Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wafahamu watu wengine maarufu waliowahi kuzabwa vibao hadharani
Mwishoni mwa wiki, muigizaji mkongwe na mshindi wa tuzo kibao za Uigizaji, Will Smith alimzaba kibao hadharani kwenye jukwaa la tuzo za Oscars, mchekeshaji, Chris Rock baada ya mchekeshaji huyo kutania kuhusu nywele za mke wa Smith, Jada Pinkett-Smith.
Lilikuwa tukio la kushtusha na kushangaza umma uliokuwa unafuatilia tuzo hizo zinazotajwa kuwa maarufu zaidi katika Sanaa ya uigizaji duniani.
Smith aliomba radhi kwa tukio hilo muda mfupi baadae katika jukwaa hilo hilo. Akiwaomba radhi waandaaji wa tuzo na wasanii wenzie waliokuwa wakiwania tuzo hizo, na baadaye nje ya jukwaa hilo akamuomba radhi Rock.
Awali lilionekana kama tukio lililopangwa, kwa sababu ya kuonekana Smith akicheka alichokuwa akisema Rock jukwaani. Lakini punde akainuka na kwenda kumzaba kibao na aliporejea kwenye kiti chake, alisikika akisema: "Jada, anasubiri kwa hamu GI Jane 2."
Utani wake kuhusu Jada na nywele zake ulikuwa ukirejea filamu ya mwaka 1997, GI Jane, ambayo Demi Moore alicheza nafasi ya mtu mwenye nywele fupi sana (karibu na kipara).
Matukio kama hayo yakushangaza na wakati mwingine kufedhehesha yamekuwa yakitokea yakiwahusisha watu maarufu wakiwemo wasanii, viongozi na wacheza mpira kuzabana vibao wenyewe kwa wenyewe ama kuzabwa vibao na mashabiki wao ama watu wa kawaida. Haya ni machache yaliyowahi kushika vichwa vya habari duniani
Salman Khan v Subhash Ghai
Kwa wafuatiliaji wa filamu za kihindi haya ni miongoni mwa majina maarufu kabisa huko Bollywood. Kama ilivyo kwa tukio la Smith, inaelezwa Subhas Ghai alisema kitu kuhusu mpenzi wa zamani wa Salman Khan, aliyeitwa Aishwarya Rai.
Hilo halikumpendeza Khan aliyemchapa kibao hadharani Ghai wakiwa mbele za watu. Hata hivyo inaelezwa Ghai alikuwa amelewa kiasi. Baadaye Salman Khan alimuomba radhi.
Salman Khan anatwaja kuwa ni mtu mwenye hasira za karibu. Mtandao wa India today uliwahi kuripoti matukio yake likiwemo la mwaka 206 la kumzaba kibao hadharani msanii mwenzake Ranbir Kapoor.
Pep Guardiola v Thiago Alcantara
Baada ya kuruhusu mabao mawili ya haraka ndani ya dakika mbili na kuifanya timu ya Bayern Munich kuwa numa kwa mabao 3-2, akili na presha a kupoteza mchezo wake wa kwanza kama kocha wa Bayern ikamuingia Pep Guardiola.
Katika mazungumzo yake ya ukali ilionekana kama kumtupia lawama, mhispania mwenzake aliyekuwa anacheza mchezo wake wa kwanza Bayern Thiago Alcantara, kabla ya kumzaba kofi usoni.
Ilikuwa dakika ya 76 ya mchezo huo wa kombe la Super Cup Ujerumani mwaka 2013 ambapo Bayern ililala kwa mabao 4-2 dhidi Borussia Dortmund iliyokuwa inanolewa na Jurgen Klopp, kocha wa sasa wa Liverpool.
Zlatan Ibrahimovic v Petrasso
Kwa wafuatiliaji wa soka hakuna asiemjua , Zlatan Ibrahimovic, mshambuliaji mkongwe wa AC Milan na Sweden ambaye amechezea katika ligi nne kubwa Ulaya, League 1 (Ufaransa) akichezea PSG, Laliga (Hispania), akiichezea Barcelona, EPL (England) alivaa uzi wa Manchester United, Seria A (Italia) anakocheza sasa akiwa na AC Milan, alichezea pia Inter Milan na Juventus.
Amecheza pia Ajax ya Uholanzi kwa mafanikio makubwa. Ni mtata akiwa uwanjani, na mara nyingi anaonekana kama mbabe wakati wote kwa wapinzani wake.
Lakini akicheza mchezo wa ligi kuu ya Marekani (MLS) mwaka 2018 kati ya timu yake ya Los Angeles Galaxy dhidi ya Montreal, Zlatan Ibrahimovic alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumzaba kibao Michael Petrasso katika dakika ya 41.
Petrasso alimkanyaga kwa bahati mbaya Zlatan wakati akirudi nyuma. Mkongwe huyo alishikwa na hasira na akaamua kumzaba kibao cha shingo.
Di Canio v Inzaghi
Mshambuliaji wa zamani wa West Ham na Itali Paolo Di Canio aliwahi kumzaba kibao mchezaji mwenzie wa wa Lazio, Simone Inzaghi. Ilikuwa tukio lakushangaza la Septemba 4, 2004 ambapo ndio kwanza Di Canio alikuwa amejiunga na Lazio na alikuwa akicheza mchezo wake wa kwanza katika ardhi ya Italia baada ya muiaka minane ya kucheza England.
Bahati nzuri Lazio ilipata penati ambayo Simone Inzaghi (ambaye kwa sasa ni kocha wa Inter Milan na kaka wa gwiji wa zamani wa soka Filipo Inzaghi) alitaka kupiga kabla ya Di Canio kufika na kutaka kupiga yeye.
Washambuliaji hao waliingia kwenye mzozo wa kugombea kupiga penati hiyo, ulioishia kwa Di Cania kumzaba kofi Inzaghi.
Di Canio alifunga penati katika mchezo huo uliomalizika kwa ushindi wa bao hilo pekee la penati. Ingawa baada ya mchezo Inzaghi alimwita Di Canio kama mtu mninafsi. Di Canio katika moja ya mahojiano aliyowahi kuyafanya miaka miwili baade alisema: "Hilo la Inzaghi, ilikuwa mechi yangu ya kwanza baada ya miaka 16 nje ya Lazio, imu yangu, matokeo yakiwa 0-0 tunapata penati - unahitaji kuwa na akili ya ukubwa wa karanga kufikiri kwamba nisingeweza kupiga penati ile".
Hayo ni machache yapo mengi mfano la Disemba mwaka 2014, Raheem Sterling wakati huo akiichezea Liverpool aliwahi kumchapa kofi mlinzi wa Swansea, muargentina Federico Fernandez.
Nyota wa zamani wa Arsenal, Gervinho alizihakiwa na Joey Barton wa Newcastle United, kwa sababu ya kujiangusha angusha uwanjani na kusababisha moja ya penati 'laini' katika mchezo wa ligi kuu England baina ya timu hizo mwaka 2011. Gervinho alikasirika na kuamua kumzaba kibao Barton kabla ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu.