Lady Mounass: Mwanamuziki wa Pop Senegal aliyetumia wimbo kueleza alivyobakwa na wanaume wawili

Chanzo cha picha, Courtesy of Lady Mounass
Kufuatia maandamano makubwa nchini Senegal kuhusu ubakaji na mauaji ya wanawake, sheria ilibadilishwa mwaka 2020 na kufanya ubakaji kuwa uhalifu mkubwa badala ya uovu tu au tabia mbaya.
Matukio hayo yalifungua mazungumzo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, aibu na uwajibikaji, yaliyoongozwa na nyota wa pop ambaye alithubutu kuimba kuhusu alichokipitia mwenyewe.
Nyumbani kwake, saa mbili kusini mwa mji mkuu wa Senegal, Dakar, nyota wa pop Lady Mounass ananiimbia wimbo katika lugha yake ya asili ya Kiwolof:
Sina nguvu ya kupigana,
Hata nguvu ya kubishana
Nilipoteza kujiamini.
Ulinisaliti
Ulichukua kile kilichokuwa kipenzi changu
Lady Mounass anajulikana kwa mashairi yake ya kuvutia na mtindo wa kuvutia, lakini wimbo huu ni tofauti sana. Inaelezea kiwewe cha kihisia alichopata baada ya kubakwa na wanaume wawili mwaka wa 2011.
''Ni vigumu sana kwangu kuimba wimbo huu bila kusindikizwa kwa sababu maneno hayo ni maelezo ya kile kilichonipata,'' asema.
''Mimi hulia ili nilale mara kwa mara. Kila siku, ninaishi na aibu inayoambatana nayo.''
Lady Mounass anasema aliripoti polisi na mmoja wa watuhumiwa alikamatwa, lakini baadaye aliachiliwa bila kufunguliwa mashtaka.
Familia yake ilimtaka anyamaze kuhusu alichokipitia, lakini wakati wa mahojiano kwenye televisheni ya Senegal mwaka jana, alifichua ukweli bila kukusudia.
''Mtangazaji aliendelea kuniuliza, ''Unaonekana kuwa na shauku fulani katika suala hili, unaonekana kuwa makini sana na mada hii.''
''Na kwa hivyo machozi yalianza kunitoka na sikuweza kuyazuia.''
Baadhi ya wakosoaji walipendekeza mtindo wake wa ''uchochezi'' ulikuwa umewapa wanaume ''hisia mbaya'', huku wengine wakidai kuwa alikuwa amefanya jambo hilo akitaka kujipatia umaarufu.
''Baadhi ya watu walijaribu kusema kwamba nilikuwa nikifanya hivyo ili kupata umaarufu - na hilo liliumiza sana hisia zangu,'' anasema Lady Mounass.
''Familia yangu ilisema, hii ndiyo sababu hasa tulikuambia usizungumze kuhusu hili hadharani.

Chanzo cha picha, Myriam Francois/BBC
Katika wiki zilizofuata, watu wengi waliwasiliana na Lady Mounass kuzungumza juu ya waliopitia wao wenyewe kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. Kulikuwa na simulizi za kuhuzunisha - mwanamke mmoja alimwambia kuwa alibakwa na babu yake.
Mwingine na baba yake, na kwamba mama yake alikataa kumuamini. Na simulizi hizo zikaendelea kumininika, Lady Mounass aliishia kuwa msemaji dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.
Alijiunga na kampeni ya serikali, kuzuru nchi ili kuhamasisha unyanyasaji wa kijinsia na usaidizi wa kisheria unaopatikana kwa wanawake. Wimbo wake ukawa wimbo wa kampeni hiyo.
Wanawake wakijadi wamekuwa wakinyanyapaliwa na kusita kuzungumza juu ya ubakaji nchini Senegal, achilia mbali ushujaa wa kutosha kutoa wimbo kuhusu hilo.
Lady Mounass aweka aibu pembeni
Lakini kwa baadhi ya wanawake, kuwa mwathirika wa unyanyasaji wa kijinsia kunamaanisha kukataliwa na familia zao na jamii.
Hiki ndicho kilichotokea kwa wasichana wawili niliokutana nao kwenye kituo cha waathiriwa wa unyanyasaji wa majumbani na kingono unaosimamiwa Senegali. Tumebadilisha majina yao.
Kiko katika kitongoji tulivu cha Dakar, kinaedeshwa na Yacine Diouf, binti wa rais wa zamani.
Tunaingia kupitia mlango mzito wa mbao, ''ili kuwazuia waume na familia zenye hasira, anasema Diouf.
Kituo hik kina uwezo wa kutoa makazi kwa wanawake 25 hadi 30 kwa wakati mmoja, pamoja na watoto wao.
Watapewa mafunzo na ujuzi wa kuwasaidia kuishi kwa kujitegemea mara tu wanapoondoka.

