Tuzo ya BBC ya Komla Dumor ya 2023 yazinduliwa

BBC inamtafuta nyota anayechipukia katika uandishi wa habari barani Afrika kwa ajili ya Tuzo ya BBC World News Komla Dumor, ambayo sasa ni mwaka wake wa nane.

Waandishi wa habari kutoka kote barani Afrika wanaalikwa kutuma maombi ya kuwania tuzo hiyo, ambayo inalenga kuibua na kukuza vipaji vipya kutoka barani humo.

Mshindi atapata fursa ya kuwa katika makao makuu ya BBC mjini London, kwa miezi mitatu kupata ujuzi na uzoefu.

Kupokelewa kwa maombi kutafungwa tarehe 14 Februari 2023 saa 23:59 GMT.

Tuzo hiyo ilianzishwa kwa ajili ya kumuenzi Komla Dumor, mtangazaji wa kipekee kutoka Ghana na mtangazaji wa BBC World News, aliyefariki ghafla akiwa na umri wa miaka 41 mwaka 2014.

Mjane wa Dumor, Kwansema Dumor alisema "anajivunia" matokeo ya mumewe katika BBC, na pia alisema familia yake "inatoa shukrani kwa BBC kwa kumkumbuka" kupitia tuzo hiyo.

BBC inawahimiza wanahabari kote barani Afrika kutuma maombi kwa ajili ya tuzo hiyo, ambayo inalenga kukuza na kusherehekea vipaji bora vya uandishi wa habari wanaoishi na kufanya kazi katika bara la Afrika

Pamoja na kupata mafunzo, atakayefaulu atapata fursa ya kusafiri katika nchi moja barani Afrika kuripoti habari ambayo wameifanyia utafiti, ripoti hiyo ikitangazwa kwa hadhira ya kimataifa ya BBC.

Akiwa anajulikana kwa kutetea uandishi wa habari dhabiti na mahiri na kwa kujitolea kwake kuripoti hadithi za Kiafrika kwa ukamilifu na uhalisi, Dumor alileta mafanikio makubwa kwa Afrika na kwingineko duniani.

Mtangazaji na mwanahabari wa televisheni ya Zambia Dingindaba Jonah Buyoya alikuwa mshindi wa mwaka jana - wa kwanza kutoka kusini mwa Afrika.

Wakati wake, alisafiri hadi Ushelisheli kuripoti jinsi mimea ya bahari ya nchi inaweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Komla Dumor alinipa hamasa, hivyo kushinda tuzo na kushiriki katika urithi wake imekuwa heshima," Buyoya alisema.

"Ninawahimiza waandishi wa habari wa Kiafrika kutuma maombi ya tuzo, ni njia ya kipekee ya kujifunza na kukuza zaidi ujuzi unaohitajika ili kusimulia hadithi zaidi za msingi barani Afrika."

Liliane Landor, mdhibiti mkuu wa BBC News International Services, alisema: "Tuzo na washindi wetu wa awali ni uthibitisho unaofaa wa kujitolea kwa Komla kusimulia hadithi za Kiafrika kwa kina na uadilifu."

Dumor alikuwa mtangazaji wa Focus on Africa, kipindi cha kwanza kabisa cha BBC cha habari za kila siku za televisheni kwa Kiingereza kwa watazamaji wa Kiafrika.

Kilitangazwa kwenye BBC World News, ambacho baadaye mwaka huu kinaunganishwa na Idhaa ya Habari ya BBC ili kuwa na Idhaa ya habari ya TV ya pamoja ya saa 24.

Pia alikuwa mmoja wa watangazaji wakuu wa kitengo cha asubuhi cha BBC World News Ulaya.

Alijiunga na BBC mwaka wa 2007 baada ya muongo mmoja wa uandishi wa habari nchini Ghana ambako alishinda tuzo ya Mwanahabari Bora wa Mwaka wa Ghana.

Kati ya 2007 na 2009 alikuwa mwenyeji wa kipindi cha Network Africa kwa BBC World Service, kabla ya kujiunga na kipindi cha The World Today.

Mwaka wa 2009 Dumor alikua mtangazaji wa kwanza wa kipindi cha habari za biashara za Kiafrika kwenye BBC World News, Africa Business Report.

Alisafiri kote barani Afrika, akikutana na wajasiriamali wakuu barani Afrika na kuripoti juu ya mitindo ya hivi karibuni ya biashara kote barani.

Mwaka 2013 Dumor alishiriki katika orodha ya jarida la New African la Waafrika 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi.

Washindi wa awali:

  • 2015: Nancy Kacungira kutoka Uganda
  • 2016: Didi Akinyelure kutoka Nigeria
  • 2017: Amina Yuguda kutoka Nigeria
  • 2018: Waihiga Mwaura kutoka Kenya
  • 2019: Solomon Serwanjja kutoka Uganda
  • 2020: Victoria Rubadiri kutoka Kenya
  • 2022: Dingindaba Jonah Buyoya kutoka Zambia