Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Ghadhabu baada IEBC kusitisha uchaguzi wa ugavana Mombasa na Kakamega
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Vyama vya kisiasa nchini Kenya vimepinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kusitisha uchaguzi katika viti vinne vya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa Jumanne.
Miungano miwili mikuu ya Azimio One Kenya na United Democratic Alliance-chama tanzu cha Muungano wa Kenya Kwanza imeelezea kusikitishwa na uamuzi huo ikidai kuna hila na ufisadi katika mpango huo mzima.
Maafisa wa chama wanahofia hitilafu hiyo inaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.
Mamlaka ya uchaguzi ilisimamisha uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Mombasa na Kakamega baada ya karatasi za kura kubainika kuwa na makosa- maelezo na picha za wagombea hazikuwa sahihi.
Wapiga kura katika maeneo bunge mengine mawili ya Pokot Kusini na Kacheliba hawatampigia kura mbunge wao.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Katibu Mkuu wa Muungano wa Azimio One Kenya Junet Mohamed ameelezea kusikitishwa na hatua hiyo akidai kuna mpango fiche kwani maeneo yaliyoathiriwa wanayazingatia kama ngome yao.
''Sisi hatujafurahishwa na hatua ya kamati ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi wa ugavana katika kaunti ya Mombasa na Kakamega. Tunaona kama kuna mpango fiche ambayo bado tunachunguza kwa nini ni hizo kaunti mbili ambayo ni ngome ya Azimio peke yake uchaguzi umeahirishwa na sio kaunti zingine'', alisema Bw Junet
Kwa upande wake mgombea wa ugavana wa United Democratic Alliance (UDA), Hassan Omar alisema yeye na mgombea mwenza wake waligutushwa na taarifa za kuahirisha uchaguzi wa ugavana wa Mombasa.
''Naona kuna njama mbaya katika uahirishaji huu uliyokusudiwa'',alisema Bw Hassan akiongeza kuwa timu yake inajadiliana na mamlaka ya chama na kwamba kauli rasmi itatolewa kuhusiana na suala hilo.
Hata hivyo pande zote mbili zimewaomba wafuasi wao kujitokeza kwa wingi na kuwampigia kura wagombeaji wanaowania nyadhifa nyingine tano za uchaguzi.
IEBC imetetea uamuzi wake ikisema dosari hiyo haikutokana na wao ikiongeza kuwa kampuni iliyopewa kandarasi ya kuchapisha makaratasi ya kupiga kura ndio ilichanganya makaratasi hayo.
Tume hiyo aidha imesema kuwa imeanza uchapishaji wa karatasi za kupigia kura na hivi karibuni watatangaza tarehe za chaguzi katika maeneo hayo.
Upigaji kura kwa nyadhifa nyingine tano za kuchaguliwa ambazo ni Urais, Seneta, Mbunge, Mwakilishi wa Wanawake na Mbunge wa Kaunti utaendelea kama ilivyopangwa.
Awali tume hiyo iliwafuta kazi wafanyikazi saba wa uchaguzi baada ya kupatikana nyumbani kwa mgombeaji kwa kile kinachoaminika kuwa mpango wa kushawishi matokeo ya uchaguzi huo.
Maandalizi ya uchaguzi wa Jumanne yamekumbwa na hofu ya wizi wa kura huku wanasiasa kutoka pande zote wakidai kulikuwa na mipango ya kushawishi matokeo ya uchaguzi huu.
Huku hayo yakiarifiwa Tume ya IEBC imesema sasa itategemea vifaa vya elektroniki kuwatambua wapiga kura ili kutii uamuzi wa mahakama ya Rufaa ambao umebatilisha uamuzi wa mahakama kuu uliokuwa umeitaka IEBC kutumia sajili ya daftari kuwatambua wapiga kura.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema hawana budi ila kufuta maagizo ya mahakama ya Rufaa .
Chama cha UDA kilikuwa kimewasilisha pingamizi kortini dhidi ya uamuzi wa hapo awali wa mahakama Kuu kuhusu matumizi ya sajili ya daftari.
Jopo la majaji watatu lilisema kuwa tume ya uchaguzi itatumia maelekezo katika kesi ya NASA ya mwaka 2017 ambapo mahakama iliamuru IEBC kutumia sajili iliyochapishwa ya wapiga kura pekee katika hali ambapo vifaa vya elektroniki KIEMS vinafeli kabisa bila uwezekano wa kukarabatiwa au kubadilishwa.
Uchambuzi
Dickens Olewe-BBC News, Nairobi
Taarifa ya kusimamisha upigaji kura katika maeneo manne, ikiwa ni pamoja na kinyang'anyiro cha ugavana kinachofuatiliwa kwa karibu, ni habari ambayo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi hangetaka kutangazasaa chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Kenya.
Wafula Chebukati tayari kibarua cha kuwaregeshea imani Wakenya baada ya uchaguzi wa urais aliokuwa akisimamia miaka mitano iliyopita kubatilishwa na kurudiwa tena.
Uchaguzi wa Jumanne ulikusudiwa kumkomboa, lakini kufuatia msururu wa visa vilivyoshuhudiwa Jumatatu, kazi yake ilizidi kuwa ngumu.
Katika saa chache zilizopita Bw Chebukati amelazimika kuwatimua maafisa kadhaa wa uchaguzi kwa sababu ya madai ya mikutano isiyofaa na wagombeaji, gari lililobeba vifaa vya kupigia kura lilishambuliwa na umma na vitu kuharibiwa, kifaa ambacho kilipaswa kutumiwa kuthibitisha wapiga kura na kutuma matokeo kimeripotiwa kupotea katika mkoa mwingine.
Amejaribu kuwahakikishia Wakenya kwamba tume hiyo ilikuwa tayari kuendesha uchaguzi lakini maneno hayo yanayumba.
Ikiwa matatizo ya kiusimamizi yataendelea kuongezeka katika saa chache zijazo na kuwa mbaya zaidi uchaguzi utakapofanyika Jumanne, basi tume ya uchaguzi itakuwa na mgogoro mkubwa mkononi mwake.
Kwa sasa, Wakenya wengi wanatumai kuwa matukio ya Jumatatu hayakukusudiwa na kwamba tume itakuwa na jukumu la kuendesha uchaguzi wa haki na wa kuaminika.
Pia unawezakusoma: