Ghana yapeleka askari wake kusaidia kuijenga upya Jamaica

Chanzo cha picha, Getty Images
Ghana imewapeleka wanajeshi 54 nchini Jamaica kusaidia jitihada za ujenzi upya baada ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Melissa nchini humo.
Wanajeshi hao watashiriki katika ukarabati wa barabara, makazi ya muda, na miundombinu muhimu ya umma iliyoharibiwa na kimbunga hicho.
Askari hao wanatoka katika Kikosi cha 14 cha wahandisi wa Jeshi la Ghana.
Ujumbe huu ni sehemu ya dhamira ya Ghana ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kutoa msaada wa kibinadamu, na kuonyesha mshikamano na mataifa ya Carrebian yanayoathiriwa na majanga ya asili.
Hatua hii iliungwa mkono na serikali ya Marekani, ambayo ilitoa ndege ya kijeshi ya mizigo aina ya C-17 kuwasafirisha wanajeshi wa Ghana pamoja na vifaa vyao hadi Kingston, Jamaica.
“Taifa letu linaelewa uchungu wa majanga ya asili na safari ndefu ya kupona. Dhamira ya leo inaimarisha kujitolea kwa Ghana katika kutoa msaada wa kibinadamu, kurejesha na kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa na majanga, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kusini kwa Kusini, mshikamano wa Pan-Afrika na Afro- Caribbean,” alisema Rais Mahama.
Serikali ya Ghana tayari imetuma misaada ya kibinadamu ikiwemo mchele, blanketi, magodoro, ndoo za plastiki, na dawa kwenda Jamaica, Cuba, na Sudan.
Kimbunga Melissa, ambacho ni cha kiwango cha tano, kilikumba Jamaica mwezi Oktoba ambapo takriban watu 32 walipoteza maisha huku maelfu wakihitaji msaada wa chakula na huduma za msingi.
Jamaica ipo katika eneo linalokumbwa mara kwa mara na vimbunga, na kwa miaka mingi imeathiriwa na dhoruba kali zilizoharibu makazi, hospitali, na miundombinu muhimu.
Soma zaidi:













