Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kassim Majaliwa: Waziri mkuu wa Tanzania apuuzilia mbali ghasia za Loliondo
Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amepuuzilia mbali ripoti za ghasia katika eneo la Loliondo kaskazini mwa Tanzania.
Wakazi waliambia BBC siku ya Ijumaa kwamba maafisa wa polisi huenda wamewafyatulia risasi wakaazi kutokana na mzozo wa ardhi unaondelea.
Kuna ripoti kwamba magari ya polisi pamoja na yale ya wanajeshi yamekuwa yakipiga doria katika eneo linalozozaniwa.
Wanaharakati wakisambaza picha na video mitandaoni wakidai kwamba watu kadhaa wamejeruhiwa kutokana na makabiliano kati ya maafisa wa usalama na wakaazi.
Wakaazi wa Loliondo waliojawa na ghadhabu wameapa kulinda ardhi yao kwa hali yoyote ile katika mitandao ya kijamii.
Hatahivyo waziri mkuu wa taifa hilo amepinga madai ya ghasia na kuwataka wakazi kutoka vijiji 14 pamoja na Loliondo kuwa watulivu wakisema kwamba hakuna mtu atakayeondolewa kinyume na ripoti katika mitandao ya kijamii.
Akizungumza katika bunge hii leo, Majaliwa amesema kwamba uwepo wa vikosi vya usalama katika eneo hilo ni kutokana hatua ya serikali kuweka alama katika maeneo yanayodai kuwa ya uwindaji.''
Eneo ambalo serikali inaweka alama liko mbali na makazi. Katika eneo la Loliondo, hakuna hata mtu mmoja atakayondolewa katika eneo hilo.
''Kwanza hakuna polisi ambaye alikwenda katika vijiji na kuwafyatulia risasi raia….video inayosamabaa haihusiki na polisi kamwe,'' alisema.
Majaliwa alisema kwamba video hiyo inayosambazwa ni mpango wa makundi fulani kuichafulia jina serikali ya Tanzania.
Ingawa hatua ya kuwahamisha wananchi wa jamii ya Kimasai kutoka Ngorongoro imekuwa ikikosolewa na baadhi ya wanaharati, serikali imekuwa ikisisitiza kwamba wananchi hao wanaondoka kwa hiari ili kupisha shughuli za uhifadhi kufanyika katika eneo hilo ambalo liko katika orodha ya urithi wa dunia.