya Ukraine sasa "yamekamilisha" "utafutaji na uharibifu" dhidi ya wanajeshi wa Urusi huko Suzha, mji ndani ya eneo la Kursk.
BBC haina uwezo wa kujitegemea kuthibitisha hili na haijulikani ni sehemu gani hasa ya eneo la Urusi huko Kursk limetekwa na Ukraine.
Hata hivyo, kama tulivyoripoti mapema kidogo, ripoti ya televisheni ya Ukraine iliyorekodiwa ndani ya mji wa Urusi wa Sudzha ilionyesha wanajeshi wa Ukraine wakiondoa bendera ya Urusi kutoka kwa shule moja.
Jeshi la Sudan lasusia mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani
Mazungumzo mapya ya amani yenye lengo la kumaliza vita vya miezi 16 vya Sudan yameanza licha ya moja ya pande zinazopigana, jeshi la taifa, kukataa kuhudhuria.
Marekani, ambayo inawezesha majadiliano, ilisisitiza kuwa tukio hilo liliendelea bila kujali kama mamilioni ya watu wanaoteseka nchini Sudan "hawawezi kumudu kusubiri".
Mapigano kati ya jeshi na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yamegharimu maelfu ya maisha, na kusababisha watu takribani milioni 10 kukimbia makazi yao.
Jeshi lilikatiza matumaini ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kususia mazungumzo ya Jumatano, likisema kwamba halitahudhuria kwa vile RSF haikutekeleza "kile kilichokubaliwa" nchini Saudi Arabia mwaka jana.
RSF haikuwa imetimiza masharti muhimu ya Azimio la Jeddah, kama vile kuwaondoa wapiganaji wake kutoka kwenye nyumba za raia na vituo vya umma, jeshi lilisema.
Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X, RSF ilisema imefika katika mji wa Uswizi wa Geneva kwa mazungumzo na kutoa wito kwa jeshi "kujitolea kutimiza matarajio ya kidemokrasia ya watu wa Sudan".
Jeshi pia lilikataa mazungumzo hayo kwa vile linapinga kuwepo kama mwangalizi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambayo inashutumu kuunga mkono RSF.
Kando ya UAE, wajumbe wanaowakilisha Marekani, Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanahudhuria.
Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, makumi ya maelfu ya vifo vinavyoweza kuzuilika vinakaribia nchini Sudan ikiwa mzozo na vikwazo vya misaada ya kibinadamu vitaendelea.
Marekani ilisema mzozo huo umefikia kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa na kuyahama makazi yao.
Unaweza kusoma;
Vikosi vya Ukraine vyasema vimewakamata wanajeshi 100 wa Urusi
Zaidi sasa kutoka kwa ujumbe uliotumwa hivi punde kwenye mitandao ya kijamii na Rais Volodymyr Zelensky.
Anaonekana akizungumza kupitia video na kamanda mkuu wa jeshi Oleksandr Syrskyi.
Syrskyi anamwambia rais kwamba vikosi vya Ukraine leo vimewakamata wanajeshi 100 wa Urusi wakati wa uvamizi wao katika eneo la Kursk la Urusi.
"Ninamshukuru kila mtu anayehusika," anaongeza Zelensky kwenye X. "Hii itaharakisha kurudi kwa vijana na wasichana wetu nyumbani."
Ukraine inasonga mbele katika maeneo mengi huko Kursk - Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky anasema kuwa vikosi vya Ukraine vinaendelea kusonga mbele zaidi katika eneo la Kursk nchini Urusi.
Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, kiongozi huyo wa Ukraine anasema vikosi vimesonga mbele umbali wa kilomita moja hadi mbili katika maeneo mbalimbali leo.
BBC haiwezi kuthibitisha hili kwa uhuru na haina uhakika ni kiasi gani hasa eneo la Urusi limetwaliwa.
Walaghai wadukua nambari ya WhatsApp ya Gavana nchini Nigeria
Watu wanaoshukiwa kuwa laghai wamedukua nambari ya WhatsApp ya Umo Eno, gavana wa jimbo lenye utajiri wa mafuta la Akwa Ibom nchini Nigeria, na kuwaomba pesa watu wanaowasiliana naye.
Akwa Ibom, kusini mwa Nigeria, ni jimbo la tatu kwa utajiri nchini humo kulingana na pato lake la ndani la kila mwaka la $19bn (£15bn).
Gavana huyo, mchungaji aliyeanzisha shirika la All Nations Christian Ministry International, alichaguliwa mwaka jana.
Wengi wa watu waliowasiliana naye kwa simu walipokea jumbe kutoka kwa nambari yake ya WhatsApp mnamo Jumanne zikiwataka wahamishe kiasi fulani cha pesa kwenye akaunti na kuahidi kulipwa baadaye.
Katibu wa gavana, Ekerete Udoh alitoa taarifa kuthibitisha kwamba nambari ya WhatsApp ya gavana huyo "ilitengenezwa" na wahalifu wanaojaribu kuwalaghai watu.
Bw Udoh alisema vyombo vya kisheria vimearifiwa. "Tunaonya kwamba ujumbe wowote unaoonekana kuomba pesa kwa walaghai hawa unapaswa kupuuzwa kabisa na umma kwa kuwa hautoki kwa Gavana," taarifa hiyo ilieleza.
Chini ya mwezi mmoja uliopita, nambari za simu zilizohusishwa na gavana mwingine ziliathiriwa katika hali kama hiyo, Ademola Adeleke wa jimbo la Osun, mjomba wa nyota wa Afrobeats Davido.
Mchambuzi wa masuala ya usalama mtandaoni Bilal Abdullahi alisema magavana wanapaswa kuongeza usalama zaidi kwa nambari zao na WhatsApp ili kuepuka masuala ya aina hii.
Unaweza kusoma;
Wafadhili wa New Zealand wasambaza peremende zenye vichocheo hatari
Polisi nchini New Zealand wanazifuatilia peremende zenye "kiwango cha hatari cha methamphetamine" baada ya kusambazwa na shirika la kutoa misaada huko Auckland.
Hadi watu 400 wanaweza kupata peremende hizo kutoka kwa Misheni ya Jiji la Auckland kama sehemu ya kifurushi cha chakula, lilisema shirika la misaada la kupambana na umaskini.
Peremende hizo zilitolewa bila kujulikana na mtu mmoja katika kifurushi kilichofungwa, iliongeza.
Takribani watu watatu, akiwemo mtoto, walitafuata matibabu baadaye ingawa hakuna aliye hospitalini kwa sasa. "Hatukujua kwamba loli hizo zilikuwa na methamphetamine ziliposambazwa," msemaji wa shirika hilo la kutoa misaada aliambia BBC.
Polisi wanasema ingawa tukio hilo linaweza kuwa la bahati mbaya badala ya operesheni iliyolengwa, hawakuwa wamefikia hitimisho lolote kwani ni "mapema kusema".
Shirika la kutoa misaada lilitahadharisha mamlaka siku ya Jumanne baada ya kuarifiwa na mpokeaji kuhusu peremende
Helen Robinson, mtendaji mkuu wa Auckland City Mission, alisema kuwa baadhi ya wafanyakazi wa shirika la usaidizi walijaribu peremende wenyewe na kukubaliana na malalamiko, baada ya kuanza "kujisikia hali isiyo ya kawaida" baadaye.
Kisha walizipeleka peremende ambazo bado zilikuwa kwenye eneo hilo kwa NZ Drug Foundation kwa ajili ya vipimo, ambayo vililithibitisha kuwa viwango vya hatari vya methamphetamine vilikuwa kwenye sampuli. a katika vifurushi hivi.
Marekani yaidhinisha mauzo ya silaha ya dola bilioni 20 kwa Israel
Marekani imeidhinisha uuzaji wa ndege za kivita zenye thamani ya dola bilioni 20 na vifaa vingine vya kijeshi kwa Israel, ambayo inaendeleza vita vyake vya miezi 10 katika Ukanda wa Gaza.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameidhinisha uuzaji wa takriban dola bilioni 19 za ndege na vifaa vya F-15, pamoja na risasi za mizinga zenye thamani ya dola milioni 774, zaidi ya dola milioni 60 za vilipuzi na magari ya kijeshi yenye thamani ya dola milioni 583. Pentagon ilisema katika taarifa.
Pentagon ilisema, "Marekani imejitolea kwa usalama wa Israel na ni muhimu kwa maslahi ya kitaifa ya Marekani kusaidia Israel kuendeleza na kudumisha uwezo imara, tayari kwa ulinzi."
Katika chapisho kwenye jukwaa la X, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Galant aliwashukuru maafisa wa Marekani kwa kuisaidia Israel kudumisha "makali yake ya kijeshi katika eneo" na kujitolea kwa Marekani kwa usalama wa Israel.
Vilevile, Rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza kunaweza kusaidia kuizuia Iran kufanya mashambulizi dhidi ya Israel.
"Tutaona Iran itafanya nini na nini kitatokea ikiwa kutakuwa na shambulio, lakini sitakata tamaa," Biden alisema wakati akishuka kutoka kwenye ndege yake wakati wa ziara ya New Orleans, Louisiana.
Hofu kuhusu hatua ya jibu la Iran kwa Israel bado imeendelea kuwepo baada ya mauaji ya mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran Julai mwaka jana, ambayo Israel haijadai kuhusika nayo.
Kwa upande wake balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Marekani inalenga "kudhoofisha" eneo la Mashariki ya Kati, huku kukiwa na hofu kwamba Iran itaishambulia Israel kwa kulipiza kisasi.
Unaweza kusoma;
Ukraine yasema imedungua ndege 117 za Urusi zisizo na rubani
Jeshi la wanahewa la Ukraine limesema limedungua ndege 17 kati ya 23 zilizorushwa na Urusi usiku kucha.
Vikosi vya Urusi pia vilirusha makombora mawili yaliyoongozwa, jeshi limeongeza.
Ndege hizo zisizo na rubani zilidunguliwa katika maeneo ya Kyiv, Kharkiv, Kirovohrad, Cherkasy, Mykolaiv, Sumy, Zhytomyr na Zaporizhzhia, jeshi la anga limesema.
Miundombinu iliharibiwa katika mikoa ya kaskazini ya Chernihiv na Zhytomyr, na nyumba mbili zilishambuliwa huko Mykolaiv kusini - lakini hakuna majeruhi walioripotiwa.
Soma zaidi:
Uvamizi wa Ukraine nchini Urusi: Tunachojua kufikia sasa
- Gavana wa eneo la mpakani la Belgorod nchini Urusi ametangaza hali ya dharura- Hili ni eneo la pili kuchukua hatua hiyo. Katika matukio mengine:
- Ukraine inasema vikosi vyake vimekuwa vikisonga mbele katika eneo la Kursk nchini Urusi. Rais Volodymyr Zelensky alisema jana Ukraine sasa inadhibiti miji na vijiji 74 katika eneo hilo - au takriban kilomita za mraba 1,000 kulingana na mkuu wake wa kijeshi.
- Urusi inasema kuwa imedungua ndege 117 za Ukraine zisizo na rubani katika eneo lake usiku kucha – katika maeneo ya ndani kabisa yaardhi yake, kama vile Voronezh.
- Urusi yajibu: Lakini makamanda wakuu wa Urusi wanadai kwamba uvamizi wa Ukraine umesitisha imesitishwa, huku Meja Jenerali Apti Alaudinov akisema jihudi za kuteka mji wa blitzkrieg hazikufanikiwa"
Urusi: Hali katika eneo la Belgorod 'ni tete', - Gavana
Gavana wa eneo la mpakani la Urusi la Belgorod ametangaza hali ya hatari, akisema mashambulizi ya makombora ya Ukraine yanaifanya hali kuwa "tete na yenye kusababisha wasiwasi mno".
Vyacheslav Gladkov amesema katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegram kwamba mashambulizi ya kila siku ya Ukraine yameharibu nyumba na kuua na kujeruhi raia.
Tangazo lake linawadia siku nane baada ya Ukraine kuanzisha uvamizi wa ghafla nchini Urusi.
Wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakisonga mbele katika eneo la Kursk nchini Urusi, na kamanda mkuu wa Ukraine alidai mapema wiki hii kwamba kilomita za mraba 1,000 za ardhi ya Urusi ziko chini ya udhibiti wao.
Uvamizi huo ulianza Jumanne iliyopita tarehe 6 Agosti, huku wanajeshi wa Ukraine wakiingia katika eneo la Kursk la Urusi kwenye mpaka.
Tangu wakati huo, Urusi inasema Ukraine imeshambulia eneo jingine la kusini - Belgorod - kutoka mpakani.
Makumi ya maelfu ya watu wamehamishwa kutoka mikoa yote miwili.
Soma zaidi:
Marekani: Polisi ashtakiwa kwa kumpiga risasi mwanamke mjamzito
Afisa wa polisi anayedaiwa kumpiga risasi mwanamke mjamzito huko Ohio ameshtakiwa kwa mauaji.
Ta'Kiya Young, 21, alikuwa na ujauzito wa karibu wiki 25 wakati wa kifo chake Agosti iliyopita.
Binti yake ambaye alikuwa bado tumboni pia alifariki dunia.
Siku ya Jumanne, jopo la majaji katika jiji la Columbus lilipata ushahidi wa kutosha kufungua mashtaka dhidi ya Connor Grubb, afisa wa polisi wa mji wa Blendon kwa mauaji, kuua bila kukusudia na kushambulia.
Kamera inayowekwa kwenye nguo iliyotolewa mwaka jana ilionyesha polisi wakijaribu kumzuia Bi Young asiondoke kwa gari lake ili waweze kumhoji kuhusu madai ya wizi dukani.
Katika video hiyo alionekana akiendesha kuelekea kwa afisa aliyefyatua risasi iliyomuua huku akimuamuru atoke nje ya gari lake.
Bi Young alishukiwa kuiba pombe katika duka la Kroger, wachunguzi wanasema.
Mawakili wa Bw Grubb wanasema alifyatua risasi ili kujilinda.
Mwanajeshi wa Marekani akiri kosa la kuuza siri za kijeshi kwa China
Mchambuzi na mwanajeshi wa Marekani amekiri mashtaka ya kula njama ya kuuza siri za kijeshi kwa China, Wizara ya Sheria imesema.
Sajenti Korbein Schultz alikamatwa mnamo mwezi Machi baada ya uchunguzi wa FBI na Jeshi la Marekani kudai kuwa alilipwa $42,000 (£33,000) kwa mabadilishano ya rekodi nyeti za usalama.
Njama hiyo ya uhalifu ilianza Juni 2022 na iliendelea hadi kukamatwa kwake, maafisa walisema.
Amepangwa kuhukumiwa mwezi Januari.
Sajenti Schultz, ambaye alikuwa na kibali cha kuweza kufikia taarifa za siri, alipanga njama ya kukusanya data na mtu ambaye aliamini kuwa anaishi Hong Kong, kulingana na nyaraka za mahakama.
Mkazi huyo anayedaiwa kuwa wa Hong Kong alimwomba sajenti Schultz kukusanya data nyeti kuhusiana na ulinzi wa makombora na mifumo ya mizinga inayohamishika, kulingana na rekodi za mahakama.
Sajenti Schultz pia alikusanya data kuhusu ndege za kivita za Marekani, mbinu za kijeshi, na mkakati wa ulinzi wa jeshi la Marekani kwa Taiwan, kulingana na kile ilichojifunza kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine.
"Kwa kula njama ili kusambaza taarifa za ulinzi wa taifa kwa mtu anayeishi nje ya Marekani, mshtakiwa huyu aliweka usalama wa taifa letu katika hatari kwa kutumia vibaya imani ambayo jeshi letu iliweka kwake," Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu Matthew Olsen wa Kitengo cha Usalama wa Kitaifa cha Wizara ya Sheria alisema.
Siku ya Jumanne, sajenti Schultz alikiri mashtaka yote dhidi yake, ikiwa ni pamoja na njama ya kupata na kufichua habari za ulinzi wa taifa na kuchukua hongo kama afisa wa umma.
Marekani yasema inalenga 'kupunguza joto' huko Mashariki ya Kati
Marekani inalenga "kupunguza joto" huko Mashariki ya Kati, balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa amesema, baada ya Iran kutupilia mbali wito wa nchi za Magharibi kujizuia kulipiza kisasi dhidi ya Israeli kwa mauaji ya kiongozi wa Hamas mwezi uliopita.
Siku ya Jumanne, Linda Thomas-Greenfield aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani inataka "kuzuia na kulinda dhidi ya mashambulizi yoyote yajayo ili kuepuka migogoro ya kikanda".
Maoni yake yanawadia huku Marekani ikiongeza juhudi zake za kufikia usitishaji vita kati ya Israeli na Hamas huko Gaza.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari iwapo kufikia makubaliano hayo kutasaidia kuzuia Iran kufanya mashambulizi dhidi ya Israeli, Rais wa Marekani Joe Biden alisema: "Hayo ndio matarajio yangu lakini tusubiri."
"Tutasubiri kuona Iran itafanya nini na kitakachotokea ikiwa kutakuwa na shambulio lolote, lakini sitakata tamaa," alisema, wakati akitoka kwenye ndege yake katika ziara ya New Orleans, Louisiana siku ya Jumanne.
Duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano imepangwa kufanyika mjini Doha au Cairo siku ya Alhamisi.
Lakini afisa wa Hamas Ahmad Abdul Hadi ameripotiwa kusema kuwa Hamas haitashiriki katika mazungumzo hayo, kwa mujibu wa ripoti za New York Times na Sky News.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken aliahirisha mpango wa kusafiri hadi Mashariki ya Kati siku ya Jumanne ili kushiriki katika mazungumzo ya kumaliza vita huko Gaza.
Soma zaidi:
Rukia Bulle wa Kenya ashinda Tuzo ya BBC Komla Dumor 2024
Mwanahabari wa Kenya Rukia Bulle ameshinda tuzo ya BBC News Komla Dumor ya 2024.
Rukia mwenye umri wa miaka 30, ambaye ni mpokeaji wa tisa wa tuzo hiyo na anafanya kazi katika kampuni ya Nation Media Group ya Kenya, anajishughulisha na masuala ya habari zinazowahudu na kuwavutia watu
Bulle pia amefanikiwa kujenga ufuasi mkubwa kwenye TikTok kupitia maudhui yake yanayohusiana na kuarifu kuhusu maisha ya mwanahabari.
Tuzo hiyo iliundwa kwa heshima ya Dumor, mwandishi wa habari wa Ghana na mtangazaji wa BBC World News, ambaye aliaga dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 41 mnamo 2014.
Alikuwa amefanya kazi bila kuchoka kuleta simulizi yenye tofauti na ya kipkee ya Afrika duniani, akiwakilisha upande wa kujiamini, wenye ujuzi na ujasiriamali.
Waamuzi walivutiwa na uthabiti wa Bulle na uwezo wake wa kushughulikia hadithi zenye changamoto, umakini wake katika kuangazia sauti zenye uwakilishi mdogo na uwepo wake mkubwa hewani.
“Kushinda tuzo hii kunamaanisha jambo kubwa kwangu. Kama mwandishi wa habari, unajitahidi kila mara kufanya uwezavyo, bila kujali kutambuliwa, kwa hivyo kutambuliwa katika jukwaa la kimataifa kupitia Tuzo ya Komla Dumor kunathibitisha sana imani yangu,” alisema Bulle, ambaye alijitokeza mwaka jana kwenye orodha ya Waislamu 100 wa Kenya wenye ushawishi mkubwa. .
"Natumai tuzo hii itawatia moyo wasichana wachanga kama mimi, ambao huvaa hijab na wanaotoka katika jamii za wachache, kuwa na ndoto kubwa na kufikia malengo yao."
Mwanahabari huyo wa Kenya atafanya kazi kwa miezi mitatu na timu za BBC News kwenye televisheni, redio na mtandaoni jijini London.
Pia atapata mafunzo na kuongozwa na wanahabari wakuu wa BBC.
Unaweza pia kusoma