Mauaji ya Thomas Sankara:Rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaoré apatwa na hatia

Rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaoré amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa wajibu wake katika mauaji ya mtangulizi wake Thomas Sankara.

Sankara, 37, aliuawa kwa kupigwa risasi pamoja na wengine 12 wakati wa mapinduzi ya 1987 ambayo yalimleta Compaoré madarakani.

Wawili hao walikuwa marafiki wa karibu na walikuwa wametwaa mamlaka kwa pamoja mwaka wa 1983.

Sankara anasalia kuwa shujaa kwa wengi barani Afrika kwa sababu ya msimamo wake wa kupinga ubeberu na maisha ya ukatili.

Baada ya kutwaa madaraka akiwa na umri wa miaka 33 tu, mwanamapinduzi huyo wa Ki-Marx anayejulikana na baadhi ya watu kama "Che Guevara wa Afrika", alifanya kampeni dhidi ya rushwa na kusimamia ongezeko kubwa la ka uimarishaji wa elimu na afya.

Upande wa mashtaka ulisema Sankara alihadaiwa kwenda sehemu alikouawa katika mkutano wa Baraza la Mapinduzi la Taifa.

Alipigwa risasi kifuani angalau mara saba, kulingana na wataalam wa balestiki ambao walitoa ushahidi wakati wa kesi hiyo.

Mwandishi wa BBC Afrika Magharibi Lalla Sy anasema uamuzi huo ulipokelewa na vifijo katika chumba cha mahakama kufuatia kesi ya miezi sita iliyokuja baada ya miaka mingi ya kampeni ya haki na familia yake na wafuasi wake.

Unaweza pia kusoma

Mjane wa Sankara, Mariam Sankara, ambaye alihudhuria kesi hiyo kwa muda wote, alisema uamuzi huo uliwakilisha "haki na ukweli" baada ya kusubiri kwa miaka 35.

"Lengo letu lilikuwa ni ghasia za kisiasa tulizo nazo nchini Burkina Faso kumalizika. Uamuzi huu utawapa watu wengi sababu ya kufikiri."

Hata hivyo, kuna uwezekano mdogo kwamba Compaoré atatumikia kifungo chake hivi karibuni.

Ameishi uhamishoni nchini Ivory Coast tangu alipoondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa mwaka 2014, na amechukua uraia wa Ivory Coast.

Hapo awali alikashifu kesi hiyo na mahakama ya kijeshi na kusema ni udanganyifu wa kisiasa.

Wengine kumi pia walipatikana na hatia, akiwemo mkuu wa usalama wa Compaoré Haycinthe Kafando, ambaye alishutumiwa kuongoza kikosi kilichomuua Sankara.

Amekuwa akikimbia kwa miaka kadhaa na pia alihukumiwa bila kuwepo. Yeye pia alipata kifungo cha maisha.

Wote wawili walikuwa wamekanusha mashtaka.

Gilbert Diendéré, mmoja wa makamanda wa jeshi wakati wa mapinduzi ya 1987 na mshtakiwa mkuu ambaye kweli alikuwepo kwenye kesi hiyo, pia alihukumiwa kifungo cha maisha. Tayari anatumikia kifungo cha miaka 20 kwa jaribio la mapinduzi mwaka 2015.

Wakili wake alieleza hukumu hiyo kuwa ni ya kali kupindukia, akisema alipaswa kupewa nafasi ya kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo, tofauti na wale waliohukumiwa bila kuwepo mahakamani.

Washtakiwa wengine wanane walipata vifungo vya kati ya miaka mitatu hadi 20, huku washtakiwa watatu wakiachiwa huru.

Akiwa madarakani, Sankara alibadilisha jina la nchi yake kutoka, Upper Volta, hadi Burkina Faso, ikimaanisha Nchi ya Watu Waaminifu.

Alipunguza mshahara wake mwenyewe, na wa watumishi wa juu wa serikali, na akauza aina mbalimbali za magari ya kifahari.

Katika kipindi cha miaka minne madarakani, alikuza uafrika, kujitegema , uhuru wa kweli kutoka kwa nchi iliyowafanyia ukoloni ya Ufaransa na usawa wa kijinsia, kwa kupiga marufuku tohara ya wanawake .

Hata hivyo, wakosoaji wake wanataja madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wapinzani wake.

Wanaharakati katika mataifa kadhaa ya Afrika bado wanampongeza, wakisema wanataka kuendeleza urithi wake.

Mnamo 2019, sanamu yake ya mita sita (16ft) ilisimamishwa katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou.