Boda-Boda: Tishio la kudumu la teksi za pikipiki,boda boda nchini Kenya

Katika mfululizo wetu wa barua kutoka kwa waandishi wa Kiafrika, mtangazaji wa Kenya Waihiga Mwaura anaangazia ghadhabu ya hivi punde inayoelekezwa kwa waendeshaji wa pikipiki na anauliza kwa nini inaonekana kuwa ni vigumu kuwachukulia hatua.

Mtu yeyote anayeendesha gari katika jiji kuu la Kenya anajua anapaswa kuwa makini na pikipiki - zinzojulikana kama boda-boda.

Kwanza unaweza kusikia sauti ya injini ikibadilika dereva anapoongeza kasi, kisha labda unaona kitu kwenye kioo - mng'ao unaojulikana wa koti la hi-viz au kofia ya chuma ya manjano inayong'aa. Na kisha ghafla wanakuzunguka - karibu na kando ya gari lako, wakiruka mbele, wakivuka njia yako.

Wakikugongea gari lako wanatoroka hata kabla uzungumze nao - na hata wakiamua kusimama huenda majibizano makali yakatokea.

Inasemekana mzozo kufuatia ajali na mashambulio yaliyofanywa dhidi ya dereva wa gari wa kike yalichangia ghadhabu ya umma kulaani vitendo vya waendeshaji boda-boda.

Video ya tukio hilo iliyosambaa kwa kasi mitandaoni inaomuonyesha mwanamka akilipiga mayowe kuomba msaada wakati akivuliwa nguo na kushikwa mwili visivyo.

Washukuiwa kadhaa wamekamatwa na miito imekuwa ikitolewa kudhibiti sekta ya boda-boda.

Ili kudhibiti uchukuzi huo maswali mawili yanajitokeza. Kwanza katika kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na pili katika dhamira ya serikali ya kuhukua hatua kuhusu pikipiki hizo.

Ikizingatiwa kwamba shambulio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ilikuwa ukumbusho kwamba wanawake bado hawajihisi kuwa salama katika jiji hili.

Kulikuwa na maandamano siku ya Jumanne huku wanawake wakiwa wameshikilia mabango yenye kauli mbiu kama vile "nisikie nikipiga kelele".

Lakini hii sio mara ya kwanza kwa shambulio kama hilo kutokea.

mnamo 2014 waandamanaji walikusanyika Nairobi kuandamana kumuunga mkono mwanamke ambaye alishambuliwa na kuvuliwa nguo na kundi la wanaume kwa sababu alikuwa amevalia sketi fupi.

Maandamano hayo yalishuhudia maelfu ya wanawake wakiandamana nyuma ya mabango yaliyoandikwa ujumbe: "Nguo yangu ni chaguo langu".

Miaka sita baadaye dereva wa matatu na kondakta wake walihukumiwa adhabu ya kifo kwa kumshambulia mwanamke.

Lakini ghadabu huelekezwa kwa visa vilivyonaswa kwenye kamera - lakini visa vingi ambavyo hufanyika bila kurekodiwa na hakuna anayevizungumzia.

Kinachojitokeza katika kisa hiki cha hivi pundi ni kwamba, inaonekana polisi walichukua hatua mara tu video ilipozua hasira - siku tatu baada ya shambulio hilo.

Hali hiyo ineelezea kwa nini baadhi ya wanawake wanahisi kwamba mamlaka haichukulii kwa uzito au kuchunguza ipasavyo malalamiko yao juu ya unyanyasaji wa aina hiyo.

Na linapokuja suala la kuimarisha nidhamu katika sekta ya uchukuzi wa pikipiki, wanasiasa wameonyesha hadharani azimio wanalolijua.

Rais Uhuru Kenyatta ameagiza msako mkali dhidi ya waendeshaji boda-boda kote nchini.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i alitangaza kwamba "lazima tulinde barabara zetu dhidi ya vitendo hivyo viovu na vya kudhalilisha".

Lakini miaka miwili iliyopita alipata ripoti kutoka kwa jopo kazi lililoundwa kuchunguza na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kudhibiti sekta hiyo na aliahidi kuchukua hatua.

Mnamo Agosti 2020 alianzisha mfumo wa usimamizi wa taarifa za boda-boda ambao ulikusudiwa kuweka kumbukumbu ya waendeshaji wote nchini na hivyo kuleta nidhamu katika tasnia hiyo.

Nini kimetokea kwa hilo?

Na sasa inaonekana huenda jopokazi lingine likaundwa ili kutafuta ufumbuzi kwa mara nyingine tena.

Mojawapo ya changamoto ni kwamba, kwa wengi, boda-boda ni njia rahisi, ya haraka na ya bei nafuu ya usafiri. Zinatoa huduma muhimu kwa wateja na vile vile ajira kwa maelfu ya vijana wa kiume.

Hata hivyo, kama ilivyobaini Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu mwezi uliopita, boda- boda pia ni hatari kubwa barabarani na baadhi ya waendeshaji wanahusika katika ujambazi na vurugu, ulanguzi wa dawa za kulevya na hata mauaji.

Pamoja na hifadhidata ya nchi nzima, ripoti yake ilipendekeza mafunzo ya msingi na mtihani kwa madereva.

Pia kuna utaratibu ambao umewekwa na nchi jirani ya Rwanda, ambapo kila dereva aliye na leseni anapewa kifaa kinachotumiwa kuduatilia kidijitali kila pikipiki kupitia mfumo wa GPS.

Na bado tuko katika hali hii.

Tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na tatizo lnalokumba uchukuzi pikipiki linajulikana.

Sasa muda wa kujadili mienendo ya waendesha boda -boda umeisha sasa ni wakati wa kuchukua hatua.

Lakini nihofia kwamba itabidi tusubiri. Kwa sasa ninatumai kuwa mwanamke aliyeshambuliwa anaungwa mkono na watu wanaompenda na wanaweza kumsaidia katika kipindi ambacho lazima kiwe kigumu sana.