Madhila wanayopitia wanaume wanaobakwa vitani

Chanzo cha picha, Getty Images
Onyo: Makala haya yana maelezo ya kusikitisha.
Ukraine na Urusi vita inaendelea kwa wiki ya nne sasa, mbali na athari zinazoonekana za vifo na majeruhi, zipo nyingine za unyanyasaji wa kingono kwa wanawake na wanaume ambazo, wanaharakati na watafiti wanataka zitazamwe sio kwa vita hiyo tu, bali hata vita na migogoro mingine inayohusisha silaha duniani.
"Ubakaji kwa wanaume unatokea, kwa namna fulani, katika kila vita duniani kote," anasema mwanasayansi wa kijamii Thomas Osorio.
Osorio ni mtafiti wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa (UN) na anasema kwamba wanaume na wanawake ni waathirika wa uhalifu wa kijinsia katika vita.
Ingawa ni kitendo cha kutisha, kwa muktadha huu wa vita kinaonekana ni kitendo cha kawaida na kinahusisha nchi zote zenye mifumo yote ya utawala ikiwemo za kidemokrasia," anasema.
Hata hivyo, Osorio anasema suala hilo bado linaonekana kama mwiko, kuanzia kwa wasomi na katika mifumo inayoshughulikia mizozo, kama vile Umoja wa Mataifa na Mahakama za kivita.
Kuna kusita kuukubali ukweli, lakini ni muhimu sio tu kutambua kwamba unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume upo, lakini pia kutaja wapi uwepo wa tatizo kama hilo, mtafiti huyo anasema, kwa sababu kupuuza tatizo hilo ni kumaanisha ni kuwapuuza waathirika na kuruhusu ukatili huo dhidi ya wanaume kuendelea.
Osorio alifahamu uwepo wa suala hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1993, wakati wa utafiti wake kuhusu mzozo wa silaha katika Yugoslavia ya zamani. Tangu wakati huo, amewahoji waathirika kadhaa wa kiume wa vita vya Balkan.
"Mara baada ya wafungwa wa kivita kuchukuliwa, hapo ndipo ukatili huanza na kuendelea mpaka ubakaji au aina nyingine nyingi za mateso ya kimwili na kisaikolojia kwa kutumia ngono kama silaha, iwe kwa njia ya udhalilishaji, kuchapwa kwenye sehemu za siri, kuingiziwa vitu, kulazimishwa ngono na hata kuhasiwa," anaelezea Osorio, ambaye katika utafiti wake kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika migogoro anashirikiana na Chuo Kikuu cha Leuven, Ubelgiji.
"Ni kana kwamba walinzi katika kambi za magereza wanachoshwa na upweke na kuwa wakali zaidi na zaidi, hadi wafikie hali ya kupotoka."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtafiti Janine Natalya Clark kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham anasema unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanaume ni silaha inayotumika katika vita (migogoro) kwa sababu humtikisa adui kwa kushambulia utu na msingi wa uanaume wao.
Katika vita vyote lengo la kumdhalilisha mwanaume , kumwadhibu mpinzani, ni kupata taarifa za upande wa pili kupitia mateso ili kudhibiti maeneo na rasilimali.
Katika vita, hakuna nchi "takatifu"
Osorio anasema wengi wa wanyanyasaji huko Bosnia Herzegovina na Croatia walikuwa polisi waliokuwa kazini au wa akiba, ambao baadaye walikuwa askari na kuwaona wafungwa wa kivita kama wasaliti kwa nchi yao.
Utafiti wao unaonesha kuwa, wakati wa vita katika Yugoslavia ya zamani, zaidi ya asilimia 50% ya wafungwa walipata mateso ya kijinsia, ikiwa ni pamoja na 80% ya wanaume katika kambi za magereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa mtafiti Valorie K. Vojdik wa Chuo Kikuu cha Tennessee nchini Marekani, Mashariki mwa Congo, 20.3% ya wanaume waliripoti kufanywa watumwa wa ngono na maadui zao wakati wa vita vilivyoikumba nchi hiyo kati ya mwaka 1998 na 2003.
Huko Iraq, kwa mfano, wapiganaji waliokuwa wakishikiliwa katika gereza la Abu Ghraib walilazimika kuwekwa karibu na mbwa wakiwa uchi na vichwa vyao vikiwa vimefunikwa.
Kwa mujibu wa Vojdik, katika gereza la Abu Ghraib, wanajeshi wa Marekani waliwanyanyasa wafungwa na kuwalazimisha kucheza uchi na kujichua mbele ya wenzao, wakiwapiga picha wakiwa katika mikao isiyo ya kistaarabu.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ya mwaka 2017 lilibaini kwamba kati ya asilimia 19.5 na 27 ya wanaume katika eneo la Kurdistan, Jordan na Lebanon walisema wamepitia unyanyasaji wa kingono.
Hiyo ni mbali na ripoti za wakimbizi wa vita ambao kwa sasa wako katika makambi mbalimbali ambao pia baadhi walikabiliana na hili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kijana mmoja, ambaye alitekwa nyara na kuwekwa kizuizini katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sri Lanka (1983-2009), alimwambia mtafiti Heleen Touquet, profesa katika Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji, jinsi alivyobakwa na wanaume kadhaa kwa wakati mmoja.
Alidai kuwa alilazimishwa kufanya ngono ya mdomo mara kwa mara na alibakwa kwa kuingizwa katika sehemu zake za siri kipande cha mbao.
Tourquet aliwahoji wanaume kadhaa ambao walikuwa waathirika wa unyanyasaji wa kingono nchini Sri Lanka na nchi nyingine kutokana na vita hivyo. Hitimisho la utafiti wake lilichapishwa mnamo Septemba mwaka 2018.
Athari mbaya
Osorio hasahau taarifa za kutisha alizosikia. Anaeleza tukio la mtu aliyekamatwa wakati wa mgogoro wa Bosnia ambaye alilazimishwa kufanya mapenzi na mtoto wake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahangahiko na mfadhaiko ulikuwa mkubwa kiasi kwamba hawakuonana tena na kijana huyo akawa mkimbizi. Hakukuwa na uwezekano wa kuwasiliana, hata kilipokaribia kifo cha baba, miaka mingi baadaye.
"Kamwe usipuuze uharibifu mkubwa wa aina hii ya uovu unaoweza kufanywa kwa familia. Baba na mtoto wanaweza kunusurika vitani, lakini hawawezi kamwe kuishinda aibu ya aina hii", alisema.
Matokeo ya kisaikolojia ni pamoja na kupoteza uwezo wa kingono, utasa, wasiwasi, na unyonge. Kingine ni kudhalilika kwa mwathirika, mambo ambayo yanaendelea kusababisha unyanyapaa.
"Katika utafiti wangu, niliwasiliana na mmoja wa waatu nilitaka kuwahoji miaka 30 iliyopita ili kujua jinsi alivyoshughulikia suala hilo wakati huo. Tulikutana mahali, lakini hakuweza kuingia na kuzungumza nami. Sitasahau kamwe kumwona akitembea karibu na lile eneo bila ujasiri."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa mtafiti Janine Natalya Clark, ripoti ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2007 inalenga tu kwa waathirika.
"Na ukweli ni kwamba (wanaume) hawaonekani hata katika dawa. Matibabu kama yapo, hayawi ya ufanisi, kwa sababu yamejielekeza zaidi kwa wanawake,", anafafanua Osorio.
Clark anasema kuwa kutambua kuwa kuna waathirika wa ubakaji wa kiume itakuwa muhimu, pamoja na hilo la kutambua tatizo, pia ni muhimu kukuza uwajibikaji na kuleta mabadiliko.
Osorio anasema, kwa kuwa kuumaliza uhalifu huo (kubakwa kwa wanaume), waathirika hawawezi kunyamazishwa. "Suluhisho ni kuzungumza juu ya maumivu," anahitimisha.