Chanzo cha picha, Myriam Francois/BBC
Deena ana umri wa miaka 19, lakini anaonekana mdogo zaidi. Akiwa amevalia fulana nyeupe na suruali ya jeans, anaangalia simu yake kila wakati.
Deena alibakwa akiwa na umri wa miaka 15. Ubakaji huo ulisababisha mimba na sasa yeye ni mama wa mtoto wa miaka mitatu.
''Mwanaume aliyenibaka alikamatwa na polisi,'' anasema.
''Alitoa ushahidi wa uongo. Walimwacha aende zake baada ya mwezi mmoja. Hata hivyo, alimtambua mtoto na kukubali kuchukua majukumu yake kama baba. Nilitumia hilo kuwasilisha malalamiko, lakini alikimbilia Guinea.''
''Maisha ni magumu. Nilikuwa shuleni lakini imenibidi niachane nayo. Sina jinsi, natakiwa kumhudumia mtoto wangu. Ni hali ngumu, wazazi wangu waliachana baada ya kilichotokea.''
Aliyeketi karibu na Deena ni Sarah, pia 19. Mwaka jana Sarah alibakwa na sasa ni mjamzito.
Hakwenda kwa polisi au kumwambia mtu yeyote kuhusu kile kilichotokea.
Ubakaji huo uligunduliwa tu wakati ujauzito wake ulipoanza kuonekana - kisha familia yake ikamfukuza.
Alifikishwa kwenye kituo baada ya kuokotwa mtaanina wafanyakazi wa kituo.
''Katika tamaduni zake, kuna aibu nyingi inayohusishwa na kubakwa, kwa hivyo familia yake ya mama na baba walimkataa,'' aeleza mfanyakazi wa wakimbizi anayemtunza Sarah.
Nchini Senegal, dhana ya ''sutura'' - busara - inaweza kushinikiza waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia kukaa kimya, anasema Fatou Warkha, ambaye anaendesha chaneli ya YouTube inayokuza haki za wanawake.
"Sutura maana yake ni kwamba wanawake wanaona ni lazima wafiche mambo haya, hivyo hiki kimekuwa kikwazo kikubwa katika kubadili namna wanawake wanavyolizungumzia suala la ubakaji pindi linapotokea," anasema.
Warkha ni sehemu ya kundi la watetezi wa haki za wanawake ambao walioamua kuja na mkakati unaoitwa Dafadoy Collective, ambayo ina maana ''inatosha''.
Mnamo mwaka wa 2019, wanaharakati walianza kutumia hashtag ya #Dafadoy na wakapanga mikutano kupinga unyanyasaji wa kingono.
Mwaka huo, mfululizo wa mashambulizi ya kijinsia dhidi ya wanawake yalisababisha maandamano makubwa. Tukio maarufu zaidi ilikuwa kisa cha Bineta Camara, 23, ambaye alinyongwa baada ya muuaji wake kujaribu kumbaka.
Kesi yake ilisababisha hasira, sio tu kati ya wanaharakati wa wanawake, lakini katika sehemu kubwa ya jamii.
El Hadji Elias Ndoye, alikuwa mmoja wa watu 3,000 waliojiunga na maandamano katika Place de la Nation huko Dakar.
"Kutokana na mfumo dume wa jamii ya hapa, uwepo wa wanaume katika maandamano haya ni muhimu," anasema Ndoye.
''Baadhi ya watu wananituhumu kuwa chini ya mwanamke, lakini ukweli ni kwamba ni wakati wa sauti za wanawake kusikika. Wanaume wengi walio kimya wako pamoja nasi kwa sababu ni mabinti zao, dada zao, wanafamilia ambao wako katika mazingira magumu.''

Chanzo cha picha, Myriam Francois/BBC
Mwingine aliyeandamana alikuwa Mamadou Maktar Gaye, mkuu wa Jamra - moja ya mashirika ya Kiislamu yenye ushawishi mkubwa nchini humo.
Yeye na Jamra walisimama pamoja na ''wanawake'' kupinga kile ambacho Gaye anakitaja kama ''janga la ubakaji''.
''Inahusu wanaume kubadili tabia zao,'' anasema.
Maandamano hayo yalilazimisha mabadiliko ya sheria ambayo wanaharakati kama Warkha walikuwa wakifanya kampeni kwa muda mrefu.
Baada ya kura ya kauli moja bungeni, Rais Macky Sall alifanya rasmi ubakaji kuwa uhalifu tarehe 10 Januari 2020. Kesi za ubakaji sasa zinasikilizwa katika mahakama ya jinai na kifungo cha miaka 10 hadi maisha, wakati hapo awali zingehukumiwa katika mahakama ya hakimu na kifungo cha juu cha miaka 10.
Ubakaji kwa mara ya kwanza ulianza kuadhibiwa na sheria nchini Senegal mwaka 1999, wakati ulipotajwa kama kosa.
Miongo miwili baadaye, mnamo mwaka 2019, kulikuwa na ripoti rasmi 1,026 za unyanyasaji wa kijinsia, ambapo nusu yao iliaminika kuhusisha ubakaji. Lakini idadi sahihi ni ngumu kupata.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Wanawake, Familia na Watu Walio Katika Mazingira Hatarishi aliiambia BBC hawakuwa na takwimu zinazohusiana na ni wanawake wangapi walioathirika - na kwamba kwa vyovyote vile, takwimu zilizoripotiwa kuhusu ubakaji zinapuuza ukubwa wa tatizo.
Hatua sasa zinachukuliwa ili kuwafanya wanawake kujisikia vizuri zaidi wanaporipoti unyanyasaji wa kijinsia kwa polisi. Vituo vya polisi vinaundwa upya ili wanawake wakutane kwenye mapokezi na kupelekwa kwenye chumba tofauti, ambapo wanaweza kuzungumza na afisa wa kike.
Mabadiliko haya ni sehemu ya mradi unaofadhiliwa na EU na kuongozwa na afisa mkuu wa polisi, Commissaire Binetou Guisse, ambaye kazi yake ni kufuatilia unyanyasaji wa kijinsia nchini kote.

Chanzo cha picha, Myriam Francois/BBC
Polisi pia hufanya kazi kwa karibu na wanawake kutoka jamii ya eneo ambao hufanya kama wasuluhishi muhimu.Wanajulikana kama ''badianu goch'' - neno linalomaanisha shangazi wa baba, mtu muhimu katika familia za Senegal.
Serikali sasa inatoa mafunzo kwa badianu goch kusaidia kuwalinda wanawake na watoto walio katika mazingira magumu.
"Wanawake hawa ndio huwa wanajua kinachoendelea na watalifikisha suala hilo polisi," anasema Guisse.
''Kuna wanaume wengi kwa sasa wanafunguliwa mashitaka lakini hadi sasa, hakuna hata mwanamume mmoja ambaye amehukumiwa - kwa sababu kwa sababu utaratibu huo mpya ni wa muda mrefu na unahitaji uchunguzi wa kina,'' anasema Aby Diallo, rais wa AJS na afisa mkuu wa zamani wa polisi.
Kwa hivyo mchakato huu mrefu wa kisheria unaweza kuwa na tija?
Diallo hafikiri hivyo.
''Ni sheria nzuri, lakini inahitaji matumizi bora zaidi, inahitaji mahakimu zaidi na inahitaji uelewa zaidi katika jamii ya eneo hilo kuhusu jinsi sheria mpya inavyofanya kazi.''
Anaelezea kuwa chini ya sheria ya zamani, wabakaji wengi walikuwa wakitoka gerezani baada ya miezi michache tu, na hii ilikuwa na athari mbaya kwa waathiriwa.
''Mwishowe, ni hukumu ngumu ambazo zinaweza kurudisha nyuma uzito wa vitendo hivi,'' anasema Diallo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini kukiwa hakuna hata hukumu moja ambayo imetolewa, ni wazi kuwa wahasiriwa wengi wa unyanyasaji wa kingono bado wanasubiri haki.
Lady Mounass anatumai wimbo ambao ameandika kuhusu masaibu yake utasaidia wanawake wengine kuzungumza.
''Nina jukwaa kama mwimbaji na ninahisi hisia ya kuwajibika. Nilihisi kwamba nilipaswa kusema kitu kuhusu hili,'' anasema.
''Ninatoa wito kwa wanaume haswa kukomesha tamaduni kuhusu ubakaji na kuacha kuifanya kuwa kitu ambacho wanawake wanahisi wanapaswa kunyamaza.''














