Mzozo wa Ukraine: Fahamu kura ya turufu ya Urusi katika azimio la Umoja wa Mataifa, je ina maana gani?

Chanzo cha picha, Reuters
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA limepitisha azimio la kuitaka Urusi kusimamisha mara moja mashambulizi yake dhidi ya Ukraine na kuyaondoa majeshi yake katika nchi hiyo.
Jumla ya nchi 96 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilishiriki katika uwasilishaji wa azimio hilo ambalo lilihitaji theluthi mbili tu ya kura za ndio ili liweze kupita.
Baraza hilo lilikutana katika kikao chake maalum cha 11 cha dharura hapo jana ambapo pamoja na kupitisha azimio hilo, limesisitiza pia azma yake ya kutambua mamlaka ya Ukraine, uhuru, umoja na mipaka yake ya majini na ardhini inayotambulika kimataifa.
Huenda likawa pigo kwa Urusi, kutokana na msimamo huo ambao unalenga kurejesha hali ya usalama katika nchi ya Ukraine kufuatia uvamizi wa wiki iliyopita wa Urusi.
Mataifa yaliyopinga azimio dhidi ya Urusi
Azimio la kuitaka Urusi kusitisha mapigano Ukraine lilipitishwa kwa kura nyingi ambapo mataifa 141 yaliunga mkono azimio hilo, mataifa matano yalipinga, na mataifa mengine 35 hayakuwepo kwenye mchakato wa kupiga kura.
Mataifa ambayo yalipinga azimio hilo wakionekana kuiunga mkono hatua ya Urusi huko Ukraine Urusi yenyewe, Belarus, Syria, Korea Kaskazini na Eritrea.
'Misimano ya mataifa haya haikua mbali na mitazamo ya Urusi, haikushangaza nchi kama Belarus kuiunga mkono Urusi, ilhali ardhi yake inatumika kuhifadhi vifaa vya kijeshi na vikosi vinavyoingia kwenye mpaka wa Ukraine', alisema Beatrice Kimaro, mchambuzi wa Tanzania.
Hata kabla ya zoezi la upigaji kura kufanyika, mataifa kama India, Korea Kaskazini, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia yalionekana kimya kuonyesha misimamo yao ya wazi kuhusu mzozo huo. China yenyewe ikiwa na msimamo vuguvugu.
" China upande wake imekuwa ikicheza karata ya diplomasia ya kuuma na kupuliza kwa pande zote mbili Ukraine na Urusi. Lakini wakati ikitoa wito wa suluhisho la amani ni wazi imeshindwa kwenda mbali zaidi kulaani uvamizi wa Urusi kwa sababu nchi hizo mbili zilikuwa zote wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zenye kura ya turufu kwanza zinahitajiana katika masuala yayohusika na siasa za dunia", anasema Mohammed Abdulrahman, mchambuzi wa Tanzania kwenye moja ya makala zake zilizochapishwa na BBC kuhusu mzozo huo.
Kwanini mataifa 35 hayajapiga kura ya azimio dhidi ya Urusi?
Miongoni mwa mataifa ambayo hayakupiga kupiga kura kati ya hayo 35 ni pamoja na Tanzania, Congo, Afrika Kusini, Burundi, Uganda, India na Mali.
Mengine baadhi ni Madagascar, Cuba, Morocco, Zimbabwe Turkmenistan, Zimbabwe na Venezuela.
Wachambuzi wanasema kutokupiga kura kunaweza kuwa na sababu nyingi.
'kwenye masuala yenye ukinzani wa namna hii, yapo mataifa ambayo huamua 'kususia', ili yasijulikane misimamo yao wazi, mengine inawezekana kwa sababu zilizokuwa nje ya uweoz wao kuhudhuria zoezi hilo, ni jambo la kawaida', alisema Raphael Kugesha, mtaalam wa masuala ya jamii anayefuatilia siasa za kimataifa kutoka Kilimanjaro, Tanzania.
Kutokupiga kura kwa mataifa hayo hakutaathiri utekelezaji wa azimio lililopitishwa na idadi kubwa ya wajumbe.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa dharura kwa mara nyingine kujadili hali inayoendelea kutia wasiwasi mkubwa nchini Ukraine na kupiga kura.
Lengo ni kuiwajibisha Urusi kuzingatia kanuni na sheria za kimataifa lakini Urusi imeamua kwa mara nyingine kutumia tena kura yake ya turufu kupinga azimio lolote dhidi yake.
Kura ya turufu ya Urusi ina maana gani
Kura ya turufu kwa jina lingine kura ya veto maana yake ni ule uwezo wa haki inayopewa taifa fulani kukataza azimio lolote kupita wala kutekelezwa hata kama limekubaliwa na kupitishwa na mataifa mengi.
Yako mataifa mengi raia yanakuwa na kura hii kukataza maamuzi fulani fulani hata kama yamepitishwa na kukubaliwa na bunge.
Kwa mfano mataifa matano ya kudumu ya umoja wa mataifa yenye kura za veto ni China, Ufaransa, Uingereza, Marekani, na Urusi. Mataifa haya kila moja linaweza kuzuia maazimio yoyote ya baraza la usalama la Umoja huo.
Wengi wanaipinga kura ya veto kwa sababu inaonekana kama inakandamiza demokrasia, na kutoa nguvu kwa mataifa haya matano kufuatwa matakwa yao. Kwamba taifa moja tu linaweza kuzuia azimio lililoungwa mkono na mataifa yote wanachama. Lakini kupitia kwa azimio la 'Uniting for Peace', lililotekelezwa mfano jana, inatajwa kuwa suluhu ya kukivuka kiunzi cha kura ya veto.
Kupitia azimio hilo, la mwaka 1950 ni kwamba nchi zenye kura ya veto haziwezi kulizuia baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kuchukua hatua muhimu katika kurejesha usalama na Amani, ikiwa imeshindikana chini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).
'Hata baada ya Urusi kupiga kura ya Veto kuzuia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua, lakini azimio la 'Uniting for Peace', linaipa mwanya Baraza kuu la Umoja wa mataifa kuendelea na azimio hilo', alisema Beatrice Kimaro, mchambuzi wa Tanzania.
Azimio la sasa, linamaanisha kwamba Urusi imetengwa na mataifa mengi, ikionekana kuungwa na mataifa machache tu ya Belarus, Syria, Korea Kaskazini na Eritrea.
Si mara ya kwanza kwa Urusi kutumia kura ya veto katika siku za hivi karibuni, ilishafanya hivyo mwaka 2017 ilipopiga kura hiyo kuzuia kupitishwa kwa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuishutumu serikali ya Syria kuhusika na shambulizi la silaha za kemikali lililosababisha vifo vya raia 80.
Watu wanasema nini na nini kinafuata baada ya kupitishwa kwa azimio hilo dhidi ya Urusi?
Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alikunuliwa na vyombo vya habari akisema kwa sasa hakuna cha kupoteza muda.
"Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limezungumza na kama Katibu Mkuu ni wajibu wangu kusimamia azimio hili na niongozwe na wito wake', alisema Guterres.
Hilo litaendelea kuiweka Urusi katika wakati mgumu wa vikwazo mbalimbali vya kiuchumi ambavyo tayari vimekwishaanza kuonyesha makali yake kwa wananchi wake.
Ni wajibu sasa wa Urusi kuamua ama kukubaliana na azimio hilo na kusisitisha uvamizi wake Ukraine au kuendelea. Iwapo ittaendelea kukaidi azimio hilo la Umoja wa mataifa ambao yenye ni mwanachama wa kudumu, Baraza lake litakutana tena kuamua hatua nyingine, ambayo huenda ikawa na madhara zaidi.
Mmoja wa Watanzania, Cadabra Junior anasema kwenye mtandao wake wa twitter kwamba vita hii ni ya wakubwa waachiwe wenyewe.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Mbali na kusubiri ripoti ya mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu kuhusu hali ya kibinadamu huko Ukraine, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdullah Shahid amewaambia waandishi wa habari kuwa kupitishwa kwa azimio hilo ni kiashiria cha hofu kubwa inayokabili jamii ya kimataifa juu ya hali inayoendelea Ukraine.
Anasema ni msisitizo kwamba mapigano yasitishwe haraka, huduma za kibinadamu ziwafikie wenye uhitaji Ukraine ikienda sambamba na mazungumzo ya diplomasia kuhusu mzozo wa Ukraine.
Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi
- MOJA KWA MOJAUrusi na Ukraine: Mlipuko wakumba Kyiv huku Urusi ikiendeleza mashambuliziShambulio la Urusi katika mtambo wa nishati wa Ukraine lasababisha moto mkubwa
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine














