Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unaujua uzuri wa kumuoa mkeo zaidi ya mara moja?
- Author, Yusuph Mazimu
- Nafasi, BBC Swahili
Ndoa ni jambo la kiibada kwa wanaoamini dini, na jambo la heshima kwenye jamii linalowagusa watu wa aina zote, matajiri na masikini.
Utamaduni wa kuoa mke zaidi ya mmoja kwa watu wenye Imani ya kiislamu ni jambo linalokubalika, lakini kitamaduni zipo jamii hasa za kichifu ambazo utamaduni wa kuwa na mke zaidi ya mmoja ni jambo linalokubalika.
Mfalme wa Eswatini amefikisha wake 11, wakiwemo wawili waliochaguliwa na viongozi wa baraza la taifa madiwani.
Haya si mageni sana kwa jamii hasa ya kiafrika. Lakini kwa sasa suala la mtu kumuoa mkewe zaidi ya mara mmoja ni jambo linaloanza kushamiri.
Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya wanasheria ya Arizona Family Law Lawyers ya Marekani, asilimia 6% ya wanandoa wanaotalakiana wanarejeana na kuoana tena.
Hata hivyo utafiti kutoka Pew Research Center inaonyesha watu wenye umri kati ya miaka 35 na 44 na 45 na 54 hawarudii kuingia kwenye ndoa mara baada ya kutengana na wenza wao.
Lakini asilimia ya wanaorudiana ama kurejea katika ndoa na wenzao wa awali imeongezeka kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 55 kutoka asilimia 55% mpaka 67%.
Kwanini umuoe mkeo zaidi ya mara moja?
Kuanzisha uhusiano mpya, sio jambo rahisi, hasa baada ya kutoka kwenye ndoa, ambayo ilikumbwa na misukosuko na kupelekea kuachana na mwenza wako.
Kumrejea mwenza wako uliyetengana naye haikuhitaji muda kwa sababu unamjua, umemzoea na pengine 'unammudu' kwa tabia, mwenendo na masuala mengine muhimu katika maisha ya ndoa.
'Wengi wanapata tabu kuanzisha uhusiano mpya, yale mazoea ya zamani ya wenza wao wa awali yanarejesha kumbukumbu muhimu zinazorahisisha kurejesha mahusiano na ndoa', anasema Mtaalama wa masuala ya maendeleo ya kijamii, Raphael Kugesha, Mtaalam wa maendeleo ya jamii.
Wanandoa wenye watoto, wanatajwa kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kurejeana baada a kuachana kuliko wale ambao hawajafanikiwa kupata watoto. Mariam John, wa Tabora, ambaye aliachana na mumewe kwa mwaka mmoja baada ya kukaa naye kwa zaidi ya miaka 10 wakipata watoto wawili wa kike, anasema haikuwa kazi rahisi kuanza upya.
'Mwenzangu aliposema tumejikwaa, turejee pamoja kulea watoto, lilikua jambo rahisi kuamua, tukafunga tena ndoa, na sasa tuna miaka zaidi ya 20 ya ndoa', alisema.
Je kumrejea na kufunga naye ndoa ya pili mwenza wako kuna faida yoyote?
Hakuna jawabu la moja kwa moja, kutokana na tafiti chache zilizofanyika kwenye suala hili.
Lakini BBC imemuuliza Mariam John, kama kumrejea mumewe na kukubali kuolewa tena ni jambo zuri.
"Inategemea, ila kwangu ni jambo zuri nilisolijutia', anasema Mariam na kuongeza "uzuri na faida ni kwamba unamjua mwenzio, mlipendana, na waliopendana kufufua penzi ni kitu rahisi, mlipojikwaa mnapajua, kukwepa mizozo ni rahisi kuliko ndoa mpya na mtu mpya', alisema.
Mifano michache ya wanandoa maarufu walioana zaidi ya mara moja
Elon Musk
Bilionea Elon Musk, mmoja wa matajiri wakubwa duniani, ambaye hivi karibuni alitangaza kuununua mtandao wa twitter kwa dola $44 billion. Tajiri huyu mwenye utajiri wa zaidi ya $200 billion amefunga ndoa mara kadhaa.
Ndoa ya kwanza ya Musk na mkewe Justin Wilson ilikuwa mwaka 2000 na kutalakiana mwaka 2008.
Mwaka 2010 akamuoa mkewe Tulah Rylie lakini ndani ya miaka miwili wakatalakiana.
Mwaka 2013 wawili hao wakarejeana na kuoana tena Musk akatangaza kumpa talaka mwaka 2014 kabla ya kufuta uamuzi huo.
Mwaka 2016 Rylie na yeye akatangaza talaka na kutengana. Wanandoa hao wana watoto watano.
Larry King
Nguli wa habari Larry King kwa mara ya kwanza alifunga ndoa na Alene Akins iliyodumu kati ya mwaka 1961-1963, na baadae wakafunga tena mwaka 1967-1972.
King ameoa kwa ujumla mara 8, ambapo ndoa zake nyingi zilidumu chini ya miaka 10.
Eminen
Marshall Mathers maarufu kama Eminen alifunga ndoa na mkewe kwa mara ya kwanza na Kim Scott, waliodumu kutoka mwaka 1999-2001. Wakatengana kabla ya kuoana tena na kutalakiana tena mwaka 2006.
Pamela Anderson
Muigizaji huu alioana tena na mumewe, Rick Salomon, mwaka 2014 lakini mwaka jhuo huo akaomba talaka, kabla ya baadae kumuomba jaji afute ombi lake la talaka.
Februari 2015, akaomba talaka kwa mara ya tatu.
Wanandoa hawa awali walioana mwaka 2007 mpaka 2008.
Lakini wanandoa hawa waliingia katika ndoa na watu wengine pia.
Anderson aliolewa na Tommy Lee (1995-1998) na Kid Rock (2006-2007). Salomon awali alifunga ndoa na Shannen Doherty (2002-2003) na E.G. Daily (1995-2000).