David Bennett: Mtu wa kwanza duniani kupandikizwa moyo wa nguruwe afariki

Daktari wa upasuaji Bartley P Griffith akipigwa picha na Devid Benett mapema mwezi huu

Chanzo cha picha, UNIVERSITY OF MARYLAND SCHOOL OF MEDICINE

Maelezo ya picha, Daktari wa upasuaji Bartley P Griffith akipigwa picha na Devid Benett mapema mwezi huu

David Bennett, ambaye alikuwa na tatizo la ugonjwa wa moyo, amedumu kwa miezi miwili tangu afanyiwe upasuaji wa kupandikiza moyo huo Januari 7 nchini Marekani.

Madaktari wanasema katika wiki chache baadaye Bennett alitumia muda na familia yake, alitazama Super Bowl na kuzungumza juu ya kutaka kurudi nyumbani kwa mbwa wake, Lucky.

Hali yake ilianza kubadilika na kuwa mbaya siku kadhaa zilizopita, madaktari wake huko Baltimore walisema.

Maelezo ya video, Wanasayansi wapandikiza jeni za ubongo wa binaadamu ndani ya tumbili

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 57 alifariki Machi 8 mwaka huu.

"Alionekana kuwa mgonjwa jasiri na mzuri ambaye alipigana hadi mwisho," alisema daktati aliyemfanyia upandikizaji huo Bartley Griffith, kupitia taarifa iliyotolewa na hospitali.

Madaktari kituo cha afya cha Chuo KIkuu cha Maryland Marekani walikuwa wakimfuatilia kwa karibu, makini na kwa uangalifu mkubwa, huku mwanae wa kiume David Bennett Jr wakati wa zoezi hilo aliliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba familia yao iko "katika hali ya sintofamu wakati huu".

Bwana Bennett alijua hatari zilizohusishwa na upasuaji huo, lakini akikubali, ilikuwa ni kama "kutupia jiwe gizani".

Upandikizaji wa moyo huo ulichukuliwa kama matumaini ya kuyaokoa maisha a Bw Bennett, ingawa haijkuwa wazi awali angeishi kwa muda gani.

''Ninafahamu kwamba ni jambo la kubahatisha, lakini ni chaguo langu la mwisho," alisema Bennett kabla ya kufanyiwa upasuaji huo.

Lakini kile kitakachotokea baadaye hakijawa wazi. Nguruwe aliyetumiwa katika upandikizaji alifanyiwa mabadiliko ya vinasaba ili kuondoa jeni kadhaa ambazo zingefanya kiungo hicho kikataliwe na mwili wa Bw Bennet, linaripoti shirika la habari la AFP.

Madaktari wa Chuo Kikuu cha Maryland wakati huo walipewa idhini maalum na wasimamizi wa matibabu kuendelea na upasuaji huo, kwa misingi kwamba kama isingikuwa hivyo Bw. Bennet angepoteza maisha.

Ilionekana kwamba hakuwa na uwezo wa kupandikiziwa moyo wa binadamu, uamuazi ambao mara nyingi huchukuliwa na madaktari wakati mgonjwa anapokuwa na afya dhoofu sana.

Uwezekano wa kutumia viungo vya Wanyama kwa ajili ya kile kinachoitwa xenotransplantation ili kufikia mahitaji umekuwa ukifikiriwa kwa muda mrefu, na matumizi ya mishipa ya moyo wa nguruwe tayari limekuwa ni jambo la kawaida.

Mwezi Oktoba, 2021, madaktari wa upasuaji mjini New York walitangaza kwamba wamefanikiwa kupandikiza figo ya nguruwe kwa binadamu.

Kwa wakati huo, upasuaji huo ulikuwa ni jaribio la teknolojia ya hali ya juu zaidi kuwahi kufikiwa.

Hatahivyo, ubongo wa mtu aliyepandikiziwa ulikufa na hakukuwa na matumaini ya kupona.